Saturday, March 10

Mvua zaua wawili, zaharibu makazi


Handeni.Watu wawili wamefariki dunia na nyumba sita zikiezuliwa na upepo wilayani Handeni mkoani Tanga kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jana, Machi 9, jioni.

Akielezea tukio hilo Diwani wa kata ya Msasa wilayani hapa Hossein Omari amesema mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Mhando (32) amefariki baada ya kupigwa na radi wakati akitoka msikitini saa kumi jioni.
Amesema shuhuda wa tukio hilo, aliyekuwa akitoka na marehemu msikitini aliwaeleza kuwa mvua wakati inanyesha alisikia mlio wa radi na baadae kuona mwenzie anatoka moshi na kubaini amepigwa na radi.

“Ndugu wanasema mwili hauna jeraha lolote ila nguo ndio zimeungua na radi huku mwili kuonekana kuwa mweusi ila hana majeraha baada ya kupigwa na radi hiyo,”alisema Diwani Hossein.
Amesema wanaendelea kufuatilia kama kuna madhara zaidi na baadae watatoa taarifa kamili ya madhara yaliyotokea kwa vyombo husika.
Katika tukio jingine,mkazi wa kijiji cha Zavuza kata ya Kiva wilayani hapa Mwanahawa Ngoma(60) amefariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati akitoka shambani kulima.

Akizungumzia madhara hayo Mtendaji wa kijiji hicho Rahma Bakari amesema walipata taarifa ya mtu kusombwa na maji na kutafutwa usiku mzima ila mwili ulionekana siku ya leo Machi 10.
Ameongeza pia nyumba sita katika kijiji hicho zimeezuliwa na upepo na kuwaacha wakazi wa eneo hilo bila makazi kutokana na kunyesha mvua iliyoambatana na upepo Ijumaa jioni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Edward Bukombe amesema hana taarifa za matukio hayo  na akaahidi kufuatilia na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na mvua hizo.  

No comments:

Post a Comment