Bashe, ambaye kusudio lake limeungwa mkono na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alieleza hayo katika barua aliyomwandikia Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai juzi.
Katika barua hiyo, Bashe anasema lengo la hoja hiyo ni chombo hicho cha kutunga sheria kuunda tume teule kuchunguza matukio hayo aliyodai kuwa yanahatarisha usalama, umoja wa Taifa na utu wa Mtanzania.
“Barua yangu tayari imeshapokewa bungeni. Wabunge kupitia vyama vyetu ni wawakilishi wa wananchi na tumepewa dhamana ya kuisimamia Serikali. Naamini hiki ninachotaka kukifanya ni kwa masilahi ya wananchi, Taifa na chama changu,” alisema Bashe katika mazungumzo na Mwananchi jana.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Kagaigai alisema barua ya mbunge huyo imeshapokewa bila kufafanua zaidi.
Katika maelezo yake jana, Bashe alisema jinsi matukio hayo yanavyojirudia, raia wanaendelea kuwa na hofu na ongezeko la mgawanyiko katika jamii kwa kuwa jambo hilo ni muhimu katika kulinda usalama wa Taifa.
Katika barua hiyo Bashe amesema, “Jukumu la msingi la Bunge ni kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63 (2) na tuhuma zote hizi zinagusa moja kwa moja taasisi zilizo serikalini.
“Nimeona kuna umuhimu wa jambo hili kupewa fursa kujadiliwa ndani ya Bunge na kuundwa Tume teule ya Bunge ambayo itafanya uchunguzi na kuwasilisha taarifa ndani ya Bunge ili kulinda usalama wa Taifa letu.”
Alifafanua katika barua hiyo kuwa ataliomba Bunge kuunda kamati kuchunguza matukio mbalimbali yanayoonyesha kutishia umoja, usalama na mshikamano wa Taifa.
Mambo manane
Mambo hayo manane ameyataja kuwa ni kusinyaa kwa demokrasia na haki za raia; kupotea, kutekwa na kuuawa kwa raia katika chaguzi mbalimbali na matukio ya uhalifu katika siasa; kupigwa risasi na kuumizwa kwa raia ndani ya nchi na kikundi ambacho kinaitwa wasiojulikana.
Nyingine ni ameyataja kuwa ni mauaji ya viongozi wa kisiasa wanaotokana na vyama halali vya siasa nchini; ukandandizwaji wa uhuru wa raia kutoa maoni, kukosoa na kushauri; matumizi mabaya ya sheria na ukandamizaji wa demokrasia ndani ya nchi; haki za kikatiba na kisheria za vyama vya siasa kutoheshimiwa na tuhuma dhidi ya vyombo vya usalama na matumizi ya silaha za moto kwa raia.
“Kwa heshima kubwa nachukua fursa hii kutoa taarifa ya hoja binafsi kwako ikiwa ni katika kutimiza majukumu yangu kama mbunge kwa mujibu wa ibara ya 63(2) pamoja na ibara tajwa hapo juu kwa kuzingatia kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari, 2016 mahsusi kanuni ya 55, fasili ya (1) na fasili ya (2) zikisomwa kwa pamoja na kanuni ya 120 fasili ya (I) mpaka ya (4) nakusudia kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano wa Bunge la 11,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Atoa ufafanuzi
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu hoja hiyo, Bashe alisema kumekuwa na matukio mengi nchini yanayoleta hali ya sintofahamu na kwamba yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi.
“Tanzania tuna mihimili mitatu; Bunge, Serikali na Mahakama. Bunge ni chombo kinachowawakilisha wananchi. Mfano ni yaliyotokea wilayani Kibiti, viongozi wa CCM waliuawa lakini mpaka leo hakuna aliyefikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema Bashe.
“Katika chaguzi ndogo kumeibuka vurugu pia hakuna waliofikishwa mahakamani na matukio haya yanatokea sana lakini bado yapo na yanaendelea kutokea.”
Alisema wanasiasa nchini wanapaswa kutokimbia wajibu wao wa kikatiba kwa sababu wamepewa dhamana na vyama vyao kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.
“Yupo Azory (Gwanda - mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi). Huyo ana zaidi ya siku 100 amepotea. Naamini hiki ninachokifanya ni kwa masilahi ya Taifa. CCM inanyooshewa kidole maana ndiyo yenye dhamana ya kuongoza nchi. Lazima kuwe na sehemu ya kuanzia na sehemu yenyewe ni bungeni,” alisema.
Lema amjia juu
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Bashe aligusia hoja hiyo na kujibiwa na mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Katika majibu yake Lema alimtaka Bashe kuacha kuwa vuguvugu na badala yake aamue kuhamia upinzani au kusimamia misingi ya chama chake kinyume na hapo atakuwa mnafiki.
Lema alisema Bashe analeta hoja ambazo anafahamu wazi kuwa Bunge haliwezi kujadili kutokana na nguvu waliyonayo wabunge wa CCM.
Alisema anachokifanya Bashe kwa sasa ni kutafuta uhalali wa kisiasa na kujionyesha kwenye jamii kuwa anasimamia misingi ya haki lakini ukweli ni kwamba anafahamu fika msimamo wa chama chake.
“Kuthibitisha kuwa anayo majibu ndiyo maana hata yeye (Bashe) alishindwa kwenda kumjulia hali mbunge mwenzake Tundu (Lissu - Singida Mashariki) aache unafiki,” alisema Lema.
Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 katika makazi yake mkoani Dodoma Septemba 7 mwaka jana, kwa sasa anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji.
Jana, Bashe alipoulizwa juu ya majibu ya Lema alisema, “Sijui bwana ila kwa ufupi Lema naye ni mbunge anaposema Bunge limekufa maana yake hata yeye ameshindwa kuisimamia Serikali. Wabunge tusikwepe majukumu yetu.”
Aungwa mkono
Wakati Lema akisema hayo, mratibu wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa alisema Bashe anatekeleza moja ya mapendekezo 17 waliyoyatoa kwa Serikali kuhusu haki za binadamu.
“Katika mapendekezo yetu 17, tulitaka Bunge liunde kamati maalumu kuchunguza vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu, kama ilivyofanya huko nyuma kwenye Operesheni Tokomeza na matukio mengine,” alisema.
“Tulitaka Bunge lifanye hivyo kwa sababu vyombo vya dola kama Jeshi la Polisi nao ni watuhumiwa wa mauaji kwa hiyo hawawezi kujichunguza. Kwa hiyo Bashe amefanya vizuri tunaamini Bunge litasimamia nafasi yake.”
Ole Ngurumwa alilikosoa Bunge la 11 akisema limeshindwa kusimamia nafasi yake ikiwa pamoja na kuiwajibisha Serikali.
“Bunge la sasa limepoteza nguvu ya kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa zamani. Kama uongozi wa Bunge unaogopa hata wabunge nao hasa wa CCM wanajaribu lakini ni wachache tu wanaojiamini,” alisema.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Naemy Silayo alisema kituo hicho kimefurahishwa na hoja hiyo.
“Huo ndiyo utendaji wa mihimili mitatu. Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali na kutunga sheria. Kazi yake ni kuiwajibisha Serikali kwa kuihoji ili kupata majibu yaliyosahihi hasa katika vitendo hivyo,” alisema Silayo.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema suala si kama hoja ya Bashe itapitishwa au la, bali hoja ni kuwa jambo hilo ni kubwa na la msingi kustahili kujadiliwa na Bunge.
“Masuala anayoibua Bashe hayajawahi kuelezwa uchunguzi wake umefika wapi, hivyo hoja ya Bashe itatoa nafasi kwa Serikali kueleza kama imefanya uchunguzi na matokeo yake nini ? Mimi binafsi ninaunga mkono hoja ya Bashe,” alisema.
“Hata kama chama chake kitaizuia, mjadala tu wa jambo hili ambao ameuibuka ni muhimu sana. Hoja hii ikiletwa bungeni nitaiunga mkono.”
Alisema Bashe ndiye alitoa hoja Bunge kuchunguza suala la Lissu kupigwa risasi na suala hilo kupelekwa kwenye kamati.
“Mpaka sasa hakuna taarifa iliyotolewa. Hoja hii binafsi ya Bashe itawezesha taarifa hiyo ya kamati ya ulinzi na usalama kuwekwa wazi. Kila Mbunge mzalendo amuunge mkono Bashe kwenye hoja hii,” alisema Zitto.
No comments:
Post a Comment