Wednesday, July 26

PROFESA MDOE AFUNGUA RASMI MKUTANO WA KIMATAIFA WA MAZIWA MAKUU ICGLR


Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya  Nishati na Madini,  Prof. James Mdoe, tarehe 25/7/2017, amefungua rasmi Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika.
Mkutano huo unaofanyika jijini Arusha kwa siku tatu umehudhuriwa na nchi wanachama 12 ambazo ni Tanzania, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Zambia, Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan  na Kenya.
Akifungua mkutano huo, Prof Mdoe alisema kuwa baadhi ya masuala muhimu yatakayojadiliwa ni pamoja na matumizi ya hati moja ya usafirishaji madini, kuwianisha sheria za nchi wanachama ili kuwa na uwiano katika kudhibiti utoroshaji madini, pamoja na urasimishaji wa shughuli za wachimbaji wadogo.
Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na uongezaji wa ushiriki wa wanawake katika shughuli za uchimbaji madini, uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uziduaji (EITI)  pamoja na uzuiaji wa watoto katika shughuli za uchimbaji madini.
Pamoja na kujadili utekelezaji wa malengo  mbalimbali ya kamati hiyo na kupeana uzoefu wa shughuli za udhibiti wa uvunaji wa haramu wa madini katika nchi hizo, ICGLR itatoka na maazimio yanayopaswa kutekelezwa na nchi wanachama ili lengo la udhibiti wa uvunaji  haramu wa madini lifanikiwe.
 Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya  Nishati na Madini,  Prof. James Mdoe akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika unaofanyika jijini Arusha.
 Baadhi ya Wajumbe  kutoka Tanzania, Sudan, Sudan Kusini na Rwanda waliohudhuria Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika unaofanyika jijini Arusha. Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka na wa pili kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini, John Nayopa.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya  Nishati na Madini,  Prof. James Mdoe (katikati,) akiwa na Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika.

No comments:

Post a Comment