Thursday, November 30

Lissu asimulia mambo mazito kwa dakika 60

Nairobi-Kenya. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesimulia hali ilivyokuwa siku ya tukio na pia kueleza ujumbe aliompa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipomtembelea hospitalini jijini hapa juzi.
Mbunge huyo, ambaye alishambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, pia amesema amepitia majaribu mengi, lakini “hili ndilo kubwa”.
Amesema hali yake inaendelea vizuri na madaktari wanamuelezea kuwa ni “muujiza unaoishi” baada ya kufanikiwa kuunganisha vipande vya mwili ulioharibiwa kwa risasi.
Lissu alisema hayo alipofanya mahojiano na Mwananchi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha habari cha Tanzania tangu ashambuliwe.
Lissu amelazwa Hospitali ya Nairobi jijini hapa tangu Septemba 7 na huenda akahamishiwa nje ya bara la Afrika kwa matibabu zaidi, ambayo yatahusu mazoezi, kabla ya kurejea nchini.
Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo, Lissu alisema sasa anaamini kuwa Rais John Magufuli anajua kuna mgonjwa Nairobi na hivyo kufungua milango kwa wengine waliokuwa na hofu.
“Mimi namuamini na naendelea kuamini kwamba kwa sababu sasa Makamu wa Rais amekuja kwa niaba ya Rais, ametambua tuna mgonjwa yupo Nairobi. Milango itafunguka kwa wale wengine wote waliokuwa na hofu ya kuja,” alisema Lissu.
“Sasa Rais mwenyewe kamtuma makamu wake kuja kunipa pole, kwa hiyo hao wengine wa taasisi zote hawana hofu ya kuja kuniona.”
Akizungumzia mazungumzo yake na Suluhu, Lissu alisema yalikuwa mazuri.
“Mama Samia ni kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Tanzania pamoja na mihimili yake kuja kunitembelea,” alisema Lissu.
“Spika wa Bunge hajaja, katibu wake na uongozi mzima wa Bunge haujaja. Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi hawajaja pamoja na kwamba mimi ni Rais wa TLS.
“Na kwa kawaida mila na desturi za mahakama zetu, bila mawakili hakuna mahakama na kama Rais wa TLS nimekuwa nikialikwa na kuhudhuria vikao mbalimbali vya kiutendaji, lakini tangu nimeshambuliwa Jaji Mkuu au uongozi mzima wa Mahakama hata kutoa salamu za pole, hakuna.
“Rais Magufuli alikuwa hajawahi kusema lolote kuhusu kushambuliwa kwangu kama nakumbuka, lakini leo (juzi) amekuja Makamu wa Rais na amenieleza na napenda kuamini ni kweli ametumwa na Rais kama sehemu yake ya shughuli zilizomleta Kenya apitie kunisalimia na kunipa pole.”
Alisema Makamu wa Rais, ambaye waliwahi kufanya naye kazi wakati akiwa waziri anayehusika na Muungano na Lissu akiwa waziri kivuli wa eneo hilo, alimuuliza kama ana jambo lolote la kumweleza Rais, naye akamweleza kuhusu gharama za matibabu.
“Mimi bado ni mbunge, ujumbe ambao nataka aupeleke ni Bunge liko wapi? Bunge ambalo lina wajibu wa kisheria wa kunihudumia nikiwa naugua?” aliuliza Lissu akirejea mazungumzo hayo na Suluhu juzi jioni.
“Nilimpa ujumbe huo na napenda kuamini ataufikisha na ujio wake peke yake unatakiwa kufungua milango kwa wale waliokuwa wanafikiri wamefungiwa.”
Alisema suala la Bunge kuwa mbali naye ni mfano mwingine unaotia shaka kuhusu kushambuliwa kwake.
“Mimi ni mbunge na ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ninatambuliwa na Sheria za Tanzania, Sheria inayohusika ni ya uedeshaji wa Bunge. Sheria inaeleza kwamba mbunge anapoumwa atapata matibabu pamoja na gharama nyingine kutoka bungeni,” alisema.
Lissu alisema kila mbunge anayeumwa analipiwa gharama zote na Bunge na vile vile kama itabidi, alazwe nje ya Dodoma iwe Dar es Salaam, Afrika Kusini, India Marekani au Kenya.
“Analipwa posho na Bunge na mtu anayemuuguza analipwa posho vile vile, nusu ya posho ya mbunge ili kumudu gharama za maisha,” alisema.
“(Lakini) Tangu nimeumizwa, Spika anajua, alitangaza bungeni mbunge mwenzetu anaumwa. Tangu wakati huo mpaka leo Spika hajaja, Katibu wa Bunge, Tume ya Bunge haijaja,” alisema Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema.
Alisema  kuna wabunge wawili CCM, Mary Chatanda (Korogwe Mjini) na  Fakharia Shomar Khamis (viti maalum na mmoja wa watumishi wa Bunge walifika siku ya Jumapili, siku ambayo si ya kazi.
“Walikuja kunipa pole, walikaa hapa wakanipa nipa pole, halafu wakaniaga. Nikawauliza mmetumwa chochote, wakasema hapana,” alisema.
“Nikamuuliza ofisa wa Bunge, ‘kuna ujumbe umetumwa uniletee, akasema hapana. Kwa hiyo hao wawili walikuja kibinafsi tu.
“Tume ya Huduma za Bunge inayoshughulikia mambo haya, haijaja mpaka leo. Kwa hiyo ukiachilia mbali matangazo ya Spika, Bunge halijaja kabisa, halijanishughulikia kwa lolote.
“Hakuna anayeomba fadhila, nataka haki, nitendewe haki, anayetendewa mbunge yoyote anayeumwa. Hakuna anayelilia fadhila hapa, hakuna anyeomba ufadhili. Nataka Bunge litimize wajibu wake wa kisheria. Hili nitalipigania, kama siwezi kudai haki yangu ya kisheria ambayo iko wazi, kama ya kwangu naona inakanyangwa kwa makusudi tu, nitapigania ya nani?”
Lissu alisema Bunge halina sababu za maana za kutomgharimia, bali ni kupiga chenga tu.
“Wameandikiwa barua na ndugu yangu mara hawajaiona, kwa hiyo lazima nipiganie haki yangu ili nipiganie haki za wengine,” alisema.
Niliona watu wawili wenye silaha
Katika mahojiano hayo na Mwananchi yaliyochukua takriban dakika 60, Lissu pia alielezea jinsi shambulio dhidi yake lilivyofanyika Septemba 7, lakini tofauti na kauli ya ndugu zake kuwa anawajua watu hao, alisema hawafahamu watu hao na kusisitiza suala la wachunguzi kutoka nje.
“Nilitoka bungeni muda wa saa saba hivi,” alisema.
“Kabla sijatoka nilichangia mjadala wa mkataba kati ya Malawi na Tanzania kuhusu Mto Songwe. Baada ya kumaliza kuzungumza nikakaa kidogo kisha nikatoka na kwenda nyumbani kwa chakula cha mchana.
Alisema alivyofika nyumbani, wakatokea watu eneo la kuegesha magari katika nyumba hizo za Serikali, ambako anaishi jengo moja na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, mbunge wa Ulanga Magharibi (CCM), Dk. Haji Mponda na mmoja wa makatibu wakuu wa wizara.
“Kwa hiyo nakaa katika nyumba za Serikali. Watu wameingia katika nyumba za Serikali zinazolindwa saa 24, block inayotazamana na nyumba yangu, anakaa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na huwa kuna polisi nje saa 24,” alisema.
“Lakini watu wameingia wenye silaha, wakaja kunishambulia. Sikuwatambua kwa sababu nilishambuliwa nikiwa katika gari sikutoka nje. Dereva wangu aliniambia kuna watu wako nyuma wananifuata nisifungue mlango.”
Alisema alijaribu kuwaangalia kwa kutumia kioo cha pembeni ya gari na kuwaona watu wawili wakitoka na bunduki. Yaliyofuata nimekuja kujikuta nipo hapa nilipo leo wiki moja baadaye.
“Kwa hiyo, siwezi kusema ninawafahamu walionishambulia. Sikutambua hata mmoja wao ila najua nilishambuliwa na watu wawili katika gari iliyokuwa na vioo vyeusi.”
Lissu alisema wiki tatu kabla ya shambulio hilo alilalamika hadharani kwamba anafuatiliwa kila anapokwenda na siku moja aliwasimamisha watu hao katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro na kuwauliza sababu za kufanya hivyo.
“Niliwauliza kwa nini wananifuata na kama kuna mtu kawatuma, mwambieni mimi si mhalifu. Lakini sikupewa ulinzi wowote,” alisema.
Wachunguzi kutoka nje
Kama ilivyo kwa familia yake na Chadema, Lissu anataka uchunguzi wa tukio hilo ufanywe na taasisi ya nje.
“Serikali inakosea sana,” alisema.
“Hili ni tukio la mbunge kushambuliwa akiwa maeneo ya Bunge. Kisheria hayo maeneo yanayoitwa ya Bunge ni pamoja na makazi ya wabunge wanapokuwa bungeni.”
Alisema huwezi kuwa bungeni kama huna sehemu ya kulala, kwa hiyo makazi yangu ni sehemu ya Bunge.
“Kitendo cha mbunge kushambuliwa wakati vikao vinaendelea-- na mbunge mwenyewe ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na anajulikana kwa kuikosoa Serikali mara nyingi kwa muda mrefu, inatia shaka,” alisema.
“Kitendo hicho peke yake kingetosha kutilia shaka uchunguzi wowote utakaofanywa na wale ambao mbunge huyo amekuwa akiwasema mara kwa mara. Kitendo hicho kingetosheleza kualika watu kutoka nje kuja kufanya uchunguzi.
“Wanakataa kwa sababu zao, tunaelekea miezi mitatu, polisi hawajasema wanamshuku nani. Hakuna mtuhumiwa hata mmoja halafu kuna jitihada kubwa imefanywa na Jeshi la Polisi kuzuia raia kumsaidia huyu mbunge.”
Alisema polisi imewazuia watu wasisali, wasimwombee Mungu apone, watu wasimchangie damu, kusiwe na dalili zozote za wazi za kumuunga mkono na huyu ambaye ameshambuliwa na watu wanasemekana hawajulikani.
“Kumekuwa na jitihada kubwa sana kuzuia watu wasimsaidie huyu kuliko kufanya upelelezi, hiyo inatoa picha kwamba bila uchunguzi huru ukweli hautajulikana, utafichwa na pengine ndivyo wanavyotaka,” alisema.
Akizungumza huku akisisitiza kwa mikono yake, Lissu alisema katika mlango wa Waziri Kalemani, kuangalia block ya Naibu Spika Dk Tulia, kuna camera za CCTV zinazofanya kazi Saa 24 hivyo kwa mtu yeyote ambaye yupo eneo hilo anaonekana, lakini akasema kuna vitu vinaashiria kuwa kunahitajika jicho la pili kuangalia hili.
Alipoulizwa nafasi ya Rais Magufuli katika suala hilo la uchunguzi, Lissu alisema: “Rais anaweza akitaka kuelekeza. Polisi ndio wenye mamlaka ya kiuchunguzi, waalike wataalamu kutoka nje.
“Haitakuwa mara ya kwanza, hatutakuwa wa kwanza kufanya hivyo na haitakuwa aibu ila ni namna nzuri zaidi ili kuondoa wingu lililotanda juu ya kushambuliwa kwangu, ukweli utajulikana na hiki kimya si kizuri.”
Lissu pia alizungumzia hali yake kiafya na matarajio yake.
“Nafikiri kiafya Lissu anaendelea vizuri na matibabu, hajapona bado lakini anaendelea vizuri, madaktari wanasema hali yangu inakuwa inatengamaa kila siku,” alisema.
“Huko tulikotoka ni kurefu zaidi kuliko tunakokwenda, vidonda vyote vya risasi vimepona, sina bandeji mwilini, sina bandeji kabisa. Maana yake vile vidonda vyote vilivyotokana na kupigwa risasi vimepoma.”
Hata hivyo, Lissu, ambaye chama na familia yake imesema ataenda kumalizia matibabu nje ya bara la Afrika, alisema bado hajajua ataruhusiwa lini, ingawa anajiona yuko katika hali nzuri.
“Madaktari hawajanipa muda, na nafikiri hawajanipa muda kwa sababu nzuri tu, majeraha niliyokuwa nayo nilipoletwa hapa, yalikuwa makubwa sana, madaktari wenyewe wamekuwa wakiniambia mimi ni muujiza unaoishi,” alisema.
“Kwa hali niliyoletwa hapa ni muujiza unaoishi. Kazi kubwa walioifanya ya kwanza ilikuwa kuhakikisha wanaokoa maisha na wameokoa maisha. Kazi ambayo inafuata ni kuniwezesha kurudi sasa katika hali yangu ya kawakida, kuweza kujitegema kimwili.”
Alisema madaktari wamemuwekea vyuma, wameunganisha mifupa.
Alisema mikono ilikuwa haifanyi kazi, lakini sasa anaweza kuichezesha na kula na kwamba tiba hiyo inachukua muda lakini tuko katika hatua ambayo si ya kuokoa maisha, bali ya kurudisha mwili katika hali ya kawaida.
“Kimawazo nafikiri sijabadilika sana, Lissu wa kabla ya Septemba 7 na Lissu wa leo kimsimamo wa kisiasa hajabadilika kabisa. Lazima tupiganie demokrasia, hiyo ndiyo salama yetu,” alisema.
“Tuwe na utawala wa kidemokrasia unaojali haki za binadamu, tuwe utawala wa sheria, tuwe na mfumo wa uongozi unaojali maisha ya wananchi, unaowajibika kwa wananchi au kwa wawakilishi wake na huu ni msimamo wangu unajulikana na bado uko vile vile.
Aadhimisha miaka 20 ya ndao wodini
Wakati akiendelea kutibiwa hospitalini hapo, jana Lissu na mkewe, Alicia walitimiza miaka 20 tangu walipofunga pingu za maisha Novemba 29, 1997 na kama kawaida walikuwa pamoja wodini.
“Mke wangu nikuzungumzieje?” alimuuliza.
“Kazi kwako,” Alicia alijibu.
“Mke wangu mpenzi anaishi kiapo chake tulipooana na kesho (jana) tunatimiza miaka 20. Tulipooana nilimsikia anasema ‘katika shida na raha’ nitampenda, nitafanya nini na nini’. Kwa hiyo mke wangu mpenzi anaishi katika kiapo chake,” alisema Lissu huku Alicia akitabasamu.
“Katika miaka hii 20, tumepitia majaribu mengi sana, lakini hili ndilo kubwa kuliko yote na nafikiri kama ni mtihani, mke wangu ameufaulu kwa daraja la juu kabisa kwa sababu amekuwepo hapa muda wote na mara nyingine ukimsikia anavyozungumza ana msimamo mkali kuliko mimi niliyeumizwa.”
Lissu alisema Alicia “ni mke wa kweli, aliyekubali kuchukua majukumu ya kuwa mke”, na kwamba anajisikia faraja na furaha ya kipekee kuwa naye na angepende wawe pamoja miaka 20 mingine.
“Najisikia mwanamme mwenye bahati sana kuwa naye. Ni mwanamke wa kipee sana kuwa naye. Tumetoka mbali sana na hii miaka 20 imekuwa mizuri sana katika maisha yangu kwa sababu ya kuwa naye,” alisema.
Alicia pia alikuwa na lake moyoni.
“Miaka 20 ni mingi, lakini nikifikiria kama ni juzi tu. Halafu nilikuwa sitaki kumkummbusha nilitaka kumfanyia ‘surprise (kumstua),” alisema huku Lissu akimsikiliza kwa makini na kutabasamu
“Lazima niwe mkweli. Kuna miaka mingine alikuwa busy (na kazi nyingi), anasahau hata siku. Tundu ni mme wangu, kikubwa naweza kusema ni rafiki yangu wa karibu sana wa miaka mingi sana, nikiwa msichana mdogo, mrembo na smart. Tumekuwa tukiishi hivyo.”
“Ujumbe wangu, Tundu siku zote aendelee kuwa Tundu tu. Tundu wa kabla ya tukio na baada ya tukio awe ni Tundu niliyemjua siku zote.”
Je, utagombea Urais 2020
Mbunge huyo wa Singida Mashariki hakutaka kuzungumzia uchaguzi wa mwaka 2020 na hata alipoulizwa kuhusu kugombea urais alistuka.
“Nafikiri huu ni mjadala unaohitaji kusubiri wakati mwafaka,” alisema.
“Si mjadala unaoweza kufanyika katika kitanda cha Hospitali ya Nairobi, Kenya. ni mjadala unaohitaji tukae, tushauriane. Kwa sababu ni chama lazima tukae tushauriane. Nafikiri hiki kitanda changu si mjadala wa kuanzisha, kama watu wananitajataja huko waendelee tu lakini mimi mjadala huu unisubiri nje ya hospitali.”Lakini Lissu alisema kwa sasa atakuwa wa tofauti kwa kuwa amepitishwa tanuru la moto na amepata uzoefu wa kutosha baada ya kujifunza mengi kutokana na tukio la Septemba 7.
“Nikitoka hapa kama Mungu amenipa pumzi ya kuendelea kuishi, haya mafunzo yatakuwa sehemu ya Lissu huyo baada ya Septemba 7. Nimejifunza kuwa Watanzania ni watu wa upendo sana. Pamoja na propaganda zote, uongo wote na ubaya wa watu, lakini Watanzania ni watu wa upendo sana,” alisema Lissu
“Wanafahamu nani anawapigania. Kuna rafiki yangu wa Dodoma ameniambia baada ya kupigwa risasi kuwa mji mzima ulihamia hospitali. Ingawa siku zote CCM wanashinda pale, siku hiyo walihamia pale (hospitali). Watanzania kila mahali walienda makanisani, misikitini, nafikiria huo upendo nitaulipaje.
“Nafikiria ni upendo ni kwa sababu ya kazi niliyoifanya bungeni na nje ya Bunge na hiyo kazi kama imewafanya wawe na upendo namna hiyo, basi nitaizidisha na nitawafanyia kazi iliyo bora zaidi.”

Mafataki wawakatishia ndoto wanafunzi 106



Ukerewe. Wanafunzi 106 wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa wamefukuzwa baada ya kubainika kuwa na ujauzito, wakati wa upimaji uliofanyika kati ya Januari na Aprili.
Katibu tawala wilaya ya Ukerewe, Focus Majumbi alisema kati ya wanafunzi hao, wawili ni wa shule za msingi huku waliosalia wakiwa ni wa sekondari.
“Sekondari ya Ilugwa iliyopo kisiwani, pekee ilikutwa na wanafunzi 11 wenye mimba,” alisema na kwamba, tayari wanaume 28 waliodaiwa kuwapa ujauzito wanafunzi hao wamefikishwa mahakamani.
Ili kukabiliana na tatizo la mimba shuleni, wilaya  imeweka mikakati ikiwamo kupiga marufuku matamasha ya muziki nyakati za usiku maarufu Mazinduke.
Naye mkuu wa Sekondari ya Ilugwa, Emmanuel Bomba alisema kati ya wanafunzi 11 waliobainika kuwa na ujauzito shuleni kwake, mmoja alipewa ujauzito na mjomba wake. Alisema kati ya wanafunzi 283 wa shule hiyo yenye mabweni mawili yanayochukua wanafunzi 96 kila moja, ni kumi pekee wazazi wao wamewalipia Sh480,000 za chakula na malazi. Shule hiyo iliyoko kwenye moja ya visiwa 38 vya Ukerewe, inapokea wanafunzi kutoka visiwa vya Kulazu na Buluza.
Kuhusu mikakati hiyo, ofisa elimu sekondari wilaya, Venance Nyamwale alisema Serikali inafanya jitihada kukabiliana na changamoto zinazokwamisha maendeleo ya wanafunzi wa kike.

Uongozi wa kijiji watishiwa kwa kuzuia uuzaji sekondari


Mwanga. Kuuzwa kwa Sekondari ya Mangio wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, kumeibua mtafaruku kwa wakazi wa kijiji hicho baada ya kununuliwa na tajiri mmoja kutokana na kukosa wanafunzi.
Inadaiwa kuwa shule hiyo imeuzwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM baada ya uongozi wake mkoani Kilimanjaro kushindwa kuiendesha na kuifunga mwaka jana.
Akizungumzia kuuzwa kwa shule hiyo, mwenyekiti wa kijiji cha Mangio, Malaki Mmbaga alisema amekuwa akipata vitisho kwa watu wasiojulikana baada ya kukuta barua chini ya ofisi yake iliyodai kwamba hana mamlaka ya kuzuia kuuzwa kwa shule  ya hiyo.
 Mmbaga alionyesha barua hiyo ya vitisho iliyoandikwa Oktoba 19 inasomeka: “Kwako mwenyekiti wa Kijiji cha Mangio, pole kwa kutetea shule isiuzwe kwa anayehitaji, kwa taarifa yako tunakujulisha shule itauzwa kama tunavyotaka wewe ni mtu mdogo sana kwetu, tunakupa onyo la mwisho funga mdomo wako kabla haujafungwa na watu wengine, tunakujua vizuri wewe hutujui, hizi ni salamu kwako ‘Funga Mdomo’.”
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo juzi, Mmbaga alisema haiwezekani shule ya wananchi iuzwe kinyemela bila kuwashirikisha wakazi na uongozi wa kijiji.
“Waliouziwa shule hii hatuwatambui, ni wezi na wavamizi haiwezekani kitu kama hicho tunaiomba Serikali iingilie kati,” alisema.
Naye mwenyekiti mwanzilishi wa kijiji hicho, Mlangeni Kimaso alisema hawatawaonea haya viongozi wa jumuiya ya CCM kwa kuuza maeneo ya wananchi kiholela.
“Wilaya hii tumeona makengeza maana hakuna hata kiongozi wa juu anayezungumzia suala hili, haiwezekani mbunge asijue shule hii imeuzwaje,” alisema Kimaso.
Mfanyabiashara Yusuf Mfinanga maarufu Njuweni alikiri kuinunua shule hiyo, lakini alikataa kutaja kiwango cha fedha na kwamba hakumbuki kwa sababu alikuwa akitoa fedha kidogo kidogo kwa  jumuiya ya wazazi makao makuu.
“Ndio nimenunua shule hiyo lakini nilianza kulipa kidogo kidogo jumuiya ya wazazi makao makuu, baada ya kumaliza kulipa walinikabidhi shule hiyo,” alisema.
Naye katibu wa wazazi mkoa wa Kilimanjaro, Hatibu Mnuwa alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa mpaka apate taarifa za kutosha kwa kuwa linaweza kuibua hisia za watu wengi na akipata muda ataliweka wazi.

Mfanyabiashara ashikiliwa polisi kwa mahojiano


Zanzibar. Mfanyabiashara, Naushad Mohamed Suleiman amekamatwa katika Uwanja wa Ndege Zanzibar alikokuwa asafirishe kilo nane za vito vya  dhahabu.
Pia amekutwa na fedha taslimu za mataifa 15.
Kaimu Kamishna wa Polisi Zanzibar, Juma Yussuf Ali amesema leo Alhamisi Novemba 30,2017 kuwa, mtuhumiwa alikamatwa jana Jumatano Novemba 29,2017 saa tatu usiku akitaka kusafiri na ndege ya Fly Dubai.
Amesema miongoni mwa fedha alizokutwa nazo ni dola 235,000 za Marekani na euro 57,000.
Juma amesema mfanyabiashara huyo alikamatwa baada ya upekuzi kufanyika kwenye mizigo yake.
Amesema ili kusafirisha madini na fedha ni lazima kuwa na vibali kutoka mamlaka husika ndiyo maana wanamshikilia na itakapobainika hakuna utaratibu uliokiukwa ataachiwa.
Juma amesema kazi ya polisi ni kufanya mahojiano na mtuhumiwa.

Mawaziri wa Uganda watua Geita kujifunza uchimbaji madini


Dar es Salaam. Mawaziri wanne wa Serikali ya Uganda wamewasili mkoani Geita kujifunza namna Serikali ya Tanzania ilivyowawezesha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa dhahabu.
Ziara ya mawaziri hao wa wizara za Madini, Uchumi, Mambo ya Ndani na Mambo ya Nje inalenga kukuza sekta ndogo ya uchimbaji madini.
Akizungumza kwa niaba ya mawaziri wengine baada ya kuwasili katika mgodi wa Busolwa, Waziri wa Nchi na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Lokeris Peter amesema wamekuja kujifunza Tanzania kwa kuwa inafanya vizuri katika sekta hiyo.
Ofisa Habari katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magesa Jumapili katika taarifa amemkariri waziri Peter akisema wamekwenda mkoani humo kwa kuwa kuna migodi mingi mikubwa na midogo hivyo wanajifunza namna wanavyochimba, kuuza, kuunganisha wachimbaji katika vikundi na wanavyodhibiti utoroshaji wa madini.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema mawaziri hao wametembelea nchi nyingine za Afrika lakini pia wameona kuna umuhimu wa kufika Tanzania kutokana na maendeleo yaliyofikiwa katika sekta ya madini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Serikali ya Uganda kwa kuona umuhimu wa kujifunza Geita na kutambua jinsi sekta ya madini inavyoweza kuleta mageuzi ya uchumi.

Majibu ya DNA ‘yayeyukia’ mitaani


Hai. Familia ya binti wa kidato cha pili anayedaiwa kubakwa na kupewa ujauzito mwaka jana na mzee wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT)  Kanda ya Usharika wa Nkuu Kiserenyi, wamemuomba mwanasheria mkuu wa Serikali kuingilia kati baada ya majibu ya vinasaba (DNA) kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Mzee huyo aliukana ujauzito huo, hali iliyosababisha hakimu mkazi wilaya ya Hai, Anold Kerekiano anayeisikiliza kesi hiyo kuamuru mtoto afanyiwe vipimo vya DNA ili kujua ukweli.
Hata hivyo, baada ya kufanyiwa vipimo majibu yalichukua mwaka mmoja na yalipotoka hayakuonekana.
Inaelezwa majibu hayo yalitolewa Juni 13, lakini hayakuwafikia wahusika hali ambayo inaitia shaka familia hiyo kuwa huenda yamechukuliwa.
Binti huyo anadai kuwa, baba huyo tangu mtoto azaliwe hajawahi kumpa matunzo mtoto wake.
Alisema anaishi maisha magumu kutokana na familia yake kuwa duni, hivyo anashinda mtoni na mtoto wake kupondaponda mawe ili kupata fedha ya kumnunulia mwanae maziwa.
Naye mama mzazi wa binti huyo, Martha Kweka aliiomba Serkali kuingilia kati suala hilo kutokana na binti yake kuishi kwa shida na ndoto zake zimeharibika.
Martha alisema binti yake ni mtoto wake wa kwanza na alikuwa akimtegemea kwa asilimia kubwa, ili baada ya kumaliza masomo angemsaidia kutokana na maisha duni wanayoishi.
Baba mzazi wa binti huyo, Kulasauko Nyuki alisema anashangaa unyama aliofanya mzee huyo na kuachiliwa wakati  watoto wake wanaendelea kusoma.
“Hii si sawa naomba sheria ifuate mkondo wake mimi nashindwa kuvumilia kuona mtuhumiwa anadunda na kutamba kuwa, hatuwezi kumfanya kitu chochote maana familia yangu ni maskini, naumia sana,” alisema Nyuki.
Hata hivyo, ofisa ustawi wa jamii wa Hai, Helga Njuyui alikiri majibu ya DNA kutumwa Juni  13, lakini inashangaza hayajawafikia.

Wanaume 70,000 kuvuliwa ‘soksi ya asili’


Simiyu. Licha ya Serikali kujiwekea malengo ya kuwafanyia tohara watu milioni tatu ikiwa ni miongoni mwa mapambano ya kupunguza uwezekamo wa kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini, wanaume zaidi ya 70,000 wanatarajiwa kufanyiwa tohara mkoani Simiyu.
Mwaka 2013, Serikali iliweka lengo la kuwafanyia tohara wanaume milioni tatu ifikapo mwaka 2015.
Akizungumzia kampeni hiyo juzi,  mratibu wa tohara Kanda ya Ziwa wa Shirika la Intra Health Tanzania, Paul Mwakipesile alisema watafanya upimaji kabla ya kumfanyia tohara mhusika kwa sababu asilimia 60 ya kufanya tohara hupunguza maambukizi ya Ukimwi.
Mwakipesile alisema wamepanga kuwafikia wanaume 71,495 katika wilaya zote za Simiyu, huku ikitarajiwa Itilima watafikiwa wanaume 26,000.
“Mwaka huu tutafikia malengo yetu kwa asilimia 100 katika vituo vya afya, maeneo yenye uhitaji tunaihusisha jamii.  Tunafanya upimaji, tunatoa kondomu na tunafundisha uzazi wa mpango,’’ alisema.
Naye mratibu wa Ukimwi mkoa wa Simiyu, Dk Hamis Kulemba alisema kwa mwaka 2016 walipanga kufanya tohara kwa wanaume 42,000, lakini waliwafikia  38,000 sawa na asilimia 91.
Akizungumzia kampeni hiyo, mkuu wa mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka aliwataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.

Ujangili wawapeleka tisa jela miaka 180



Serengeti. Washtakiwa tisa waliokuwa wakikabiliwa na kesi nne tofauti za kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh107 milioni, wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.
Hakimu mkazi mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Serengeti, Ismael Ngaile alitoa hukumu baada ya kuwatia hatiani washtakiwa kwa makosa ya kukutwa na meno ya tembo, mafuta ya simba, mikia ya nyumbu, nyama ya ngiri, swalapala na ngozi ya nyati. Washtakiwa wawili waliachiwa.
Waliohukumiwa ni Mniko Masero (28), Silasi Ndarawa (26), Chacha Wambura (39), Jonas Mturi (45), Maseboka Mavuno (47), Nyaibane Nyaronge (29), Hinga Marwa (32), Ikwabe Marwa (36) na Josephat Luharamagara (42).
Awali, wakili wa Serikali Emmanuel Zumba aliieleza Mahakama kuwa Desemba 19, 2016 washtakiwa walikamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

LHRC yakemea vurugu katika uchaguzi

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Novemba 26,2017 kimebaini kuwepo uvunjifu wa haki za binadamu.
Uchaguzi ulifanyika katika kata 43 zilizo kwenye halmashauri 36 za mikoa 19 nchini.
Akizungumza leo Alhamisi Novemba 30,2017 Kaimu Mtendaji Mkuu wa LHRC, Anna Henga amesema uchaguzi ulikuwa na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, watu kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa.
"Vitendo hivi vimeripotiwa kufanywa na vyombo vya dola, watu wasiojulikana na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa vyama vya siasa vikiwemo CCM na Chadema,” amesema.
Amesema kutokana na matukio hayo, vyombo vya dola vinapaswa kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuhusika kwa njia moja au nyingine.
Henga amesema matukio hayo yasipokemewa ni kiashiria kibaya na msingi mbaya utakaoathiri chaguzi zingine ukiwemo wa Serikali za Mitaa wa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Ajali yaua diwani CCM, wawili wajeruhiwa


Songea. Diwani wa viti maalumu (CCM), Mariam Yusuph (53) amefariki dunia katika ajali iliyojeruhi wengine wawili mkoani Ruvuma.
Ajali ilitokea walipokuwa wanakwenda kwenye uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Ruvuma.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Songea, Dk Magafu Majura amesema amepokea majeruhi wawili na mwili wa diwani huyo leo Alhamisi Novemba 30,2017 saa 3:30 asubuhi.
Amesema majeruhi waliowapokea ni Asia Sapwela (52) ambaye ni diwani wa viti maalumu aliyevunjika mkono wa kulia, mbavu na ana michubuko miguuni.
Dk Majura amesema majeruhi mwingine ni Atingala Ally (48), ambaye ni diwani mstaafu wa Tunduru aliyeumia mbavu na mguu wa kulia. Amesema majeruhi wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushi akizungumzia ajali hiyo amesema imetokea katika Kijiji cha Lumecha wilayani Songea ikihusisha gari aina ya Toyota Carina.
Amesema gari hilo lilikuwa likitokea wilayani Tunduru kwenda Songea.
Kamanda Mushi amesema gari hilo likiendeshwa na Osam Ulaya liligonga kingo za barabara kabla ya kupinduka.
Amesema Mariam alifariki dunia papo hapo baada ya kujigonga kichwani.
Dereva Ulaya amepelekwa katika Hospitali ya Peramiho kwa matibabu na polisi wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.

Ocean Road: Upatikanaji dawa za saratani wafikia asilimia 80


Dar es Salaam. Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), imesema upatikanaji dawa, vifaatiba na vitendanishi vya maabara kwa sasa ni asilimia 80 kutoka nne za mwaka 2015.
David Lyimo, anayeuguza ndugu yake katika taasisi hiyo aliliambia gazeti hili jana: “Taarifa ambazo awali tulikuwa tukizisikia kuhusu kero ya dawa hapa kwa sasa hatujazikuta, mgonjwa wangu anapatiwa dawa, ni aina moja tu tunayotakiwa kununua  lakini mionzi na dawa zingine tunapata hapa.”
Akizungumza na  watendaji wa taasisi hiyo na Bohari ya Dawa (MSD), mkurugenzi mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage alisema upatikanaji  dawa, vifaatiba na vitendanishi ilikuwa tatizo katika utendaji na changamoto kwa wagonjwa ambao walilazimika kununua kwa bei ghali.
Dk Mwaiselage alisema bajeti ya taasisi hiyo mwaka 2015 ilikuwa ni Sh790 milioni, sasa ni Sh7 bilioni  huku ikiwa na akiba ya Sh4.3 bilioni za dawa.
Naye mkurugenzi mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema taasisi hiyo inatambua dawa za saratani ni ghali lakini atahakikisha zinaendelea kupatikana kwa wakati ili kuokoa maisha ya Watanzania.
“Ocean Road ni mteja muhimu, hivyo nipo tayari muda wote kuwahudumia leteni orodha ya mahitaji ya dharura hata leo,” alisema.
Katika ziara hiyo, Bwanakunu alitembelea hospitali za Amana, Mwananyamala na Sinza Palestina.

Bunge lazungumzia barua ya waliokuwa wabunge CUF


Dodoma. Ofisi ya Bunge imesema hakuna sehemu katika uamuzi wa Mahakama Kuu dhidi ya wabunge wanane wa viti maalumu CUF waliofukuzwa uanachama na chama hicho inayosema  wanatakiwa kurudishwa bungeni.
Uamuzi wa Mahakama Kuu ulitolewa Novemba 10,2017 katika Kanda ya Dar es Salaam umeizuia CUF kujadili na kuwafukuza uanachama wabunge hao na madiwani wawili wa viti maalumu.
Hata hivyo, Mahakama ilitoa uamuzi huo huku tayari chama hicho kikiwa kimeshawavua uanachama na baadaye kupoteza nafasi zao za ubunge.
Wabunge hao ni Miza Bakari Haji, Saverina Mwijage, Salma Mwasa, Raisa Mussa, Riziki Mngwali, Hadija Salum Al-Qassmy, Saumu Sakala na  Halima Mohamed.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 30,2017, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema shauri lililofunguliwa ni kupinga uamuzi wa CUF kuwafukuza uanachama na kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama bado uamuzi wa mwisho haujatolewa.
"Uamuzi uliotolewa na Mahakama ni wa awali kuhusu pingamizi na uliwalenga walalamikiwa ambao ni baraza la wadhamini wa CUF na uongozi wake ambao uliamuru walalamikiwa wasitishe utekelezaji wa uamuzi wa kuwafukuza uanachama na vilevile, kutojadili suala lolote kuhusu uanachama  wa walalamikaji hao hadi Mahakama itakapokamilisha shauri la msingi," amesema.
Amesema ifahamike vyema kuwa hakuna sehemu yoyote katika uamuzi huo wa Mahakama inapoelekezwa wabunge hao wanatakiwa kurudishiwa ubunge.
Kagaigai amesema kumekuwapo tafsiri isiyo sahihi ya uamuzi huo wa Mahakama inayotolewa na baadhi ya watu na vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya jamii kusambaza taarifa potofu kuwa wabunge hao wamerejeshwa bungeni kwa uamuzi huo wa Mahakama  baada ya kurejeshewa uanachama wa CUF.
Amesema wabunge hao waliiandikia ofisi ya Bunge barua wakiomba kufahamishwa utaratibu utakaotumika kuwarejesha bungeni.
"Tunapenda umma uelewe kwamba, nafasi za ubunge zilizoachwa wazi baada wabunge husika kufukuzwa uanachama zilijazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria na wabunge waliopatikana kujaza nafasi hizo wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya kibunge ipasavyo," amesema.

Duh! Zanzibar Heroes waenda Kenya na basi


ZANZIBAR. KIKOSI cha Zanzibar Heroes, kimeondoka Unguja leo kwenda Kenya kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji yanayotarajia kuanza Desemba 3, wakitumia usafiri wa basi na boti.
Msafara huo wa watu 34, wachezaji 24 na viongozi 10, wamendoka majira ya saa 3:00 asubuhi na boti ya Kilimanjaro kwenda Dar es Salaam.
Wakifika Dar es Salaam, watapanda basi kwenda Kenya, wakipita njia ya Tanga.
Mkuu wa msafara, Khamis Haji: “
Matarajio ya safari yetu, itakuwa yenye matumaini kwani kila mmoja amejiandaa vema kwa ajili ya kuhimili mawimbi ya bahari pamoja na upepo wa njiani tutakapokuwa  ndani ya mabasi.”
“Tumaini la safari yetu hii itakuwa yenye mafanikio makubwa kwa  Zanzibar nzima, kikubwa tunaomba dua zenu tusafiri salama kwenda na kurudi,” alisema Kocha wa timu hiyo Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi hicho ni pamoja na Ahmed Ali ‘Salula’, Nassor Mrisho, Mohammed Abdulrahman ‘Wawesha’, Abdallah Haji ‘Ninja’, Mohd Othman Mmanga, Ibrahimm Mohammed ‘Sangula’ , Adeyum Saleh ‘Machupa’, Haji Mwinyi Ngwali, Issa Haidar ‘Mwalala’, Abdulla Kheir ‘Sebo’, pamoja na Ibrahim Abdallah .
wengine ni Abdul-swamad Kassim, Abdul Aziz Makame, Mudathir Yahya, Mohammed Issa ‘Banka’, Amour Suleiman ‘Pwina’, Hamad Mshamata,
Suleiman Kassim ‘Seleembe’, Kassim Suleiman ,  Feisal Salum ,  Khamis Mussa ‘Rais’, Mwalimu Mohd, Seif Abdallah ‘Karihe’ na Ibrahim Hamad Hilika.
Awali wachezaji hao walikuwa 30 na kulazimika kuachwa 6 ambao wengine waliachwa kwasababu ya majeruhi akiwemo Matteo Anton (Yanga), Ali Badru (Taifa ya Jang'ombe), Salum Songoro (KVZ) na Abubakar Ame "Luiz" (Mlandege) huku wengine walioachwa ni Mbarouk Marshed (Super Falcon) na Omar Juma ‘Zimbwe’ (Chipukizi).
Hata hivyo kwa upande wa viongozi ambao wanaungana na wachezaji hao katika msafara wa kuelekea nchini Kenya kwa ajili ya mashindani ya Chaleng na Hemed Sulaman Morocco Kocha Mkuu, Ali Sulaiman Kocha Msaidizi, Khamis Haji Mkuu wa msafara, Abdul Wahab Dau Meneja wa timu, Mohamed Yussuf Daktar wa timu, Hafidh Muhidini Msaidizi wa shughuli za timu pamoja na Abubakar Khatib Mwandishi wa Habari.

Maonyesho ya viwanda kufanyika Dar


Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa maonyesho ya viwanda Desemba 7 hadi 11,2017 katika viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
Maonyesho hayo yenye kauli mbiu "Tanzania sasa tunajenga viwanda" yatawakutanisha zaidi ya wenye viwanda 500 ambao watapata fursa ya kuonyesha bidhaa zao.
Akizungumzia maonyesho hayo leo Alhamisi Novemba 30,2017; Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema yanalenga kuwaleta pamoja wafanyabiashara ili kubadilishana uzoefu katika kazi.
Mwijage amesema maonyesho hayo pia yatawakutanisha wenye viwanda na taasisi zilizo chini ya wizara kama vile Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani (FCC), Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc) na Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (Tirdo).
"Ninawaalika wenye viwanda; wasomi na watafiti watakuwepo. Ninaomba watumie maonyesho hayo kuandika tafiti kwa kutumia mazingira halisi ya Tanzania na si ya Ulaya," amesema.
Mwijage amesema wizara inaweka mkazo katika kujenga uchumi wa viwanda ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Ili kufikia azma hiyo, amesema wizara  inahamasisha ujenzi wa viwanda.

TAKWIMU NA UCHUMI: Uvumilivu unahitajika kukuza, kuimarisha miundombinu ya uchumi

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.
Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880. 
Miundombinu ya uchumi husaidia kufanikisha malengo ya taifa ililojiwekea kwa muda mfupi na mrefu. Serikali hutumia mapato na rasilimali nyingine kutoka ndani na nje ya kuwekeza kwenye miundombinu itakayosaidia kukuza na kuendeleza uchumi kwa kipindi kirefu kijacho.
Miundombinu ya uchumi inajumuisha miradi ya usafirishaji na uchukuzi kama vile ujenzi wa reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege, ununuzi wa meli, na ndege. Uwekezaji katika sekta ya umeme, afya, maji na elimu pia ni miundombinu miundombinu muhimu kutokana na mchango wake kwenye uchumi wa taifa.
Kuimarisha miundombinu ya uchumi ni pamoja na kuzuia baadhi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ili kuimarisha na kuendeleza soko la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani pamoja kukuza sekta nyingine zinazohusiana na viwanda.
Soko la viwanda vya ndani likilindwa, litavijengea uwezo wa kuimarisha ubora na kuweza kushindana kwenye soko la kimataifa ambako kuna bidhaa za mataifa kutoka mataifa mbalimbali.
Nchi yeyote inayohitaji kukuza, kuimarisha na kuendeleza miundombinu ya uchumi ni lazima ielekeze fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kurahisisha uanzishaji na uendeshaji wa biashara za aina tofauti kuliko matumizi ya kawaida.
Kubana matumizi na kuhakikisha kila senti inayopatikana ama kwa njia ya misaada, mikopo au makusanyo ya ndani inaelekezwa kwenye shughuli iliyopangwa kwa kuzingatia thamani ya fedha ni jambo linalopaswa kuzingatiwa.
Tanzania sasa hivi imejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya uchumi, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imejikita katika uendelezaji na uimarishaji wa miundombinu ya uchumi kwa kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha ‘standard gauge’.
Mradi huu unatajwa kugharimu kiasi cha Sh16 trilioni mpaka utakapokamilika. Mradi mwingine ambao ni sehemu ya miundombinu ya uchumi ni ununuzi wa ndege ambazo zitaongeza idadi ya watalii pamoja na fedha zitakazokusanywa kutoka eneo hilo.
Tayari ndege mbili zimeshanunuliwa na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nyingine nne zinatajwa kugharimu Sh227.6 bilioni yameshafanyika.
Licha ya kuongeza idadi ya watalii watakaotembelea nchini kutokana na kurahisishwa kwa usafiri huo wa anga, ndege hizo ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi marafiki wa kiuchumi.
Zikiwapo za kutosha zitakazokuwa zinaenda kwenye mataifa yamayofanya biashara zaidi na Tanzania, yatawapunguzia wajasiriamali gharama za kuunganisha ndege huku zikitoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani kuzitumia jambo litakaloongeza mchango wa sekta ya usafirishaji kwenye pato la Taifa.
Serikali pia inaendelea kupanua, kuboresha na kujenga viwanja vipya vya ndege sehemu mbalimbali nchini jambo litakalotoa nafasi kwa usafiri huo kuwahudumia wasafiri wanaofanya safari za ndani hata kimataifa.
Serikali pia inaendelea na mchakato wa kujenga bawawa la umeme  la Stigler’s Gorge wakati usambazaji wa nishati hiyo vijijini ukiendelea. Dhamira iliyopo ni kuhakikisha kila kijiji kinapata huduma hiyo ili kuwa chachu ya maendeleo vijijini. Kiasi cha Sh389.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) kwa kipindi Julai, 2016 mpaka Machi.
Barabara kadhaa zimeendelea kujengwa nchini kwa kiwango cha lami huku baadhi zikijengwa kwa changarawe kuhakikisha huduma ya usafiri na usafirishaji inakuzwa na kuimarishwa.
Ili kuendeleza usimamizi wa barabara na miundombinu yake na kuongeza mchango wake kwenye uchumi, Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura).
Usafirishaji wa bidhaa hasa kutoka na kwenda vijijini ambako bidhaa nyingi huzalishwa ni changamoto iliyokuwapo kwa muda mrefu. Kadri inavyoshughulikiwa ndivyo maisha ya wananchi husika yanavyoendelea kuimarika.
Serikali inadhibiti upotevu wa mapato katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengineyo ikiwemo Tanga na Mtwara. Pamoja na mambo mengine, inahakikisha bandari zinatumika kama lango kuu la kukuza uchumi.
Sekta ya elimu haijasahaulika, Serikali imeendelea kutoa elimu bure kwa Watanzania wanyonge na masikini kuanzia awali hadi sekondari mpango unaoigharimu wastani wa  Sh18.77 bilioni kwa mwezi ambazo nisawa na Sh225.24 bilioni kwa mwaka.
Miradi mingi ya maendeleo inasimamiwa na kuendelezwa na Serikali. Kukuza, kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya uchumi ni sawa na kulima au kutafuta mali juani, tukitarajia kuvuna kisha kulia kivulini wakati ukifika.
Utekelezaji wa miradi hii huchukua muda mrefu mpaka kukamilika kwake. Baadaye huanza kufanyakazi na taratibu wananchi huanza kuona faida zake.
Baadhi huchukua muda mwingi kabla matunda yake hayajaonekana kwa wananchi. Tuendelee kuvumilia kwani mambo mazuri yanakuja.