Monday, July 31

Majaliwa aahidi kumaliza tatizo la maji Mbeya


Amesema mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais John Magufuli ya kumtua mama ndoo.
Wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumapili, Julai 30 alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
Amesema Mkoa wa Mbeya umetengewa Sh10.383 bilioni kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake Sh2.72 bilioni zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Wilaya ya Rungwe.
Waziri Mkuu ametaja mradi mwingine unaotekelezwa wilayani Rungwe ni pamoja na mradi wa maji wa Masoko wenye thamani ya Sh5.3 bilioni, utakaohudumia jumla ya vijiji 15.
 “Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayojengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa fedha za ndani,” amesema.
Amesema mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.
Pia, Waziri Mkuu amesema wananchi lazima wazingatie sheria ya mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
“Hatuwezi kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria,” amesema.

No comments:

Post a Comment