Saturday, November 4

MAKAMU WA RAIS AONGOZA MATEMBEZI YA HISANI KWA AJILI YA KUSOMESHA WAUGUZI


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Ssuluhu Hassan akizungumza jambo na Waziri wa Afya Mh.Ummy Mwalimu, huku wakitembea mapema leo wakati akiongoza a matembezi ya hisani kwa ajili ya kusomesha Wauguzi Wakunga , matembezi hayo ya kilometa 4.5 yalianzia kwenye viwanja  vya Green Grounds, Oysterbay jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).




Picha ya pamoja na Washiriki wa Matembezi hayo ya Hisani
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania  Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki katika Matembezi ya Hisani ya Kilomita Nne na Nusu yenye lengo la kukusanya fedha zitakazosaidia kugharamia mafunzo ya uuguzi na ukunga.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Green Ground- Oysterbay mara baada ya matembezi hayo, Makamu wa Rais alisema takwimu za vifo vya kina mama zimeongezeka, hivyo wazo la kusaida kuongeza idadi ya wakunga ambao watasaidia kupunguza vifo hivyo ni zuri sana.

Makamu wa Rais alisema “nimefarijika kusikia kuwa mwaka 2016 matembezi haya ya hisani yalikusanya wastani wa shilingi milioni 290 pesa ambayo iliwekwa katika fungu la kusomesha wauguzi wakunga wapya 75 katika mafunzo ya ngazi ya cheti” . Makamu wa Rais alionesha kufurahishwa na malengo yaliyowekwa kwa miaka miwili ijayo ya kukusanya kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kusomesha wakunga wauguzi 400 katika ngazi ya cheti na diploma kwas njia ya masafa.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa moja ya chanzo cha vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua ni ukosefu wa wataalam wa kuwahudumia. Takwimu za Tanzania zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya akina mama hawaendi kujifungua katika vituo vyetu vya kutolea huduma kutokana na kukosekana kwa wataalam wa kuwahudumia akina mama hao.

Makamu wa Rais aliwahakikishia wadau wote wa sekta ya afya kwamba serikali ipo nao bega kwa bega katika kuhakikisha wanaotaka kuwekeza katika sekta hii wanafanikisha malengo yao. Aidha, alisema serikali inaendeleza juhudi za kuinua uchumi kwa kuongeza idadi ya viwanda ikiwa ni pamoja na viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili kuongeza upatikanaji na uboreshaji wa huduma muhimu za afya kwa binadamu.

Makamu wa Rais aliiagiza Wizara ya afya iusimamie kikamilifu mwongozo unaotaka kila kifo cha mama na mtoto kinachotokana na matatizo ya uzazi kijadiliwe ndani ya saa 24 katika kituo au hospitali husika kwa lengo la kubaini chimbuko la kifo hicho na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi huduma zinazotolewa katika kituo husika. 
Mwisho,Makamu wa Rais aliwashukuru wadau ,wahisani na wananchi waliojitokeza kwa wingi kwenye matembezi hayo na kuwaomba kuendelea kushiriki na kuchangia fedha kwa ajili ya kusomesha wakunga wauguzi.

DK. HAMISI KIGWANGALLA AMEAGIZA RASIMU YA SERA MPYA YA MISITU IKAMILIKE NDANI YA MWEZI HUU WA NOVEMBA

Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwasili katika ukumbi wa Hoteli ya Morena mjini Dodoma jana kwa ajili ya kufungua warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo.

Na Hamza Temba - WMU
............................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameagiza kukamilishwa haraka kwa rasimu mpya ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 2016 ili kuwezesha upatikanaji wa Sera, Sheria na Kanuni mpya za usimamizi wa rasilimali za misitu nchini kwa ufanisi zaidi.

Ameagiza wataalamu wa Wizara hiyo kukamilisha rasimu hiyo mwezi huu wa Novemba na iwasilishwe kwake mapema mwezi ujao (Desemba) ili aweze kupata ushauri zaidi wa wataalamu wengine huru kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri na baadaye kutungiwa Sheria na Kanuni za utekelezaji.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana mjini Dodoma wakati akifungua warsha ya siku moja ya wadau wa misitu iliyolenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo.

“Natoa agizo mchakato huu ukamilike ndani ya mwezi huu wa 11, tarehe moja mwezi wa 12 mlete rasimu ambayo nyie wataalamu mmeridhika nayo, muiwasilishe kwangu mimi na Mhe. Naibu Waziri, na siku hiyo mtakayoiwasilisha kwetu mniletee timu ya wataalamu watakaonishauri kwenye maeneo mbalimbali.

“Pamoja na hao wataalamu washauri nataka watu wengine huru wahusike kwenye kunishauri, ili nipate picha ya watu wengine huru kabla hatujatengeneza andiko ambalo tutalipeleka kwenye kikao cha baraza la Mawaziri, waje wanishauri maeneo yanayotaji maboresho, kuongeza ubunifufu au kukazia zaidi”. Aliagiza Dk. Kigwangalla.

Alisema amelazimika kuharakisha zoezi hilo ili Sera hiyo ikamilike haraka iweze kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo ongezeko la watu linalosababisha misitu mingi kuteketezwa kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kupitia shughuli za kilimo na uanzishwaji wa makazi mapya.

Alisema pamoja na misitu kuonekana inachangia kidogo kwa asilimia 3.5 kwenye pato la taifa, bado mchango wake ni mkubwa kuliko inavyochukuliwa hivi sasa. Alisema tafiti zilizofanywa awali hazikuzingatia mambo muhimu ikiwemo mchango halisi wa misitu kwenye upatikanaji wa maji ambayo huzalisha umeme, hunywesha mifugo na wanyamapori, matumizi ya majumbani na kilimo cha umwagiliaji.

Alisema ili kupata mchango halisi wa misitu kwenye uchumi mpana wa taifa letu, Wizara yake imeshaandaa andiko maalum kwa ajili ya kuendesha utafiti mkubwa wa kubaini mchango huo na kazi inayofanyika hivi sasa ni ya utafutaji wa fedha kutoka kwa wadau mbalimbali kufanikisha utafiti huo.

Akizungumzia Uhifadhi Shirikishi Jamii, Dk. Kigwangalla alisema kwa zaidi ya asilimia 32 ya maeneo yote nchini yamehifadhiwa kisheria, hivyo njia rahisi ya kuyalinda ni kupitia ushirikishwaji wa wananchi. “Bila kufanya hivyo hatuwezi kusema tuna askari wa kutosha kulinda misitu yote, mbuga zote za wanyama au mapori yote tengefu nchini.

“Lakini nje ya maeneo hayo kuna maeneo ya vijiji ambayo pia yamehifadhiwa, yote haya huwezi kusema utayalinda kirahisi sana bila ushiriki wa wananchi, kuwaleta wananchi kwenye uelewa wa pamoja, kwamba tunahifadhi kwa faida yao.

“Tuwaelimishe, kwa mfano usipohifadhi misitu kiwango cha mvua kitashuka, usalama wa chakula utaathirika, upatikanaji wa maji safi na salama utaathirika, upatikanaji wa umeme nao pia utaathirika, hivyo tunahifadhi kwa faida ya jamii kwa ujumla”. alisema Dk. Kigwangalla.

Awali akiwasilisha mada kuhusu hali ya sekta ya misitu nchini, Prof. Romanus Ishengoma wa Chuo Kikuu cha Sokoine - SUA alisema changamoto kubwa inayoikabili sekta hiyo ni ukataji holela wa miti ambapo takwimu za NAFORMA zinaonyesha kuwa Tanzania inapoteza hekta 372,000 za misitu kwa mwaka.

Alisema changamoto nyingine ni uchomaji moto misitu, uvunaji wa mkaa, uingizaji mifugo kwenye maeneo ya hifadhi, kukosekana kwa mpango bora wa matumizi ya ardhi, utegemezi uliokithiri kwenye mazao ya misitu, uanzishwaji wa makazi mapya na utegemezi wa nishati ya kuni. Alisema changamoto hizo zinahitaji Sera madhubuti za kukabiliana nazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Dk. Ezekiel Mwakalukwa alisema, Rasimu hiyo ya Sera mpya ya Misitu itakamilika kwa wakati kama alivyoelekeza Waziri Kigwangalla na kwamba maoni yote ya wadau yatazingatiwa katika Rasimu hiyo.


Warsha hiyo ya siku moja iliyofanyika mjini Dodoma iliandaliwa kwa ushirikiano wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Shirika la Uendelezaji wa Nishati Endelevu za Kisasa Tanzania (TATEDO), Kundi la Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TFCG), Wizara ya Maliasili na Utalii na Ubalozi wa Switzerland nchini. 
Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza wakati wa ufunguzi wa  warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu iliyofanyika mjini Dodoma jana. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo.
Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akiteta jambo na Balozi wa Switzerland hapa nchini, Florence Matli muda mfupi baada ya kufungua warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu iliyofanyika mjini Dodoma jana. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo. 
Baadhi ya wajumbe walioshiriki warsha hiyo wakiwemo baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mauzo wa Kampuni ya Charcoal Briquettes ltd, Abdala Seushi kuhusu nishati mbadala ya mkaa mkombozi wa afya na mazingira muda mfupi baada ya kufungua warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu iliyofanyika mjini Dodoma jana. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo.
Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mauzo wa Kampuni ya Charcoal Briquettes ltd, Abdala Seushi kuhusu majiko banifu ya mkaa muda mfupi baada ya kufungua warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu iliyofanyika mjini Dodoma jana. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Dk. Ezekiel Mwakalukwa akizungumza katika warsha hiyo.
Balozi wa Switzerland hapa nchini, Florence Matli akizungumza katika warsha hiyo.
Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kushoto) akipokea zawadi ya nishati mbadala ya mkaa mkombozi wa afya na mazingira kutoka kwa Afisa Mauzo wa Kampuni ya Charcoal Briquettes ltd, Abdala Seushi (wa tatu kushoto) muda mfupi baada ya kufungua warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu iliyofanyika mjini Dodoma jana. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Dk. Ezekiel Mwakalukwa. 
Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza na Balozi wa Switzerland hapa nchini, Florence Matli muda mfupi baada ya kufungua warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu iliyofanyika mjini Dodoma jana. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo. 
 Prof. Romanus Ishengoma wa Chuo Kikuu cha Sokoine - SUA akiwasilisha mada kuhusu hali ya sekta ya misitu nchini katika warsha hiyo.
Picha ya pamoja.
Meza kuu, Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Uhifadhi wa Misitu Tanzania, Charles Meshak (wa pili kushoto), Balozi wa Switzerland hapa nchini, Florence Matli (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Doto Biteko (kulia).
Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandhishi wa habari muda mfupi baada ya ufunguzi wa warsha ya siku moja ya wadau sekta misitu iliyofanyika mjini Dodoma jana. Warsha hiyo ililenga kujadili maboresho ya Rasimu ya Sera mpya ya Misitu na Nyuki, pamoja na changamoto na mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo. 

BOT YAWAJENGEA UWEZO WA KUTAMBUA NOTI BANDIA WATU WENYE ULEMAVU WA KUTOSIKIA WILAYANI CHATO

Bw,Patrick Fata ambaye ni Mhelimishaji kutoka BOT akielekeza na kutoa elimu namna ambavyo unaweza kutambua Noti bandia. 
Meza kuu ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Chato Shaaban Ntarembe. 
Maafisa wa BOT wakifuatilia maelezo ya Meneja Msaidizi wa Idara ya Uhusiano wa BOT, Vicky Msina wakati alipokuwa akielezea juu ya elimu ambayo wanaitoa kwa viziwi. 
Meneja Msaidizi wa Idara ya Uhusiano wa BOT, Vicky Msina akielezea malengo ya kutoa elimu ya kuwawezesha viziwi kutambua alama za usalama zilizopo kwenye noti ili kuzitofautisha na noti bandia pindi wanapokuwa katika shughuli zao za utafutaji. 
Mwenyekiti wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (Kisuvita), Habibu Mrope akizungumza changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo watu ambao ni walemavu hususani wakati wanapokuwa wanakwenda kwenye huduma za kibenki. 
Bw,Patrick Fata ambaye ni Mhelimishaji kutoka BOT,akisisitiza swala la alama za fedha ambazo zinakuwepo kwenye noti. 
Kifaa ambacho kinatumika kuangalizia noti bandia na ile ambayo ni ya harari. 
Noti ambazo zinakuwa zimeharibiwa zikiwa kwenye mafungu fungu lenye rangi nyekundi ni elfu kumi na yenye rangi ya blue ni elfu tano. 


NA JOEL MADUKA,CHATO.

Benki kuu ya Tanzania (BOT)imekutana na kundi la watu wenye ulemavu wa kutokusikia na wale ambao hawaoni Wilayani Chato lengo likiwa ni kuwapatia na elimu ya utambuzi wa Noti bandia Wilayani humo.

Akizungumza kwenye semina ambayo imefanyika kwenye ukumbi wa KKKT Wilayani Humo,Meneja msaidizi wa idara ya uhusiano wa BOT, Vicky Msina alisema elimu wanayoitoa imelenga kuwawezesha viziwi kutambua alama za usalama zilizopo katika noti ili kuzitofautisha na noti bandia wanapokuwa katika shughuli zao kwani mtu yeyote akikutwa na noti bandia ni kosa la jinai, hivyo wanawapa mafunzo ili wasikumbwe na kadhia hiyo.

“Ni muda sasa walituomba kuwapa mafunzo na hii ni kutokana na wengi wao kutokujua noti bandia wamekuwa wakijikuta wanabambikiwa na pia wanapo kwenda benki kupeleka fedha zao wahudumu huwadharau na wakati mwingine kwa wale wanao kwenda kuchukua fedha hupatiwa noti chafu jambo ambalo lilitusukuma kuwaelimisha juu ya hatua za kufuata ilikupatiwa haki zao za msingi kwenye huduma hizo,”alisema Msima.

Mwenyekiti wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (Kisuvita), Habibu Mrope alisema kuna tatizo kubwa la kutotambua noti bandia kwa Walemavu hali ambayo imechangia kuwarudisha nyuma kwani wanapokutwa na noti hizo huchukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo kutokana na tatizo hilo Mkuu wa wilaya ya Chato Shaaban Ntarambe aliwaahidi watu ambao wanamatatizo ya kutokusikia kufunguliwa kwa shule ambayo itawasaidia kujifunza lugha za alama kwania ya kuboresha mawasiliano kwenye jamii.

“Idadi ya wilaya yetu kuna Viziwi 347 ambapo ni sawa na asilimia 90 ya watu wenye ulemavu wa kusikia hawajui lugha za nyakati upekee idadi hii ni kubwa sana ni lazima Serikali ifanye jitihada za kuwa kwamua watu hawa ambapo kwa kushirikisha wadau mbali mbali, nitahakikisha ujenzi wa shule hiyo unaanza mara moja,”alisisitiza Tarambe

Kwa upande wake mmoja wa washirki wa semina hiyo, Issa Pastori, mkazi wa Buziku wilayani humo alishukuru kupatiwa mafunzo hayo na kwa upande wa suala la uanzishwaji wa shule maalum ya lugha za alama ameomba mchakato huo uanze haraka kwani ni mkombozi kwao.

DC SHINYANGA AKUTANA NA WAKULIMA WA PAMBA SHINYANGA VIJIJINI KUHAMASISHA KILIMO CHA KISASA

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro leo Ijumaa Novemba 3,2017 amewatembelea wakulima wa zao la pamba katika kijiji cha Sayu kata ya Pandagichiza halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kuwahamasisha kulima zao hilo kwa njia za kitaalamu/kisasa ili kilimo hicho kiwe na tija kwa ajili ya kujikomboa kiuchumi.

Akizungumza katika kikao na wananchi wa kijiji hicho ambacho ni maarufu kwa kilimo cha pamba,Matiro aliyekuwa ameambatana na wataalamu wa zao la pamba,aliwataka wakulima wa zao hilo wilayani humo kulima kisasa kwa kufuata kanuni 10 za kilimo ikiwemo kulima kwa kutumia kamba.

Alisema wananchi katika wilaya hiyo wamekuwa mstari wa mbele katika kulima zao la pamba lakini wamekuwa hawapati faida kutokana na kulima njia zisizo za kitaalamu.

“Tunataka kufanya kilimo biashara ili kiwe na tija,hatupati mazao ya kutosha kutokana na kutolima kitaalamu,naomba mwaka huu tuwasikilize wataalamu wetu wanatuambia nini,nataka tubadilishe maisha yetu kupitia pamba”,alisema Matiro.

Aliwashauri wananchi ambao hawana uwezo wa kunua mbegu za pamba wajiorodheshe majina yao,ijulikane wapo wangapi na wanahitaji mbegu kiasi gani ili serikali ya wilaya hiyo ione namna ya kuwasaidia ili waweze kulima kisasa.

“Tutaongea na wadau wa pamba ili tujue tunafanya nini,sasa hivi tunaingia katika msimu wa pamba,hatutaki pamba yetu kufanyiwa mambo yaliyokuwa yanafanyika huko nyuma,tunataka tuwe na chama cha ushirika ili hata tukiamua kuwapa mbegu wale walioshindwa waweze kupata kupitia chama chao cha ushirika”,alieleza Matiro.

“Kijiji hiki kinasifika kwa kilimo cha pamba na mazao mengine kama choroko na dengu,naomba mujitahidi kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo lakini msisahau kulima mazao ya chakula na muepuke kuuza chakula chote”,alieleza.

“Serikali haina shamba,jitahidini mnapolima mazao ya biashara limeni pia mazao ya chakula na mhakikishe mazao yale mnahifadhi kwa ajili ya chakula cha baadae”,aliongeza.

Aidha aliwahamasisha wananchi hao kupanda miti ili kukabiliana na tishio la jangwa mkoani Shinyanga ambapo kupitia kampeni ya Shinyanga Mpya,Mti Kwanza kila kaya inatakiwa kupanda miti kuanzia mitatu.

Katika hatua nyingine aliwataka wataalamu wa kilimo kukaa na wakulima na kuwashauri njia nzuri za kufuata katika kilimo.Mmoja wa wakulima katika kijiji hicho,Samwel Nkilijiwa alieleza kuwa tatizo kubwa wanalokabiliana nalo kuwa ni pembejeo ambao dawa za maji zinazotumika kuua wadudu hazijafanyi kazi kama ilivyokuwa kwa dawa za mafuta ambazo sasa hazitumiki.

“Hii dawa ya maji wanayotupa haiui wadudu wanaoshambulia pamba yetu,kwanza inawasha sana huwezi hata kumsogelea mke wako,tunaomba ile dawa ya mafuta tuliyokuwa tunaitumia zamani,hii haifai”,aliongeza Nkilijiwa.

Hata hivyo Mkaguzi wa pamba wilaya ya Shinyanga,Benjamini Madama alisema tatizo la wakulima kulalamikia dawa ya maji inatokana na kipindi cha nyuma wafanyabiashara wa dawa hiyo walikuwa wanachakachua dawa hiyo na kuonekana feki na sasa serikali imechukua hatua hivyo hakuna dawa feki kinachotakiwa wakulima wafutae ushauri wa wataalamu wa pamba.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sayu kata ya Pandagichiza leo akiwahamasisha kufuata njia za kisasa kulima zao la pamba-Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa Sayu
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akisisitiza wananchi kulima mazao ya biashara pamoja na yale ya chakula
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga
Mkulima wa Pamba Nicholaus Selena akieleza kero yake kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Mkulima wa Pamba Samwel Nkilijiwa akieleza changamoto wanayopata pale wanapotumia dawa ya maji ya kuua wadudu ambapo alisema dawa hiyo haiui wadudu hivyo kuomba dawa ya mafuta waliyokuwa wanatumia zamani 
Afisa Kilimo wa wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu akitoa ufafanuzi kuhusu kilimo cha pamba
Diwani wa kata ya Pandagichiza Charles Masele Kabogo akizungumza katika kikao hicho
Afisa tawala wa wilaya ya Shinyanga Charles Maugira akizungumza katika kikao hicho
Mkulima wa pamba katika kijiji cha Sayu Ezekiel Nchange akishikana mkono na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro baada ya kumpatia shamba mkuu huyo wa wilaya ili alime zao la pamba katika kijiji hicho
Mkaguzi wa pamba wilaya ya Shinyanga,Benjamini Madama akitoa elimu kwa wakulima wa pamba juu ya njia ya kisasa ya kulima zao hilo
Mkaguzi wa pamba wilaya ya Shinyanga,Benjamini Madama akionesha kamba zinazotakiwa kutumika katika kilimo cha pamba
Kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Sayu Paul Selena akizungumza katika kikao hicho
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipokelewa katika shule ya msingi Sayu kwa ajili ya kupanda mti
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akipanda mti wa kumbukumbu katika shule ya msingi Sayu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya Shinyanga Mpya Mti Kwanza ambapo wananchi wamekuwa wakihamasishwa kupanda miti ili kukabiliana na hali ya jangwa mkoani Shinyanga
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiendelea na zoezi la kupanda mti katika shule ya msingi Sayu
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Sayu ambapo aliwasisitiza kuwa mabalozi wa upandaji miti katika jamii
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na baadhi ya viongozi na wananchi wa kijiji cha Bulambila kata ya Mwalukwa ambapo pia ni maarufu kwa kilimo cha zao la pamba ambapo pia aliwahamasisha kulima zao hilo kwa njia za kisasa ili lilete tija
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiteta jambo na Diwani wa kata ya Mwalukwa,Ngassa Mboje ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog