Wednesday, July 26

Waharibifu wa Vyanzo vya Kibakwe Maji Kukiona – Waziri Simbachawene


Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais (Tamisemi),  George Simbachawene (kulia) akizungumza na wananchi baada ya kupokea malalamiko yao katika Kijiji cha Lukole kuhusu shida ya maji wanayoipata, wakati alipokwenda kwenye bomba la Kijiji kuzungumza na wakinamama ambao ndio waathirika wakubwa wa tatizo hilo na kuwataarifu namna ambavyo amekwishaanza kushughulikia kero hiyo.

Na Nteghenjwa Hosseah - Kibakwe.

Uharibifu wa vyanzo  vya maji ni tatizo lililokithiri katika maeneo mengi Nchini Tanzania huku wananchi wa maeneo hayo wakiendelea kushuhudia na kuvumilia uharibifu huo eti kwa sababu tu wahusika ni ndugu, jamaa ama  marafiki wa jamii husika.

Pasipo kujali athari zinazoweza kutokea kutokana na uharibifu wa mazingira hususan vyanzo vya maji wananchi wameendelea kulima, kufuga, kuchunga  pamoja na kuishi katika maeneo hayo pasipo kuwa na shaka yoyote na kusababisha ukosefu wa maji kwa jamii inayotegemea vyanzo hivyo. 

Athari zaidi zimethibitija katika Kijiji cha Chinyika na Lukole  vilovyopo kata ya Chinyika kwa kukosa maji kutokana na Uharibifu uliofanywa na baadhi wa wananchi katika chanzo cha maji kwenye milima ya wota ambacho ndio chanzo kikuu cha maji ya mtiririko kwa wananchi zaidi ya elfu saba.
Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais (Tamisemi),  George Simbachawene (katikati aliyekaa) akisimikwa kuwa Chifu wa Kigogo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kingiti.

Hali hii imepelekea wananchi wa vijiji hivyo vyenye vitongoji zaidi ya kumi na tano kuwekeana zamu ya kuchota maji ambapo kwa wiki kila Kijiji hupata maji kwa siku tatu na kila kaya huchota Ndoo nne kwa siku ya zamu yao ambapo kiasi hicho hakiwajawahi kuwatosha mahitaji ya Kaya.

Wananchi wa Kijiji cha Chinyika wamepaza sauti zao kwa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais (Tamisemi),  George Simbachawene wakati wa ziara yake katika vijiji hivyo na kulalamikia tatizo la upungufu wa maji na adha wanayopata kutokana na hali hiyo.

Waziri Simbachawene ameshuhudia foleni ndefu ya ndoo za wakinana wakiwa bondani kusubiria kupata japo maji ya kupikia chakula cha Familia, Wakinamama hao hushinda zaidi ya siku nzima bombani hapo au pengine kukesha ili kuwa na uhakika wa kupata japo ndoo moja ya maji kwa matumizi ya nyumbani.

Akizungumza na wakinamama Waziri Simbachawene amesema anatambua adha wanayoipata na amewahakikishia kwamba ataanza kutatua changamoto hiyo kwa kuhakikisha wale wote wanaharibu vyanzo vya maji katika Wilaya ya Mpwapwa wanatiwa nguvuni na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais (Tamisemi),  George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kingiti wakati wa zaiara yake katika Jimbo la Kibakwe.

 “Ninajua kwamba waharibifu wa vyanzo hivi ni watu wenye nguvu lakini na mimi ntaongeza nguvu kwenye Kikosi kazi cha Wilaya ili kuhakikisha kwamba wale wote wanaoishi karibu na vyanzo hivyo wanahamishwa na mazao yao yanaharibiwa, mifugo inaondolewa na wanapelekwa Mahakamani” alisema Mhe. Simbachawene.

Pia aliongeza kuwa Fedha zimekwishatengwa zaidi ya Tsh Mil 160 kwa ajili ya ukarabati ya miundombinu inayotoa maji kutoka katika Milima ya Wota kupitia Kingiti hadi kufika Lukole na Halmashauri ya Mpwapwa imeanza utekelezaji wa mradi huu utakaokuwa na manufaa kwa wananchi na ataongeza Tsh Mil 13 kwa ajili ya kuchimba kisima. 

Naye Mhandishi wa Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Apolonia Temu ameelezea sababu ya ukosefu wa maji katika vijiji hivyo kuwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira, ongezeko la watu ukilinganisha na hapo awali  na uchakavu wa miundombinu ambayo kwa sasa imeanza kukarabatiwa.

Waziri Simbachawene ameendelea na ziara yake katika Jimbo la Kibakwe na kwa siku ya tatu ametembelea vijiji vya Lukole, Kingiti na Itenge ambapo amefanya mikutano ya hadhara, amesikiliza kero za wananchi pamja na kukagua miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment