Utafiti huo uliofanyika mwaka 2017, unaonyesha kuwa asilimia 81 ya Watanzania wanaamini kwamba kupitia ukosoaji huo wanaweza kuisaidia Serikali kutofanya makosa, huku asilimia 71 wakiwa hawataki kuwaita wanachama wa vyama vya siasa ‘wapumbavu na malofa’.
“Idadi kubwa ya wananchi hawajisikii huru kumkosoa Rais (asilimia 60), Makamu wa Rais (asilimia 54) na Waziri Mkuu (asilimia 51). Hata hivyo, idadi kubwa ya wananchi wanasema wanapaswa kuwa huru kuikosoa Serikali na Rais kwa kufanya maamuzi mabaya na kutosikiliza ushauri (asilimia 80),” alisema Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze.
Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbasi aliyekuwapo wakati wa uwasilishaji wa utafiti huo alisema Rais ni mtu mkubwa kiasi ambacho kumshauri kunahitaji utafiti.
“Kuna mtu anadhani kukosoa ni kufanya chochote; yaani kutukana, anaweza akadhalilisha mtu mwingine. Kwa mfano, ukizungumzia kumkosoa Rais maana yake ni kwamba ametenda jambo una mawazo tofauti. Sasa kama unataka kumkosoa Rais, ni mtu mkubwa sana,” alisema Dk Abbasi.
Huku akitoa mfano wa nadharia ya Ubuntu kutoka Kusini mwa Afrika, Dk Abbasi alisema kuna ngazi za kumshauri Rais zinazofanana na heshima katika familia.
“Sisi kwenye mambo ya media tunatumia theory inaitwa Ubuntu inaeleza ‘levels’ (ngazi) jinsi ya kumkosoa mtu hata katika familia, baba na kaka wakikosea, kaka unaweza kumwambia lile neno letu kwamba umebugi lakini baba kuna namna ya kumwambia,” alisema.
Dk Abbasi alisema, “Mimi kama mshauri mmojawapo wa Rais, namshauri kila siku na anasikiliza. Wewe umemshauri wapi? Rais ana power, anaweza kuwa na taarifa nyingi. Unaweza kuja na kataarifa kako unataka kumshauri wakati hujafanya hata utafiti.”
Mbali na hilo, Eyakuze alisema asilimia 70 ya Watanzania wanaziamini taarifa zinazotolewa na Rais, akifuatiwa na Waziri Mkuu kwa asilimia 64.
Wengine wanaoaminiwa kwa kutoa taarifa ni wenyeviti wa vijiji kwa asilimia 30, wabunge wa chama tawala asilimia 26, wabunge wa upinzani asilimia 12 na viongozi wa Serikali kwa jumla asilimia 22.
Akichangia mjadala huo, Profesa Marjorie Mbilinyi alisema suala la kukosoa viongozi wa umma si haki tu, bali ni wajibu wa kila mwananchi.
“Ni wajibu wa raia kukosoa Serikali. Dk Abbasi nimefurahishwa na maelezo yako, lakini nataka kuuliza au kuna Serikali zaidi ya moja? Kwa sababu kwenye Serikali za mitaa kijana akiuliza maswali anawekwa ndani?” alisema.
Profesa Marjorie alisema, “Watu wanaposema kuna woga si kama tunadanganya, woga upo. Watu wanawekwa ndani na hawana makosa. Viongozi wa Serikali ni watumishi na mimi nitasema chini mpaka juu. Ni haki na wajibu wa wananchi kuuliza maswali.”
Akizungumzia utafiti huo, wakili maarufu nchini, Harold Sungusia alisema kuna hatari kubwa ya kuwanyima watu fursa ya kuzungumza.
“Ripoti inatuambia kuwa ‘freedom of speech ina shrink’ (uhuru wa habari unasinyaa), maana yake ni kwamba ukiwanyima watu kuzungumza kawaida huwa wanafanya kwa vitendo,” alisema Sungusia.
“Samahani kama kuna mtu hapa ni bubu, tulipokuwa shule ya msingi tuliambiwa, hakuna mtu mwenye hasira kama bubu lakini kwa nini ana hasira? Vitendo vya watu kuwa na hasira na kuhamaki vinaweza kupungua unapowapa uhuru wa kuongea.”
Haki ya kupata taarifa
Akifafanua kuhusu haki ya kupata taarifa, Eyakuze alisema licha ya wananchi wengi kuunga mkono kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa, asilimia 95 hawajawahi kuomba taarifa katika ofisi za Serikali; asilimia 93 hawajaomba taarifa kwenye mamlaka za maji; na asilimia 93 hawajawahi kuomba taarifa kwenye vituo vya afya.
Badala yake, alisema wananchi wameendelea kutegemea vyanzo vilevile vya taarifa hususan televisheni ambayo alisema utegemezi wake umepanda kutoka asilimia saba mwaka 2013 hadi asilimia 23 mwaka 2017.
Hata hivyo, Eyakuze alisema, “Imani kwa aina mbalimbali za vyanzo vya habari inashuka, redio imeshuka kutoka asilimia 80 mwaka 2016 hadi asilimia 64 mwaka 2017; runinga kutoka asilimia 73 mwaka 2016 hadi asilimia 69 mwaka 2017.”
Pia, alisema imani kwa maneno ya kuambiwa nayo imeshuka kutoka asilimia 27 mwaka 2016 hadi asilimia 13 mwaka 2017.
Licha ya imani kushuka, alisema bado wananchi wanaunga mkono uhuru wa vyombo vya habari na asilimia 62 wanapendekeza gazeti lililochapisha habari za uongo liombe radhi na kuchapisha marekebisho; huku asilimia 54 ya wananchi wakitaka Serikali ipate ridhaa ya Mahakama kufanya uamuzi wa kuliadhibu gazeti.
Eyakuze alitaja changamoto ya wananchi kutozijua sheria zinazohusu masuala ya habari akisema ni asilimia 10 tu wanaoijua Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015; huku asilimia nne tu ya wananchi wakiifahamu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.
Wakosoa utafiti ulivyofanywa
Akizungumzia methodolojia ya utafiti huo, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema japo matokeo yake yanaakisi hali halisi, lakini kitendo cha Twaweza kuingia mkataba na wahojiwa kina walakini.
“Kama umesema methodolojia uliyotumia ni ileile, ni dhahiri kwamba kuna walakini. Ukiachilia mbali kwamba mmepata sampuli lakini mmeingia nao mikataba na mmewawezesha simu. Kwa hiyo, kama wahojiwa wanajua taarifa zao mnazo inaweza kuathiri kueleza wanachokiamini,” alisema Dk Mbunda.
“Si kila mtu anaweza kukosoa, ukosoaji unafanywa na watu wanaofuatilia mambo na hao watu wanapatikana zaidi mijini. Kwa hiyo, sampuli inatakiwa ichanganye watu wa vijijini na mijini wanaotumia WhatsApp, Facebook na mitandao mingine.”
Godfrey Bonaventure kutoka taasisi ya HakiElimu aliunga mkono hoja ya Dk Mbunda akisema, “Nimekuwa nikiwauliza Twaweza je, hao wahojiwa ni walewale kila mwaka. Kwa mfano, hapa tulipo wangapi wana imani zaidi na televisheni kupata taarifa, au redio au WhatsApp?”
Utata wa wahojiwa pia uligusiwa pia na Sungusia aliyesema Watanzania wengi wana hofu ya kutoa maoni,
“Sijajua ubora wa respondents (wahojiwa) wetu. Kwa sababu kama respondents wametawaliwa na hofu, wana shaka, basi hakuna linalofanyika.”
“Sijajua ubora wa respondents (wahojiwa) wetu. Kwa sababu kama respondents wametawaliwa na hofu, wana shaka, basi hakuna linalofanyika.”
Alisema, “Utafiti ni mzuri lakini aina ya watu tuliowauliza hatujui wakoje kwamba ni aina ya watu waliofundishwa kukaa kimya. Tangu shule za msingi tulifundishwa kukaa kimya.”
Akifafanua, Sungusia alisema jamii za Kiafrika, Tanzania ikiwamo zina utamaduni wa kifalme ambao hauruhusu kuhoji viongozi.
“Utamaduni wetu unazungumzia mfalme, huwa hahojiwi, haulizwi swali. Sisi kama nchi za Afrika tumekuja kurithi demokrasia bila kuwa na misingi yake ya mwanzo,” alisema.
“Utamaduni wetu unazungumzia mfalme, huwa hahojiwi, haulizwi swali. Sisi kama nchi za Afrika tumekuja kurithi demokrasia bila kuwa na misingi yake ya mwanzo,” alisema.
Aliitaja misingi hiyo kuwa ni demokrasia ya kimiundombinu, demokrasia ya kiufundi na demokrasia ya kisasa akisema Waafrika tuliruka hatua hizo na kuingia kwenye ile ya kisasa.
“Sasa sisi tumeruka hizo hatua tunakuja kuzungumzia uhuru wa maoni. Kwa jamii nyingine hiyo ni hatua ya mbele mno kwa tamaduni zetu. Ndiyo maana utaona wahojiwa wanasema wana imani lakini huku wanasema hawawezi kuhoji,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Eyakuze alisema wamelazimika kuendelea na sampuli hiyo ili kuepuka gharama.
No comments:
Post a Comment