Wednesday, April 4

Miezi mitatu ya mjadala Bunge la bajeti Dodoma


Dar es Salaam. Kuanzia leo, wabunge wanatarajia kutumia takriban miezi mitatu kujadili Bajeti ya Taifa kwa mwaka ujao wa fedha.
Katika bajeti iliyopita, moja ya mambo ambayo yaliwavutia wengi ilikuwa ni kufutwa kwa tozo ya barabara (road license) na kuondoa ushuru wa mazao chini ya tani moja yanayosafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kingine kilichopendezesha mjadala wa Bunge la Bajeti lililopita ni mabadiliko ya sheria tatu za madini ambazo zilikuwa na michango iliyokinzana kutoka kwa wawakilishi hao 364 wa wananchi.
Baada ya bajeti hiyo ya 2018/19, itabaki nyingine moja ya 2019/2020 kuhitimisha awamu ya kwanza ya miaka mitano ya Rais John Magufuli kumalizika.
Wakati wadau wa Serikali za Mitaa wakiendelea kukuna vichwa kutafuta vyanzo mbadala, vya kudumu kuziba pengo lililoachwa baada ya kodi ya majengo kuhamishwa, vipaumbele vipya vinatarajiwa kubainishwa kwenye mjadala huu.
Majibu yanayosubiriwa
Wakati wananchi wakisubiri kufahamu vipaumbele vya mwaka ujao wa fedha, yapo maeneo yaliyopendekezwa kufanyiwa kazi kwenye bajeti inayoendelea kutekelezwa ambayo bado hayajaonyesha mafanikio.
Baadhi ya changamoto za utekelezaji wa bajeti zimekuwa zikijirudia mara nyingi hivyo kero zake kuendelea kuwasumbua wananchi na wabunge wanatarajiwa kuzijadili na kutafuta suluhu kuanzia leo, vikao hivyo vinapoanza.
Kilimo
Kwa muda mrefu, tangu kupitishwa kwa Azimio la Maputo mwaka 2003 linalozitaka Serikali kuelekeza asilimia 10 ya bajeti nzima kwenye kilimo, Tanzania haijawahi kufanya hivyo. Kwenye bajeti ya mwaka 2017/18, ni Sh267.86 bilioni pekee kati ya Sh31.7 trilioni zilitengwa kwa ajili ya Wizara ya Kilimo sawa na asilimia 4.8.
Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alisema kila nchi ina mfumo tofauti wa kusimamia sekta zake na kwamba suala lililopewa uzito katika bajeti ya 2017/18 ni upatikanaji pembejeo.
“Azimio la Maputo halizungumzii mifumo ya nchi mbalimbali. Kwa mfano, sisi mfumo wetu wa kilimo unashikiliwa na wizara nyingi siyo ya kilimo tu. Kwa hiyo, ukijumlisha mchango wa wizara zote zinaweza kufikia hiyo asilimia 10,” alisema Dk Tizeba.
Katiba na Sheria
Miongoni mwa vipaumbele vya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria mwaka 2017/18 ilikuwa kukuza na kutetea haki za binadamu hususan makundi yenye mahitaji maalumu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Hata hivyo, wizara hiyo itapaswa kuandaa majibu ya kutosha kuhusiana na madai ya kutokuwapo kwa uhuru wa kujieleza. Katika suala la utoaji haki za binadamu, wakili wa kujitegemea, Harold Sungusia anasema Tanzania imerudi nyuma.
“Taifa tumerudi nyuma, hata simung’unyi maneno. Uhuru wa kujieleza umepotea kabisa. Hata haki ya kupata habari za Bunge imeminywa tofauti na zamani ambapo watu waliangalia Bunge moja kwa moja ‘live’. Hata kwenye mitandao ya jamii watu hawako huru kutoa maoni yao,” alisema.
Sungusia alitoa mfano wa uvunjaji wa nyumba zilizojengwa kwenye hifadhi ya barabara uliofanyika katika Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam kwamba wapo baadhi ya waathirika ambao walikuwa na zuio la Mahakama, lakini nyumba zao zilivunjwa.
Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Jesse James alisema: “Hakuna fedha ilitengwa kwa ajili ya mabadiliko ya Katiba jambo linalomaanisha hakutakuwa na mchakato huo. Hata Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora haipati bajeti ya kutosha, kwa hiyo usitegemee ufanisi mkubwa.”
Viwanda
Tangu mwishoni mwa mwaka jana, kumekuwa na changamoto ya sukari ya viwandani ambayo ni muhimu kwa uzalishaji wa bidhaa zao.
Mbali ya changamoto hiyo, mkuu kitengo cha ununuzi wa kampuni ya dawa ya Shelys Pharmaceuticals, James John alisema hata ulipaji wa kodi za aina mbalimbali unapaswa kutazamwa upya.
“Tunaambiwa tulipe VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) kwenye vifungashio pamoja na malighafi ingawa zina msamaha. Hutukuchukua zaidi ya wiki kufuatilia suala hilo hivyo kulazimika kulipa gharama za kutunza mzigo bandarini kwani Mamlaka ya Bandari hutoa siku saba tu mhusika awe amekamilisha utaratibu wote na kuondoka na mzigo wake” alisema.
Maeneo mengine ambayo sekta binafsi inapenda yafanyiwe marekebisho ni kodi ya kampuni, malipo ya makandarasi na waliotoa huduma serikalini, fidia ya asilimia 15 ya uagizaji wa sukari ya viwandani.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi alisema endapo mfumo wa kodi utaangaliwa na kufanyiwa marekebisho muhimu, “Tutashuhudia ongezeko kubwa la biashara hivyo kuimarisha mzunguko wa fedha.”
Mazingira bora pia ni kilio cha wasanii wa muziki na sinema. Baada ya nyimbo kadhaa kufungiwa baadhi walilalamika kutoungwa mkono na Serikali. Bunge litalazimika kutafuta majibu ya namna ya kuwawezesha wasanii hao pamoja na wanamichezo.
Elimu
Ukiacha changamoto za muda mrefu kama vile miundombinu ya madarasa na madawati yasiyokidhi mahitaji pamoja na upungufu wa walimu, yapo maeneo mengine yanayotarajiwa kujadiliwa.
Hayo ni pamoja na ruzuku inayotolewa kufanikisha elimu bure kwenye shule zote za umma, muundo wa elimu wa kuishia darasa la sita unaotajwa kuanza kutumika badala ya miaka saba ya sasa na mfumo wa elimu kwa ujumla.
Hivi karibuni, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alisema kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi, utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kutafuta suluhu ya kudumu.
Alisema hayo kutokana na shule za Serikali kuendelea kufanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Madini
Yapo mambo mengi kwenye sekta ya madini ambayo wananchi watapenda kupata mrejesho baada ya kutofanyiwa kazi kama ilivyoahidiwa kwenye Bunge lililopita.
Akisoma bajeti ya iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini mwaka jana, Charles Mwijage alisema: “Wizara ilipanga kukusanya Sh370.68 bilioni mwaka 2016/17 ikilinganishwa na Sh286.66 bilioni za 2015/16. Mwaka 2017/18, wizara inatarajia kukusanya Sh727.5 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 96.3.”
Mwaka jana, Serikali iliahidi kuanza kuweka akiba ya dhahabu na madini mengine ya vito, kuanzisha kampuni ya kusimamia uchimbaji madini, kuendeleza utafutaji wa helium, kuwarasimisha wachimbaji wadogo na kufanikisha uchenjuaji wa madini nchini.
Kuongeza ushiriki wa Watanzania, Serikali iliahidi kusimamia usajili wa kampuni za madini kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na uuzaji wa hatifungani za Williamson Diamonds, Dangote, TanzaniteOne, Mgodi wa Geita (GGM), Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na Mgodi wa Luika.
Afya
Msisitizo mkubwa sasa umeelekezwa kujenga uchumi wa viwanda utakaosaidia kuifanya Tanzania kuwa na kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Kufanikisha lengo hilo, afya za wananchi watakaotoa nguvukazi hiyo ni muhimu. Kuzikabili changamoto za sekta ya afya zinazojumuisha ujenzi na uendelezaji wa viwanda vya dawa, utoaji wa bima ya afya kwa wote na mfumo wa rufaa nchini ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa kwa kina.

No comments:

Post a Comment