Monday, July 31

VYUO VIKUU VYATAKIWA VIZALISHE WATALAAM WA KUSAIDIA TAIFA KWENYE MAENDELEO


Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii

Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe Juma ameviasa vyuo vikuu nchini vizalishe wataalam ambao watakuwa msaada kwa taifa.

Waziri huyo ameyasema hayo wakati akifunga maonesho ya vyuo vikuu nchini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inasisitiza viwanda hivyo lazima vyuo vijenge dhana hiyo kwa kuzalisha wataalam wataofanya viwanda hivyo viwepo kutokana na ujuzi walionao.

Waziri Riziki ametaka vyuo vikuu kutokana na maonesho kuwa na mitazamo mipya ya kuwa na mitaala ambayo itazalisha wataalam wenye uwezo katika soko la ajira na hata kujiajiri.

Amesema kuwa serikali inaangalia vyuo vikuu vinavyofanya kazi ikiwa ni pamoja na kuangalia utafiti kwa ajili ya maendeleo ya taifa  pamoja na watu wote.

Nae Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), Profesa Eleuther Mwageni amesema kuwa maonesho yajayo wataboresha na kuangalia uwezekano wa kuongeza siku kutokana na maoni ya wadau wa vyuo vikuu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe Juma akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya vyuo vikuu nchini katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), Profesa Eleuther Mwageni akizungumza wakati maonesho ya vyuo vikuu nchini katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

WAKAZI WA DAR, PWANI KUKOSAMA MAJI KWA SAA KADHAA KUPISHA UBORESHAJI WA MTAMBO MPYA WA UZALISHAJI MAJI WA RUVU JUU


Shirika la MajiSafi na Majitaka Dar-es-salaam (DAWASCO), linawatangazia wateja wake wote wa jiji la Dar-es-salaam, pamoja na Mji wa Kibaha Mkoani Pwani kuwa mtambo wa uzalishaji Maji wa Ruvu Juu utazimwa kwa wastani wa Saa 8, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni, siku ya Jumatatu tarehe 31/07/2017.

Sababu ya kuzimwa kwa Mtambo : Kumruhusu Mkandarasi (WABAG), kukamilisha Mfumo wa umeme katika mtambo mpya wa uzalishaji Maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi mkoani Pwani.

Maeneo yatakayoathirika na Kuzimwa Kwa Mtambo huu:

Mlandizi Mjini, Ruvu Darajani, Vikuruti, Disunyara, Kilangalanga, Janga, Mbagala, Visiga, Maili 35, Zogowale, Misugusugu, Tanita, Kibondeni, Kwa Mathias, Nyumbu, Msangani, Kwa Mbonde, Picha Ya Ndege, Sofu, Lulanzi, Gogoni, Kibamba, Kibamba Njia Panda Shule Kibwegere, Mloganzira, Kwembe, Kibamba Hospitali, Kwa Mkinga, Luguruni, Kimara, Ubungo, na baadhi ya maeneo ya Tabata.

Toa taarifa Dawasco kupitia vituo vya wateja  Dawasco kimara 0743-451865, Dawasco Tabata 0743-451867, Dawasco Kibaha 0743-451875.

Dawasco inawaomba wateja kutunza Maji ya kutosha pindi Mtambo utakapokamilika
Kwa taarifa zaidi wasiliana nasi: Kituo cha huduma Kwa wateja 0800110064 (BURE) au Tembelea: www.dawasco.go.tz

JAFO AHIMIZA WANANCHI KUTUNZA MIRADI YA MAJI


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo amewataka wananchi wa wilaya ya Ukerewe kutunza miradi ya Maji kwa kuwa serikali inaigharamia kwa fedha nyingi.

Jafo aliyasema hayo alipotembelea mradi mkubwa wa maji wa Kazilamkanda ambao utahudumia vijiji vipatavyo 13 wilayani humo.

Amesema serikali inafanya jitihada za kuwatatulia wananchi wake kero mbalimbali ikiwemo ya upatikanaji wa huduma ya maji, hivyo ni vyema wakatunza miundombinu ya miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Akikagua mradi huo, Jafo alimpongeza Mkandarasi aliye jenga chanzo na tanki la kuhifadhia maji la lita 680,000 ambaye ni Lutare Make Enginnering Ltd kwa kazi nzuri.

Amesisitiza kukamilishwa kwa usambazaji wa Maji katika vijiji vyote 13 kabla  ya Disemba 30 mwaka huu.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kulazwa mabomba yaliyo na ubora ili kuepusha kupasuka kwa mabomba endapo mabomba hayo yatakuwa hayana viwango na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi na halmashauri baada ya kukabidhiwa mradi husika.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Rutala wilayani Ukerewe mkoani Mwanza juu ya utunzaji wa miradi ya maji.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akipata taarifa kuhusu miradi ya maji wilayani Ukerewe.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akifanya ukaguzi wa tenki la maji.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akifanya ukaguzi wa mashine za kusukumia maji.

Gari la mkurugenzi aliyepotea wa IEBC lapatikana


 Gari la Naibu Mkurugenzi aliyepotea wa idara ya mawasiliano ya kimtandao (ICT) wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Chris Musando limekutwa katika eneo la maegesho la TRM mjini hapa.

Gari hilo aina ya Land Rover Discovery lilikutwa likiwa kamilifu katika Barabara ya Thika saa 7.00 usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Julai 31.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa Jiji la Nairobi, Ireri Kamwende amesema gari hilo halikuharibiwa na msako umeimarishwa ili kumpata ofisa huyo mwandamizi.
Mwenyekiti wa Tume, Wafula Chebukati amesema Musando alionekana kwa mara ya mwisho Ijumaa usiku.
"Mawasiliano ya mwisho kutoka kwake yalikuwa ujumbe mfupi wa SMS ambao ulitumwa kwa mmoja wa marafiki zake saa 9.00 usiku wa kuamikia Jumamosi,” amesema Chebukati.

Ameongeza kwamba ujumbe huo ulionyesha Msando alikuwa na fahamu zake na anayejua uelekeo wa siku hiyo.

Musando alikuwa anajaza nafasi ya mkurugenzi wa ICT wa IEBC, James Muhati ambaye alilazimishwa kwenda likizo ya siku 30 baada ya kushindwa kutoa ushirikiano na idara ya ukaguzi.

Majaliwa aahidi kumaliza tatizo la maji Mbeya


Amesema mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais John Magufuli ya kumtua mama ndoo.
Wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumapili, Julai 30 alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
Amesema Mkoa wa Mbeya umetengewa Sh10.383 bilioni kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake Sh2.72 bilioni zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Wilaya ya Rungwe.
Waziri Mkuu ametaja mradi mwingine unaotekelezwa wilayani Rungwe ni pamoja na mradi wa maji wa Masoko wenye thamani ya Sh5.3 bilioni, utakaohudumia jumla ya vijiji 15.
 “Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayojengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa fedha za ndani,” amesema.
Amesema mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.
Pia, Waziri Mkuu amesema wananchi lazima wazingatie sheria ya mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
“Hatuwezi kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria,” amesema.

Gwajima mgonjwa, ashindwa kufika mahakamani


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Agosti 30, 2017 itatoa hukumu katika kesi ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi inayomkabili Askofu wa Kanisa la ufufuo na uzima, Josephat Gwajima na wenzake watatu.
Hukumu hiyo ilipaswa kutolewa leo Jumatatu, Julai 31 kwa Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha lakini ilishindikana kwa sababu hakimu huyo alikuwa na udhuru.
Hata hivyo, Wakili Peter Kibatala amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa wakati kesi ilipoitwa mbele yake kuwa Askofu Gwajima ni mgonjwa na mahakamani hapo amewakilishwa na mdhamini wake.
Hayo yametokea baada wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kuiambia mahakama kuwa washtakiwa George Mzava, Msaidizi wa Askofu Gwajima, Yekonia Bihagaze (39) na Georgey Milulu wapo mahakamani lakini Askofu Gwajima hayupo.
Pia, amedai kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa hukumu lakini wamepata taarifa Hakimu Mfawidhi, Mkeha anayeisikiliza kesi hiyo anaudhuru.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo kesi imeahirishwa hadi Agosti 30, 2017 ambapo watasomewa hukumu.
Mzava, Bihagaze na Milulu wao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa wakimiliki bastola aina ya berretta pamoja na risasi 20 kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa siku hiyo na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha mara baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi kutoa ushahidi wao na kuufunga.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Shedrack Kimaro na Joseph Maugo.
Huku upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Peter Kibatala ambapo washtakiwa walijitetea pamoja na mashahidi wao wawili akiwamo Nesi wa hospitali ya TMJ, Devotha Bayona na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima George Kiwia.
Katika ushahidi wa upande wa utetezi wa shahidi, Devotha alidai kuwa yeye ni afisa muugizi daraja la pili katika Hospitali ya TMJ na yupo kitengo cha ICU.
Machi 29, 2015 aliingia zamu usiku akipokea zamu toka kwa Nesi Rebecca ambaye aliacha kazi 2016 wakati huo Askofu alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo kwa siku ya tatu.
Anakumbuka siku hiyo walikwenda askari wawili na mtu mwingine Bihagaze wakagonga mlango wa ICU wakahitaji begi la mgonjwa, walivyojitambulisha alitaka kuhakikisha ni kweli akamfuata Gwajima na kumuuliza. Alieleza ushahidi.
Amedai Gwajima alimueleza ni kweli Bihagaze ni msaidiziwake na kwamba Bihagaze alimwambia yupo pamoja na askari hao wanataka begi la mgonjwa.
Muuguzi huyo amesema Gwajima alisema hawezi kutoa begi hadi wapewe maelezo maalumu na kwamba begi hilo lilikuwepo pembeni ya kitanda cha Gwajima.
Baada ya kupewa majibu hayo na Gwajima, aliwaambia polisi amesema hawezi kulitoa hadi polisi waandike maelezo, wakamueleza wanachohitaji ni begi na maelezo wataandika kesho.
Wakati wanajibizana Gwajima alisikia na akamwambia nesi atawapa hilo begi kwa sababu ndani Lina silaha yake.
“Polisi walitaka kuingia kinguvu nikawaambia hapa ni ICU hamuwezi kuingia kinguvu, " alieleza nesi huyo na kwamba Gwajima alimwambia kama wanalihitaji kinguvu chukua begi mpe Bihagaze awape polisi.
Amedai kabla hajampatia begi hilo Bihagaze polisi walimpokonya, akafunga mlango akaendelea na mgonjwa wake lakini alimuona mgonjwa anamawazo.
Washtakiwa wengine mbali na Gwajima wao wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A walikutwa wakimiliki Bastola aina ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Imeendelea kudaiwa kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1) na cha 34 (1) (2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Pia, wanadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao pia walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun.
Washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti waliyopewa ya kuwa kila mshtakiwa awe na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye alisaini hati ya maneno ya dhamana yenye thamani ya Sh1 milioni.

Maduro adai kupata ushindi Bunge la Katiba


Rais Nicolas Maduro amedai kupata ushindi mkubwa katika kura ya kumwidhinisha kuchagua wajumbe wa Bunge la kuandika Katiba mpya ya nchi huku jumuiya ya kimataifa ikilaani upigaji kura uliogubikwa na ghasia zilizosababisha watu 10 kuuawa.
Baraza la Taifa la Uchaguzi la Venezuela lilitangaza jana kwamba zaidi ya watu milioni nane walipiga kura kumpa Rais Maduro mamlaka yasiyo na kikomo katika uundwaji wa Bunge la Katiba.
Watu waliojitokea kupiga kura walikuwa mara mbili kinyume cha matarajio ya wapinzani wa Serikali na wachambuzi huru.
"Tumepata Bunge la Katiba,” alisema Maduro katika hotuba yake kwa mamia ya wafuasi wake katikati ya Jiji la Caracas baada ya tume kusema waliojitokeza walikuwa asilimia 41.5.
“Huu ni ushindi mkubwa ambao wanamapinduzi wameupata katika historia ya miaka 18,” alisema.
Takriban watu kumi wameripotiwa kuuawa katika siku inayotajwa kuwa ya umwagikaji damu baada ya miezi minne ya machafuko.
Kumekuwa na mapambano kati ya polisi na waandamanaji ambao wanapinga Bunge hilo la Katiba ambapo wamekuwa wakiweka vizuizi barabarani.

Urusi kufukuza wanadiplomasia 755 wa Marekani


 Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameagiza kuondolewa wanadiplomasia na wafanyakazi 755 wa Marekani waliopo nchini humo na anafikiria kuchukua hatua za nyongeza kulipiza kisasi kwa vikwazo vya uchumi ilivyowekewa nchini hiyo.
Putin alisema jana katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa kwamba aliagiza hatua hizo kwa sababu “alifikiri ulikuwa wakati wa kuonyesha kwamba hawawezi kubaki bila kujibu mapigo."
Utekelezwaji wa agizo la usitishwaji shughuli za wafanyakazi hao wa ubalozi wa Marekani nchini Urusi unatarajiwa kuwa Septemba Mosi mwaka huu. Watabaki wafanyakazi 455.
Desemba 2016, aliyekuwa rais wa Marekani, Barack Obama aliamuru kutimuliwa wanadiplomaisa 35 wa Urusi kutokana na tuhuma za Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani kupitia njia ya mtandao.
Jumanne iliyopita mabunge yote mawili ya Congress ya Marekani yaliidhinisha kwa wingi wa kura vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi.

Al Shabaab waua wanajeshi 24 wa AMISOM


Wanajeshi 23 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM) na askari mmoja wa Somalia wameuawa katika mtego wa kuvizia ulioandaliwa na wapiganaji wa Al Shabaab Kusini Magharibi mwa Somalia.
Mapigano yalizuka baada ya wanamgambo wa Al-Shabaab kuvamia vikosi vya AMISOM mapema Jumapili katika Wilaya ya Bulamareer ya Mkoa wa Lower Shabelle kilomita 140 Kusini Magharibi mwa mji wa Mogadishu.
"Tumechukua miili 23 ya askari waliouawa wa AMISOM na askari mmoja wa Somalia kutoka kwenye eneo ambalo Al Shabaab waliweka mtego wa kuvizia na kuvamia,” alisema Ali Nur, naibu gavana wa Lower Shabelle.
Wapiganaji hao wa Al Shabaab ambao wamekuwa wakipigana na majaeshi ya serikali ya Somalia inayoungwa mkono na nchi za Magharibi wamedai kwamba wameua askari 39 wa AMISOM.

Sunday, July 30

NEC imeteua Wabunge 8 kuziba nafasi ya waliotimuliwa CUF

Ni siku moja baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai kumuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendelea na hatua zinazostahili kujaza nafasi za Wabunge waliofutwa uanachama na CUF kwa mujibu wa Sheria.
Leo July 27, 2017 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ‘NEC’ imefanya uteuzi wa Wabunge 8 wa Viti Maalum ambao wataziba nafasi za Wabunge ambao wamevuliwa uanachama na Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba.
Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kikao chake cha July 27, 2017 imewateua wafuatao kuwa Wabunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi CUF.

View image on Twitter

NCHI ya Uturuki Yaomba MSAADA Tanzania

Tanzania imeombwa kuisaidia Uturuki kiwango cha Tani 20 ya Korosho kufuatia nchi hiyo kuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo yenye uhitaji zaidi nchini Uturuki.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara kutoka Uturuki ijulikanayo kama 'Turkish Exportetrs Assembly' (TIM) Bwana Kemal Batuhan Yazici amesema kuwa, kiwango cha korosho kilichopo nchini kimeshuka wakati mahitaji ya nchi ni Tani 20, hivyo wanaitegemea Tanzania kuondoa uhaba huo nchini mwao.

Kemal Batuhan Yazici amesema, Korosho inayohitajika nchini Uturuki ni ile ambayo tayari imechakatwa na kufungwashwa vyema kwa viwango vya kimataifa na sio malighafi hivyo ni vyema wafanyabiashara hiyo wakaandaa utaratibu wa haraka kuhakikisha Korosho zinasafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchini Uturuki.

Kwa muda wa miezi sita, kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kimeongezeka kwa asilimia 9 kwa bidhaa za Tanzania zinazosafirishwa kutoka nchini Tanzania kwenda nchini Uturuki hivyo ongezeko hilo linaashiria Tanzania kupata soko lenye tija nchini Uturuki.

Katika siku za hivi karibuni nchi ya Uturuki imeongeza ushirikiano wake wa kibiashara na nchi ya Tanzania ambapo nchi hizo zimepata fursa mara kadhaa kuonesha maeneo yao ya uwekezaji baina yao ili kuongeza faida na kuleta maendeleo.

TAMKO TOKA IDARA YA UHAMIAJI


Idara ya Uhamiaji   imesema jukumu la Udhibiti  wa Uingiaji na Utokaji  wa raia  wa kigeni nchini, linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji  Sura ya 54 (Rejeo la 2016) na wala  haiwalengi  wafanyakazi  wa  Kampuni ya Madini ya Acacia  peke yake.

Ni hitajio la kisheria  kwa kila raia wa kigeni  anayeingia na kutoka nchini  kukaguliwa  ili kujiridhisha  iwapo  hakuna  dosari zozote za Uhamiaji, Ulinzi na Usalama.

Sheria ya Uhamiaji inaitaka Idara ya Uhamiaji  kumhoji  mtu yeyote awe raia wa Tanzania au kigeni  bila kujali anafanya  kazi  kwenye Kampuni au Shirika  gani, pale  inapotaka kujiridhisha  juu ya  uhalali  wa ukaazi wake hapa nchini na ikijiridhisha kuwa mtu huyu  hana dosari zozote inamwachia huru kama ilivyofanyika  kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Madini ya Acacia  waliohojiwa  na kuruhusiwa kuendelea na safari yao hivi karibuni.

Idara ya Uhamiaji  inapenda kuuarifu Umma kuwa hakuna sababu zozote  nje ya matakwa ya  Sheria  ya Uhamiaji zinazopelekea  Idara ya Uhamiaji   kuweka kizuizi  cha kuja au kutoka kwa wafanyakazi wa kigeni wa Acacia.

Tunapenda kuujulisha Umma kuwa  ni muhimu  kwa watanzania na raia wa kigeni wanaokusudia kuingia na kutoka nchini kuhakikisha wanafuata  Sheria za Uhamiaji  ili  kutimiza hitajio la kisheria.

Imetolewa na
Ally M. Mtanda
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji

29 Julai 2017

MBUNGE ROSE TWEVE WATENDAJI FANYENI KAZI ACHENI MAJUNGU




Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi CCM Rose Tweve akizungumza na madiwani na wananchi wa halmashauri ya Mafinga Mjini wakati wa baraza la madiwani
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mafinga Mjini Charles Makoga akizungumza wakati wa baraza la madiwani lilofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo
Baadhi ya madiwani,viongozi pamoja na wananchi waliohudhuria baraza la madiwani lilofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Mafinga Mjini.
 
Na fredy Mgunda, Mafinga.
 
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi CCM Rose Tweve amewata watendaji wa halmashauri ya Mafinga Mjini kufanya kazi kwa kujituma na kuwa tumikia wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini ambalo linaongozwa na mbunge Cosato Chumi.
 
Akizungumza wakati wa baraza la madiwani wa halmashauri ya Mafinga Mjini alisema kuwa watendaji wengi wamekuwa wakilalamikiwa kutokana na kufanya kazi chini ya kiwango na kuwapelekea wananchi kuwa na changamoto ambazo hazina sababu.
 
“Hivi watendaji kitu gani kinachosababisha msifanye kazi kwa weledi kama ambavyo mlivyokuwa mnaomba kazi,jamani serikali ya awamu ya tano haitaki mfanye kazi kwa mazoea kama zamani saizi mnatakiwa kufanya kazi kutokana na kasi ya kimaendeleo ya serikali ya awamu ya tano”alisema Tweve
 
Tweve alisema kuwa watendaji wanaohusika na sekta ya maji katika halmashauri ya Mafinga Mjini wamekuwa hawafanyi kazi kwa weledi kwani tatizo kuwabambikia bili wananchi limekuwa Sugu na kuongeza malalamiko mengi huko mitaani hivyo lazima mbadilike maana swala la bili limekuwa kero sana hapa Mafinga Mjini lazima mlitafutie ufumbuzi.
 
“Toka nimerudi nimekuwa nikipokea malalamiko mengi yanayohusu bili za maji naombeni tembeleeni nyumba kwa nyumba kuandika bili sahihi na sio kutoa bili kwa kukisia hii inaalibu sura nzima ya viongozi wa halmashauri ya Mafinga Mjini, narudia tena watendaji fanyeni kazi kwa kujituma acheni mazoea kazini”alisema Tweve
 
Aidha Tweve alimuomba Mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanafanya kazi za wananchi na sio kukaa tu ofisini kitu kinachosababisha kuongezeka kwa matatizo kwa wananchi, hivyo mtalazimika kuwafuata wananchi kujua changamoto zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Mafinga Mjini Charles Makoga alisema kuwa ahakikisha watendaji wote wanaenda kufanya kazi kwa wananchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyokuwa miaka ya huko nyuma na kuendelea kutekeleza Sera za chama cha mapinduzi CCM na kuendena na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John pombe Magufuli na kuwaletea maendeleo wananchi.
 
“Watendaji wangu mmekisikia alichosema mbunge Rose Tweve kuhusu wajibu kwa kweli hii ni aibu kubwa inatupaswa kujilekebisha ili kuendelea kutekeleza Sera za serikali ya awamu ya tano la sivyo nitaanza kuwatumbua mmoja baada ya mmoja ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa halmashauri ya Mafinga Mjini”alisema Makoga
 
Lakini Makoga aliwasifu wabunge Wawili ambao ni mbunge Cosato Chumi na Rose Tweve kwa kufanya kazi kwa nguvu na kuleta maendeleo ya wananchi wa wilaya ya Mufindi kwa ujumla maana kila siku tunapata mambo mapya ya kimaendeleo kupitia migongo yao na kuwaomba waendelee kutafuta njia nyingine za kuiletea maendeleo Mufindi.
 
“Miaka yote tungekuwa na wabunge kama hawa wawili leo hii Mufindi ingekuwa mbali sana kimaendeleo kutokana na Juhudi zao tunaziona maana saizi kila secta wameigusa kwa kuleta maendeleo au mikakati ya kutatua changamoto za maeneo husika” alisema Makoga
 
Nao baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo wasema kuwa bado wazitafutia ufumbuzi changamoto za Mji wa Mafinga licha ya kuwa na ufinyu wa bajeti za kimaendeleo kwenye miradi waliyoiomba hivyo wakipewa bajeti na kuajiri baadhi ya watumishi kila kitu kitaenda vizuri na changamoto za wananchi zitatuliwa kwa wakati.

Neno La Leo: Ni Heri Kuwa Na Adui Mwerevu Kuliko Rafiki Mjinga....!

Image may contain: 1 person, sitting and outdoor


Ndugu zangu, 

Katika dunia hii tunayoishi, wakati mwingine ni heri mwanadamu ukawa na adui mwerevu kuliko kuwa na rafiki mjinga. 

Rafiki yako akitokea kuwa ni mtu mjinga, basi, naye atakushauri mambo ya kijinga. Na pengine asiwe na hata la kukushauri. 

Mwanadamu usikimbilie kumchukia adui yako, na hususan akiwa ni mwerevu. Yumkini kuna ya kujifunza kutoka kwa adui mwerevu.

Angalizo: Mwanadamu unapaswa pia kuusikiliza kwa makini ujinga wa rafiki yako mjinga. Yumkini katika ujinga wake anaokueleza, waweza ukaambulia moja au mawili ya kujifunza. Hivyo, usimdharau rafiki yako mjinga.

Ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa.