Saturday, November 4

MAKAMU WA RAIS AONGOZA MATEMBEZI YA HISANI KWA AJILI YA KUSOMESHA WAUGUZI


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Ssuluhu Hassan akizungumza jambo na Waziri wa Afya Mh.Ummy Mwalimu, huku wakitembea mapema leo wakati akiongoza a matembezi ya hisani kwa ajili ya kusomesha Wauguzi Wakunga , matembezi hayo ya kilometa 4.5 yalianzia kwenye viwanja  vya Green Grounds, Oysterbay jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).




Picha ya pamoja na Washiriki wa Matembezi hayo ya Hisani
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania  Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki katika Matembezi ya Hisani ya Kilomita Nne na Nusu yenye lengo la kukusanya fedha zitakazosaidia kugharamia mafunzo ya uuguzi na ukunga.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Green Ground- Oysterbay mara baada ya matembezi hayo, Makamu wa Rais alisema takwimu za vifo vya kina mama zimeongezeka, hivyo wazo la kusaida kuongeza idadi ya wakunga ambao watasaidia kupunguza vifo hivyo ni zuri sana.

Makamu wa Rais alisema “nimefarijika kusikia kuwa mwaka 2016 matembezi haya ya hisani yalikusanya wastani wa shilingi milioni 290 pesa ambayo iliwekwa katika fungu la kusomesha wauguzi wakunga wapya 75 katika mafunzo ya ngazi ya cheti” . Makamu wa Rais alionesha kufurahishwa na malengo yaliyowekwa kwa miaka miwili ijayo ya kukusanya kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kusomesha wakunga wauguzi 400 katika ngazi ya cheti na diploma kwas njia ya masafa.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa moja ya chanzo cha vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua ni ukosefu wa wataalam wa kuwahudumia. Takwimu za Tanzania zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya akina mama hawaendi kujifungua katika vituo vyetu vya kutolea huduma kutokana na kukosekana kwa wataalam wa kuwahudumia akina mama hao.

Makamu wa Rais aliwahakikishia wadau wote wa sekta ya afya kwamba serikali ipo nao bega kwa bega katika kuhakikisha wanaotaka kuwekeza katika sekta hii wanafanikisha malengo yao. Aidha, alisema serikali inaendeleza juhudi za kuinua uchumi kwa kuongeza idadi ya viwanda ikiwa ni pamoja na viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili kuongeza upatikanaji na uboreshaji wa huduma muhimu za afya kwa binadamu.

Makamu wa Rais aliiagiza Wizara ya afya iusimamie kikamilifu mwongozo unaotaka kila kifo cha mama na mtoto kinachotokana na matatizo ya uzazi kijadiliwe ndani ya saa 24 katika kituo au hospitali husika kwa lengo la kubaini chimbuko la kifo hicho na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi huduma zinazotolewa katika kituo husika. 
Mwisho,Makamu wa Rais aliwashukuru wadau ,wahisani na wananchi waliojitokeza kwa wingi kwenye matembezi hayo na kuwaomba kuendelea kushiriki na kuchangia fedha kwa ajili ya kusomesha wakunga wauguzi.

No comments:

Post a Comment