Saturday, September 23

Asilimia 75 ya kadi za mwendokasi hazitumiki


Mtendaji Mkuu wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Lwakatare amesema kati ya kadi 200,000 zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumika katika Mfumo wa Mabasi Yaendayo haraka ni kadi 50,000 hadi 60,000 ndizo zinazoonekana kutumiwa na wananchi katika mfumo huo.

Amesema kadi ambazo zinatumika kwa sasa ni sawa na asilimia 25 tu huku asilimia 75 zikiwa  ziko mifukoni mwa wateja ambao wamechukua kadi mara mbili.

Mhandisi Lwakatare amesema  kwamba kutotumika kwa kadi  hizo nyingi kumechangia kuwepo kwamisururu ya abiria kwenye vituo vya mabasi yaliyopo kwenye mfumo huo.
“Kusudi ni kwamba kadi moja kwa mtu mmoja, lakini inaonekana mtu mmoja anamiliki kadi zaidi ya moja, jambo ambalo si sahihi,” ameeleza.
Amefafanua kwamba wakati utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo Serikali ilinunua kadi 200,000 kutokana na makadirio iliyoyafanya kabla ya kuanza kutoa huduma.
Amesema  kadi hizo zilipaswa kutumiwa na wananchi wanapohitaji kusafiri lakini imebainika kwamba nyingi ya kadi hizo hazitumiki.
“Takwimu zinaonyesha kati ya kadi 200,000 zilizonunuliwa ni asilimia 25 hadi 30 zinazotumika, hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa kadi katika mfumo,” amesema.
Kufuatia hali hiyo Mtendaji Mkuu amewataka Wananchi wanaozimiliki kadi hizo wazitumie ili kurahisisha usafiri kwani ndizo zilizokusudiwa kutumika katika mradi.

Mhandisi Lwakatare aliongeza kuwa kulingana na takwimu zilizopo  wananchi 200,000 hadi 250,000 ndiyo  wanaotumia huduma hiyo kila siku ni dhahiri kuwa endapo kadi hizo zingekuwa zinatumika kusingekuwa na msururu wa abiria kupanga foleni ya kukata tiketi.
Kuhusu suala la kuongeza kadi nyingine katika mfumo huo ili ziendane na mahitaji ya sasa ya ongezeko la watumiaji wa huduma hiyo, Mhandisi Lwakatare alisema kuwa Serikali inalipa kipaumbele suala hilo ambapo kufikia sasa utaratibu wa kumpata mtoa huduma wa kukusanya nauli unaendelea vizuri.
Amesema kuwa mtoa huduma huyo atakapopatikana ndiye atakuwa na jukumu la kuongeza kadi, kuzisimamia na kukusanya nauli.
Hata hivyo , Mhandisi huyo alisema kwamba kuna wananchi wengi ambao wanaishi  nje ya mkoa wa Dar es Salaam ambao hawatumii usafiri huu na wamechukua kadi hizo.

“Nawashauri nyie ambao hamtumii kadi hizi mrudishe ofisi za Udart au muwape hata ndugu zenu wazitumie kwani haziharibiki  zaidi ya kuoengezewa pesa tu’’alisema

NMB yaipa ‘mkwanja’ Alat


Benki ya NMB imetoa hundi ya Sh100 milioni kuwezesha mkutano mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Alat), utakaofanyika Oktoba 2 hadi 6 jijini Mbeya.
Richard Makungwa, ofisa mkuu wa idara ya wateja wakubwa na Serikali wa NMB   amesema wametoa fedha hizo kuunga mkono jitihada za Alat na kuiwezesha iwajibike ipasavyo kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
"Halmashauri zipo karibu na wananchi ambao sisi tunawahudumia, kwa hiyo mchango wetu unalenga kuona malengo waliyopanga yanafikiwa," amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Alat, Steven Mhapa amesema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utahimiza halmashauri zote kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.
"Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli, mkutano huu utawahusisha pia wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya, majiji na manispaa nchini," amesema.
Amesema katika mkutano huo watatumia siku moja kuzungumzia mamlaka mpya iliyoundwa kwa ajili ya masuala ya barabara za miji na vijiji kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa uchumi.

Sailo teknolojia bora ya kuhifadhi nafaka

Huu ndio mwonekano wa maghala ya kisasa

Huu ndio mwonekano wa maghala ya kisasa yaitwayo sailo yanayoweza kutumika kuhifadhia mazao ya nafaka na yale ya jamii ya mikunde. Picha na mtandao 
Hawalimi, hawana uwezo wa kulima wala kuvuna lakini wana afya njema.
Wakati wote wamenawiri kuliko hata wakulima hutumia nguvu kubwa kulima kwa ajili yao wanawiri.
Hawa ni wadudu waharibifu wa mazao ambao ni adui mkubwa wa wakulima. Hujineemesha kwa kushambulia mazao tangu shambani mpaka nafaka zinapohifadhiwa ghalani.
Wadudu hao ni pamoja na dumuzi na kiwavi chake wanaoathiri mazao kama mahindi.
Ni wazi kwamba wadudu hao na wengine wamekuwa wakisababisha mateso kwa wakulima wengi, licha ya juhudi za kuwadhibiti ambazo zimekuwa zinafanywa.
Pamoja na kuwepo viuatilifu ambavyo hutumika katika kuwadhibiti wadudu wasishambulie mazao shambani, bado wengine hufanikiwa kushambulia baada ya kuvunwa.
Sailo kama mkombozi kwa wakulima
Wadudu wharibifu wakiwa kero kwa wakulima kwa kuwapa hasara, wataalamu hawapo nyuma kuwasaidia wakulima. Wamekuwa wakijitahidi kubuni mbinu mbalimbali za kuwadhibiti wadudu hao.
Miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na vifaa vya kiteknolojia vya kuhifadhi mazao baada ya kuvunwa ikiwamo ghala la kisasa liitwalo Sailo.
Kwa mujibu wa kitabu cha Teknolojia za Utayarishaji, Usindikaji na Hifadhi ya Mazao ya Nafaka baada ya Kuvuna kilichoandikwa na wataalam wa Wizara ya Kilimo mwaka 2013, kuna umuhimu mkubwa wa kuhifadhi nafaka kwenye ghala bora kama sailo.
Wataalamu wanasema sailo ni maghala yanayojengwa kwa dhana ya kutokuwepo na mzunguko wa kawaida wa hewa ndani yake.
Hatua hiyo husaidia wadudu waharibifu na vimelea vya magonjwa kutoweza kustawi na kuharibu nafaka kwa sababu wanakosa hewa.
Wataalamu hao wanabainisha kuwa Sailo hujengwa kwa kutumia bati la chuma ngumu kisha kusiribwa kwa matofali ya kuchoma au ya saruji.
Hata hivyo, wanabainisha kuwa Sailo za bati hazifai kujengwa katika maeneo ambayo mabadiliko ya vipindi vya joto na vya baridi ni makubwa kwa sababu wakati wa joto bati linapata joto kwa haraka.
Aidha, wakati wa baridi bati hupoa kwa haraka na kupa
ta unyevu kwa ndani, jambo ambalo husababisha nafaka au mazao jamii mikunde iliyohifadhiwa kuoza.
“Lengo la uandaaji wa kitabu hiki ni kuelimisha jamii kuhusu teknolojia sahihi za uvunaji, utayarishaji, ufungashaji, usindikaji na hifadhi ya mazao ya nafaka baada ya kuvuna,” inaelezwa.
Wanabainisha kuwa uwezo mdogo na maghala duni yanayotumiwa na wakulima vijijini kwa kuhifadhi, huruhusu upotevu wa nafaka hadi asilimia 10
“Huu ni mwongozo kwa wakulima na wadau wengine, ili kuziweka bayana teknolojia sahihi na mbinu bora za kutunza baadhi ya mazao ya nafaka baada ya kuvuna ili kupunguza
upotevu,” kinasema kitabu hicho.
Wanaeleza kuwa wakulima wengi nchini huhifadhi nafaka kwa kutumia njia za asili kama vile vilindo, mitungi au vibuyu ambazo ni duni na husababisha upotevu wa nafaka kwa kiasi kikubwa.
“Pia hifadhi ya namna hii mara nyingi haikidhi mahitaji ya kaya, ili kuepuka upotevu wa mazao wakati wa kuhifadhi, hivyo ni muhimu kutumia maghala bora yanayokidhi mahitaji ya mkulima.
Faida za Sailo
Hupunguza gharama kwa mkulima kununua magunia kila mwaka. Hutumia nafasi ndogo ya eneo la kuhifadhi. Huzuia wadudu waharibifu na wanyama kama vile pannya kuharibu nafaka.
Ni nzuri kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya nafaka ambayo ni pamoja na mahindi, kunde, maharage na choroko. Lina sehemu ya juu ya kuwekea na sehemu ya chini ya kutolea nafaka.
Faida nyingine ni kudhibiti matumizi kwa kuweka kufuli, bei nafuu ili kumwezesha mkulima kumiliki na kuwa na usalama wa chakula. Linapatikana kwa ujazo mbalimbali kuanzia Kg250 hadi Kg 2000 kulingana na mahitaji.
Vyakula vya nafaka vinaaminika kuwa vinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu ikilinganishwa na mazao mengine ya chakula.
Inabainishwa kuwa iwapo wakulima wakiitikia wito na kutumia teknolojia hiyo ya kisasa ambayo imefanyiwa utafiti, vyakula vyao vitakuwa salama .
Mwitikio wa wakulima kuhusu teknolojia hii
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ulaya, wilayani Kilosa Julius Lumambo anaeleza kuwa wakulima wengi wamekuwa wakipoteza sehemu kubwa ya vyakula baada ya kuvuna kutokana na kukosa elimu.
“Kuna wakati tuliwekwa kwenye mradi wa kuzuia upotevu wa nafaka,lakini hakukuwa na mwitikio mzuri kwa wakulima, pengine wengi hupenda kuuza muda mfupi baada ya kuuza,” anasema.
Anasema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwatesa wakulima wengi kwa njaa hasa inapozuka mabadiliko ya hali ya hewa, mvua ikiwa nyingi au ikichelewa kunyesha kwa wakati.
Mkulima Malekela Kayombo wa kijiji cha Malangali mkoani Iringa anaeleza kuwa anahifadhi mazao yake kwenye viroba.
“ Kuna watu wamepita kuja kutuelimisha kuhusu uhifadhi wa mazao kwenye Sailo, nimevutiwa nayo kwa sababu sitohitaji kunyunyuzia dawa kwenye mahindi au mazao mengine ya nafaka, jambo ambalo ni la kiafya zaidi,”anasema.
Kayombo anabainisha kuwa ameshindwa kuwa na kifaa hicho kwa sasa kwa sababu kinauzwa kwa gharama ya Sh190,000 ambapo ukubwa wake ni sasa na gunia 40, hivyo amejipanga kununua msimu mwingine wa mavuno.
Mkulima mwingine Laurian Mbale wa Kijiji cha Msolwa wilayani Kilosa, anasema kuwa kwa sasa amekuwa anahifadhi mazao yake kwa kutegemea kunyunyuzia dawa, lakini ana lengo la kununua kifaa hicho.
“ Natamani kununua kwa ajili ya kuhifadhi mahindi maana pamoja na kwamba nalima na mpunga, lakini wadudu wanashambulia zaidi mahindi ingawa huwa najitahidi kuhakikisha yamekauka vizuri lakini bado wanasumbua,” anasema Mbale.

Beatrice: Mrembo aliyeamua kushika jembe kukuza kipato


Tofauti na vijana wengi wa rika lake, huwezi kuamini kwa ajira aliyonayo kama Batrice Haule angekuwa na hamu ya kujishughulisha na kilimo.
Umuonapo kazini au barabarani, mwonekano wake ni kama ule wa wanawake wengi wanaoijipenda ambao muda mwingi wanafikiria kuonekana warembo.
Lakini msichana huyu ana sifa ya ziada, siku za mwisho wa wiki au likizo, badala ya kupumzika nyumbani, yeye anatumia nafasi hiyo kusimamia miradi kadhaa ya kilimo anayoiendesha mkoani Ruvuma.
Beatrice mwenye umri wa miaka 28 anaishi Njombe na anafanya kazi katika shirika moja la kimataifa kama ofisa takwimu.
Pamoja na kuwa na ajira ambayo kwa baadhi ya watu ingetosha kumtuliza kimaisha, yeye anaamini katika dhana ya kuwekeza. Kwake maisha kama anavyosema; ‘’…ni kuwekeza, ni kupambana.’’
Ili kutekeleza dhana ya maisha ni kuwekeza akaamua kuwekeza mtaji wa akili na fedha zake kwenye sekta ya kilimo anayosema inalipa kuliko hata ajira rasmi. Anaamini kilimo ni zaidi ya ajira, kwani faida anazozipapata kutoka shambani ni kubwa mno
‘’Kwa zama hizi kama mtu anataka kufanikiwa katika maisha yake ni kilimo pekee. Kilimo ni fursa nzuri ambayo kijana anaweza kuifanya na kumpa mafanikio. ‘’ anasema na kuongeza:
‘’Kama upo kwenye ajira, hakikisha hiyo ajira yako iwe mbegu na anza kwa kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji. Mshahara haununui gari, mshahara haujengi nyumba, mshahara hausomeshi watoto shule nzuri, ila mshahara unaweza kuwa chanzo cha kufanya hayo yote.’’
Tangu mwaka 2015, Beatrice amekuwa akijishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali, na sasa anaendesha miradi yake mitatu ya kilimo na usambazaji wa maziwa aina ya mtindi.
Hii ni kwa sababu alibaini kuwa ajira pekee haitoshi kuendesha maisha yake.
Shauku ya kilimo
Zao la ufuta ndilo liloanza kumpa shauku ya kulima kama anavyosema:
“’Kwa mara ya kwanza nilianza kulima ufuta Chalinze mkoani Pwani, baada ya kuona mafanikio katika zao hilo nikaona kumbe fursa ipo kwenye kilimo,”, anasema.
Kwa kuwa kilimo kwake ni biashara, hakuridhika na zao moja la ufuta baada ya hapo aliongeza miradi mingine miwili ya mazao ya soya na tangawizi mkoani Songea.
INAENDELEA UK 28
INATOKA UK 25
“Mwaka jana nilipata taarifa kuwa kijiji cha Mkongo kuna ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo cha soya, sikutaka kupoteza muda nilikwenda kuona hali halisi baada ya kujiridhisha nikaanza na heka 20,”anasema.
Anasema mbali na ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo hicho alifanya utafiti kujua soko la soya na wateja wake. Baada ya hapo alilima akiwa na uhakika wa soko kwa asilimia 100.
“Kosa tunalolifanya sisi wakulima ni kulima bila kujua soko likoje; mazao haya ni ya biashara hivyo kabla ya kulima cha kwanza kujua ni soko na ndivyo nilivyofanya mimi” anaeleza.
Anasema sababu ya kulima zao zaidi ya moja na katika maeneo tofauti, ni kufanya kilimo kama sehemu ya biashara hivyo anaangalia mazao yenye faida na ambayo hata soko lake halisumbui.
Kwa zao kama soya ambalo hutumiwa na watu kama lishe na hata chakula cha kuku, wake soko kubwa anakouzia ni katika kampuni ya kutengeneza chakula cha mifugo ya Silverland Intrenation iliyopo iringa.
Mkulima hachoki
Kama ilivyo kawaida, mtafutaji hachoki, Beatrice aliamua tena kuongeza mradi mwingine kwa kulima zao la tangawizi hukohuko mkoani Songea katika kijiji cha cha Mkongotema kwa kulima heka moja pekee.
“Hili zao nilijaribu tu, kuna ndugu yangu mmoja alinieleza katika kijiji hicho tangawizi inakubali sana nikasema ngoja nikajaribu, kwa kweli sikutarajia mana zao limekubali hadi nikajuta kulima heka moja,” anaeleza.
Anavyomudu kilimo na ajira
Pamoja na kuwa mwajiriwa, lakini ajira yake haimzuii kufanya shughuli zake za kilimo, kwa kuwa hupangilia ratiba zake vizuri ili kilimo kisiathiri majukumu mengine ya kazi.
“Huwa naingia kazini asubuhi hadi saa nane mchana, hivyo kwa siku za wiki sipati muda mzuri wa kutembelea miradi yangu hivyo natumia vyema siku za mapumziko kwenda shambani, ‘’ anasema na kuongeza:
“Pia wakati wa likizo ndio muda mzuri kwangu kishirikiana na vijana wangu walioko shambani.’’
Changamoto
Kwa sasa mapenzi yake yameelemea kwenye kilimo, lakini kwa kuwa bado ni mwajiriwa, anajikuta katika mtanziko mkubwa wa kusimama miradi yake kiasi cha kufikiria kuacha kazi.
Kwa kuwa miradi yake ipo katika maeneo tofauti, anasema wakati mwingine anashindwa kuitembelea yote, kitu ambacho ni kosa kwa mkulima makini kama yeye.
“Raha ya miradi yako uwe nayo karibu, lakini inapokuwa mbali sina Amani, hivyo natamani siku moja nihamie katika mashamba yangu” anasema.
Ajivunia kilimo
Kwake kilimo sio tu kwa ajili ya kuvuna mazao mengi na kujipatia kipato. Anasema kupitia kilimo amejifunza mengi.
“Sasa hivi nimekuwa kama bwanashamba, kwani najua aina mbalimbali za dawa za kilimo,’’ anaeleza.
Anasema kipato anachokipata kupitia kilimo, asingeweza kukipata kama angetegemea ajira pekee. Kilimo hicho kwa sasa kimemwezesha kusomesha wadogo zake
“Asikwambie mtu hakuna njia nyingine ya mafanikio kama kilimo, yaani najivunia kutunza familia yangu kupitia kulimo lakini pia hata mahitaji yangu nayamudu sio kama zamani” anasema.
Kufahamiana na watu ni moja ya mafanikia kwa Beatrice, anasema kupitia kilimo amefahamiana na watu mbalimbali ambao hakutarajia kuonana nao ambao wamechangia mafanikio yake hasa kwa kutoa ushauri juu ya kilimo.
“Nimejenga jina kupitia kilimo hivi sasa ukiuliza Beatrice watakuambia yule mkulima, kwa hiyo jina limekua kupitia kilimo na sio cheo changu kazini” anaongeza.
Ndoto zake
Ukiondoa shauku ya kutaka kuwa mkulima mkubwa Afrika na duniani kwa jumla, Beatrice ana ndoto ya kuwasukuma wanawake kuingia kwenye kilimo.
“Nataka wanawake sasa waone kuwa kushika jembe sio ushamba, tusitegemee tu ajira ambazo hata kipato chake ni mara tatu zaidi ya kile kinachopatikana shambani”.
Aidha, anatamani kuwa mjasiriamali mkubwa kwani mbali na kilimo ana mradi wake wa kuuza maziwa mahala anapoishi.
“Katika hili nawaambia Wanawake wenzangu tusimame imara kwani tunaweza na tusikate tamaa mapema, tusichague kazi, hivi sasa kutegemea ajira pekee utachelewa kimaendeleo,’’ anasema.

Ecobank yazindua njia salama ya malipo kwa mtandao

Mkuu wa Kitengo cha wateja wa Reja Reja wa

Mkuu wa Kitengo cha wateja wa Reja Reja wa Ecobank Ndabu Lilian akizungumza wakati wa Uzinduzi  huduma ya Malipo kwa njia ya Mtandao, inayayojulikana kama MasterPass na Mvisa. Ecobank Tanzania ni Benki ya kwanza nchini kuzindua huduma ya Mobile App ambayo inakuwa ni suluhisho kwa huduma za kifedha. 
Dar es Salaam. Ecobank imeboresha aplikesheni yake ya simu za mkoni kwa kuanzisha utaratibu utakaowawezesha watu kulipia bidhaa moja kwa moja kupitia simku zao za mkoni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Mwanahiba Mzee, amesema hatua hiyo inalenga kuwarahisisha wateja wa benki na watu wengine kudhibiti fedha zao.
Applikesheni hiyo ya simu za mkononi inayojulikana kama Ecobank Mobile App, imekuja na huduma mpya za  MASTERPASS na MVISA ambazo zinamwezehsa mmilikiw a simu ya mkononi kulipia bidhaa na huduma kupitia simu yake.
“Mtanzania yeyote ataweza kutumia teknolojia hii ya mpya kulipia gharama mbali mbali kwa kutumia simu ya mkononi kwa kutumia kodi iitwayo Quick Response au QR,” amesema.
Applikesheni ya Ecobank Mobile ilizinduliwa Februari mwaka huu lakini kwa sasa imeboreshwa zaidi ili wateja wa Ecobank na wasio wateja wa bank waweze kuitumia duniani kote.
“Applikesheni ya Ecobank Mobile App ni njia rahisi ya kujipatia huduma za kibenki ndani ya nchi 33 ambazo Benki yetu inafanya biashara lakini pia unaweza kuitumia ukiwa kokote duniani,” ameongeza.
Kwa upande wake, mkuu wa kitengo cha wateja binafsi, Swere Ndabu, amesema: “Ili kutumia huduma hii wateja wa Ecobank na wasio wateja wanatakiwa kupakua Applikesheni ya Ecobank Mobile App kwenye smartphone zao kisha wanajisajili kwa kutumia kadi ya Visa au Master au kufungua akaunti ya Ecobank Xpress papo hapo na kuanza kufanya miamala ya malipo.”
Swere aliongeza kuwa kwa kutumia Ecobank Mobile App, mteja anaweza kuhamisha fedha kwenye akaunti yake ya Ecobank akiwa hapa nchini au nje ya nchi, pia ataweza kuhamisha fedha kwenda benki nyingine ndsni ay nje ya nchi au kwenda kwenye kadi za Visa duniani kote.
“Pia huduma hii itamwezesha kuunganishwa na huduma za kifedha za simu za mkononi za M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money,” amesema.

Hospitali anakotibiwa Lissu wapokea hela kutoka Tanzania


Ofisa Kitengo cha Habari na Itikadi wa Chadema, Hemed Ali amesema Hospitali na Nairobi nchini Kenya imethibitisha kupokea fedha kutoka Tanzania lakini zikiwa hazina maelezo.
Jana ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kuelezea mchakato wa utumaji wa fedha hizo kiasi cha Sh 43 milioni ikisema kuwa zilitumwa tangu Agosti 20. Ofisi hiyo ilikuwa ikifafanua taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyewaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa hajapa mchango huo wa wabunge.
Ali aliyepo Nairobi amesema amethibitishiwa na Hospitali ya Nairobi kupokea fedha hizo kutokaTanzania ingawa kulikuwa hakuna maelezo zaidi.
“Wamenieleza kuna fedha zimeingizwa kutoka Tanzania ila hazina maelezo ndiyo wanafuatilia benki,” amesema ofisa huyo.

Polisi: Watu hawataki kufuata sheria


Kamishna wa Polisi Jamii, Musa Ali Musa amesema Serikali inaheshimu misingi ya utawala bora lakini tatizo lililopo ni kwamba watu hawataki kufuata sheria.
Akizungumza leo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Amani duniani ambayo Kitaifa imefanyika Wilayani Temeke na kushirikisha asasi mbalimbali, mashirika ya kimataifa pamoja na Jeshi la Polisi viongozi wa dini.
Kamishna huyo amesema amani iliyopo hapa nchini haitakiwi kuchezewa na kwamba Jeshi hilo halitavumilia vitendo vya uvunjaji wa Sheria utokanao na itikadi za kisiasa, dini au makabila.
Amesema, nchi yoyote yenye amani, watu wake wanafuata misingi ya Sheria na taratibu za nchi hivyo ili kudumisha amani ni lazima kila mwananchi akubali kuheshimu sheria.
"Tanzania ni nchi inayoheshimu haki na misingi ya utawala bora lakini Kuna fikra imejengeka kuwa kuwa huru ni kufanya jambo lolote bila kufuata taratibu za nchi, "amesema
"Jeshi la Polisi litafanya lolote liwezekanalo ili amani iliyopo idumishwe."
Pia, ameonya juu ya usambazaji wa taarifa za kichochezi kupitia mitandao ya kijamii hasa vijana na kuwataka kujishughulisha na shughuli za maendeleo.
Ametolea mfano, Mlipuko wa mabomu ya  Mbagala ya mwaka 2014 na kusema kuwa licha ya kuwa ilikuwa bahati mbaya jamii ijifunze kuheshimu amani ili hali kama hiyo isije kujitokeza.
Mratibu wa Mtandao wa kutetea haki za watoto, GNRC, Yusuph  Masanja amesema ni muhimu kwa jamii kuheshimu haki za watoto ili kuwa na kizazi bora siku zijazo.

Lissu kufanyiwa upasuaji kesho


Wakati Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki (chadema) Tundu Lissu kesho  anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mwingine, fedha zilizochangwa na wabunge hatimaye  mchana zimeonekana katika akaunti ya hospitali ya Nairobi.
Lissu ambaye tangu Septemba 7 amekuwa akipatiwa matibabu,katika hospitali hii kesho  atafanyiwa upasuaji tena na jopo la madaktari kutazama athari zaidi katika mwili wake.
Akizungumza na mwananchi mmoja wa wauguzi wa hospitali ya Nairobi, ambaye ameomba kuhifadhiwa jina, amesema upasuaji unahusu eneo la nyonga.

Nyanduga: Serikali inawajibika kulinda haki ya watu kuishi


Hivi karibuni kumekuwa na hali ya wasiwasi wa usalama kutokana na matukio kadhaa ya mauaji, kutekwa, kupotea au kushambuliwa kwa risasi kwa wananchi.
Mapema mwaka huu kulitokea mauaji ya kuvizia katika Wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani ambapo zaidi ya watu 40 wakiwamo askari Polisi waliuawa. Hata hivyo, mauaji hayo yalikuja kudhibitiwa kwa kuwakamata baadhi ya wahusika na wengine kuuawa.
Kabla ya mauaji hayo kulikuwa na tukio la maiti sita zilizookotwa kando ya mto Ruvu mkoani Pwani zikiwa ndani ya viroba mwishoni mwa mwaka 2016, huku na kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane.
Tukio la karibuni ni la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu katika eneo la Area D mjini Dodoma Septemba 7, mwaka huu.
Kufuatia matukio hayo, Gazeti la Mwananchi limefanya mahojiamo maalumu na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga ambaye pamoja na mambo mengine, anasema hali ya usalama nchini ina changamoto kubwa kutokana na kutishiwa kwa haki ya kuishi. Endelea.
Swali: Naomba kupata historia ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na unaonaje upatikanaji wa haki hizo nchini kwa sasa?
Jibu: Tanzania imekuwa ni nchi iliyojikita katika kuheshimu haki za binadamu na hali hiyo imetoka na historia yake tangu tupate uhuru.
Katika tamko la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa anatangaza Tanzania kujiunga na Umoja wa Mataifa alisema nchi hii itakuwa inaheshimu Azmio la Ulimwengu la Haki za Binadamu.
Azimio lile lililokuwapo tangu mwaka 1948 linazungumzia mambo mengi zikiwamo haki za siasa na uraia, uchumi na kijamii na kiutamaduni na jinsi miaka ilivyokwenda zimetanuka zikahusisha haki za makundi.
Haki hizo zilikuja kuwekwa kwenye mikataba mbalimbali, kuna mikataba ya kikanda iliyokubalika katika Bara la Afrika.
Katika ngazi ya Taifa, haki hizi zilikuwa zinaheshimiwa tangu wakati huo, Mwalimu Nyerere aliona ili Taifa ambalo limetoka kutawaliwa lipate haki hizo, inabidi watu wawe huru, wafanye kazi na ndiyo maana kukawa na misemo kama uhuru na kazi, uhuru na maendeleo.
Yalikuwa ni matamko ya kisiasa lakini ni ya haki za binadamu. Sasa kitaifa haki hizi zilionekana kama matamko ya kisiasa, lakini zilikuja kuundwa taasisi za kuyalinda.
Mwaka 1965 Serikali ya awamu ya awamu ya kwanza iliunda Tume ya Kudumu ya Uchunguzi ambayo jukumu lake kubwa lilikuwa kuhakikisha watawala wanawatendea haki wananchi ndani ya misingi ya sheria. Kipindi kile kilikuwa cha mfumo wa chama kimoja, kwa hiyo ikaundwa ili kuwadhibiti viongozi.
Pale kiongozi wa umma anapozidi madaraka yake anawajibishwa.
Hapo mihimili kama Bunge, Mahakama ilikuwapo pamoja na Tume ile.
Hiyo iliendelea hadi mwaka 1984 ambapo haki za binadamu ziliingizwa kwenye Katiba. Mikataba ambayo Serikali iliibali iliingiza kwenye Katiba. Kulikuwa na mijadala iliyosababisha mabadiliko hayo.
Hakukuwa na mfumo wa kupata haki mpaka ilipoundwa sheria ya kuzitambua haki za msingi ilikuwa ikimwezesha mtu kama haki zile zikivunjwa aweze kuzidai mahakamani.
Inaendelea uk 24
INATOKA UK 23
Hiyo ilikuwa miaka ya 1990 na ilipofika mwaka 2001 ilianzishwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora ambayo ilianzishwa na ikawa mbadala wa Tume ya Uchunguzi. Hapo ikaongezewa majukumu, ikiwa pamoja na watumishi walioko ndani ya mipaka ya Serikali kuhakikisha wanafuata sheria na vilevile ikatoa fursa ya mwananchi kulalamika kwa kuwa hiyo ni haki ya msingi.
Majukumu ya Tume ni pamoja na kupokea malalamiko ya wananchi, kuyachunguza na kuyatolea mapendekezo. Nyingine ni kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na kuishauri Serikali pale inapoona misingi inavunjwa.
Swali: Kwa hiyo hali ya haki za binadamu ikoje kwa kipindi cha walau miaka miwili hadi sasa?
Jibu: Tuna maeneo au mafungu makubwa matano ya haki, kwa mfano, haki ya kuishi au uhai (haki mama), haki ya uhuru wa kwenda popote mtu anapotaka, fungu la uhuru wa maoni na kujieleza, haki ya kuabudu na imani, haki ya utu wa mtu yaani utu wako uheshimiwe, kuna haki ya ushiriki wako katika maamuzi yanayokugusa, au jinsi jamii inavyoendeshwa.
Vilevile kuna haki ya kupata huduma za msingi, haki ya kutambuliwa hasa pale kunapokuwa na unyonge katika hali au kundi kama watoto, wanawake, wazee, wote hawa wana haki.
Kwa ufupi naweza kusema haki hizi zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuna maeneo ambayo kuna changamoto au hatujafanikiwa.
Swali: Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya mauaji kama yale yaliyotokea wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, watoto kutekwa, maiti kuokotwa mtoni kwenye viroba na tumeona Mbunge Tundu Lissu akishambuliwa kwa risasi. Mnayachukuliaje matukio haya kwa kigezo cha haki ya kuishi?
Jibu: Cha msingi katika hilo kuna changamoto na ili kuiona kuwa ni changamoto ni vizuri tujue kwamba kimataifa, kwa sababu Tanzania siyo kisiwa, katika msingi wa jumuiya ya kimataifa, jukumu la usalama ni la Serikali.
Kutokana na hiyo dhana, kila mtu aliyeko ndani ya mipaka ya nchi, anastahili kulindwa haki yake ya uhai, na ndiyo maana kuna vyombo vya ulinzi na usalama.
Changamoto hii ukiichambua kwa matukio hayo uliyotaja moja moja, inabidi tuwe na maelezo ya kitaalamu yanayozungumzia taaluma ya ulinzi na usalama.
Kama Tume, tunasema kumekuwa na changamoto, lakini ni kwa nini changamoto zinajitokeza kwa maana kwamba utaona zinatokana na vyombo vyenye taaluma ya ulinzi.
Kama ni uhalifu ndiyo maana nikasema katika ile jukumu la Serikali, ni lazima vyombo vya ulinzi na usalama vishughulikie matatizo haya au changamoto hizi kwa misingi ya kisheria.
Kama watu wanauawa au kuna matukio ya vifo, kwa haki ambayo inapotea, ni lazima ipatikane sababu ya kiini. Dhana iliyopo ya utawala wa sheria, lazima sheria zitumike katika kujua tatizo ni nini na suluhu yake ni nini.
Baada ya mambo hayo ndiyo utajua tatizo la upatikanaji wa miili huko Mto Ruvu, mauaji ya Kibiti na mengineyo, panahitajika kufanyika uchunguzi wa kubainisha chanzo chake ni nini.
La msingi ni kwamba haki lazima ilindwe, sheria zifuatwe, kwa sababu kuna msemo unaosema, sheria ichukue mkondo wake.
Sasa sheria imetokea, ichunguzwe limetokana na nini chanzo chake kikijulikana sheria ichukue mkondo wake. Kuna dhana muhimu ambayo ni utawala wa sheria katika nchi inayojiendesha katika mfumo wa kidemokrasia na utawala bora. Ukiifuatilia kwa kiwango kikubwa unaweza kutetea haki za binadamu.
Swali: Pamoja na matukio hayo, kumekuwa na malalamiko ya ukandamizaji wa demokrasia na hapa tumeona vyama vya siasa vikilalamikia katazo la mikutano ya hadhara na maandamano lililotolewa na Serikali. Nini kauli yako?
Jibu: Kama tulivyosema awali, hizi ni changamoto zilizojitokeza ambazo, kweli Katiba na sheria zinatamka matamko yote ya haki hizo. Zinapotokea changamoto inatakiwa zizungumzwe na zitatuliwe.
Zimechukuliwa hatua kadhaa za kutafuta haki hizi kwa kwenda mahakamani kutafuta tafsiri ya sheria hizo.
Labda niseme kwenye utawala wa sheria na demokrasia na utawala bora, zinapotokea changamoto hizi, ni vizuri zitafutiwe tafsiri ya kikatiba.
Mnapokuwa na nchi ambayo mihimili inafanya kazi, mihimili hiyo inafanya kazi katika dhana ya ‘check balance’, mihimili inategemeana, lakini mhimili mmoja usiingilie mwingine. Huu ni utenganifu wa mihimili.
Inapotokea changamoto ya mhimili mmoja kuingilia mwingine, hatuna budi kufuata taratibu zinazowezesha kuchanganua kama mchanganyiko umetokea.
Katika haya, Katiba iko wazi, uhuru wa maoni upo, haki ya vyama kufanya mikutano, sasa ikishindikana mihimili kufanya kazi, itakuwa ni tatizo kubwa.
Lakini ninavyoliona, naamini kuna kesi zimefikishwa mahakamani zinazojaribu kuhoji, je mihimili inaingiliana? Kama haki ya vyama kufanya mikutano.
Sasa ni mpaka hapo mahakama zitakapotoa majawabu, ndiyo tutajua tafsiri.
Swali: Vipi kuhusu uhuru na mamlaka ya Tume hii? Mnawezaje kuiwajibisha Serikali ikiwa yenyewe ndiyo inawapa bajeti na inateua viongozi wake?
Jibu: Hizi tume ziko nchi nyingi tu na ziko hivihivi. Kwa sababu unaposema kuiwajibisha Serikali, sisi siyo polisi. Tume haifanyi kazi kama hivyo. Wananchi wanadhani ili uiwajibishe Serikali lazima utumie mabavu, utawala wa sheria unasema lazima liwe dude lenye maguvu.
Katika dhana ya uwajibikaji, mathalani, Tume inafanya kazi kwa kupokea malalamiko na kutoa mapendekezo. Ni tofauti na hukumu ya mahakama. Kwa maana ya kwamba amri ya mahakama inatekelezeka moja kwa moja, wakati pendekezo la tume lina utaratibu wa kutekelezwa.
Kwa maana kwamba anayeshauriwa anatakiwa achukue sheria ya kurekebisha.
Ni utaratibu wa kiutawala kwamba kwa sababu kuna sheria ambazo ni administrative (za kiutawala) na nyingine ni judicial (kimahakama), zile za kimahakama zinatakiwa ziheshimike.
Kwa hiyo Tume siyo Mahakama, lakini ikitoa mapendekezo lazima yaheshimiwe. Kutokuheshimika kwa mapendekezo ndiyo kunaifanya tume ionekane kama haina mamlaka.
Meno ya tume yanatokana na Katiba kwa sababu imeundwa na Katiba, kwa hiyo usipotekeleza maana yake huheshimu Katiba.
Pili, mapendekezo yale yasipotekelezwa yanaweza kuwekewa sheria. Kwa hiyo Tume imepewa mamlaka hayo ili iweze kutekeleza utawala bora.
Mara nyingi malalamiko yanayohusu uvunjifu au kukiuka madaraka au utendaji. Kwa hiyo yule anayelalamikiwa anatakiwa atekeleze kwa sababu uchunguzi wa tume utakuwa umejua ni kigezo gani kilichovunjwa.
Kwa hiyo kutotekeleza ni namna ya kutowajibika, ni kutowajibika kwa sababu anawajibika kufuata sheria.
Suala la kulipwa mshahara na Serikali wala isingekuwa kigezo, kwa sababu mbona Mahakama wanalipwa na Serikali? Mbona majaji wanateuliwa na Serikali? Hilo wala wananchi wasifikirie hivyo.
Kitu cha msingi ni kujiuliza, je, Tume inafanya majukumu inayotakiwa kufanya? Je, inapotoa mapendekezo yanatekelezwa katika dhana ya kuheshimu sheria na uwajibikaji?
Sasa hapo suala la msingi ambalo wenye mamlaka au wale wanaolalamikiwa zaidi wajue kwamba kutekeleza maelekezo ya Tume haina maana kwamba lazima ifike hatua ya kupelekana mahakamani.
Kwa hiyo unaposema tume haina meno haimaanishi kwamba inafanya kazi kama polisi kukuweka rumande, bali inafanya kazi kwa kuheshimu sheria.
Tume hii haiko chini ya kitu chochote, iko huru na imeundwa na Katiba, inapokea malalamiko ya wananchi na kutoa mapendekezo. Kwa hiyo haipokei maagizo kwamba usifanye hiki au ufanye hiki, inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba.
Swali: Hivi karibuni Tume yako ilitoa tamko baada ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kutoa kauli za kejeli kwa wananchi wasiokuwa na mapenzi na chama tawala (CCM), lakini kauli kama hizo zinaendelea kutolewa na viongozi wengine walioko madarakani na hamkemei?
Jibu: Nadhani kama ni mizania uko huru kutupima, mimi siko hapa kutetea kila kitu. Hilo sitaliingilia.
Pili, nimekwambia kuna kesi zinazoulizia uhuru wa vyama vya siasa na kesi zikishaingia mahakamani sisi hatuingilii. Lakini, unaweza kuweka mizania, kwa sababu siyo kila kitu kikitokea unatoa tamko.
Kuna vitu vya msingi tunavyozungumzia, hatufanyi kazi kwa vyombo vya habari tu. Suala la Mkapa tulizungumzia kwa sababu ya dhana. Kuna suala la ushirikishwaji, kuheshimu hoja za kila mtu, lakini linapoonekana linakuwa la jamii, la kukwaza watu na hasa linapojirudia, maana lilianza mwaka 2015, sasa utauliza mbona lilipotokea hamkutoa tamko?
Watanzania tusiwe watu wa kusukuma majukumu, ibara ya 26 ya Katiba inawataka Watanzania kuilinda katiba hiyo.
Wajibu wa kulinda na kutetea Katiba lisiwe la Chadema au tume tu, ni la kila raia, ni wajibu wa msingi wa kila raia kuilinda Katiba.
Kama hatuna utamaduni wa kuitetea tunangoja wengine tunakuwa hatuitendei haki Katiba.

Sekta ya benki yaanza kuona nuru mpya

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba Mzee(kushoto) akiwa katika mahojiano maalumu leo katika ofisi za Mwananchi. 
Dar es Salaam. Sekta ya benki nchini imeanza kupata matumaini ya kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika kutokana na kuanza kuimarika kwa biashara.
Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba Mzee ameiambia Mwananchi katika mahojiano maalumu leo Alhamisi kuwa kwa miaka miwili iliyopita sekta ya benki ilipata misukosuko kidogo kutokana na wafanyabiashara kuyumba lakini sasa kuna mwelekeo chanya.
Amesema sekta ya benki iliyumba kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kucheleweshewa malipo ya kandarasi zao na kutofanya vyema kwa baadhi ya sekta muhimu kama ya gesi jambo lililofanya washindwe kurejesha mikopo kwa wakati.
Mzee aliyetembelea ofisi za Mwananchi amesema athari zozote zinazowakumba wafanyabiashara zinaathiri pia benki na sekta ya majengo, ambayo sehemu kubwa hutumika kama dhamana ya mikopo.  
Mikopo chechefu ni ile ambayo wakopaji wameshindwa kuilipa kwa taasisi za fedha ndani ya muda unaotakiwa ambao ni siku 90.
“Kandarasi nyingi bado hazijalipwa na sehemu kubwa ya dhamana za mikopo hiyo ni majengo ambayo yanashuka thamani kwa sababu wanunuzi ni wachache… hii ni hali ngumu kwa wateja,” amesema.
Amesema benki nyingi hazijapoteza fedha walizokopesha ila ni utaratibu wa kibenki unaofanya zionekane kama ni mikopo isiyolipika ilihali wanaodaiwa watailipa siku zijazo licha ya mdhibiti kutotaka kujua sababu za wateja kushindwa kulipa kwa wakati.
“Sasa hivi hata wasafirishaji waliokuwa wamepaki malori wameanza kupata biashara kwa sababu mambo yameanza kurekebishwa. Malipo ya mikopo yameanza kuja hivyo biashara nyingi zinazidi kuimarika.
“Inawezekana mwishoni mwa mwaka huu bado hali ikawa ngumu kwa sababu ndiyo wanaendelea kuimarika lakini mwakani hali itakuwa nzuri na tutaanza kuona tofauti,” amesema.
Ecobank ni miongoni mwa benki zilizokuwa na kiwango kikubwa cha mikopo chechefu kwa kuwa na asilimia 57 ya mikopo yote katika robo ya kwanza mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 38 ya robo ya mwisho wa mwaka jana.
Bosi huyo mpya amesema kazi yake kubwa kwa sasa ni kupunguza kiwango hicho cha mikopo isiyolipika ambayo imekuwa ikiisumbua benki na kuathiri faida ambayo hupatikana katika uendeshaji.
“Malengo ya Ecobank Group ni kuwa na wateja milioni 100 ifikapo 2020 lakini hapa Tanzania nataka tuwe na wateja zaidi ya milioni katika kipindi hicho na kuifanya benki iwe na faida zaidi,” amesema Mzee aliyeteuliwa kuiongoza benki hiyo kuanzia Julai.

Friday, September 22

WAZIRI KAIRUKI AZINDUA BODI YA PILI YA UONGOZI INSTITUTE

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema kuwa wakurugenzi walioteuliwa katika bodi ya Taasisi ya Uongozi  ni watu makini na wenye uzoefu wa muda mrefu katika nafasi mbalimbali ,hivyo watatoa ushauri mzuri kwenye taasisi hiyo.

Waziri Angellah aliyasema hayo katika uzinduzi wa bodi ya pili ya Taasisi  ya Uongozi uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini  Dar es Salaam. Amesema bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo wamepita katika utumishi na wazalendo katika sehemu zao mbalimbali ambapo watakuwa msaada mkubwa kwa taasisi hiyo katika  kutoa ushauri.

Amesema kuwa Uongozi Institute ilianzishwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi wa Afrika katika kuangalia maendeleo endelevu ya bara la Afrika  hivyo wajumbe wa bodi ni wa kimataifa na wanatambulika.

Angellah amesema kuwa walioteuliwa na Rais Dk.John Pombe Magufuli watatimiza majukumu yao na wataendelea kupewa ushirikiano pamoja na viongozi wengine wa Afrika katika kuwa na ajenda ya kuandaa viongozi.

Amesema uongozi Institute inatakiwa kutimiza mambo matatu moja ni bidhaa ya huduma iliyo na kiwango bora, kuangalia rasilimali  ya kuweza  kufanya taasisi hiyo ikue katika kuangalia vyanzo vya mapato pamoja na kujengea uwezo wa kuendelea kutekeleza ajenda ambazo zimeibuliwa.

Walioteuliwa katika bodi hiyo Mwenyekiti ni Balozi wa Finland Inchini Afrika Kusini, Kari Alanko , Makamu wa Rais Profesa Idris Kikula wengine ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora  Dk. Laureane Ndumbaro,  Katibu Mtendaji wa SADC Dk. Stergomena Tax, Profesa Penina Mlama wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Christina Duarte Waziri wa Zamani wa Fedha , Mipango na Utumishi wa Cape Verde, Mkurugenzi wa Nodic Afrika ya nchini Sweeden Lina Soiri, pamoja Mkurugenzi wa zamani wa shule ya utawala ya nchini Uingereza , David Walker.

Nae Afisa Afisa Mtendaji Mkuu wa Uongozi Institute, Profesa Joseph Semboja  amesema kuwa chombo hicho kilianzishwa katika kuwajengea viongozi wa Afrika ambao waliridhia kuundwa kwa chombo hicho.

Amesema kuwa Taasisi hiyo imetoa mafunzo mbalimbali tangu kuanzishwa kwake na itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki akizungumza katika uzinduzi wa bodi ya pili ya Wakurugenzi wa Uongozi Institute , uliofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Uongozi Insitute, Profesa Joseph Semboja akizungumza katika uzinduzi wa bodi ya Uongozi Institute  juu ya taasisi hiyo inavyofanya kazi  katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Uongozi Institute ,Balozi wa Finland Inchini Afrika Kusini, Kari Alanko akitoa shukurani kwa Waziri Kairuki  mara baada ya kuzinduliwa  bodi hiyo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki akigawa vitabu vya miongozo kwa wajumbe wa Bodi hiyo.
 Sehemu watendaji mbalimbali wa serikali waliohudhuria uzinduzi wa bodi ya pili ya oungozi institute.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na bodi ya ya wakurugenzi ya Uongozi Institute, jijini Dar es Salaam.