Wednesday, July 12

Rooney aiteka Dar

Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Everton, Wayne Rooney amekuwa kivutio wakati msafara wa timu hiyo ulipowasili jijini Dar es Salaam leo asubuhi.
Everton iliyowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JNIA) ilipokelewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Ndege binafsi ya Everton iliwasili JNIA saa 2:39 Asubuhi, kabla ya wachezaji kuanza kuingia kwenye basi lao maalumu huku wakipitia kwa Waziri Mwakyembe na kumpa mkono kuanzia saa 2:55.
Wakati wachezaji wa Everton wakiingia kwenye basi, mashabiki waliokuwa nyuma ya geti la kuingilia VIP kila mmoja alionyesha shauku ya kumuona mubashara 'live' Rooney ambaye kana kwamba msafara huo ulilitambua hilo na Rooney kuwa wa mwisho kushuka.
Aliposhuka Rooney alikwenda kumpa mkono Waziri Mwakyembe na kisha kuelekea kwenye basi maalumu la timu hiyo, wakati akielekea kwenye basi baadhi ya mashabiki wake waliokuwa uwanjani hapo walianza kupaza sauti wengine wakitaka ageuke asimame na kupunga mkono, lakini wala hakuwa na habari nao zaidi ya kwenda moja kwa moja kwenye basi.
"Jamani hii timu ndiyo imewasili, ni timu kubwa na Tanzania tunafarijika kwa ujio huu, niwambie tu Watanzania hata nyinyi Waandishi wa Habari, ulinzi umeimarishwa na katika mazoezi yao hata ruhusiwa mtu yoyote asiyehusika kwenda.
"Watu wakae nyumbani watulie wasubiri siku ya mechi (kesho) waende uwanjani kushuhudia," alisema Waziri Mwakyembe mara baada ya msafara wa Everton kuingia kwenye magari tayari kwa safari ya kuelekea Hotelini saa 3:10 asubuhi.
Everton itacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kesho kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

WAZIRI MWAKYEMBE AIPOKEA EVERTON JIJINI DAR LEO


Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akisalimiana na Kiungo Mshambuliaji wa timu ya Everton ya nchini Uingereza, Wayne Rooney muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa J.K. Nyerere, Jijini Dar es salaam asubuhi ya leo. Timu ya Everton ikiwa na kikosi kamili cha wachezaji 46 pamoja na viongozi na kocha mkuu wa timu hiyo Ronald Koeman, Kimewasili mapema leo tayari wa Mchezo wao na Mabingwa wa SpotiPesa Gor Mahia ya nchini Kenya, unaotarajiwa kuchezwa kesho katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.  
ORODHA YA WACHEZAJI WA EVERTON
1 – Jordan Pickford
2 – Morgan Schneiderlin
3 – Leighton Baines
4 – Michael Keane
5 – Ashley Williams
6 – Phil Jagielka
7 – Yannick Bolasie
8 – Ross Barkley
9 – Sandro Ramirez
10 – Wayne Rooney
11 – Kevin Mirallas
12 - Aaron Lennon
16 – James McCarthy
17 – Idrissa Gana Gueye
18 – Gareth Barry
20 – Davy Klaassen
21 – Muhamed Besic
22 – Maarten Stekelenburg
23 – Seamus Coleman
25 – Ramiro Funes Mori
26 – Tom Davies
29 – Dominic Calvert-Lewin
30 – Mason Holgate
31 – Ademola Lookman
33 – Joel Robles
34 – Oumar Niasse
38 - Matthew Pennington
43 - Jonjoe Kenny
46 - Joe Williams
Mshambuliaji wa timu ya Everton Wayne Rooney pamoja na wachezaji wenzake wa wakielekea kwenye basi tayari kwa safari ya kuelekea hotelini kwa mapumziko mafupi. 
Wachezaji wa Everton wakiingia basini.

UTILIAJI SAINI MKATABA WA USHIRIKIANO WA MANISPAA YA MJINI UNGUJA NA JIJI LA POSTDOM WAFANYIKA ZANZIBAR.



Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mjini Zanzibar Abdulrahman Khatib kulia akitiliana saini na Mstahiki Meya wa Postdam Ujarumani Jan Jacob kuhusiana na mkataba wa mashirikiano kati ya Baraza la manispaa ya mjini na Jiji la Postdam la Ujerumani katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.



Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mjini Zanzibar Abdulrahman Khatib kulia wakibadilishana hati baada ya kitiliana saini na Mstahiki Meya wa Postdam Ujarumani Jan Jacob kuhusiana na mkataba wa mashirikiano kati ya Baraza la manispaa ya mjini na Jiji la Postdam la Ujerumani katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar. 
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mjini Zanzibar Abdulrahman Khatib kulia akiwa pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Postdam Ujarumani wakionesha hati walizotiliana saini kuhusiana na mkataba wa mashirikiano kati ya Baraza la manispaa ya mjini na Jiji la Postdam la Ujerumani katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mjini Zanzibar Abdulrahman Khatib akitoa hotuba katika Sherehe ya kusaini mkataba wa mashirikiano kati ya Baraza la manispaa ya mjini na Jiji la Postdam la Ujerumani katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar. 
Mstahiki Meya wa Postdam Ujarumani Jan Jacob akitoa hotuba katika Sherehe ya kusaini mkataba wa mashirikiano kati ya Baraza la manispaa ya mjini na Jiji la Postdam la Ujerumani katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar. 

MAONESHO YA SABASABA 2017: WATU ZAIDI YA 500 WATEMBEELA BANDA LA PSPF, ASILIMIA 70 YA HAO WAJIUNGA NA PSS



Mwanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, akipitia taarifa ya michango yake, baada ya kukabidhiwa na Maafisa wa Mfuko huo, alipotembelea banda la PSPF kwenye maonesho ya 41 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam, leo Julai 12, 2017. Wakati wa maonesho hayo yakitarajiwa kufikia kilele kesho Alhamisi Julai 13, 2017, zaidi ya watu 500 wametembeela banda la Mfuko huo hadi mchana huu na kati ya hao asilimia 70 walifika kujiunga na Mpango wa uchangiaji wa Hiari, (PSS), unaomuwezesha mwananchi yeyote ambaye anafanya kazi za kumuingizia kipato kuwa mwanachama. Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko huo, Bw. Abdul Njaidi, alisema na kuongeza faida za mwanachama kujiunga na PSS, ni pamoja na kupata bima ya afya. (NA K-VIS BLOG/Khalfan Said) 
Afisa Msaidizi wa Uendeshaji wa PSPF, Bw.Mussa Mfaki, (kulia), akimkabidhi kadi ya kujiunga na PSPF kupitia Mpango wa uchangiaji wa Hiari, PSS, Bi.Damare B. Nampwani, leo Julai 12, 2017.
Bi.Damare B. Nampwani, akionyesha kadi yake baada ya kukabidhiwa.
Mwananchi akijaza fomu ya lujiunga na PSPF kupitia Mpango wa PSS, huku Mwanasheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti MHifadhi ya Jamii, (SSRA), Bi.Imani Masebu, (kulia), na Mhandisi Ally Shanjirwa, (katikati), wakishuhudia.
Mwananchi akionyesha dole gumba baada ya kujaza fomu.

Mwananchi akijaza fomu.
Afisa Michango wa PSPF, Bw. Noah Amri, akiwa kwenye mashine ya kutoa vitambulisho vya papo kwa hapo.
Afisa Uhusiano wa PSPF, Bi. Coleta Mnyamani, (kulia), akimkabidhi kadi ya uanachama ya PSPF, Afisa wa Polisi wa Usalama Barabarani, David S.Mlilo.
Afisa Uhusiano wa PSPF, Bi. Coleta Mnyamani, (kulia), akimkabidhi kadi ya uanachama ya PSPF, Afisa wa Polisi wa Usalama Barabarani, Salvatory A. Chacky.
Moja ya faida azipatazo Mwanachama wa PSPF,ni kuwa na uwezo wa kukopa kiwanja cha ujenzi wa nyumba na hapa ni Afisa Mipango Miji kutoka kampuni mshirika ya Adhi Plan Limited, Bi. Anna Lukando, (kulia), akimpatia maeelzo ya jinsi gani mwanachama anaweza kupata mkopo wa kiwanja au kununua kabisa.
Hiki ndio kikosi kazi cha PSPF ambacho kwa takriban wiki moja na nusu kimekuwa kikitoa huduma kamambe kwenye banda la Mfuko huo kwenye jengo la Wizara ya Fedha na Mipango kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, ambako kumekuwa na maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Kutoka kushoto waliosimama ni Isack Kimaro, Mussa Mfaki, Chaula Miteko, Mhandisi Ally Shanjirwa, Abdul Njaidi, Noah Amri,Win-God, Bw.Msina. Waliokaa kutoka kushoto, ni Bi. Coleta Mnyamani, Bi. Mariam Saleh, Bi. Irine Musetti na Bi. Asmahan H.Haji.
Win-God, (kushoto), Afisa wa uendeshaji msaidizi wa PSPF, akiwahudumia wananchi waliofika banda la Mfuko huo leo Julai 12, 2017. 

Afisa Uendehsji wa PSPF, Bw. Isack Kimaro, (kulia), akiagana na Mwananchi huyu aliyefika kupatiwa huduma
Afisa Uendeshaji wa PSPF, anayeshughulikia Mpango wa Uchangiaji wa Hiari, (PSS), Bi. Asmahan Haji (kulia), akimsaidia mwanachama huyu wa PSPF kuelewa michango yake. 

WATEJA WAFURAHIA TECNO DUDE


Baada ya mzigo mpya kutoka Tecno kuingizwa mtaani kwaajili ya Watanzania wiki moja iliyopita baadhi ya watumiaji wa bidhaa hiyo warudisha majibu mazuri kwa angle tofauti tofauti kuhusiana na simu hiyo #TecnoDude kwa uzoefu waliyoupata katika kipindi hiki kifupi toka wainunue.
Hawa ni baadhi ya wateja wanafamilia wa #TecnoDude #TecnoWashaDude wakijidaiya mambo waliyoyakuta ndani ya simu hiyo kupitia mitandao yao ya kijamii hususan Instagram na  Facebook. 
Wateja mbali mbali wakifurahia sim mpya kutoka Tecno Toleo liitwalo " Wx3Lte" yenye uwezo mkubwa wa 4g, camera na memory ya kutosha. Maarufu kwa jina la "TecnoDude" simu hii inapatikana maduka yote ya  Vodacom nchini @sanchosong @jrjunior5 @eric_mkomoye #tecnodude #tecnowashadude

MASHINE YA KUZALISHA MKAA MBADALA UTOKANAO NA TAKATAKA YATENGENEZWA


 Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Kujanakushoka Tools Manufactures Group Bw. Leonard Kushoka (kushoto) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitambulisha mashine ya kuzalisha mkaa mbadala utokanao na takataka, kulia ni mmoja ya wafanyakazi wa kampuni hiyo Bi. Zainabu Mtiga.
blu2
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Kujanakushoka Tools Manufactures Group Bw. Leonard Kushoka wakati akitambulisha mashine ya kuzalisha mkaa mbadala utokanao na takataka mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
blu3
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Kujanakushoka Tools Manufactures Group Bw. Leonard Kushoka akielekeza waandishi wa habari (hawapo pichani) namna mashine inavozibadili takataka na kuwa nishati ya mkaa mbadala.

Sunday, July 9

WAZIRI DKT. MPANGO AHIMIZA UCHUMI WA VIWANDA KATIKA MAONESHO YA SABASABA


 Afisa Mwandamizi wa Idara ya Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adam Msumule akitoa elimu ya Bajeti kwa wananchi waliotembelea katika banda la Wizara hiyo katika maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipeana mkono na Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. LU Youqing, walipokutana katika viwanja vya Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara (sabasaba), Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia) akitoa maelekezo kwa wafanyakazi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuhusu namna ya kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kukata bima ili kujikinga na majanga, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango lilipo katika viwanja vya maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara (sabasaba), Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Bw. Sam Kamanga.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akisikiliza maelezo ya Mkurugenzi wa uendeshaji wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), Naftal Sigwejo baada ya kuulizwa kuhusu ubora wa baadhi ya bidhaa zinazotolewa Serikalini baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akimpongeza Mzazi wa kijana Msuya Mageta (katikati) aliyejiunga na Mfuko wa Pensheni wa PPF kupitia mpango wa Wote Scheme katika Banda la Wizara ya Fedha na Mipango kwenye Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa saba kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mfuko wa Pensheni wa PPF baada ya kutembela Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia) akiwa tayari kupokea fomu ya kujiunga kupitia mfumo wa uchangiaji wa hiari kupitia Mfuko wa Pensheni wa PSPF kutoka kwa Msanii Mrisho Mpoto baada ya kutembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipata maelezo kutoka Mfuko wa Pensheni wa GEPF kuhusu huduma na mchango wa mfuko huo katika maendeleo ya viwanda, alipotembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipata maelezo kutoka  Banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuhusu njia ya kisasa ya ufugaji Samaki alipotembelea Banda hilo katika Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akimpongeza mtumishi wa Suma JKT baada ya kutoa maelezo ya mtambo wa kuvuta maji katika viwanja vya maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)

NDOTO YA MWALIMU YATIMIA, LUGHA YA KISWAHILI LULU YA AFRIKA


Na Judith Mhina - MAELEZO

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muasisi aliyeenzi lugha adhimu na tamu ya Kiswahili na anastahili tuzo maalum kwa kutambua umuhimu wa lugha  hiyo katika kuleta umoja, mshikamano, na maendeleo barani Afrika.

Mwalimu kwa kutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili, alianza kuweka mfumo wa matumizi ya lugha hiyo katika utendaji wa serikali, jamii nzima ya Tanzania na Umoja wa Afrika. Aidha, sera za Tanzania za kushiriki katika kupigania Uhuru wa nchi kadhaa za Afrika na uwepo wa wakimbizi nchini kwa idadi kubwa imewezesha lugha hii kuvuka mipaka na kuenea kote kusini mwa Afrika.

Mwalimu amepata wapiganaji mahiri wa lugha ya Kiswahili ambao wapo wengi, lakini kwa uchache makala yangu itaangazia viongozi yaani, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, na Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano, Marais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Rwanda, Paul Kagame, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila na Jemedari wa kuenzi lugha ya Kiswahili anayeifanya lugha hii kuwa Lulu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli. 

Mtakubaliana nami mchango wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi katika kutumia lugha ya Kiswahili fasaha, katika shughuli zote za Serikali na za kijamii zilisukuma mwamko wa gurudumu la kiswahili kusonga mbele haswa kwa wale wanaodhani lugha za kigeni ni bora kuliko lugha yao.

Mwinyi, alipata ushirikiano wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kutoka kwa Marais walio wengi wa Afrika Mashariki ambao kwa njia moja au nyingine walikaa Tanzania wakati wa kupigania uhuru wa nchi zao au kama wakimbizi wakati wa machafuko katika nchi husika.

Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhesimiwa Joachim Arbeto Chisano ni kati ya wapigania uhuru ambao waliishi nchini Tanzania kwa miaka kadhaa na kufanikiwa kufahamu Kiswahili, alithibitisha hili alipohutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kwa Kiswahili kwa mara ya kwanza alipokuwa akifunga mkutano huo na kumaliza muda wake wa kuwa mwenyekiti wa Umoja huo Julai 2004 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Amini usiamini huu ukawa ni mwanzo wa lugha za kiafrika kutumika katika mkutano mkubwa wa viongozi wa Umoja wa Afrika yaani Kiswahili ambapo Mwalimu Nyerere alilitamani siku zote kwa kusema: “Sio kama lugha za kigeni ni nzuri kuliko za kwetu bali ukoloni mamboleo ndio umetufikisha hapa”

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ambaye ameishi na kusoma Tanzania, anafahamu lugha ya Kiswahili na mara zote anapokuwa Tanzania mara nyingi hutumia lugha adhimu na pendwa ya Kiswahili kuonyesha ubora na umuhimu wa lugha hiyo katika masuala ya serikali, siasa, kijamii, udugu na katika ujirani mwema.

Rais Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pia ni miongni mwa wasomi na walioishi Tanzania kwa miaka mingi, ambapo Kiswahili chake hakina tofauti na Mtanzania yeyote kwa ufupi kama humjui utasema huyu Mtanzania ametoka wapi huku Kongo – DRC.

Rais Kabila amekuwa akipendelea kutumia lugha hiyo adhimu yenye utajiri wa maneno, nyepesi kujifunza na kueleweka kutokana na matamshi yanaelekeza jinsi ya kutamka silabi moja kwa moja tofauti na baadhi ya lugha ambazo matamshi huwa yanapishana na maandiko ya lugha husika.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ni mtaalamu mzuri wa lugha ya Kiswahili ambaye ameipamba lugha hiyo kwa kuona umuhimu wa elimu itolewayo nchini kwake, ijumuishe lugha ya Kiswahili kama somo, ili kuwaunganisha Wanyarwanda na wanajumuia ya Afrika Mashariki kwa ukaribu zaidi.

Kagame anastahili pongezi kwa kuweka mitaala ya Kiswahili na kutoa fursa kwa walimu kutoka Tanzania,  kufundisha lugha hiyo tangu shule za msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu. Rais huyo ametambua njia rahisi ya kuwaunganisha wana Jumuia ya Afrika Mashariki, aghalabu atumie filosofia ya Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere kwa kuleta mshikamano, umoja wa wananchi katika kunufaika na soko la pamoja la Jumuia na kuleta maendeleo kwa ujumla. 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila ni mdau mkubwa wa lugha ya Kiswahili ambapo amewezesha wafanyabiashara na wanamuziki wengi kutoka nchini kwake wanaongea lugha ya Kiswahili na kuiimba kwa ufasaha. Kama tujuavyo muziki ni tasnia muhimu sana katika upelekaji wa ujumbe aidha, wa kuunganisha au kubomoa, hivyo lugha ya Kiswahili ikitumika vizuri katika mataifa ya kiafrika kama ilivyo sasa tunafanya biashara na kuendeleza tasnia ya muziki kwa faida ya nchi zetu.

Kwa kuwa nimeitaja tasnia ya muziki japo sio kiongozi wa nchi, ni vema nikaeleza umuhimu wake katika matumizi ya lugha yetu ambaye ni mwana Diplomasia wetu kupitia muziki Naseeb Abdul au kwa jina maarufu Diamond Platnum. Mwanamuziki huyu ni miongoni mwa wasanii wanaopenyeza lugha ya Kiswahili katika nchi zote ambazo muziki wake unapigwa. Mfano nitapenda kuwa shuhuda kwa kuonyesha wanamuziki kutoka nchini Nigeria anaoshirikiana nao katika kuimba nyimbo zake au zao na kufanya Kiswahili kitumike sana katika muziki wa Afrika Magharibi.

Binafsi nimekutana na Wacameroon waliofika nchini kwa masuala ya utalii nikashangaa wanapenda sana nyimbo za Naseeb Abdul na kupata wasaa wa kuchambua maneno anayoimba kwa Kiswahili na wanaelewa maana yake, hivyo ni vema balozi huyu akatambua mchango wake  wa lugha kwa ufasaha na usahihi katika uimbaji na kufika ujumbe utakaochangia kuleta umoja, mshikamano na maendeleo barani Afrika. Hii ina maana Naseeb Abdul atakuwa ni mwalimu mzuri wa lugha ya Kiswahili.

Msumari wa mwisho katika wapiganaji na viongozi wa lugha ya Kiswahili katika makala yangu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli anavyoithamini na kuijali kwa hali ya juu lugha ya Kiswahili. Rais ameleta msisimko wa pekee na kuwafanya hata viongozi wengine barani  Afrika ambao walikuwa wanaona lugha ya Kiswahili “si mali kitu iwe mali kitu”.

Pengine viongozi hao wametambua filosofia ya Mwalimu Nyerere ya kuleta umoja na kuunganisha wananchi kwa kutumia lugha, kuwa na uelewa wa pamoja na masikilizano katika nchi, pia katika kunufaika na soko la pamoja la Jumuia na kuleta maendeleo kwa wananchi, ambapo Rais Magufuli amelitambua hilo mapema.

 Magufuli amekuwa akitumia muda wake wote katka kuwatumikia wananchi wa Tanzania, kila mara  afanyapo chochote kile, huwaita wanahabari na kuhakikisha tukio hilo analiwasilisha kwa lugha ya Kiswahili ili kueleweka kwa Watanzania wote. Hii inafanya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ya uwazi    zaidi pia, kueleweka kwa wananchi wote nini anafanya, hili ni suala muhimu sana katika uongozi bora.

Hakika mwenye macho haambiwi tazama, utakubaliana nani Rais amepaisha lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa kwa uamuzi wake wa kutumia lugha ya Kiswahili, kila anapokwenda iwe kwenye mikutano ya taifa au ya kimataifa, hivi karibuni pale Addis Ababa Ethiopia alihutubia kwa Kiswahili.

Aidha, kutokana na utendaji wa Rais na  Serikali ya Awamu ya Tano uliotukuka, kazi zote anazofanya husambaa dunia nzima na kila kiongozi anayeifikiria Tanzania kwa sasa anaona umuhimu wa kujua lugha ya Kiswahili kwa kuwa Rais ameishikia bango na ndiyo anayoitumia kuwafafanulia jambo wananchi.

Matokeo ya bango la Rais Magufuli kutumia lugha ya Kiswahili imezaa ajira lukuki za kufundisha lugha hiyo nchini Ethiopia, Rwanda, Afrika ya Kusini, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambazo ni rasmi. Pia kuna ajira za kufundisha lugha ya Kiswahili sehemu mbalimbali duniani kwenye vyuo vya kimataifa ambapo Watanzania wako huko hizi ni zile ambazo sio rasmi.

Huu ni uthibitisho tosha kuwa Mwalimu Nyerere alilitambua hili na hakika amepata wapiganaji sahihi wakiongozwa na Dkt Magufuli, hakika wanastahili pongezi na daima wanakuenzi,   “Pumzika kwa Amani Mwalimu”.
Lugha ya Kiswahili kwa sasa inatumika katika nchi zote za Afrika Mashariki, Kati na Pembe ya Afrika, yaani Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Malawi, Burundi, Somalia, Msumbiji, Zambia, visiwa vya Comoro na Mashariki mwa Kongo. Hivyo zaidi ya  watu milioni 150 kwa sasa wanaongea Kiswahili hii ni neema kwa Tanzania.

Azimio la kuteuliwa kwa Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi na ya kazi ya Umoja wa Afrika lilifanyika huko Durban, Afrika Kusini tarehe 9 – 11 mwezi Julai mwaka 2002 wakati wa kikao hicho chini ya Uenyekiti wa Rais Levy Mwanawasa (aliyekuwa Rais wa Zambia)

KIJANA MJASILIAMALI AIOMBA SERIKALI IZITAMBUE BIDHAA ZA MBAO ILI APATE KIWANDA


Na Karama Kenyunko-Globu ya Jamii

, Mjasiliamali anayejihusisha na utengenezaji wa extension za Umeme kwa kutumia mbao, anaiomba Serikali izitambue bidhaa za mbao ili apate kiwanda kikubwa ambacho kitamuwezesha kutoa ajira kwa vijana na bidhaa hizo kufika hadi nje ya nchi.

Charles Antoni Sanga, ambaye ni mwafrica wa kwaza kugundua ujuzi wa kupitisha umeme kwenye mbao, ameongea hayo katika maonyesho ya 41 ya biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema, upitishaji wa Umeme kwenye mbao ni bora na siyo rahisi kusababisha shoti ya Umeme, pia ujuzi huo unatoa fursa kwa kuwainua wajasiliamali wanaochaji simu vibandani.

"Ninahamasidha kauli mbiu ya Mh.Rais kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana sababu kuna vitu tunavyobuni watanzania ambayo ni imara kuliko vile vya kutoka nje ya nchi".

Aidha ameiomba Serikali na wadau mbali mbali wanaopenda bidhaa hizo za mbao kujitokeza na kumuinua kwani anafanya kazi katika mazingira magumu kwani hata TBS walimuagiza kuwa awe na karakana na machine Au hata jengo lakini hana chochote kwani hana fedha za kumuwezesha kuwa na vifaa hivyo.

Akielezea safari yake ya iliyomfikisha hapo anasema, alikuwa akiishi bila ya kipato chochote ndipo akaamua kubuni kitu ambacho hajawahi kukiona mahali popote ndipo akaja na wazo la extension ya mbao.

Anasema, alipokamilisha moja, watu wengi walivutiwa nayo ndipo akaamua kutengeneza kwa oda hiyo ilikuwa mwaka 2012 ambapo baadae alishiri maonyesho ya SIDO nyanda za juu kusini, huko alikutana na viongozi kutoka nchi mbali mbali wakiwemo TBS ambao walishangaa ubunifu huo ambao hawakuwa wameuona mahali popote duniani.

Sanga anaongeza, TBS walimshauri kwenda Tume ya Sayansi yabTeknolojia ili wachunguze kama bidhaa hiyo ipo mahali popote duniani lakibi haikuonekana mahala popote na kumfanya awe Mwafrica wa kwanza kupitisha umeme kwenye mbao.

Anasema, baada ya uchunguzi alifanikiwa kupata cheti cha ugunduzi (Patent) kwenda kwa mwanasheria Mkuu wa ugunduzi ambaye alisubiri pingamizi kwa muda wa miaka miwili lakini hakukuwa na pingamizi.

Sanga anawaomba wadau wajitokeze na kumuunga mkono ili aweze kutoa ajira kwa vijana hali kadhalik serikali imsaidie kuwezesha jambo hilo.
 Mgunduzi wa Soketi ya Mbao Charles Sanga akieleza Kwa Makini jinsi alivoweza kutengeneza Soketi hizo
 Charles Sanga akionesha moja ya Soketi aliyoitengeneza

STAMICO SASA KUMEKUCHA NA MAKAA YA MAWE


· Yaanza kuuza makaa hayo kwa kasi
· Yakiri kuwa na akiba ya makaa ya mawe ardhini ya kuchimba kwa zaidi ya miaka mia moja. 

Na Koleta Njelekela-STAMICO

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza rasmi kuuza makaa ya mawe yanayozalishwa katika Mgodi wake wa Kabulo ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wakiwemo viwanda vya saruji na nguo na hivyo kukuza Pato la Taifa.

STAMICO ilianza uzalishaji wa majaribio wa makaa ya mawe katika mgodi wa Kabulo uliopo Kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe mnamo tarehe 30 Aprili 2017 na mpaka sasa imeweza kuzalisha tani 6,197.

Akihojiwa na Mwandishi wa Habari hii, mara baada ya zoezi la uuzaji makaa ya mawe kuanza rasmi huko Kabulo jana (6 Julai 2017), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bwana Hamis Komba, amesema Shirika kupitia mradi wake wa makaa ya mawe wa Kabulo, sasa linaweza kukidhi mahitaji ya watumiaji wote wa makaa ya mawe nchini, katika kipindi cha miaka mia mfululizo kutokana na kuwepo kwa mashapo ya kutosha (mineral resources) na nyenye ubora wa juu katika mgodi huo.

Bwana Komba amesema matarajio ya Shirika ni kuongeza kiwango cha uchimbaji makaa ya mawe kutoka tani 600 hadi tani 1000 kwa siku, hatua ambayo itaiwezesha STAMICO kuzalisha zaidi ya tani 300,000 kwa mwaka. 

“Nchi yetu ina rasilimali nyingi za madini yakiwemo makaa ya mawe, hivyo tunapenda kuwahikishia wenye viwanda vinavyotumia makaa hayo hususani viwanda vya Saruji (Cement), kwamba nchi ina makaa ya kutosha hivyo Serikali haitoshindwa kutosheleza mahitaji na makaa yam awe huku ikitekeleza kwa vitendo azma yake kujenga Tanzania yenye viwanda, ili kukuza uchumi wa Taifa" Alifafanua Bwana Komba.

Amewataka wenye viwanda nchini, kuwasilisha maombi ya kununua malighafi ya makaa ya mawe, ili STAMICO iweze kuwauzia makaa hayo, ambayo yana viwango vya ubora vinavyofaa katika uzalishaji wa nishati ya umeme viwandani. 

Aidha Kiongozi Mtendaji Mkuu wa STAMICO amesema hivi sasa Shirika linaendelea kuimarisha mradi huo wa Kabulo, kwa kuboresha miundombinu, maabara ya kudhibiti ubora wa makaa na kununua mashine mpya (Crusher) kwa ajili ya kuponda makaa, kulingana na mahitaji mahususi ya vipimo vinavyhitajiwa na wateja katika soko.

“changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mradi huu ni pamoja na mtaji mdogo, mabadiliko ya hali ya hewa hasa nyakati za mvua na ubovu wa kipande cha barabara yenye urefu wa zaidi ya kilomita 15 kutoka katika eneo la mgodi, mpaka eneo la mauzo, ambapo barabara hiyo haiwezi kumudu malori ya zaidi ya uzito wa tani 15 kupita”. alibainisha Bwana Komba.

Awali Mratibu wa Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo-Kiwira Bwana Alex Rutagwelela, amesema amefurahishwa na matokeo chanya ya mradi huo ya kufikia hatua ya uuzaji makaa ya mawe, kwani ni fursa nzuri kwa Shirika, baada ya Serikali kuweka zuio la kuagiza makaa ya mawe kutoka nchi za nje; wakati nchi ikiwa na makaa mengi ya mawe ardhini.

Amesema STAMICO kupitia mradi huo, itaendelea kuimarisha viwango vya uzalishaji wa makaa ya mawe ili kuwafikia wateja wote kulingana na mahitaji yao

“Uwezo wetu na utaalam katika uchimbaji makaa ya mawe ni wa kimkakati ili kuweza kukidhi soko la ndani na nje ya nchi. Lengo kuu la mradi huu ni kutosheleza mahitaji ya kuzalisha umeme wa viwango mbalimbali katika Mradi wa Umeme wa Kiwira na pia kutosheleza mahitaji ya Viwanda nchini vikiwemo vya saruji.”

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa STAMICO, Bwana Deusdedith Magala amewasihi watumishi na wataalam wa Shirika hilo, kuendelea kujifunga mkanda na kufanya kazi kwa bidii ili kuivusha salama STAMICO katika kipindi hiki cha mpito, ambapo Shirika linafufua miradi yake ya uchimbaji madini; itakayoleta mafanikio makubwa na yenye maslahi mapana kwa Taifa.

Bwana Magala amesema STAMICO imeweza kuanza uzalishaji wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo kwa kutumia mtaji mdogo na kubana matumizi; hatua ambayo imedhihirisha kwamba STAMICO tumethubutu na tunaweza kutekeleza miradi yetu kwa wakati, pamoja na hali ngumu ya kifedha inayolikabili Shirika kwa sasa.

“ni matumaini kuwa katika kipindi cha muda mfupi ujao, watumishi wote STAMICO tutafurahi, kwani tutaweza kupanua uzalishaji wa makaa ya mawe huku tukileta matokeo makubwa ya uzalishaji yenye maslahi makubwa kwa Shirika” Alifafanua Bwana Magala.

Awamu ya kwanza ya Mradi wa uchimbaji makaa ya mawe wa Kabulo inatekelezwa kupitia leseni zake mbili za uchimbaji mdogo wa madini Primary Mining Licences (PMLs) zilizopo ndani ya leseni ya utafiti ya Kabulo zenye ukubwa wa Hecta 16.52. 

Leseni hizo mbili za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo, zina zaidi ya tani milioni 35 zilizothibitishwa za mashapo ya makaa ya mawe, yaliyoko karibu na uso wa ardhi, katika mgodi huo wa Kabulo. 

Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka akiwa katika picha ya pamoja na timu wa wataalam wa STAMICO (wanaotekeleza Mradi wa Uchimbaji Makaa ya Mawe-Kabulo) alipotembelea Mgodi huo hivi karibuni kukagua maendeleo ya mradi huo ambao ulianza rasmi uzalishaji makaa yam awe tarehe 30 Aprili, 2017 na kufanikiwa kuzalisha tani 6197 mpaka sasa. Soko la ndani la makaa hayo linawalenga wazalishaji viwandani hususani wale wa viwanda vya Saruji (Cement) na watengenezaji wa nguo, pamoja na magereza na watumiaji wengine wa majumbani.

Shughuli za Uchimbaji Makaa ya Mawe zikiendelea katika mgodi wa Kabulo Kiwira, uliopo katika Kijiji cha Kapeta, wilaya ya Ileje, Mkoa wa Songwe. Leseni za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo, zina zaidi ya tani milioni 35 zilizothibitishwa za mashapo ya makaa ya mawe, yaliyoko karibu na uso wa ardhi, katika mgodi huo wa Kabulo. Mashapo hayo yanaweza kuchimbwa kwa mfululizo kwa miaka mia moja ijayo.

Mratibu wa Mradi wa Uzalishaji Mkaa ya Mawe wa Kabulo-Kiwira Bwana Alex Rutagwelela ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa STAMICO akielekeza kuhusu zoezi zima la upakiaji makaa ya mawe katika Malori tayari kwa ajili ya kupeleka katika eneo la mauzo lililopo katika kijiji cha Kasumulu, Wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya. Mgodi huo wa Kabulo-Kiwira uliopo katika kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe unamilikiwa na kuendeshwa na STAMICO kwa niaba ya Serikali.
Malori ya Kampuni ya Lake Cement yakipakia Makaa ya Mawe katika eneo la mauzo ya makaa hayo, lililopo umbali wa kilometa mbili kutoka katika barabara kuu ya Mbeya, iendayo nchini Malawi. Eneo hilo la mauzo lipo katika kijiji cha Kasumulu, Wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya. Makaa hayo ya Mawe yanazalishwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), katika mgodi wake wa Makaa ya Mawe wa Kabulo, ulipo katika kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe.