Sunday, August 13

TFF KUANZA KUCHAPISHA TAARIFA YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWENYE MAGAZETI


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na wajumbe wa TFF (hawapo pichani) baada ya kutangazwa na kuapishwa kwa viongozi wapya wa TFF Mkoani Dodoma.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Wallace Karia akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF kumwezesha kushika nafasi ya urais, wakati wa Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika katika Ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akiteta na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Michael Wambura (kushoto) baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa TFF uliofanyika jana katika ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma.

 Na Genofeva Matemu - WHUSM

Uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umetakiwa kufikia Januari mwakani kuwajibika kama mashirika mengine ya mpira wa miguu duniani yanavyowajibika kuchapisha taarifa ya mapato na matumizi kwenye magazeti ili wananchi wapate fursa ya kufahamu namna fedha zinavyopatikana na jinsi zinavyotumika katika kuboresha na kuendeleza usimamizi bora wa soka nchini.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na katika ukumbi wa St. Gasper Mkoani Dodoma Aidha Mhe. Mwakyembe amewapongeza viongozi wapya waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne kwa kuwataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku akiwapongeza washiriki wote waliothubutu kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi Mkuu wa TFF wa mwaka huu.

Kwa upande wake Rais mpya wa TFF Bw. Wallace Karia amewaahidi wapiga kuwa wake kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwani nafasi aliyopewa na wajumbe hao kwa kumuamini ni deni ambalo atalilipa kwa kuleta mafanikio makubwa katika mchezo wa soka.

Bw. Karia amesema kuwa furaha waliyonayo viongozi wote waliochaguliwa kuiongoza TFF kwa muda wa miaka minne iende kuwa furaha ya kazi kwa kufanya yale watanzania wanatarajia kutoka kwao.

RIDHIWAN KIKWETE :AHIMIZA WANANCHI WAJITOLEE KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

 Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan utete kata ya Pera,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan.
Balozi wa Pakistan nchini,Amir khan wa kushoto na Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete,wakizindua majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan utete kata ya Pera,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan.
Balozi wa Pakistan nchini Tanzania,Amir Khan akizungumza baada ya kuzindua majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu yaliyokarabatiwa na marafiki wa Pakistan katika shule ya msingi Pakistan utete iliyopo kata ya Pera,kushoto kwake ni Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete.
Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwan Kikwete kushoto akiagana na balozi wa Pakistan nchini Amir Khan baada ya kuzindua majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan utete kata ya Pera,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete,amewahimiza wananchi kujenga tabia ya kujitolea katika shughuli za kimaendeleo pasipo kuachia serikali/halmashauri na wahisani pekee.
Aidha amesema ofisi yake na halmashauri wataendelea kuunga mkono juhudi za wafadhili na wadau wanaojitokeza kushirikiana nao kutatua changamoto zinazowakabili jimboni hapo ikiwemo elimu.
Ridhiwani alitoa rai hiyo, wakati wa uzinduzi wa majengo ya madarasa sita na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Pakistan Utete iliyopo kata ya Pera,Chalinze wilayani Bagamoyo,yaliyokarabatiwa kwa ufadhili wa marafiki wa Pakistan,kwa gharama ya sh.milioni.30.
Alisema baadhi ya wafadhili wanasaidia endapo wanaona jamii husika ikichukua juhudi  na kufikia hatua mbalimbali .
Aliwataka wananchi wa Chalinze kushirikiana na serikali,halmashauri na wafadhili wanaojitokeza ili kukamilisha miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao.
“Ajenda kubwa tuliyonayo ni kuboresha na kutatua changamoto katika sekta ya elimu”
“Pamoja na shughuli zinazofanywa na wahisani lakini haina budi wananchi mkajitolea katika shughuli za maendeleo ili tukienda kuomba msaada kwa wafadhili waweze kukubali kirahisi kwa kuona hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa  “alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema wakati marafiki wa Pakistan wakiwezesha ukarabati huo,lakini halmashauri ya Chalinze imeshatenga fedha kwa ajili ya kujenga matundu ya vyoo nane katika shule ya Pakistan Utete.
Hata hivyo,mbunge huyo alieleza kwamba,pia wanajenga matundu ya vyoo katika shule ya msingi Mbala sanjali na madarasa mawili ya shule ya msingi Makombe.
Ridhiwani alieleza,ujenzi wa matundu ya vyoo utasaidia kuondoa kero ya uchafu wa mazingira ambapo baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijisaidia ovyo maporini ,vichakani .
“Kwasasa kilichobakia ni usimamizi katika hatua ya ujenzi unaoendelea kwenye shule hizo ”alisema Ridhiwani.
Akizungumzia msaada walioupata kutoka kwa marafiki wa Pakistan,Ridhiwani aliomba ushirikiano ulioonyeshwa usiishie hapo .
Alimpongeza mwenyekiti wa kitongoji Hussein Mramba na diwani wa kata ya Pera kwa jitihada walizozichukua kusukuma jambo hilo.
Ridhiwani hakusita kumuomba balozi wa Pakistan nchini Tanzania,Amir Khan ,kuwasaidia ujenzi wa jengo la kulaza wagonjwa  na mashine za kupima magonjwa katika kituo cha afya Chalinze.

Akizindua majengo hayo,balozi wa Pakistan nchini Khan,alisema amefurahishwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi hiyo na Tanzania,na alishauri kuwepo na mahusiano kati  ya wabunge wa Pakistan na Tanzania.

“Nilipoambiwa kuja shuleni hapa ni km 120 kutoka Dar es salaam nikaona nije kutembea na kuona kilichofanyika,Nawapongeza kwa kuanzisha ujenzi huu  ili watoto wapate elimu”alisema Khan.
Alisema ili watoto hao wasome vizuri ni vyema kukajengwa uzio katika shule hiyo ili kuweka usalama zaidi hivyo wanatasaidia kuujenga.
Balozi huyo,aliahidi na kukubali ombi la kusaidia mashine na vifaa vya kituo hicho cha afya lakini kwasasa wanachotakiwa kufanya ni kuandika maombi ya msaada huo.

WALLACE KARIA ASHINDA URAIS WA TFF

WALLACE KARIA ASHINDA URAIS WA TFF, MICHAEL WAMBURA KUWA MAKAMU WAKE




Azam TV – Hotuba ya kwanza ya Rais mpya TFF Wallace Karia mjini Dodoma
Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini TFF umehitimishwa kwa aliyekuwa makamu wa Rais wa Shirikisho hilo Wallace Karia  (kulia) kushinda kwa jumla ya kura 95 na kuwabwaga wapinzani wake.
Uchaguzi huo umefanyika leo mkoani Dodoma ukiwa wa amani kwa wajumbe wa mkutano mkuu pamoja na wagombea wenyewe.
Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi wa TFF, Wakili Revocatus Kuuli akitangaza matokeo hayo ambapo alimtangaza Wallace Karia kama mshindi wa kinyang'anyiro kwa kura 95 kati ya kura 127 zilizopigwa.



Wagombea Urais wa TFF na kura zao ni: Emmanuel Kimbe (1). Frederick Mwakalebela (3), Imani Madega (8), Richard Shija (9)  Ally Mayai  (9) na Wallace Karia  (95).
Kuuli ametangaza kuwa, katika nafasi ya makamu wa Rais, Michael Richard Wambura (kushoto) ameshinda nafasi hiyo kwa kura 85.
Kwa upande wa wajumbe wa mkutano mkuu kumekuwa na maingizo mapya kutoka kanda mbalimbali za nchini kama ifuatavyo:
Zone 1: Saloum Chama 
Zone 2: Vedastus Lufano 
Zone 3: Mbasha Matutu 
Zone 4: Sarah Chao 
Zone 5: Issa Bukuku 
          Zone 6: Kenneth Pesambili 
Zone 7: Elias Mwanjala 
Zone 8: James Mhagama 
Zone 9: Dunstan Mkundi 
                                                    Zone 10: Mohamed Aden 
                                                 Zone 11: Francis Ndulane 
                                              Zone 12: Khalid Abdallah 
                                                 Zone 13: Lameck Nyambaya

IGP SIRRO AWAAGA ASKARI NA MAOFISA WANAOKWENDA SUDANI




Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akiwakabidhi bendera ya taifa askari kumi (10) waliopata uteuzi wa kwenda kuiwakilisha nchi ya Tanzania kwenye kazi ya Ulinzi wa Amani nchini Sudani ya Kusini (UNMISS) IGP Sirro, amewataka askari hao kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya sheria na taratibu. Picha na Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akiwa kwenye picha ya pamoja na askari waliopata uteuzi wa kwenda kuiwakilisha nchi ya Tanzania kwenye kazi ya Ulinzi wa Amani nchini Sudani ya Kusini (UNMISS) IGP Sirro, amewataka askari hao kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya sheria na taratibu. Picha na Jeshi la Polisi.

WAZIRI MKUU ASEMA SERIKALI ITALIPA MADENI YOTE YA WATUMISHI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali italipa madeni yote ya watumishi ambayo yamehakikiwa na kukutwa kuwa ni halali. 

“Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli alisitisha malipo sababu ya zoezi la kubaini watumishi hewa, sasa kazi hiyo imeshakamilika, yale yaliyobainika kuwa ni halali yatalipwa. Tunataka watumishi mfanye kazi ya kuwahudumia wananchi kwa bidii,” alisema.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Agosti 12, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora. 

Akiwa katika wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui, Waziri Mkuu alielezwa na baadhi ya wabunge wa mkoa huo kwamba kuna watumishi ambao walihamishwa kutoka manispaa kwenda wilaya za jirani lakini hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu ambaye ameweka utaratibu wa kukutana na watumishi wa umma kila anapofanya ziara za kikazi mikoani, aliwaeleza watumishi wa wilaya hizo kwamba Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.

“Hivi sasa tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni ya matibabu, ya likizo au ya masomo. Kila mtumishi anaruhusiwa kujiendeleza, lakini ni lazima kwanza aandike barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuelezea nia yake na akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi kwenye vyuo. Mtumishi akiamua kuomba chuoni moja kwa moja ndipo alete madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni nje ya utaratibu,” alisema.

Akifafanua utendaji kazi wa mfumo huo, Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa  na kwamba unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha  taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja ama kustaafu.

Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.

“Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo,” alisema.

“Mimi nimekuwa kwenye utumishi wa umma kwa muda mrefu, sijawahi kuona mtu anaandikiwa barua ya kupandishwa daraja halafu anakataa. Kikubwa ni kwa maafisa utumishi kuona kama kuna watumishi wanastahili kupandishwa madaraja, watume taarifa zao mapema (kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi ili waingizwe kwenye mfumo huu, kisha wawaandikie barua za kuwajulisha wahusika. Hata barua ikichelewa kumfikia mtumishi, mshahara wake hautachelewa na kwa njia hii tutaepuka kuweka madeni yasiyo na tija,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.

“Napenda kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha utendaji wa watumishi lakini pia Serikali hii haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na mla rushwa. Tukikukamata hatuundi tume kwa sababu tume nazo zinamaliza fedha tu. Tukiwa na ushahidi wa kutosha, tunamalizana hapohapo,” aliongeza.

Magufuli afuta shamba jingine la Sumaye


Waziri Mkuu wa mstaafu, Frederick Sumaye ameingia matatani tena baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kumpokonya shamba lake lenye ukubwa wa ekari 326 kwa madai ya kutoendelezwa huku ikisema Rais John Magufuli ameridhia hatua hiyo.
Hili ni shamba la pili Sumaye kunyang’anywa baada ya ekari 33 zilizopo eneo la Mabwepande kuchukuliwa Novemba mwaka jana huku Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi akisema Serikali ilifikia uamuzi huo baada ya kiongozi huyo mstaafu kushindwa kuliendeleza kama notisi ya siku 90 ilivyoeleza.
“Oktoba 28, mwaka huu, Rais John Magufuli alibatilisha hati ya kumiliki ardhi ya shamba namba 3,074 lililopo Mabwepande. Shamba hilo lilikuwa na hati namba 53086. Jina la mmiliki lililoandikwa katika hati ni Frankline Sumaye,” alisema Hapi.
Jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero, Frolent Kyombo alisema Rais Magufuli amekubali kufutwa kwa umiliki wa shamba hilo kupitia ilani ya ubatilisho ya Mei mwaka huu.
Kabla ya kupokonywa shamba hilo, Kyombo alisema Sumaye alipewa notisi ya siku 30 iliyomtaka kueleza sababu za kutoendeleza matumizi ya shamba hilo kwa shughuli za kilimo kama lilivyosajiliwa lakini hakutoa sababu zilizoweza kushawishi kutofanyika kwa mabadiliko hayo.
“Hatua ya pili, tukatoa ilani ya ubatilisho wa shamba hilo, kuna maelezo alitoa lakini tuliona hayakuwa na uzito, tukayatupilia mbali, shamba hilo alikuwa anaendesha shughuli za kilimo pamoja na ufugaji. Alikuwa anatumia asilimia 15 hadi 20 tu ya shamba lote,” alisema Kyombo.
Alisema mbali na kutumia sehemu ndogo huku nyingine ikiwa haitumiki, Mwenyekiti huyo wa Chadema Kanda ya Pwani alikuwa amekiuka Sheria ya Mipango Miji, namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999.
“(Sumaye) alitakiwa kutumia shamba hilo kwa ajili ya kilimo tu na siyo kwa shughuli nyingine za ufugaji, hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria hizo. Kwa hiyo mchakato umeashaanza wa kuligawa shamba hilo kwa wananchi na tunategemea miezi minne ijayo tutakuwa tumemaliza taratibu zote,” alisema.
Desemba 15, 2015, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza kiama kwa watu wanaomiliki mashamba bila kuyaendeleza huku wakiyatumia kama dhamana ya kukopea fedha benki.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli, alisema kuna watu wamehodhi mashamba makubwa lakini hawayaendelezi, hawayalipii kodi na mbaya zaidi, wanayatumia kukopa fedha benki.
Kabla ya DED huyo kulithibitishia Mwananchi habari hizo, mapema asubuhi ya jana, taarifa iliyoelezwa kuwa imeandikwa na Sumaye, ilisambaa kwenye mitandao ya jamii ikieleza hatua kwamba Rais Magufuli amechukua shamba jingine la kiongozi huyo.
“Mtakumbuka baada tu ya kuingia Serikali hiyo madarakani, ilitishia muda mrefu kuchukua mashamba yangu bila sababu za msingi, hata wakati wa kampeni baadhi ya viongozi wa CCM walitamka hadharani kuwa huyu dawa yake ni kumnyang’anya mashamba yake,” taarifa hiyo inamnukuu Sumaye.
Hata hivyo, akizungumza hatua za upokonyaji wa mashamba yasiyoendelezwa katika Halmashauri ya Mvomero, Kyombo alisema katika awamu ya kwanza mwaka 2014, iliorodhesha mashamba makubwa 63 na saba kati ya hayo, Rais Magufuli aliyafuta.
“Awamu ya pili nikiwa tayari DED wa Mvomero, tuliwasilisha mapendekezo ya ubatilisho kwa mashamba matatu na yote Rais Magufuli aliyafuta, yalikuwa na ukubwa tofauti. Kwa sasa tumepeleka mapendekezo ya ubatilisho wa mashamba mengine manne kwa Rais, lakini bado hayajajibiwa,” alisema Kyombo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendelezo ya Makazi, utaratibu wa ilani ya ubatilishaji umeanza kufanyika baada ya Serikali kuagiza halmashauri zote nchini kukagua mashamba na kuwasilisha taarifa zake wizarani kwa hatua stahiki ili kama kutakuwa na ambayo hayajaendelezwa, wakurugenzi husika watume ilani hizo kwa wamiliki.
Baada ya siku 90 kumalizika, halmashauri hizo zitatakiwa kuwasilisha mapendekezo ya ubatilisho wizarani.
Akizungumzia ubatilishwaji huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Jonas Zeeland alisema walipewa taarifa hiyo katika baraza la madiwani lililokutana Ijumaa Agosti 11.
“Ni kweli umiliki wa shamba hili umebatilishwa kutoka kwa Sumaye na taarifa tulipewa jana (juzi) kwenye kikao cha baraza,” alisema Zeeland.
Mwenyekiti huyo alimpongeza Rais kwa kuridhia kubatilisha umiliki wa shamba hilo akisema kwa muda mrefu walikuwa wakiomba warejeshewe.
Alisema bado kuna mashamba mengi katika halmashauri hiyo ambayo hayajaendelezwa hivyo amemuaomba Rais kuharakisha ubatilishaji wake ili waweze kuyapangia matumizi mengine.
Hata hivyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Mashariki, Juliana Pilla alisema mashamba waliyoombea kubatilishwa ni zaidi ya ekari 30,000.
“Kuna wamiliki wamesharejea na kuanza kuendeleza mashamba yao baada ya kutoa notisi, kama Mvomero waliombea mashamba 26 lakini hadi sasa wamiliki 17 wamesharudi na wanaendeleza mashamba yao,” alisema kamishna huyo.
Alisema ameziagiza Halmashauri zote kufanya uhakiki kwa mara ya mwisho ili mashamba hayo yabatilishwe huku akizitaja wilaya za Mvomero, Morogoro na Kilosa kuwa ndizo zenye mashamba mengi yasiyoendelezwa.
Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 10 mfululizo kuanzia Novemba 27, 1995 mpaka Desemba 28, 2005, alisema hawezi kuzungumza suala hilo mpaka atakapowasiliana na mawakili wake.

RAIS MSTAAFU AWAMU YA PILI ALI HASSAN MWINYI AWAASA MADEREVA KUZINGATIA SHERIA ZA BARABARANI ILI KUEPUSHA AJALI


Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, akisikiliza maelezo kutoka kwa Inspekta Ibrahim Samwix, wakati alipotembelea mabanda mbalimbali kwenye Tamasha la Usalama Barabarani lililofanyika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi (aliyevaa suti), akisikiliza maelezo jinsi uvunjaji wa sheria za usalama barabarani unavyoweza kusababisha ajali, wakati alipotembelea banda la Maaskari wa usalama barabarani, kwenye Tamasha la Usalama Barabarani lililofanyika jana Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akimkabidhi tuzo Mgeni Rasmi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, wakati wa Tamasha la Usalama Barabarani lililofanyika jana Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani (kushoto), akipokea zawadi kutoka kwa Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwa kutambua mchango wake katika suala nzima la Usalama Barabarani wakati wa Tamasha la Usalama Barabarani lililofanyika jana, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.Kulia ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 
Balozi wa Usalama Barabarani, Samira Abuu (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,Mhandisi Hamad Masauni, baada ya kupokea cheti cha kutambua mchango wake katika masuala ya Usalama Barabarani wakati wa Tamasha la Usalama Barabarani lililofanyika jana, Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 
Mgeni Rasmi,Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, akizungumza wakati wa Tamasha la Usalama Barabarani ambapo aliwaasa watumiaji wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazosababisha ulemavu na vifo.Tamasha hilo limefanyika jana, Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Muda wa uhakiki wa mashirika binafsi wasogezwa

Muda wa uhakiki wa mashirika yasiyo ya kiserikali umeongezwa kutoka siku 10 hadi siku 14.
Awali Msajili wa mashirika hayo, alitangaza kuwa usajili ungechukua siku 10 kuanzia Agosti 21 hadi Agosti 31 lakini sasa utamalizika Septemba 4,mwaka huu.
Akizungumza leo Jumapili,Katibu wa Baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali,Ismael Suleiman amesema wanamshukuru msajili kwa kuongeza muda.
Amesema kuongezwa kwa muda huo kutayawezesha mashirika hayo zaidi ya 8000 kufanya uhakiki.
Amesema walihitaji muda zaidi kwa sababu usajili huo unafanyika kwenye kanda tano hivyo wahusika wanahitaji kusafiri umbali mrefu.

Wananchi watakiwa kuchangamkia fursa


Ili kuendana na sera ya awamu ya tano ya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025,  vijana wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa nchini ili kwenda sambamba na sera hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Raisi wa Kujitegemea (PTF) , Haighat Kitala, ameyasema hayo leo wakati walipotembelea wajasiriamali walionufaika na mkopo unaotolewa na mfuko huo.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 mfuko huo , umetoa mikopo 2,093 yenye thamani ya Sh 1.37bilioni ambapo  Sh 209 milioni kati ya hizo zilitolewa kwa vijana wa kiume na Sh 1.16 bilioni kwa vijana wa kike na wanawake.
Kitala amesema kiasi hicho cha fedha kimetolewa katika mikoa  mitano inayohudumiwa na mfuko huo ambayo ni  Dar Es Salaam, Pwani, Morogoro, Njombe na Lindi
"Hivyo  badala ya vijana kusubiria kuajiriwa, wanafursa ya kujiunga katika vikundi na hivyo kuwa rahisi kwa wao kupata mkopo ambao utawainua kwa kukuza kipato chao pamoja na kukuza uchumi" amesema Kitala .
"Vile vile mfuko  huu unatoa mkopo kwa kundi maalumu la walemavu na vijana waliookolewa kutoka katika matumizi ya dawa za kulevya" ameongeza
Kitala amefafanua kuwa katika kipindi hicho wametoa mafunzo  kwa vijana na wanawake 2,956, huku wateja wapya ambao wamejiunga na mfuko huo wakiwa 1410.
"Lakini tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, PTF imetoa mikopo 2,856 yenye thamani ya Sh.1.8 bilioni ambapo Sh 346 milioni kati ya fedha hizo zilitolewa kwa vijana wa kiume na Sh 1.5bilioni zilitolewa kwa vijana wa kike na wanawake,
" Pia katika mwaka huo 2015 tumefanikiwa kutoa  mafunzo kwa vijana na wanawake 4,470, huku wateja wapya waliojiunga na mfuko huu wakiwa 1992 " amebainisha Kitala.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko huo,  Nattu Msuya amesema lengo la kutembelea wajasiliamali hao ni kuona kuwa mkopo huo umetolewa kwa walengwa ambayo wamekidhi vigezo vilivyowekwa na mfuko au laa.
"Tumekagua miradi ili tuweze kupata mrejesho kwa hawa wajasiriamali waliopata mikopo kama waliipata bila kuzungushwa na maafisa mikopo wetu na je wamezionaje huduma zetu,  lakini pia  tulitaka kujiridhisha kama walengwa wa mikopo hii wamepitia katika vyuo vya ufundi stadi" amesema Msuya.
Kwa upande wao Jackline Magheme na Aneth Gerana ambao ni wanufaika wa mkopo , wamesema kuwa mkopo waliochukua umewasaidia kutengeneza ajira za watu wengine zaidi ya 20 kupitia vikundi vyao.
Naye, Ebeneza Habati ambaye ni fundi selemala amesema mkopo aliochukua umemuwezesha kununua kiwanja lakini  baada ya kumaliza kulipa mkopo , ataomba mwingine kwa ajili ya kufungua ofisi kubwa.

Uingereza yashauri uwekezaji nchini


Watanzania wameshauriwa kuwekeza kwenye viwanda vya kisasa vya machinjio ya nyama ili viweze kuongeza thamani ya mifugo yao na kuweza kupata soko la uhakika nje ya nchi.
Hayo yalisemwa jana na Meneja masoko wa Afrika mashariki ,Gaula Willard kutoka kampuni ya Abachem Engineering ya Uingereza inayojihusisha na ujenzi wa viwanda vya machinjio ya kisasa.
Amesema kuwa, Tanzania kuna fursa kubwa Sana ya kuwekeza kwenye viwanda vya nyama kutokana na kuwa ndio nchi yenye mifugo mingi na hivyo kuna umuhimu wa kuwekeza kwenye viwanda vya machinjio ya kisasa ili kuongeza thamani ya mifugo .
Gaula alisema kuwa, wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika machinjio ya kisasa ambapo wameweza kufunga viwanda vya machinjio ya nyama 80 duniani.
"Kwa sasa hivi tumeamua kuja Tanzania kwani kuna fursa kubwa Sana na tunataka kuleta utaalamu wetu hapa nchini kwa kuhakikisha kunakuwepo na viwanda vya kisasa Kama vya wenzetu wa nje ya nchi ambavyo Vina uwezo wa kuhudumia mifugo mingi kwa wakati mmoja kutokana na teknolojia zilizopo "amesema Gaula.

Nchemba ashangazwa na kituo cha polisi


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba ametembelea kituo cha polisi cha wilaya ya mkalama mkoani singida kuangalia hali ya kituo na utendaji kazi wa askari polisi na mazingira wanayofanyia kazi askari hao.
Waziri Mwigulu amejionea hali ambayo si nzuri ya kituo cha polisi cha wilaya ya mkalama ambayo ni wilaya mpya iliyomegwa kutoka wilaya ya Iramba.
Waziri huyo alisema kwamba kituo hiki cha wilaya ya mkalama hali si nzuri kwani ni chakavu sana na kidogo ambacho kina mahabusu moja ya wanaume tu huku wanawake wakiwekwa mapokezi.
Waziri Mwigulu amesema atakaa na wenzake wa wizarani akiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro kupanga utaratibu wa kumalizia ujenzi wa vituo vyote polisi ambavyo ujenzi wake umekwama hasa wa hizi wilaya ya mpya ambazo zimemegwa katika wilaya mama.
 Amewahidi kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na mkuu wa wilaya ya mkalama kuwa ujenzi wa kituo hicho utaisha na anakwenda kuonana na IGP kupanga kumalizia ujenzi wa vituo hivyo mapema.
Naye Kamanda wa Polisi wilaya ya Mkalama (OCD) John Ntilima amesema kwasasa wanatumia kituo kidogo cha polisi Nduguti kama kituo cha polisi cha wilaya ambacho ni kidogo sana hakitoshelezi kwa ufanyaji kazi wake kwani wanatumia ofisi tatu ambazo ni mbovu na chakavu  hivyo wana ujenzi wa kituo kikubwa cha kisasa lakini wamekwama kumalizia na kumuomba waziri awasaidia katika kukamilisha hilo.

Mbunge alia na unyanyasaji



Mbunge wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Anatropia Theonest(Chadema) amesema watoto 244 wamefanyiwa vitendo vya unyanyasaji katika halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka huu. 
Akizungumza leo, Agosti 13 Mbunge huyo amesema takwimu zilitolewa na Idara ya Ustawi wa jamii kwenye baraza la Madiwani zimeonyesha kati yao 85 walibakwa, 74 wakitelekezwa na 20 walilawitiwa.
Amesema matukio hayo yameongezeka kutoka 107 mwaka 2006 huku mtoto wa kike akiwa kwenye hatari ya kukosa haki ya elimu kutokana na kupata mimba.
"Ni lazima tusimame kwa pamoja tuweze kupaza sauti kwasababu tukiacha vitendo hivi viendelee tutajenga kizazi cha aina gani? cha walemavu?,"alisema 
Aidha, amesema atawasilisha bungeni hoja binafsi ya kutaka marekebisho ya Sheria ya mwaka 1979 ili kuwapa haki watoto wanaopata mimba kupata haki ya kuendelea na masomo.

Lukuvi ataka vibali vya ujenzi vitolewe haraka



Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza viongozi wa halmashauri na majiji nchini kuharakisha utoaji wa vibali vya ujenzi na kuachana na urasimu unaosababisha kuwepo kwa ujenzi holela .
Lukuvi ameyasema  hayo alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa nyumba  kumi za  mfano za mradi wa mji wa kisasa wa  Safari City  zilizopo eneo la Mateves sambamba  na kutoa hati miliki kwa wanunuzi 100 wa kwanza wa viwanja zinazotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Amesema kuwa kumekuwepo na ucheleweshaji mkubwa wa vibali vya ujenzi unaosababishwa na wahusika wenyewe na hivyo kuchangia  wananchi hao kujenga kiholela kutokana na kuchoka kusubiri  kwa muda mrefu. 
Aidha kufuatia hali hiyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kufanya ukaguzi wa mafaili ya vibali vya ujenzi na kuweza kugundua idadi ya watu ambao hawajapatiwa vibali vyao mpaka sasa hivi.
"Unajua idadi kubwa ya wananchi wanaojenga kiholela siyo kwamba wamevunja sheria bali wanafanya hivyo kwa ajili ya ucheleweshaji wa vibali  na msiwalazimishe wananchi kusubiri kwa muda mrefu sana bila kuwapatia majibu yanayoeleweka kwani nyie wenyewe ndio mtakuwa mnachangia ujenzi holela. "amesema Lukuvi. 
Lukuvi amesema kuwa, ni aibu na fedheha wananchi kukaa katika maeneo holela kwani wanachangia kuharibu madhari ya Jiji ,na hivyo kuwataka kujenga maeneo yaliyopimwa. 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nyumba la taifa Nehemia Mchechu amesema kuwa mradi huo wa kitovu cha mji wa kisasa wa safari city jijini hapa una ukubwa wa hekari 559.4 na ni sehemu ya miji iliyopangiliwa kitaalamu na kwa kuzingatia sheria za mipango miji.
"Mradi huu ulibuniwa na shirika la nyumba kwa lengo la kupunguza uhaba wa makazi kwenye jiji hili ambapo tumetenga maeneo kwa ajili ya waendelezaji kujenga sehemu za biashara,burudani ,utalii,hospitali, elimu,huduma za kijamii kama vile polisi,na zimamoto lakini pia yapo maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo na mapumziko"amesema Msechu.