Everton iliyowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JNIA) ilipokelewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Ndege binafsi ya Everton iliwasili JNIA saa 2:39 Asubuhi, kabla ya wachezaji kuanza kuingia kwenye basi lao maalumu huku wakipitia kwa Waziri Mwakyembe na kumpa mkono kuanzia saa 2:55.
Wakati wachezaji wa Everton wakiingia kwenye basi, mashabiki waliokuwa nyuma ya geti la kuingilia VIP kila mmoja alionyesha shauku ya kumuona mubashara 'live' Rooney ambaye kana kwamba msafara huo ulilitambua hilo na Rooney kuwa wa mwisho kushuka.
Aliposhuka Rooney alikwenda kumpa mkono Waziri Mwakyembe na kisha kuelekea kwenye basi maalumu la timu hiyo, wakati akielekea kwenye basi baadhi ya mashabiki wake waliokuwa uwanjani hapo walianza kupaza sauti wengine wakitaka ageuke asimame na kupunga mkono, lakini wala hakuwa na habari nao zaidi ya kwenda moja kwa moja kwenye basi.
"Jamani hii timu ndiyo imewasili, ni timu kubwa na Tanzania tunafarijika kwa ujio huu, niwambie tu Watanzania hata nyinyi Waandishi wa Habari, ulinzi umeimarishwa na katika mazoezi yao hata ruhusiwa mtu yoyote asiyehusika kwenda.
"Watu wakae nyumbani watulie wasubiri siku ya mechi (kesho) waende uwanjani kushuhudia," alisema Waziri Mwakyembe mara baada ya msafara wa Everton kuingia kwenye magari tayari kwa safari ya kuelekea Hotelini saa 3:10 asubuhi.
Everton itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kesho kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
No comments:
Post a Comment