Tuesday, September 26

Upinzani kuandamana Kenya

Polisi wamekita kambi katika makao ya tume ya uchaguzi Nairobi
Image captionPolisi wamekita kambi katika makao ya tume ya uchaguzi Nairobi
Chama cha upinzani nchini Kenya NASA kimeitisha maandamano Jumanne nje ya makao makuu ya tume ya uchaguzi IEBC mjini Nairobi.
Hatua hii ni ya kushinikiza kujiuzulu kwa baadhi ya maafisa wa juu wa tume hiyo walioshiriki kuandaa uchaguzi mkuu wa August 8 mwaka huu uliobatilishwa na mahakama ya juu nchini.
NASA umeeleza kwamba hautovamia makao ya tume ya IEBC kama ilivyotajwa awali kuwatimua kwa lazima maafisa hao, badala yake unasema maandamano yatakuwa ya amani katika barabara za mji mkuu Nairobi kushinikiza kujiuzulu kwao.
Hilo ni mojawapo ya masharti iliyotoa NASA kushiriki uchaguzi wa marudio uliotangazwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu.
Image captionVinara wa upinzani Kenya Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Musalia Mudavadi
Rais Uhuru Kenyatta ametoa onyo kwa wapinzani ambao amesema watakumbana na mkono wa sheria iwapo maandamano yao yataingilia shughuli za kiuchumi za raia wa nchi hiyo.
Amesema, 'Endeleeni na maandamano yenu, mukigusa mboga za mama wanaouza barabarani, tuko na nyinyi. Mukigusa maduka ya watu tuko na nyinyi. Lakini kama hamuna lingine lolote la kufanya isipokuwa kutembea - tembeeni. Mimi nawaambia hata mukinitukana mpaka asubuhi, haitabadilisha dunia'.
Image captionRais Uhuru Kenyatta ameuonya upinzani kuwa watakumbana na mkono wa sheria iwapo maandamano yatakumbwa na ghasia
Upinzani unasisitiza kuwa una haki ya kuandamana kwani hata upande wa serikali - Muungano wa Jubilee - umeshafanya maandamano kama hayo hivi juzi walipoelekea katika mahakama ya juu zaidi wakitaka majaji wa mahakama hiyo waondolewe.
Mmoja ya vinara waandamizi wa kambi ya upinzani, Musalia Mudavadi ameiambia BBC, kuwa mahakama ya juu zaidi ilisema IEBC ilishindwa kuandaa uchaguzi mkuu kulingana na sheria.
Ameeleza, 'Tume ya IEBC sio vyombo tu, bali ina watu ndani ambao ni maafisa wanaohudumu katika kitengo cha usajili wa watu, masuala ya teknolojia ya mawasiliano na kadhalika, walishindwa kutekeleza wajibu wao na ndio wanaoweza kuondolewa.
Muungano wa NASA unataka jumla ya maafisa 12 wa tume hiyo washtakiwe kwa kutowajibika katika uchaguzi uliobatilishwa wa Agosti 8.
Unataka pia mfumo wa teknolojia uliotumiwa wakati wa uchaguzi huo ubadilishwe.

Rais mpya nchini Angola ameapishwa

Joao Lourenco alikula kiapo baada ya chama tawala cha MPLA kushinda uchaguzi.
Image captionJoao Lourenco alikula kiapo baada ya chama tawala cha MPLA kushinda uchaguzi.
Rais mpya wa Angola ameapishwa katika sherehe zilizofanyika kwenye mji mkuu Luanda.
Joao Lourenco alikula kiapo baada ya chama tawala cha MPLA kushinda uchaguzi.
Bw. Lourenco, ambaye ni waziri wa zamani wa usalama anachukua mahala pa Jose Eduardo Dos Santos, ambaye aliondoka madarakani baada ya kuiongzoa nchi kwa miaka 38.
Bwana Dos Santos atakuwa na ushawishi kwenye chama akiwa na haki ya kumteua mkuu wa polisi pamoja na mkuu wa majeshi.
Image captionJoao Lourenco alikula kiapo baada ya chama tawala cha MPLA kushinda uchaguzi.
Wakosoaji wanasema watoto wake, akiwemeo mwanamke tajiri zaidi barani Afrika, Isabel Dos Santos wamepewa nyadhifa za kudhibiti uchumi.
Licha ya Angola kuwa na utajiri wa mafuta, bado kuna mwanya mkubwa
Chama cha MPLA kimeitawala Angola tangu ipate uhuru wake kutoka Ureno mwaka 1975.

Mpalestina awapiga risasi na kuwaua Waisrael 3

Scene of attack at Har Adar (26/09/17)Haki miliki ya pichaEPA
Image captionMpalestina awapiga risasi na kuwaua raia watatu wa Israel
Watu watatu raia wa Israel wameuawa kwa kupigwa risasi na raia wa Palestimna katika mlango wa kuingia kwenye makao ya walowezi wa kiyahudi eneo la Har Adara lililo ukingo wa magharibi.
Mtu mwenye bunduki wa umri wa miaka 37 kutoka kijiji kilicho karibu pia alipigwa risasi na kufariki baadaye.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema mauaji hayo yamesababishwa na uchochezi upande wa palestina.
Mauaji hayo yanafanyika wakati mjumbe wa Rais Donald Trump eneo la Mashariki ya Kati Jason Greenblat, anapowasili Jerusalem kufufua mazungumzo kati ya Israeli na Palestina.
Image captionZaidi ya wayahudi 600,000 wanaishi karibu makao 140 yaliyojengwa tangu mwaka 1967
Ikulu ya Marekani inasema kuwa imejaribu kufanya mikakati wa kuyafufua mazungumzo tangu Donald Trump aingie madarakani mwezi Januari lakini hakujakuwa na dalili za kuwepo hatua.
Mazungumzo ya amani kati ya pade hizo mbili yalivunjika mwezi Aprili mwaka 2014.
Polisi wanasema kuwa mtu huyo mwenye silaha anayetajwa na vyombo vya habari nchini Israeli kama Nimer Jamal, alishambulia baada ya kugundua kuwa alishukiwa na walinzi karibu na mlango wa eneo la Har Adar.
Aliwapiga risasi walinzi wawili na polisi wa mpaka kwa karibu, na kumjeruhi vibaya mtu mwingine kabla ya kupigwa risasi na vikosi vya usalama.
Image captionAliwapiga risasi walinzi wawili na polisi wa mpaka kwa karibu, na kumjeruhi vibaya mtu mwingine
Alitoka kijiji cha Beit Surik, karibu maili moja mashariki mwa Har Adar.
Eneo hilo liko karibu kilomita 18 kaskazini magharibi mwa Jurusalem.
Karibu Wapalestina 36,000 wana vibali vya kufanya kazi katika makao ya wayahudi ambapo ulinzi wa kuyalinda dhdi ya mashambulizi ni mkali.
Zaidi ya wayahudi 600,000 wanaishi karibu makao 140 yaliyojengwa tangu mwaka 1967, kwenye ukingo wa magharibi na Mashariki mwa Jerusalem.
Image captionPolisi walitoa picha ya bunduki aliyoitumia

Almasi iliyopatikana nchini Botswana yauzwa kwa dola milioni 53

Almasi iliyopatikana nchini Botswana yauzwa kwa dola milioni 53
Almasi yenye haijakatwa ya ukubwa wa mpira wa tenisi, iliyopatikana kwenye mgodi wa Korowe nchini Botswana mwezi Novemba mwaka 2015, imeuzwa na kampuni yenye makao yake nchini Canada ya Lucara Diamond kwa kima cha dola milioni 53
Almasi hiyo yenye karati 1,109 ambayo kwa sasa ndiyo kubwa zaidi ambayo bado haijakatwa duniani, ilinunuliwa na kampuni ya Uingereza ya Graff Diamonds kwa dola 47,777 kwa kila karati na sasa itakatwa.
Kampuni ya Canada awali ilijaribu kuiuza almasi hiyo kwenye mnada mwezi Juni mwaka 2016, lakini haikupata bei ilikuwa inahitajika.
Almasi hiyo kwa jina Lesedi La Rona au mwangaza wetu kwa lugha ya taifa nchini Botswana inatajwa kuwa ya miaka bilioni 2.5 hadi bilioni 3.
Kampuni ya Laurence Graff, ilisema kuwa ni hashima kubwa kuwa sasa inamiliki almasi hiyo.

Hofu ya kulipuka volkano katika kisiwa cha kitalii cha Bali

A farmer moves cattle from his land in the Kubu subdistrict of Karangasem Regency on the Indonesian resort island of Bali on 26 September 2017, as Mount Agung volcano looms in the background.Haki miliki ya pichaAFP/GETTY IMAGES
Image captionWakulima wamekuwa wakihama
Indonesia imeonya kuwa mlima wa volcakano katika kisia cha kitalii cha Bali umefikia kiwango kibaya huku kukiwa na hofu ya kutokea kwa mlipuko ya volkano.
Mamia ya mitetemeko midogo ya ardhi imerekodiwa siku ya Jumatatu kwenye mlima Agung ishara ya kutokea kwa mlipuko wa volkano.
Lakini maafisa wanasisitiza kuwa huwawezi kutabiri ni lini mlima huo unaweza kulipuka.
Zaidi ya watu 75,000 wanaoishi karibu na mlima huo wamehamishwa kutoka makwao, na eneo hilo sasa liko chini ya tahadhari kubwa ya volkano.
Image captionHofu ya kulipuka volkano katika kisiwa cha kitalii cha Bali
Msemaji wa shirika la taifa la majanga nchini Indonesia Sutopo Purwo Nugroho aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kuwa mlima dalili zinaendelea kuongezeka.
Alisema kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa mlima huo utalipuka, lakini akasema kuwa haijulikana mlima huo utalipuka lini.
Zaidi ya mitetemeko midogo 560 ya volkano ilirekodiwa siku ya Jumatatu pekee.
Image captionHofu ya kulipuka volkano katika kisiwa cha kitalii cha Bali
Maeneo kuu ya kitalii ya Kuta na Seminyak, yaliayokaribu kilomita 70 kutoka mlima huo hayajaathiriwa kwa sasa na safari za ndege zinaendelea kama kawaida.
Lakini nchi kadha zikiwemo Uingereza, Ausralia na Singapore zimetoa onyo la kusafiri kwa raia wao zikionya kuwa huenda kukawa na tatiza ya safari za ndege.
Zaidi ya watu 1000 waliuawa wakati mlima Agung ulilipuka mwaka 1963.
Image captionHofu ya kulipuka volkano katika kisiwa cha kitalii cha Bali

Inspekta aeleza jinsi Manji alivyoumwa gerezani

Mfanyabiashara Yussuf Manji akizungumza na

Mfanyabiashara Yussuf Manji akizungumza na wakili wake katika katika Chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.   Picha na Omar Fungo 
Daktari Mfawidhi wa Gereza la Keko, Inspekta Eliud Mwakawanga ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi maisha ya mfanyabiashara Yusufu Manji yalivyokuwa gerezani kwamba alikuwa akitumia vidonge kati ya 25 mpaka 30 kwa siku.
Ameeleza kuwa walikuwa wakipatia dawa hizo alipokuwa akisikia aumivu hasa ya mgongo na kwamba kuna kipindi alikuwa anaamka akiwa na hali ya kutetemeka au kuchanganyikiwa.
Pia ameeleza kuna wakati Manji alikuwa anaamka anashindwa hata kutembea na wakati mwingine alikuwa akitumia mkanda kufunga mgongo.
Shahidi huyo wa sita wa upande wa mashtaka ametoa ushahidi huo leo Jumanne katika kesi ya  kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin inayomkabili Manji.
Ameeleza kuwa Julai 6, 2017 walimpokea Manji akitokea Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha Moyo cha JKCI ambapo waliambiwa ni mshtakiwa lakini ni mgonjwa.
“Nilienda kumuona, tukazungumza naye na tulikaa naye gerezani hadi alipokuja kuachiwa,”
"Tangu nimempokea hali yake kiafya haikuwa nzuri na alikuwa mtu anayetumia dawa wakati wote na alikuja na dawa zake za aina sita kutoka Muhimbili ambazo alikuwa akizitumia, pia kulingana na hali yake na mazingira anayokuwa anajisikia, tulikuwa tukimpatia dawa gerezani mbali na hizo."
Ameeleza kuwa utaratibu wa kuwapatia dawa mahabusu na wafungwa huwa wanakaa nazo wao wataalam na wanawapa kutokana na maelezo ya daktari yaliyopo kwenye cheti ambapo Manji kuna dawa alikuwa anakunywa asubuhi na jioni na nyingine kulingana na hali yake ya siku hiyo.
Shahidi huyo ameeleza kuwa wao huwa hawatoi dawa za kulevya kwa mgonjwa ila wanatoa dawa.
Alisema hivyo baada ya kuulizwa na Wakili Hajra Mungula kuwa dawa walizompatia Manji zinahusiana vipi na dawa za kulevya.
"Sijachunguza sana kuona zina uhusiano gani na dawa za kulevya,” ameeleza na kusisitiza wao hawatoi dawa za kulevya kwa mgonjwa wanatoa dawa.
Kesi hiyo bado inaendelea mahakamani hivi sasa kwa taarifa zaidi soma gazeti la Mwananchi

Aliyekuwa mbunge wa Longido aomba muda zaidi

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Onesmo Ole

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Onesmo Ole Nangole 
Arusha. Kesi ya kupinga  kutenguliwa matokeo ya ubunge katika Jimbo la Longido mkoani Arusha imetinga tena Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ambapo aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Onesmo Ole Nangole ameomba kuongezewa muda wa kukata rufaa kupinga kutenguliwa ubunge wake.
Kesi hiyo imetajwa leo Jumanne mbele ya Jaji Modester Opiyo wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ambapo Nangole amewakilishwa na wakili John Mallya kwa niaba ya Tundu Lissu na aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Stivin Kiluswa aliwakilishwa na wakili Daud Haraka.
Jaji Opiyo baada ya kueleza kupokea maombi ya warufani namba 108/2017 aliwataka mawakili wa pande zote kujibu kutoa hoja zao kwa maandishi.
Mawakili upande wa rufaa wametakiwa kuwasilisha hoja zao Oktoba 3 na upande wa utetezi  wanapaswa kujibu kwa maandishi hoja zao Oktoba 10 mwaka huu.
Jaji Opiyo amesema Oktoba 16 pande zote watafanya majumuisho ya hoja na Oktoba 17 itapangwa tarehe ya kusikilizwa maamuzi.

Mahakama yaamuru ndugu sita kunyongwa hadi kufa


Sumbawanga. Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa imewahukumu adhabu ya kifo watu sita ambao ni ndugu wakazi wa Kalambo baada ya kupatikana hatia ya kumuua ndugu yao.
Ndugu hao wamedaiwa kwamba walifikia uamuzi wa kumuua ndugu yao huyo kwa madai ya kwamba anajihusisha vitendo vya kishirikiana. 
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne na Jaji Mahakama hiyo, Dk Adam Mambi baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka uliopeleka mashahidi sita ili kuthibitisha mashitaka hayo.
Waliokutwa na hatia katika shauri hilo ni Ferdinand Kamande, Peter Mpandisharo, Edes Kamande, Stephen Sikanda, Henrick Nguvumali na Anatory Kamande huku Alistid Kamande na Will broad Kamande wakiachiwa huru kwa kutokutwa na hatia.
Katika shauri hilo upande wa mashitaka uliongozwa na mawakili wa serikali ambao ni Scolastica Lugongo na Adolf Lema huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Mathias Budodi, ambapo ilidaiwa kwamba washitakiwa walitenda kosa hilo Septemba 27, mwaka 2014.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa siku ya tukio nyakati za usiku washitakiwa wakiwa na silaha za jadi kama vile mapanga, nondo, mawe, majembe walivamia nyumba ya Kamande na kugonga dirisha kisha kuvunja mlango ambapo Kamande alikimbia kuelekea kusikojulikana. 
Ilielezwa kwamba baada ya hapo waliichoma moto nyumba hiyo na kuteketeza kila kitu kilichokuwemo ndani kisha kuondoka zao. 
Wakati nyumba hiyo ikiteketea kwa moto Kamande aliyekuwa amekimbia ili kunusuru maisha yake, alikamatwa na watu hao na kuanza kupigwa huku wakimtuhumu kuwa ni mchawi na baada ya kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake walimchoma moto na kufariki papo hapo. 
Ilidaiwa kwamba  washitakiwa hao walikamatwa na polisi Oktoba 10, 2014 na baada ya kuhojiwa na polisi walikana shitaka hilo.
Awali kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili wa Serikali waliiomba mahakama kutoa adhabu kali iwe fundisho kwani watu wamekuwa wakichukulia sheria mkononi na kuua watu kinyume cha sheria wakiwatuhumu kuwa ni washirikina.
Akitoa adhabu hiyo Jaji wa Mahakama hiyo, Dk Mambi amesema ameridhishwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka hivyo kwa kutumia Kifungu cha Sheria ya Makosa ya Jinai Namba 196 Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo 2002 anawahukumu watu hao sita kifo kwa kunyongwa.

Besigye akamatwa, polisi wazingira ofisi zake, Bunge

Kiongozi mkuu wa chama cha Former Forum for

Kiongozi mkuu wa chama cha Former Forum for Democratic Change (FDC) Dk Kizza Besigye 
Kampala, Uganda. Kiongozi mkuu wa chama cha Former Forum for Democratic Change (FDC) Dk Kizza Besigye amekamatwa leo saa moja kabla ya Bunge kuanza kujadili pendekezo la kuondoa ukomo wa umri wa rais.
Besigye, aliyewahi kugombea urais mara nne na akishindwa kwa Rais Yoweri Museveni alikamatwa mjini hapa alipokwenda kuwahamasisha wafuasi wake kupinga kufutwa Ibara ya 102 (b) kwenye Katiba iliyoweka ukomo wa kugombea urais kuwa miaka 75.
Besigye alikataa kushuka kutoka kwenye gari lake hali iliyowalazimisha maofisa wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kampala (DPC) wakiongozwa na Joseph Bakaleke kulivuta gari lake hadi kituoni hapo. Hadi sasa Besigye bado yuko ndani ya gari.
Vilevile Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Fred Mukasa Mbidde alikamatwa kuhusiana na suala hilo hilo. Zilikuwepo taarifa za kukamatwa vijana wengi katika maeneo mbalimbali yalikofanyika maandamano ya kupinga pendekezo hilo. Maeneo mengine yalikofanyika maandamano ni Mbale, Arua, Mbarara, Masaka na Pader
Polisi wazingira
Katika hatua nyingine, maofisa polisi walisambazwa katika maeneo mengi muhimu katika jiji la Kampala ulinzi unaohusiana na pendekezo la kufutwa Ibara ya 102 (b) ya Katiba likilenga kuondoa ukomo wa umri wa rais.
Makao makuu ya ofisi za chama cha FDC yalizingirwa na polisi wa kawaida, wa kuzuia ghasia na wa kupambana na ugaidi. Ofisi hizo zilizopo Najjanankumbi katika barabara ya Kampala-Entebbe zimezungukwa na polisi wenye silaha.
Msemaji wa Polisi Asan Kasingye alisema juzi kwamba maofisa hao wamesambazwa kwa ajili ya kukabiliana na kitisho cha aina yoyote. Kadhalika maeneo mengi nyeti, eneo lililojaa shughuli za kibiashara na Bunge yote yanalindwa.
Polisi wa kijeshi pia wamesambazwa maeneo ya Constitution Square ambako wameweka mahema sawa na bungeni, eneo muhimu kwa ajili ya mjadala uliotarajiwa kuwasilishwa jana kuhusu kuondolewa ukomo wa umri.
Kusambazwa kwa wingi kwa askari hao kumefanyika katikati ya kampeni zinazofanywa na za vikundi vya kisiasa na sasi za kiraia kupinga marekebisho ya katiba yanayolenga kufuta ukomo wa umri wa rais wa miaka 75. Hoja ya marekebisho hayo ilitarajiwa kuwasilishwa jana baada ya kushindikana Alhamisi iliyopita.
Mjadala ni mkali ndani ya bunge na chama tawala cha NRM wakiwemo baadhi ya wenyeviti wa majimbo ambao wamepinga pendekezo la kufuta Ibara ya 102 (b) ya Katiba wakisema ni jaribio la kupindua sheria mama.
Baraza la Viongozi wa Dini nchini limeongeza uzito kwa kutoa wito kwa serikali kuruhusu hoja ya ukomo wa umri wa rais iamuliwe na wananchi wote kwa kupiga Kura ya Maoni.
Baraza hilo linalojumuisha wakuu saba wa madhehebu makubwa ya dini nchini limesema katika taarifa yao ya pamoja wiki iliyopita kwamba watu waruhusiwe kuamua hatima yao.
“Mjadala kuhusu kuondolewa kwa ukomo wa umri wa rais si suala la upande mmoja ambalo linahodhiwa na wanasiasa na au wabunge...wananchi wana maoni tofauti kuhusu sauala hilo, hivyo kuna haja ya kusikiliza kwa utulivu pande zote bila ya kuegemea upande mmoja na kuutisha mwingine.
Hivi karibuni wabunge wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) na wa kujitegemea walipitisha uamuzi wa kuondolewa ukomo wa umri wa miaka 75 uliowekwa katika Katiba.
Ikiwa marekebisho hayo yatapitishwa bungeni, itakuwa na maana kwamba Rais Museveni mwenye umri wa miaka 73 sasa ataweza kugombea uchaguzi ujao mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 77. Mwaka 2005, katiba ilifanyiwa marekebisho ukaondolewa ukomo wa mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.

Hukumu ya Manji Oktoba 6


Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu ya Mkazi Kisutu, imepanga Oktoba 6, mwaka huu kutoa  hukumu katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili Yusuf Manji(41).
Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi , Cyprian Mkeha, baada ya wakili wa utetezi Hajra Mungula kusema kuwa ameshafunga ushahidi wa mashahidi saba.
Mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wametoa ushahidi wao dhidi ya mshtakiwa Daktari Mfawidhi wa Gereza la Keko, Inspekta Eliud Mwakawanga ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi maisha ya mfanyabiashara Yusufu Manji yalivyo kuwa gerezani kwamba alikuwa akitumia vidonge kati ya 25 mpaka 30 kwasiku.
Ameeleza kwamba  walikuwa wakimpatia dawa hizo alipokuwa akisikia maumivu hasa ya mgongo na kwamba kuna kipindi alikuwa anaamka akiwa na hali ya kutetemeka au kuchanganyikiwa.
Ameeleza kuwa Julai 6, 2017 walimpokea Manjia kitokea Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha Moyo cha JKCI ambapo waliambiwa ni mshtakiwa lakini ni mgonjwa.
“Nilienda kumuona, tukazungumza naye na tulikaa naye gerezani hadi alipokuja kuachiwa,”

Mo Dewji ajutia mambo mawili


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji ametaja mambo mawili ambayo anayajutia kwa kutoyafanya na anahisi kuwa amechelewa kuyafanyia maamuzi.
Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes anashika nafasi ya 21 kwa watu matajiri Afrika amesema kuwa kushindwa kuwekeza katika benki na mawasiliano ya simu ni mambo ambayo yanamuumiza kichwa akiendelea kuyajutia.
Mfanyabiashara huyo ametuma sehemu ya mahojiano kwenye mtandao wake wa Twitter akielezea mambo hayo.
Akijibu swali lililotaka atoe ushauri wake nini ambacho hajakifanya Dewji alianza kwa kusema, “Nimekosa mambo mengi katika maeneo ambayo nilipaswa kuwekeza...nilipaswa nimewekeza katika benki. Ingawa sasa najaribu kununua benki lakini nadhani nimechelewa. Na jambo la pili ambako nimekosea ni kwa kushindwa kuwekeza katika biashara ya mawasiliano ya simu.”
Amesema hakuwa na mwamko wa kujiingiza katika uwekezaji wa mtandao wa mawasiliano ya simu kwa vile alihisi wananchi wengi walikuwa hawana uwezo kumudu kununua simu na kuwasiliana.
“Unajua nilikuwa nikifikiri kuwa hivi watu hawa watapata wapi fedha kununua simu lakini sasa ukiangalia kama Tanzania kila mtu anamiliki simu ya mkononi...Haya ndiyo mambo mawili ambayo nayajutia,” amesema mfanyabiashara huyo.
Miongoni mwa wafanyabiashara waliopata mafanikio makubwa kutokana na kuwekeza katika mtandao wa mawasiliano ya simu ni Mo Ibrahim raia wa Uingereza ambaye jarida la Forbes limemtaja kuwa ni mtu 692 kwa watu matajiri duniani.
Mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Sudan sasa anasimamia taasisi yake ijulikanayo Mo Ibrahim Foundation ambayo inahimiza dhana ya utawala bora barani Afrika.

Wabunge wakunjana kutaka kupigana


Kampala, Uganda. Pendekezo tata la ukomo wa umri limezidi kuwa moto baada ya kuibuka fujo ndani ya Bunge muda mfupi baada ya Spika Rebecca Kadaga kusema Ratiba ya Shughuli za Bunge imefanyiwa marekebisho ili kuingiza pendekezo hilo tata la Mbunge wa Igara Magharibi, Raphael Magyezi.
Baadhi ya wabunge wa upinzani waliibuka na kudai kwamba mmoja wa wabunge aliingia bungeni na bunduki hali iliyozua hofu na fujo hadi baadhi kufikia kushikana mashati kutaka kupigana.
Shughuli za Bunge zilitatizika kwa dakika 20 huku Spika Kadaga akitumbua macho. Mbunge wa Busongora Kaskazini, William Nzoghu, alidai kwamba baadhi ya wabunge waliingia na bunduki na akaongeza kuwa hata Spika hakuwa salama kusimamia mjadala.

Mbunge wa Busiro Kusini Merdard Lubega Sseggona alimuomba spika aahirishe Bunge kwa sababu za kiusalama. Lakini Spika Kadaga alikataa akisema hawezi kuahirisha shughuli za bunge kwa kusikia uvumia tu.

Majibu hayo hayakutatua hali kwani wabunge walianza kuvurumishana. Kadri hali ilivyozidi kuzorota viti vilianza kurushwa na wabunge wakawa wanakimbilia maeneo salama huku wengine wakiwatuliza wenzao waliokuwa wanataka kumwaga damu ya wenzao.
Waziri wa Maji Ronald Kibuule ndiye alishutumiwa na wapinzani na wa kujitegemea kuwa aliingia na bunduki, madai ambayo aliyakanusha. Wabunge wa Kaunti ya Lwemiyaga, Theodore Ssekikubo na Kibuule walikunjiana ngumi wakitaka kutwangana.
Baadaye wabunge walitulia na ikatolewa amri ya kufanya msako kubani walioingia na bunduki.
Hoja ya ukomo wa umri ilitarajiwa kuwasilishwa mchana.

Polisi watumia mabomu ya machozi kuwatawanya Nasa, Jubilee


Nairobi, Kenya. Polisi wamelazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa vyama vya Jubilee na muungano wa upinzani wa Nasa baada ya kuzua vurugu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) zilizoko jengo la Anniversary Towers.
Wafuasi wa Nasa waliokuwa wakiimba nyimbo “Chiloba lazima ang’oke” walikabiliwa na wafuasi wa Jubilee waliokuwa wakiimba “Tunataka amani”. Makundi yote mawili yalitimua mbio baada ya polisi wa kuzuia ghasia kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.
Huku wakikohoa na wakitafuta mahali salama, wote walikimbia kukwepa kukamatwa.
Maandamano hayo yamefanyika kuitikia wito uliotolewa jana na kiongozi mkuu wa Nasa Raila Odinga kwamba wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kuandamana hadi kwenye makao makuu ya IEBC lengo likiwa kumtoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC Ezra Chiloba kwa madai ya kuhusika kuvuruga uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.
Maandamano hayo yanafanyika siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Katika mji wa Kisumu, ambao unatajwa kuwa moja ya ngome za Nasa baadhi ya wakazi waliandamana hadi ofisi za IEBC na baada ya kufika walitoa wito maofisa wa ngazi za juu akiwemo Ezra Chiloba wajiuzulu.
Walimshutumu Chiloba na kikundi chake kwa kufanya njama za kuingilia mchakato wa uchaguzi mkuu ambao matokeo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta yalifutwa na Mahakama ya Juu.
Waandamanao waliokuwa wamebeba matawi ya miti, mabango huku wakipiga yowe na honi za pikipiki walianzia barabara ya Obote wakaenda mtaa wa Oginga Odinga kabla ya kuchukua Barabara Kuu ya Kenyatta na baadaye Mtaa wa Ang’awa katikati ya jiji.

Mwigulu ‘awagomea’ Chadema



Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba 
Singida. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema hakuna haja ya kuanza kuhangaika kutafuta wachunguzi kutoka nje kwa ajili ya kufuatilia wahusika wa shambulizi la Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema), Tundu Lissu kwa vile vyombo vya ulinzi na usalama nchini vinajitosheleza na vina weledi na kazi hiyo.
Waziri huyo amesema haoni kwa nini baadhi ya watu wanasisitiza kuletwa kwa wataalamu wa nje kwani hata kama wataletwa bado watalazimika kufanya kazi kwa mazingira ya Kitanzania wakitumia wataalamu waliopo na hata ikiwekezana watahukumiwa kwa kutumia sheria za nchini.
“Nchi yetu inajitegemea hakuna haja ya kuleta vyombo vya nje kufanya uchunguzi...upelelezi utafanywa na vyombo vyetu, watafikishwa katika vyombo vya muhumu na watahukumiwa na watoto wetu,” alisema.
Hivi karibuni Chadema ilitaka wachunguzi nje kuendesha upelelezi kuhusiana na tukio la kushambuliwa kwa Lissu ikidai kuwa hatua yake hiyo haimaanishi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo bali vimetuhumiwa katika tukio hilo.
Hata hivyo, Waziri Nchemba alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama daima viko macho na vinaendelea na kazi ya kuwasaka wale wote wanaojihusisha na matukio ya kushambulia watu.
Amesema suala la uchunguzi haliwezi kukamilika kwa siku moja akitolea mfano jinsi Marekani ilivyotumia muda mwingi kumsaka mtuhumiwa wa ugaidi, Osama bin Laden aliyekuwa kiongozi wa kundi la Al Qaida.
“Uchunguzi hauna ukomo...unaisha pale tu wanapokamatwa wahusika wote lakini vinginevyo uchunguzi hauishi maana hata Marekani walimtafuta Osama kwa muda mrefu sana hawakusema sasa tumesitisha kumsaka,” amesema.
Kiongozi huyo wa Al Qaida aliuawa Mei 2, 2011 na vikosi vya Marekani vilivyoendesha operesheni maalumu iliyoratibiwa kutoka Pentagon na kufuatiliwa kwa karibu na Rais Barack Obama ambaye hivi sasa amestaafu.
Osama alikuwa amejichimbia katika maficho yake nchini Pakistan katika eneo lililojulikana Abbottabad.
Waziri Nchemba aliwatumia salamu wale wanaojulikana kama ‘watu wasiojulikana’ akisema kasumba ya wahalifu wachache kufanya mauaji na kisha kujinadi kwa jina la watu wasiojulikana inaelekea ukingoni.
Ameeleza kuwa dakika za wale wanaojihusisha na uhalifu huo kufikishwa kwenye mkono wa sheria zinahesabika.