Friday, March 16

Serikali, Watanzania wengi watanufaika na uchumi wa gesi


Mradi wa gesi asilia Iliyosindikwa (LNG) unaweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa uchumi wa nchi kutokana na uwezekano wa kuleta mageuzi kwenye sekta tofauti endapo itasafirishwa na kuuzwa nje ya nchi.
Utakapokamilika, ndio utakuwa mradi mkubwa kupita yote uliowahi kujengwa nchini. Ikumbukwe, mara ya kwanza, Tanzania iligundua gesi asilia katika Kitalu cha Songosongo mwaka 1974 ambacho bado kinaendelea na uzalishaji wa rasilimali hiyo mpaka leo.
Nishati jumuishi
Mradi jumuishi uwekezaji shirikishi unaowaleta pamoja wadau mbalimbali kufanikisha lengo lililopo. Lengo kuu la mradi huu wenye thamani ya Dola 30 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh66 trilioni) ni kuendeleza visima vya gesi vilivyopo kina kirefu cha bahari.
Licha ya visima hivyo vilivyo mbali na ufukwe, mradi utahusisha kujenga kiwanda cha kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) pamoja na mitambo ya kuzalisha gesi kwa matumizi ya nyumbani na miundombinu mingine kuhakikisha mradi unastawi.
Tanzania ina hazina ya zaidi ya futi trilioni 57.25 iliyothibitishwa. Hiki ni kiasi kikubwa ambayo sehemu kubwa ya gesi hiyo, takribani futi 49.5 za ujazo trilioni zipo baharini, katika kina kirefu chini ya Bahari ya Hindi.
Hii ina maana kwamba, japo wataalamu wanajua mahali gesi ilipo, mitambo ya teknolojia ya juu sana itahitajika ili kuichimba.
Mradi ni wa hadhi ya juu kwa kigezo cha ukubwa wake na matamanio yanayoambatana nayo, ndio maana kuna uangalifu wa hali ya juu katika utekelezaji wake. Ni kwa faida ya pande zote zinazohusika kuhakikisha kila kitu kinapangwa kimkakati na kila kipengele cha kazi kinawekwa wazi na kinachunguzwa kwa umakini.
Kwa kiasi kikubwa mradi, unajengwa katika misingi ya uvumilivu, ustahimilivu na ukamilifu huku ukizingatia utaratibu ambao ni lazima kuufuata. Kwa Watanzania kunufaika na mradi huu, ni muhimu mazingira rafiki yakaafikiwa na fursa ajira zikapatikana.
Kwa wawekezaji ambao tayari wameshatumia zaidi ya Dola bilioni nne za Marekani, mradi umewahakikishia fursa ya kutengeneza faida.
Serikali inatarajia kupata takriban theluthi mbili ya mapato ghafi ya mradi, kiasi ambacho ni kikubwa kwa nchi kuimarisha uchumi wake endapo zitaelekezwa kwenye miradi inayowagusa wananchi wengi.
Hata hivyo, mradi huu utatoa ajira, fursa mbalimbali kwa kampuni za ndani, miundombinu mipya na kuinuka kwa shughuli za kiuchumi. Mazingira yakiwa wezeshi, wananchi wengi watanufaika ama moja kwa moja hata vinginevyo.
Kuna shauku kubwa miongoni mwa Watanzania na Serikali kwa ujumla kuona nchi inakuwa kitovu cha viwanda na sekta hiyo inachangia zaidi kwenye uchumi wa nchi.
Ikiwa na shauku hiyo, Serikali inakaribisha wawekezaji watakaosaidia kufanikisha hilo na sekta ya gesi tu inatoa mfano sahihi wa kutangaza uwezo wa Tanzania kuanzisha na kuendesha miradi mikubwa kwa mafanikio bali inaongeza hamasa kutokan ana mchango wake kwenye sekta nyingine za uchumi.
Tanzania itanufaika
Wengi hawana uhakika kama Tanzania itanufaika vya kutoshamradi utakapokamilika. Jambo muhimu kwa mradi wowote mkubwa unaotekelezwa Tanzania kuinufaisha nchi kwa kufungua fursa za ajira na kuimarisha uchumi kwa jumla.
Maendeleo ya viwanda ya muda mrefu na yaliyo endelevu ndio shabaha ya muda mrefu kwa Serikali. Tanzania ni nchi iliyohamasika na matarajio yake bila shaka yanafikika. Huu ndio ufunguo wa kuhakikisha miradi yote mikubwa inatayarishwa katika njia sahihi ili kuhamasisha ukuaji wa uchumi unaoweza kuendelezwa na vizazi vijavyo.
Kuna uwezekano mkubwa wa kukua kwa uchumi na maendeleo nchini Tanzania hivyo kuwapata wadau, hususan Serikali, wafanyabiashara na umma kwa jumla kwenye meza moja ni muhimu sana.
Sio tu mbinu ya pamoja itakuwa na manufaa kwa mtazamo wa kifedha kwa wahusika wote, bali itaifanya Tanzania kuwa nchi ya kuvutia zaidi mbele ya wawekezaji watarajiwa.
Wakati mradi wa gesi asilia na gesi asilia iliyosindikwa utaleta manufaa kiuchumi, ni mradi utakaoacha urithi mkubwa vilevile endapo uwekezaji wa kuziimarisha sekta nyingine utafanyika kwa wakati.
Mradi huu utakuwa na manufaa zaidi utafungua fursa za kibiashara zitakazokuwa na manufaa kwa miaka ijayo wakati miundombinu mbalimbali ikiimarishwa na kutanua shughuli za uchumi zenye kipato kinachokidhi mahitaji kwa wananchi.
Bado kuna safari ndefu kabla mradi haujaanza kuzalisha na kuuza gesi ingawa upo kwenye uelekeo sahihi.
Wawekezaji wa mradi huo ambao ni Shell, Statoil, ExxonMobil, Ophir Energy na Pavilion Energy huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likitarajia kujiunga katika hatua za baadaye wanaendelea kuutekeleza kwa umakini.
Kuanzia kipindi hiki mpaka mradi utakapokamilika, fursa mbalimbali zinajitokeza ambazo Watanzania wanaweza kuzichangamkia kwa kuzingatia vigezo vilivyopo kwa kila hatua.

No comments:

Post a Comment