Friday, March 16

Polisi wadaiwa kumjeruhi kijana kwa risasi Dar

  

Alex Suke (18) akiwa amelazwa katika Hospitali
Alex Suke (18) akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke baada ya kujeruhiwa na risasi, eneo la Buguruni Relini jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita. Na Mpigapicha Maalumu 

Dar es Salaam. Kijana Alex Suke (18) amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke baada ya kudaiwa kupigwa risasi na Polisi waliokuwa wakituliza vurugu eneo la Buguruni Relini, Ijumaa iliyopita.
Kijana huyo anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo baada ya kujeruhiwa kwa risasi kifuani upande wa kulia na mkono wa kulia ambao risasi imeutoboa na kutokea upande wa pili.
Mashuhuda wa tukio hilo, waliliambia Mwananchi kuwa Ijumaa, majira ya saa tano asubuhi, kulizuka vurugu baina ya bodaboda na dereva wa gari dogo aina ya Toyota Carina aliyedaiwa kugonga wanafunzi Ilala.
Walisema vurugu hizo ziliwafanya Polisi waliokuwapo karibu na eneo hilo, kuingilia kati ili kuzituliza na baadaye walilazimika kufyatua risasi kuwatawanya watu hasa madereva wa bodaboda.
Mwananchi lilifika eneo la tukio hilo na kuzungumza na mmoja wa mashuhuda hao, Juma Liwanje ambaye ni mfanyabiashara wa mbao katika eneo hilo.
“Kuna vijana wa bodaboda walikuwa wanatokea maeneo ya Ilala wanamkimbiza dereva wa gari aina ya Carina, inasemekana alikuwa amegonga wanafunzi,”alisema.
Alisema baada ya kufika eneo hilo, dereva wa gari alisimama na kuomba msaada kwa watu wa eneo hilo ambalo ni maarufu kwa biashara ya vifaa vya ujenzi hususan mbao.
“Aliposimama pale sisi tukasema msimpige na bahati nzuri walitokea askari, tulimkabidhi kwa wale askari na wakasogea naye pembeni kidogo. Kuna baadhi ya raia waliotoka Ilala wakasema haiwezekani muondoke naye hivihivi tumpige kidogo,”alisema.
Alisema kitendo cha polisi kumchukua dereva huyo kilizua vurugu miongoni mwa bodaboda na kusababisha watu zaidi kukusanyika eneo hilo.
“Yule askari katika kuwatawanya watu akapiga risasi mbili za juu baadaye akashusha chini ikampata yule mjomba (Alex),” alisema.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa jana kuhusu tukio hilo, alimtaka mwandishi awasiliane na Kamanda wa Polisi wa Ilala.
Lakini, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema tukio hilo limetokea nje ya mipaka yake na kwamba awasiliane na Polisi wa Temeke.
Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi wa Temeke, Emmanuel Lukula ziligonga mwamba baada ya simu yake kutopatikana.
Mwananchi lilikwenda hadi katika Hospitali ya Temeke na mhudumu wa mapokezi (jina linahifadhiwa) alikiri kuwa kijana huyo yupo wodi namba 7.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk Amani Malima alisema hadi mchana wa jana hakuwa na taarifa za kuwapo kwa mgonjwa wa aina hiyo.
Alisema, “Labda baadaye lakini hadi sasa sijapata taarifa ya mgonjwa wa kupigwa risasi.”
Mama mzazi wa kijana huyo, Aghata Mwangambo alisema mtoto wake alipigwa risasi moja ambayo imemsababishia jeraha kifuani na kumtoboa mkono wa kulia.
Mama mdogo wa kijana huyo, Eva Sindika alisema, “Ijumaa Machi 9 nilipigiwa simu kwamba Alex amepigwa risasi na ni kitu ambacho kilinishtua sana.”
Kwa mujibu wa Sindika, wanafamilia hiyo walimpigia simu Kamanda Mambosasa na wanadai aliwaahidi kuwasaidia kimatibabu na kwamba yupo pamoja nao.
Babu wa kijana huyo, Barnabas Mwangamba, aliyekuwa na Alex wakati wa tukio hilo, alisema mjukuu wake alipigwa risasi siku hiyo wakiwa eneo lao la kazi huku akiitaka Serikali kusaidia matibabu yake.
Tukio hilo limetokea siku chache tangu kuuawa kwa kupigwa risasi aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwilini wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana Kinondoni.

No comments:

Post a Comment