Saturday, December 2

Zimbabwe: Mnangagwa atangaza baraza jipya la mawaziri

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametangaza baraza lake jipya la mawaziri. Maafisa wakuu wa jeshi na makada wa chama tawala cha ZANU PF ndio wamepewa nafasi katika baraza hilo lenye mawaziri 22.

Simbabwe Emmerson Mnangagwa in Harare, 2014 (picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi)
Wakosoaji  nchini Zimbabwe wanasema fungate fupi baada ya harusi imemalizika na ukweli wa mambo sasa unadhihirika, kilichotarajiwa ni kwamba Rais Emmerson Mnangagwa angelichanganya baraza lake, lakini kuna ishara chache mno za mabadiliko. Akizungumza na waandishi habari muda mfupi kabla baraza jipya la mawaziri kutangazwa, kiongozi mkuu wa upinzani Morgan Tsvangirai alisema Mnangagwa alikuwa na nafasi ya kuonyesha kuwa yeye ni tofauti na Mugabe lakini hapakuwepo na majadiliano yoyote baina yao na uongozi huo mpya.
Ishara haba za mabadiliko
Tsvangirai anasema hakuna mabadiliko hadi sasa na jambo ambalo linatia wasiwasi ni jinsi rais mpya alivyoanza. Tsvangirai amesema kuna wasiwasi juu ya msingi anaojaribu kuuweka rais huyo mpya wa Zimbabwe katika kuyashughulikia mambo na kutoa mpango madhubuti wa kufufua uchumi.
Morgan Tsvangirai kiongozi mkuu wa upinzani wa Zimbabwe (Getty Images)
Kiongozi mkuu wa upinzani wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai
Mnangagwa amemchagua meja jenerali Sibusiso Moyo, kamanda wa jeshi ambaye wiki mbili zilizopita alitangaza kwenye televisheni hatua ya wanajeshi ya kuingilia kati baada ya nchi hiyo kukabiliwa na mkwamo wa kisiasa hatua ambayo hatimaye wiki iliyopita ilisababisha kuufikisha mwisho utawala wa kiongozi maarufu wa zamani wa nchini Zimbabwe Robert Mugabe. Rais huyo mpya pia amempa nafasi ya uwaziri wa ardhi na kilimo jemadari Perrance Shiri aliyehudumu kwa muda mrefu kwenye kikosi cha jeshi la anga la Zimbabwe.
Chinamasa arejea katika wizara ya fedha
Kulingana na taarifa zilizotolewa rais Mnangagwa hata hivyo amewabakisha mawaziri wachache kutoka kwenye baraza la zamani la aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe miongoni mwao ikiwa ni Patrick Chinamasa ambaye amerudishwa kuhudumu kama waziri wa fedha, wizara aliyokuwa anaishikilia kabla ya kuondolewa wakati Mugabe alipofanya mabadiliko katika baraza la mawaziri manamo mwezi Oktoba.
Meja jenerali Sibusiso Moyo wa jeshi la Zimbabwe (Reuters/ZBC)
Meja jenerali Sibusiso Moyo
Chris Mutsvangwa kiongozi wa mashujaa katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe za mwaka 1980 na aliyeongoza katika juhudi za kumlazimisha Mugabe aachie madaraka ndiye waziri mpya wa habari. Hata hivyo rais Mnangagwa hakuwajumuisha wapinzani katika baraza hilo la Mawaziri.
Wakili mmoja ambaye pia ni mkosoaji Alex Magaisa aliweka kwenye mtandao wake wa Tweeter picha ya rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe na mkewe Grace wakiwa wanacheka pamoja na ujumbe wa maneno uliosema "pale walipoliona baraza la mawaziri”.
Biti: Kipindi cha fungate kimekwisha
Naye aliyekuwa zamani waziri wa fedha Tendai Biti ameandika ujumbe kwenye Tweeter uliosema kipindi cha fungate kimekwisha hata kabla hakijaanza na kumalizia kwa kusema "Ni aibu! Ni sawa na kupoteza nafasi adimu”.
Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 75, aliapishwa Ijumaa iliyopita baada ya matukio makubwa katika nchi hiyoya kusini mwa Afrika pale jeshi lilipoidhibiti nchi ya Zimbabwe na kusema walitaka kuwakamata wahalifu katika serikali waliokuwa wanamzunguka Mugabe mwenye umri wa miaka 93.

Je ni nini lengo la Kim Jong Un wa Korea Kaskazini kwa Marekani?

Korea kaskazini inadai kuwa makombora yake yanaweza kufikia kila kona ya Marekani. Lakini je hilo ndilo analolitaka kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un?

Nordkorea Kim Jong-Un (Getty Images/AFP/STR)
Lengo lake pekee ni kudhibiti mamlaka yake madarakani, anasema, Jürgen Hanefeld anayeongoza ofisi ya mashariki mwa Asia ya kituo cha umma cha Ujerumani ARD huko mjini Tokyo nchini Japan. 
Miaka minne iliyopita wakati Kim Jong Un alipotangaza kwamba mpango wa makombora wa Korea Kaskazini utakamilishwa mwishoni mwa 2017, hakuna mtu aliyemsikiliza. Alichukuliwa kama ni mwenda wazimu au mtu asiyetabirika. Wengine walipuuza uwezo wake wa kutawala, wakijiuliza kwa muda gani angeweza kuwa mamlakani?
Na Kim alipotangaza kwamba Korea ya Kaskazini inaelekea kuwa na silaha za nyuklia miaka miwili baadaye, na kwamba alikuwa tayari kuongea na Marekani kuhusu upunguzaji wa silaha za kivita, kila mmoja alimcheka.
Hata hivyo, sasa vicheko vimepungua na kila mtu anapaswa kukabiliana na ukweli kwamba jamaa huyo anapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
Siku ya kihistoria?
Jürgen Hanefeld (NDR/Christian Spielmann)
Jürgen Hanefeld anayeongoza ofisi ya mashariki mwa Asia ya kituo cha umma cha Ujerumani ARD huko Tokyo
Bila shaka hakuna mtu anayejua kama makombora yake yanaweza kuisambarisha miji ya New York au Washington, DC. Lakini je tunataka kujua kweli?
Je, si itakuwa jambo la maana zaidi kutathmini hatari badala ya kukubali? Kwa hatua hii hatuwezi kujua kama jaribio la kombora la Jumatano itakumbukwa kama siku ya kihistoria lakini inawezekana.
Korea Kaskazini imejitangaza yenyewe kuwa na nguvu za nyuklia! Hiyo sio maana tu ya tishio kubwa, pia inatoa fursa.
Kila mtu anajua kwamba hata kama makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini yanaweza kugonga mahali popote Marekani, wangeweza tu kufanya mara moja.
Baada ya hapo hapatakuwa na Pyongyang tena, wala Korea kwa jambo hilo - Kaskazini au Kusini.
Kwa hiyo Kim anataka nini? Anataka tu kujikinga. Anataka kudhibiti mamlaka yake madarakani. Na hiyo ndiyo sababu anataka kukutana na Marekani kama taifa lenye nguvu sambamba na Marekani.
Na sio Korea Kusini, nchi ambayo Marekani inaidhibiti angalau kijeshi.
Na sio na china ambayo imekuwa ikiiunga mkono na kusitasita ikizingatia maslahi yake ya kiuchumi na mikakati wa umuhimu wa eneo hilo kwa China.
Hapana, Kim dhidi ya Donald Trump ni mchezo ambao Korea Kaskazini inawekeza fedha zake.
Hii ni kuhusu amani
Mtu anaweza kudhani ni kiburi lakini inaonekana kwa mtamazo mwengine, hakuna njia nyingine mbadala.
Trump hana uwezo wa kufanya kitu chochote – haijalishi ndege ngapi za kivita anazituma na licha ya faida kubwa ya kijeshi ya nchi yake - isipokuwa kama yuko tayari kuiweka Korea Kusini hatarini na hatimaye kusababisha kitisho cha kutokea kwa vita vya dunia ya tatu.
Je si ingekuwa bora angeweka kando kiburi chake kama rais wa marekani angeketi chini na kuzungumza na Kim badala ya kutumia mtandao wa Twitter?
Haitokuwa mara ya kwanza kwamba rais wa Marekani anakaa chini na viongozi dikteta ili kuwashawishi wajirekebishe.
Mara nyingi mikutano hiyo na viongozi hao ni kuhusu mafuta, silaha au fedha. Wakati huu ni juu ya jambo muhimu zaidi: Amani.

Utafiti: Upara na nywele za kijivu ni ishara za magonjwa ya moyo

'Upara na nywele za kijivu ni ishara za magonjwa ya moyo'
Image caption'Upara na nywele za kijivu ni ishara za magonjwa ya moyo'
Wanaume wanaokuwa na upara kichwani mbali na wale wenye nywele za rangi ya kijivu wako katika hatari kubwa ya kupatikana na magonjwa ya moyo miongoni mwa wanaume walio chini ya umri wa miaka 40, utafiti unasema.
Utafiti uliofanyiwa zaidi ya vijana 2000 nchini India ulionyesha kuwa wengi waliokuwa na ugonjwa wa moyo walikuwa na upara na nywele za kijivu ikilinganishwa na wanaume walio na nywele kichwani.
Utafiti huo wa Idara ya magonjwa ya moyo barani Ulaya utasomwa katika kongamano la kila mwaka la magonjwa ya moyo nchini India.
Lakini wakfu wa Uingereza unaosimamia magonjwa ya moyo umesema kuwa sababu nyengine hatari pia ni muhimu.
Daktari Mike Knapton, aliambia BBC: Utafiti huu unasema kuwa miongoni mwa wanaume wenye upara na nywele za kijivu unaweza kuwagundua wale walio na hatari ya matatizo ya magonjwa ya moyo.
Hatahivyo hilo sio jambo ambalo linaweza kubadilishwa na watu, wakati ambapo unaweza kudhibiti hali ya maisha mbali na sababu zinzoweza kuhatarisha maisha kama vile viwango vya juu vya mafuta na shinikizo la damu.Hivi ni vitu muhimu zaidi kufuatilia.

Hawaii yafanyia jaribio king'ora cha kuonya shambulizi la nyuklia

A tsunami warning tower in between palm trees at Kakaako Waterfront Park in Honolulu, Hawaii, November 28, 2017Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionHawaii yafanyia jaribio king'ora cha kuonya kuhusu shambulizi la nyuklia
Kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa vita baridi jimbo la Hawaii nchini Marekani limefanyia jaribio king'ora cha kuonya kuhusu shambulizi la nyuklia
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya jaribio la kombora la masafa marefu lililofanywa na Korea Kaskazini mapema wiki hii.
Hawai kawaida ina ving'ora ambavyo huonya kuhusu majanga ya asili kama tsunami.
Kingora cha nyuklia kina mlio tofauti ambacho huwaonya watu kusalia manyumbani wakisubiri ushauri zaidi.
Lakini king'ora hicho kilisikika tena Ijumaa na kitarudiwa klila jumatatu ya kwanza ya mwezi.
Kombora linalorushwa kutoka Korea Kaskazini linaweza kushambulia Hawaii ndani ya dakika 20 baada ya kufyatuliwa.
Hivi majuzi Korea ilifyatua kombora mpya la masafa marefu ambalo inadai kuwa linaweza kushambulia ndani ya Marekani.
Map locator
Image captionKombora linalorushwa kutoka Korea Kaskazini linaweza kushambulia Hawaii ndani ya dakika 20

Panya na mende ni tatizo Ikulu ya White house Marekani

Panya na mende ni tatizo kubwa katika ikulu ya Whotehouse nchini Marekani
Image captionPanya na mende ni tatizo kubwa katika ikulu ya Whotehouse nchini Marekani
Panya, mende, wadudu na vyoo vilivyovunjika ni miongoni mwa vitu vingi vilivyoripotiwa kwa wafanyikazi wa kufanya marekebisho katika ikulu ya Whitehouse nchini Marekani.
Ripoti ya vitu vinavyofaa kurekebishwa katika ikulu ya White house iliopatikana na chombo cha habari cha NBC Washington ilishirikisha ripoti nyengine ya mwaka uliopita kutoka kwa utawala wa rais Obama.
Panya wanadaiwa kuonekana katika chumba cha kulia cha maafisa wa jeshi la wanamaji.
Walionekana katika majengo, kulingana na Brian Miller, aliyekuwa inspekta jenerali wa kikosi cha huduma za jumla ambacho husimamia marekebisho katika jumba hilo la rais.
''Mtu yeyote kati yetu ambaye anamiliki nyumba ya zamani anajua kwamba inahitaji kazi nyingi''.
Mende walikuwa tatizo katika chumba cha kulia huku wadudu wakionekana katika nyumba anayoishi afisa mkuu wa jeshi kulingana na ripoti hiyo.
Wadudu na mende pia walionekana katika chumba cha wanahabari.
Mbali na kukabiliana na wadudu ,ripoti hiyo ya marekebisho ya Ikulu inaonyesha kazi nyingi zilizohitajika kufanyika baada ya utawala mpya kuingia mwanzoni mwa mwaka huu.

Wanaume wanaotoa talaka 3 'kwa mpigo' kufungwa jela India

Utamaduni unashirikisha mwanamume wa Kiislamu anayetamka talaka mara tatu kwa njia nyingi ikiwemo kupitia ujumbe ama barua pepe.Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionUtamaduni unashirikisha mwanamume wa Kiislamu anayetamka talaka mara tatu kwa njia nyingi ikiwemo kupitia ujumbe ama barua pepe.
Wanaume waliopo katika ndoa ambao hujaribu kutoa talaka ya 'hapo kwa hapo' huenda wakahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela chini ya rasimu ya sheria zinazopendekezwa nchini India.
Utamaduni unashirikisha mwanamume wa Kiislamu anayetamka talaka mara tatu kwa njia nyingi ikiwemo kupitia ujumbe ama barua pepe.
Ilitangazwa kuwa kinyume na katiba na mahakama ya juu ya India mwezi Agosti lakini maafisa wanasema kuwa imetekelezwa tangu wakati huo.
Sheria hiyo pendekezi inatoa faini na usaidizi kwa wanawake walioathirika.
Muswada wenye sheria rasimu za kuwalinda wanawake sasa umetumwa kwa serikali za kijimbo kwa majadiliano.
Muswada huo utapiga maraufu italaka kwa mujibu wa hukumu ya mahakama ya juu na kutoa sheria za marupurupu mbali na usimamizi wa mwanamke aliyeathirika.
Sheria hizo zimewekwa ili kuhakikisha kuwa ''iwapo mume atamtaka mkewe kuondoka katika nyumba wawanayoishi basi atatoa ulinzi wa kisheria.
Chini ya sheria hiyo wale watakaopatikana na hatia hawataruhusiwa kuachiliwa kwa dhamana.
Vilevile watapiga marufuku sheria hiyo kwa njia yoyote ile ikiwemo kupitia maandishi ama ujumbe.

Trump kutambua Jerusalem ni mji mkuu wa Israel

Donald Trump kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel
Image captionDonald Trump kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel
Maafisa nchini Marekani wanasema kuwa Rais Trump anatarajiwa kutangaza wiki ijayo kuwa Marekani inatambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel hatua ambayo wakosoaji wanasema kuwa itachochea mzozo zaidi katika eneo hilo.
Hali kamili ya mji huo inakumbwa na utata huku pande zote mbili za Israel na Palestina zikidai kuwa ndio mji wao mkuu.
Trump alitoa ahadi ya kampeni ya kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.
Mji wa Jerusalem
Image captionMji wa Jerusalem
Mwandishi wa BBC anasema kwa kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, Trump anaashiria hatua ya kutekeleza ahadi yake ya kampeni.

RAIS WA ZANZIBAR DK SHEIN AHUDHURIA MAULID YA KUZALIWA MTUME MUHAMMAD SAW ZANZIBAR

MAKAMU wa Rais Mstaaf Dkt Mohammed Gharibi Bilal akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud, wakati akiwasili katika viwanja vya maisara kuhuhudhuria sherehe za Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad SAW, yaliofanyika Kitaifa katika viwanja vya maisara Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Al hajj Ali Mohamed Shein, akisalimia na Mwenyekiti wa Kamati ya Maulid ya Mfungo Sita Zanzibar Sheikh Shirali Champsi alipowasili katika viwanja vya maisara Zanzibar kuhudhuria katika sherehe za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W)


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Al hajj Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Makamu wa Rais Mstaaf Dkt. Mohammed Gharib Bilal alipowasili katika viwanja vya maisara kuhudhuria Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliofanyika katika viwanja vya maisara Zanzibar.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Al Hajj Ali Mohamed Shein, akiwa na Viongozi mbalimbali wa Dini na Serikali wakiwa wamesimama wakati wakutoa Salamu za kumkaribisha qaswida iliokuwa ikisomwa na Madrasatul E Itiswam ya Chukwani Zanzibar
MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein akiwa na Wananchi na Viongozi wakisimama wakati wa kutoa salamu ya kumkaribisha Mgeni Rasmin Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Alhajj Ali Mohamed Shein alipowasili katika viwanja hivyo kuhudhuria Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W)


WANAFUNZI wa Madrasatul E’itiswam ya Chukwani Zanzibar wakisoma Qwasid ya Salamu ya kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Al Hajj, Ali Mohamed Shein, katika viwanja vya maisra Zanzibar.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Alhajj Ali Mohamed Shein, alkisoma ratiba ya hafla ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliofanyika katika viwanja vya maisara kushoto Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na kulia Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji.
KADHI Mkuu wa Zanibar Sheikh Khamis Haji akitowa maelezo kabla ya kuaza kwa hafla ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliofanyika katika viwanja vya maisara Zanzibar
BAADHI ya waalikwa katika hafla ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) wakifuatilia hafla hiyo katika viwanja vya maisara Zanzibar.Picha na Ikulu

BALOZI SEIF IDDI MGENI RASMI BARAZA LA MAULIDI RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Wanawake Waislaam Tanzania, Shamim Khan baada ya kushiriki Katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likanglal wilayani Ruangwa Desemba 1, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia washiriki wa Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) baada ya kushiriki Baraza hilo kwenye uwanja wa Shukle ya Msingi Likangala wilayani Ruangwa Desemba 1, 2017.
Baadhi ya washiriki wa Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati alipohutubia kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Ruangwa Desemba 1, 2017
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya (wapili kushoto) na kulia ni Mwenyekiti wa Wanawake Waislaam, Shamim Khan wakati alipowasili kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala kushiriki katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S. A.W). Mgeni Rasmi kaaika Baraza hilo alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Mgeni Rasmi katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W), Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kuingia kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Rungwa Desemba 1, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mgeni Rasmi katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W),Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani RUangwa Desemba 1, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Rungwa Desemba 1, 2017. Mgeni Rasmi katika Maulidi hayo alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (wapili kushoto) na baadhi ya Viongozi walioshiriki katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) wakimsikiliza Mgeni Rasmi Balozi Seif Ali Iddi wakati alipiwahutubia kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Ruangwa Desemba 1, 2017. Wengine kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Wanawake Waislaam Tanzania, Shamim Khan, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Ikupa Stella Alex , Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya na Mbunge wa Viti Maalum,Hamida Muhammad Abdallah
Askofu Mkuu, Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi akizungumza katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Ruangwa, Desemba 1, 2017.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mgeni Rasmi katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W),Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani RUangwa Desemba 1, 2017. Kushoto ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubacary Zubeiry Ally.


Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

WIZARA YA AFYA YATOLEA UFAFANUZI KUHUSIANA NA UZINDUZI WA MKAKATI WA KONDOM

Kumekuwa na taarifa mbalimbali, hamaki na kejeli zinazoenea katika mitandao ya kijamii kuhusiana na taarifa iliyotolewa tarehe 27 Novemba 2017, Mnazi Mmoja kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kondom kuhusu mpango wa Serikali kununua na kusambaza kondom 500,000,000 katika kipindi cha miaka mitatu 2018 hadi 2020.

Tunapenda kuukumbusha umma wa Watanzania kwamba maambukizi ya VVU na UKIMWI bado ni tatizo katika nchi yetu. Takriban watu 1,400,000 wanakadiriwa kuwa na VVU. Hivyo katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI Serikali inaendeleza afua mbalimbali ili kuzuia maambukizi mapya. 

Asilimia 40% ya maambukizi mapya yanatokea miongoni mwa vijana wenye umiri wa miaka 15-24. Aidha makundi maalum kama vile wanaojidunga madawa ya kulevya, wanaofanya biashara ya ngono na wale wanaoamiiana wa jinsia moja wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi.  Makundi mengine ya walio katika hatari ni waendesha magari ya masafa marefu, wavuvi na wananchi wa kwenye migodi.

Wizara inatekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushauri nasaha na kupima uwepo wa VVU, na kisha kuanza tiba na matunzo, pamoja na kutoa dawa za kufubaza kwa watakao kuwa na maambuzi ya VVU. Kuna afua pia za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto, kutoa elimu ya VVU/UKIMWI na afya uzazi kwa vijana, elimu kuhusu VVU/UKIMWI kwa jamii na tohara kwa wanaume. 

Matumizi ya kondom ni moja wapo ya afua katika kuzuia maambukizi mapya. Hata hivyo utafiti wa viashiria vya Malaria na UKIMWI wa mwaka 2011/12 umebaini kuwa kuna matumizi duni ya kondom, kwani ni asilimia 27 tu ya watu wenye wenza zaidi ya mmoja waliokiri kutumia kondom mara ya mwisho walipofanya ngono. Hivyo Serikali itaendelea kununua na kusambaza kondom kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na mimba zisizo tarajiwa ikiwa ni mojawapo ya afua hizo za kudhibiti maambukizi ya VVU.
Tunasisitiza kuwa Wizara na wadau wake inaendelea kutoa elimu ya kondom sambamba na elimu ya kusubiri kufanya ngono kwa wale ambao hawajaanza na wale ambao wameanza lakini wanapaswa kusubiri (Abstinence) na elimu ya kuwa waaminifu kwa mwenza mmoja aliye mwaminifu na anaejua hali yake ya maambukizi ya VVU (Be faithfull). 

Hivi sasa nchini kuna vyanzo vya upatikanaji wa kondom vya aina tatu. Kwanza ni kondom zinazopatikana kupitia sekta ya umma  ambazo husambazwa na Serikali kwa wananchi bila malipo. Pili, kuna kondom zinazosambazwa na wadau ambazo zinauzwa kwa bei ya chini kwa kuwa wadau wamechangia. Mfano kondom za Salama na Dume, na chanzo cha tatu ni kondom za kibiashara ambazo zinauzwa kwa bei ya kati na ya juu.

Kondom za sekta ya umma husambazwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na huduma za mkoba ngazi ya jamii, Kondom za wadau na zile za biashara husambazwa katika maduka ya dawa, maduka ya bidhaa mbambali, baa na nyumba za wageni.

Kwa mwaka 2016/17 Serikali iliboresha kondom zinazopatikana kupitia ya sekta ya umma kwa kuipa kifungashio kipya na jina la ZANA, ambapo kondom 36,916,911 zilisambazwa. Kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2018 hadi 2020 Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa kudhibiti malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu inatarajia kununua kondom za kiume takribani 500,000,000. 

Kondom hizi zitasambazwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na katika maeneo hatarishi yanayoaminika kuwa na watumiaji wengi. Aidha, kwa vile imebainika kuwa watu ambao hawaumwi hawaendi vituo vya afya kwa  ajili  ya kuchukua kondom tu na hivyo kupelekea kutofikia walengwa, usambazaji na ugawaji huu utalenga maeneo ambayo
Kunamatukio ambayo yanaendana na ngono na yana walengwa wa afua za kondom. Maeneo haya ni kama baa, nyumba za kulala wageni, maeneo yenye mikusanyiko ya magari ya masafa marefu, maeneo ya uvuvi na migodini.

Aidha ikumbukwe kwamba nchi yetu ina sera sheria, mila, desturi na maadili yetu kama watanzania,  Hivyo kondom zote haziruhusiwi kusambazwa bila kufuata miongozo ya Wizara, ili kulinda zisifike kwa wasiolengwa.

Hivyo basi, iwapo tunataka kuzuia na kumaliza maambukizi ya VVU na UKIMWI ifikapo 2030 tunapaswa kama nchi kuwekeza katika kuzuia maambukizi mapya. Matumizi ya kondom, ununuzi wa vifaa tiba, vitendanishi, dawa za ARV na za magonjwa nyemelezi ni afua muhimu. Tunaomba wanahabari na wananchi waunge mkono juhudi hizi kwa kuwa tunahitaji watanzania wenye afya bora na uwezo wa kuzalisha ili kuijenga Tanzania ya Viwanda.

MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AZITAKA ASASI ZA KIRAIA NA MADHEHEBU YA DINI KUONGEZA JUHUDI KATIKA KUCHANGIA MASUALA YANAYOHUSIANA NA UKIMWI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka asasi za kiraia na madhehebu ya dini kuendelea kuongeza juhudi katika kuchangia masuala yanayohusiana na ukimwi katika maeneo yao ikiwemo kuhimiza maadaili na tabia njema katika jiamii.

Makamu wa Rais aliyasema haya wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika jijini Dar es Salaam.Makamu wa Rais alisema kuwa kila mtu anapaswa kukumbuka kuwa jukumu kuu la kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi linaanza na mtu binafsi, jamii na hatimaye sote kama nchi.

“Ndugu Wananchi Ukimwi umeendelea kuathiri nguvu kazi ya Taifa, wafanyakazi wa taasisi za serikali na zisizo za serikali wanapata maambukizi kama wana jamii wengine hii inapelekea kupungua kwa ufanisi makazini na kuathiri uchumi kwa ujumla”Makamu wa Rais amezipongeza Taasisi zote ambazo zina mikakati ya kupambana na ukimwi mahala pakazi kwa kuwakinga wafanyakazi wao na pia kuwahudumia bila kuwabagua wala kuwanyanyapaa wale wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Makamu wa Rais alisema Serikali ina nia thabiti ya kutafuta mikakati endelevu ya kufikia TISINI TATU ifikapo mwaka 2020 na kumaliza kabisa ukimwi ifikapo 3030.Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha miundo mbinu ya afya na kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya ikiwa ni pamoja na kuongeza watoa huduma kote nchini.

Makamu wa Rais amesema Serikali imeanzisha mfuko wa ukimwi (AIDS TRUST FUND) ukiwa na lengo la kuboresha rasilimali kwa ajili ya kuboresha huduma za ukimwi yakiwemo matibabu, upimaji wa virusi vya ukimwi na kutokomeza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa motto pamoja, kuhudumia watoto yatima na ujenzi wa vituo vya kutolea elimu ya ukimwi hivyo uwepo wa mfuko huu utapunguza utegemezi na kuongeza kasi na ufanisi katika mapambano dhidi ya ukimwi.

Makamu wa Rais alihimiza elimu ya ukimwi itolewe mashuleni ili vijana wawe na ufahamu wa kutosha .Makamu wa Rais alimaliza kwa kuwapongeza UNAIDS na wadau wote wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya ukimwi na kuwahakikishia serikali ipo pamoja nao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Da es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Friday, December 1

Polisi wamshikilia mwanamke aliyemvika mwenzake pete ya uchumba


Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mtumishi wa mgodi wa GGM, Milembe Suleiman anayetuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsi moja.
Mfanyakazi huyo ambaye ni ofisa ugavi kitengo cha manunuzi anashikiliwa baada ya ‘video’ inayomwonyesha akimvisha pete ya uchumba mwanamke mwenzake kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Video hiyo ambayo imezua mijadala hasa ikizingatia kwamba iko kinyume cha utamaduni wa Kitanzania na Serikali ambayo imekuwa ikikemea na kupiga marufuku vitendo vya mapenzi ya jinsi moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amesema wanamshikilia kwa uchunguzi kwa kuwa nchi hairuhusu mambo hayo.
Ofisa Habari wa GGM, Dili Tenga amesema hayo ni masuala binafsi ya mfanyakazi hivyo wao kama mgodi hawawezi kuyazungumzia lakini wanaviachia vyombo vya dola viendelee na uchunguzi wake.