Kampala, Uganda. Pendekezo tata la ukomo wa umri limezidi kuwa moto baada ya kuibuka fujo ndani ya Bunge muda mfupi baada ya Spika Rebecca Kadaga kusema Ratiba ya Shughuli za Bunge imefanyiwa marekebisho ili kuingiza pendekezo hilo tata la Mbunge wa Igara Magharibi, Raphael Magyezi.
Baadhi ya wabunge wa upinzani waliibuka na kudai kwamba mmoja wa wabunge aliingia bungeni na bunduki hali iliyozua hofu na fujo hadi baadhi kufikia kushikana mashati kutaka kupigana.
Shughuli za Bunge zilitatizika kwa dakika 20 huku Spika Kadaga akitumbua macho. Mbunge wa Busongora Kaskazini, William Nzoghu, alidai kwamba baadhi ya wabunge waliingia na bunduki na akaongeza kuwa hata Spika hakuwa salama kusimamia mjadala.
Mbunge wa Busiro Kusini Merdard Lubega Sseggona alimuomba spika aahirishe Bunge kwa sababu za kiusalama. Lakini Spika Kadaga alikataa akisema hawezi kuahirisha shughuli za bunge kwa kusikia uvumia tu.
Majibu hayo hayakutatua hali kwani wabunge walianza kuvurumishana. Kadri hali ilivyozidi kuzorota viti vilianza kurushwa na wabunge wakawa wanakimbilia maeneo salama huku wengine wakiwatuliza wenzao waliokuwa wanataka kumwaga damu ya wenzao.
Waziri wa Maji Ronald Kibuule ndiye alishutumiwa na wapinzani na wa kujitegemea kuwa aliingia na bunduki, madai ambayo aliyakanusha. Wabunge wa Kaunti ya Lwemiyaga, Theodore Ssekikubo na Kibuule walikunjiana ngumi wakitaka kutwangana.
Baadaye wabunge walitulia na ikatolewa amri ya kufanya msako kubani walioingia na bunduki.
Hoja ya ukomo wa umri ilitarajiwa kuwasilishwa mchana.
No comments:
Post a Comment