Friday, March 16

Taasisi za Serikali kukatiwa maji


Moshi. Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira mjini Moshi (Muwsa), imepanga kusitisha huduma ya maji kwa taasisi nyeti za Serikali, kuanzia Jumatatu ya Machi 19 mwaka huu kutokana na kulimbikiza madeni
ya ankara za maji.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Mkuu wa Muwsa, Joyce Msiru amesema taasisi zitakazositishiwa huduma ya maji ni Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Magereza pamoja na Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi
(CCP) ambao wanadaiwa Sh1.8 bilioni.
Msiru amesema katika kuadhimisha wiki ya maji ambayo itaanza Machi 16 hadi Machi 22 mwaka huu, watafanya mambo mbalimbali ikiwamo kufuatilia wadaiwa sugu wa ankara za maji ikiwa ni pamoja na kusitisha
huduma, ili kuwezesha fedha hizo kulipwa.
“Tutasitisha huduma ya maji kwa taasisi hizo kutokana na madeni kuanzia  Julai 2017 hadi sasa ambayo ni zaidi ya Sh313 milioni kwa kuwa madeni ya nyuma yanahakikiwa na ofisi ya hazina,” amesema Msiru.
Amesema tayari wamesitisha huduma ya maji kwa wateja 1,503, na kwamba katika kipindi hiki cha wiki ya maji, watakaolipa madeni,watarudishiwa huduma bure bila kulipia ada ya kurudishiwa huduma hiyo
ambayo ni Sh 20,000 kwa wateja wa manyumbani na Sh 25,000 kwa wateja wa viwandani.
“Tumetoa ofa kwa wateja watakaotaka kurudishiwa huduma, hawatalipia gharama za kuunganishiwa huduma hiyo, lakini pia tutatoa ofa kwa wanaotaka kuunganishiwa huduma ya maji taka, ambapo katika
kipindi hiki cha wiki ya maji, wateja wakilipa nusu, wataweza kuunganishiwa huduma, na fedha inayobaki wataendelea kulipa kidogokidogo kwenye bili yao ya mwezi,”amesema Msiru.
Amesema kutolipwa kwa madeni kwa wakati,kumewafanya, kushindwa
kutekeleza mipango yao mbalimbali ya kuboresha huduma.
Meneja Biashara wa Muwsa, John Ndetico  amesema wateja 1,503 ambao wamesitishiwa huduma ya maji, wanadaiwa Sh143.7 milion na kwamba fedha hizo zikilipwa katika kipindi hiki,zitawasaidia, kutekeleza majukumu mbalimbali.
Akichanganua madeni ya taasisi za Serikali, Ndetico amesema Magereza wanadaiwa Sh295 milioni,huku deni ambalo haliko kwenye yale yanayohakikiwa ili yalipwe na hazina yakiwa Sh71.3 milioni.
“Ofisi ya RPC wao wanadaiwa Sh 904.1 milioni, deni la kuanzia Julai 2017 hadi sasa ni Sh 124 milioni, huku CCP
wakidaiwa Sh649.7 milioni na deni ambalo haliko kwenye uhakiki wa Hazina likiwa  Sh118 milioni,”amesema.
Amesema tayari wamewaandikia barua kueleza nia yao ya kusitisha huduma ambapo watatekeleza hilo kuanzia Machi 19.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,Hamis Issah, alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, hakuwa tayari.
Katika kuadhimisha wiki ya maji, pia mamlaka hiyo itapanda miti katika maeneo ya vyanzo vya maji, pamoja na kufanya usafi katika Soko la Manyema lililopo  Manispaa ya Moshi.

No comments:

Post a Comment