Mikakati hiyo inayotekelezwa kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau wengine wa sekta hiyo, inalenga kuongeza idadi ya watalii kutoka nchini Marekani kufikia 300,000 kwa mwaka kutoka 60,000 wa sasa.
Mpango wa kuongeza watalii kutoka nchini Marekani ifikapo 2020, unatekelezwa kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Mafanikio tayari yameanza kuonekana baada ya idadi ya watalii wanaotembelea nchini kufikia zaidi ya milioni 1.3, huku Taifa likiingiza zaidi ya Dola 1.9 bilioni za Marekani kwa mwaka.
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane haipo nyuma katika utekelezaji wa mikakati hiyo baada ya kuzindua kampeni maalumu ya siku kumi ya kuanzia Aprili Mosi hadi 10, kwa kutoa mafunzo ya uhifadhi na utalii wa ndani kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu jijini Mwanza.
Mhifadhi Mkuu wa Kisiwa cha Saanane, Abel Mtui anasema kampeni hiyo imelenga kuwafikia zaidi ya wanafunzi 5,000 kutoka vyuo vya Mtakatifu Augustine (Saut) Mwanza, Chuo cha Mipango, Chuo cha Biashara (CBE), Chuo cha Tiba Bugando (CUHAS) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).
Akizungumza ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Mtui amesema licha ya elimu kwa vitendo na kutembelea hifadhi, wanafunzi hao watapata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu masuala ya uhifadhi miongoni mwao na watumishi wa Tanapa.
Kisiwa cha Saanane ndiyo pekee kati ya hifadhi za Taifa 16 zilizopo nchini ipo katikati ya mji ukiwa na vivutio kadhaa, wakiwamo Simba jike na dume walioko kwenye banda maalumu, pundamilia wapole ambao wageni wanaweza kupiga nao picha kwa mtindo wa selfie, swala, nguchiro, tumbuli na aina mbalimbali za ndege wakiwamo tausi.
Pia, kuna mawe yaliyobebana na mengine kusimama yenyewe yenye urefu wa zaidi ya mita 20, maeneo ya kupumzikia na kupiga picha na mwamba mkubwa ambao mtu akiruka juu yake na kupigwa picha, huonekana kama anayepaa juu ya maji ya Ziwa Victoria.
Hifadhi zingine nchini ni Arusha, Gombe, Katavi, Mlima Kilimanjaro, Kitulo, Milima ya Mahale, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Kisiwa cha Rubondo, Saadani, Serengeti, Tarangire, Manyara na Milima ya Udzungwa.
“Uhifadhi ni ajenda endelevu inayotakiwa kuhusisha makundi yote ya kijamii; tumeanza na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu kabla ya kufikia makundi mengine wakiwamo wanafunzi wa shule za sekondari na msingi,” anasema Mtui.
Anasema kampeni hiyo itatumika kusajili mabalozi wa uhifadhi wa Kisiwa cha Saanane miongoni mwa wanafunzi, ambao watatumika kuhamasisha utalii wa ndani badala ya kutegemea watalii kutoka nje ya nchi.
Mmoja wa waandaaji wakampeni hiyo, mhadhiri wa Saut, Judith Wanga anasema elimu kwa umma ikitiliwa maanani siyo tu itarahisisha kazi ya ulinzi wa rasilimali za Taifa, bali itapunguza gharama zinazotumika kuhifadhi na kulinda rasilimali hizo kwa njia ya sheria na adhabu.
“Elimu shirikishi itawapa wananchi fursa ya kuelewa umuhimu na faida ya kuhifadhi; jamii iliyoelimika na inayoona fadia italinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa. Tuanze kujenga uelewa huo kwa vijana ambao ndiyo Taifa la kesho,” anasema Judith.
Ofisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Michael anaunga mkono hoja ya elimu kwa umma itakayohimiza uhifadhi na ulinzi shirikishi kwa jamii na hatimaye kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii hasa utalii wa ndani.
Vivutio na watalii
Licha ya hifadhi na mbuga zenye wanyama wengi na misitu, Tanzania imejaaliwa vivutio kadhaa vya utalii vikiwamo maeneo ya kihistoria na ya kiakiolojia, fukwe zisizochafuliwa na wingi wa utamaduni wa makabila 158.
Mwambao wa bahari wenye urefu wa zaidi ya kilomita 804, visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia, Ziwa Victoria ambalo ni pili duniani kwa ukubwa na chanzo cha mto Nile na Ziwa Tanganyika ambalo ni la pili kwa kina kirefu duniani na la kwanza barani Afrika, ambalo ni miongoni mwa vivutio vinavyoipa sifa Tanzania.
Mwaka jana, mtandao wa Kimataifa wa SafariBookings.com uliitangaza Tanzania kuwa kituo bora kwa utalii barani Afrika baada ya kuchambua maoni kutoka kwa zaidi ya watalii 2,500 waliotembelea nchi za Afrika, wengi waliitaja Tanzania kuwa bora kuliko nchi nyingine kwa kuwa na eneo kubwa lenye wanyamapori wengi na misitu inayovutia.
Baadhi ya watu mashuhuri duniani akiwamo mwanamuziki wa Marekani, Usher Raymond, mwanasoka David Beckham aliyewahi kuchezea timu ya Taifa ya Engalnd na timu za Manchester United na Real Madrid wametembelea vivutio vya utalii nchini katika miaka ya hivi karibuni.
Mcheza filamu maarufu wa Marekani, Will Smith, mchezaji wa zamani wa timu ya Liverpool ya Uingereza, Mamadou Sakho na Morgan Schneiderlin wa timu ya soka ya Everton, pia wametembelea nchini kwa nyakati tofauti.
No comments:
Post a Comment