Saturday, December 2

MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AZITAKA ASASI ZA KIRAIA NA MADHEHEBU YA DINI KUONGEZA JUHUDI KATIKA KUCHANGIA MASUALA YANAYOHUSIANA NA UKIMWI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka asasi za kiraia na madhehebu ya dini kuendelea kuongeza juhudi katika kuchangia masuala yanayohusiana na ukimwi katika maeneo yao ikiwemo kuhimiza maadaili na tabia njema katika jiamii.

Makamu wa Rais aliyasema haya wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika jijini Dar es Salaam.Makamu wa Rais alisema kuwa kila mtu anapaswa kukumbuka kuwa jukumu kuu la kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi linaanza na mtu binafsi, jamii na hatimaye sote kama nchi.

“Ndugu Wananchi Ukimwi umeendelea kuathiri nguvu kazi ya Taifa, wafanyakazi wa taasisi za serikali na zisizo za serikali wanapata maambukizi kama wana jamii wengine hii inapelekea kupungua kwa ufanisi makazini na kuathiri uchumi kwa ujumla”Makamu wa Rais amezipongeza Taasisi zote ambazo zina mikakati ya kupambana na ukimwi mahala pakazi kwa kuwakinga wafanyakazi wao na pia kuwahudumia bila kuwabagua wala kuwanyanyapaa wale wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Makamu wa Rais alisema Serikali ina nia thabiti ya kutafuta mikakati endelevu ya kufikia TISINI TATU ifikapo mwaka 2020 na kumaliza kabisa ukimwi ifikapo 3030.Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha miundo mbinu ya afya na kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya ikiwa ni pamoja na kuongeza watoa huduma kote nchini.

Makamu wa Rais amesema Serikali imeanzisha mfuko wa ukimwi (AIDS TRUST FUND) ukiwa na lengo la kuboresha rasilimali kwa ajili ya kuboresha huduma za ukimwi yakiwemo matibabu, upimaji wa virusi vya ukimwi na kutokomeza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa motto pamoja, kuhudumia watoto yatima na ujenzi wa vituo vya kutolea elimu ya ukimwi hivyo uwepo wa mfuko huu utapunguza utegemezi na kuongeza kasi na ufanisi katika mapambano dhidi ya ukimwi.

Makamu wa Rais alihimiza elimu ya ukimwi itolewe mashuleni ili vijana wawe na ufahamu wa kutosha .Makamu wa Rais alimaliza kwa kuwapongeza UNAIDS na wadau wote wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya ukimwi na kuwahakikishia serikali ipo pamoja nao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Da es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

No comments:

Post a Comment