Sunday, August 13

Wananchi watakiwa kuchangamkia fursa


Ili kuendana na sera ya awamu ya tano ya Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025,  vijana wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa nchini ili kwenda sambamba na sera hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Raisi wa Kujitegemea (PTF) , Haighat Kitala, ameyasema hayo leo wakati walipotembelea wajasiriamali walionufaika na mkopo unaotolewa na mfuko huo.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 mfuko huo , umetoa mikopo 2,093 yenye thamani ya Sh 1.37bilioni ambapo  Sh 209 milioni kati ya hizo zilitolewa kwa vijana wa kiume na Sh 1.16 bilioni kwa vijana wa kike na wanawake.
Kitala amesema kiasi hicho cha fedha kimetolewa katika mikoa  mitano inayohudumiwa na mfuko huo ambayo ni  Dar Es Salaam, Pwani, Morogoro, Njombe na Lindi
"Hivyo  badala ya vijana kusubiria kuajiriwa, wanafursa ya kujiunga katika vikundi na hivyo kuwa rahisi kwa wao kupata mkopo ambao utawainua kwa kukuza kipato chao pamoja na kukuza uchumi" amesema Kitala .
"Vile vile mfuko  huu unatoa mkopo kwa kundi maalumu la walemavu na vijana waliookolewa kutoka katika matumizi ya dawa za kulevya" ameongeza
Kitala amefafanua kuwa katika kipindi hicho wametoa mafunzo  kwa vijana na wanawake 2,956, huku wateja wapya ambao wamejiunga na mfuko huo wakiwa 1410.
"Lakini tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, PTF imetoa mikopo 2,856 yenye thamani ya Sh.1.8 bilioni ambapo Sh 346 milioni kati ya fedha hizo zilitolewa kwa vijana wa kiume na Sh 1.5bilioni zilitolewa kwa vijana wa kike na wanawake,
" Pia katika mwaka huo 2015 tumefanikiwa kutoa  mafunzo kwa vijana na wanawake 4,470, huku wateja wapya waliojiunga na mfuko huu wakiwa 1992 " amebainisha Kitala.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko huo,  Nattu Msuya amesema lengo la kutembelea wajasiliamali hao ni kuona kuwa mkopo huo umetolewa kwa walengwa ambayo wamekidhi vigezo vilivyowekwa na mfuko au laa.
"Tumekagua miradi ili tuweze kupata mrejesho kwa hawa wajasiriamali waliopata mikopo kama waliipata bila kuzungushwa na maafisa mikopo wetu na je wamezionaje huduma zetu,  lakini pia  tulitaka kujiridhisha kama walengwa wa mikopo hii wamepitia katika vyuo vya ufundi stadi" amesema Msuya.
Kwa upande wao Jackline Magheme na Aneth Gerana ambao ni wanufaika wa mkopo , wamesema kuwa mkopo waliochukua umewasaidia kutengeneza ajira za watu wengine zaidi ya 20 kupitia vikundi vyao.
Naye, Ebeneza Habati ambaye ni fundi selemala amesema mkopo aliochukua umemuwezesha kununua kiwanja lakini  baada ya kumaliza kulipa mkopo , ataomba mwingine kwa ajili ya kufungua ofisi kubwa.

No comments:

Post a Comment