Saturday, March 31

Maaskofu wakana njama za kumpindua Museveni


Kampala, Uganda. Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Kampala, Dk Cyprian Kizito Lwanga Ijumaa alipuuza ripoti zinazodai kwamba anafanya njama za kumpindua Rais Yoweri Museveni.
Kauli ya Dk Lwanga imekuja baada ya kupigiwa simu na mtu asiyejulikana akidai kwamba serikali imepata habari zinazomhusisha askofu na njama za kuipindua serikali. Mpiga simu huyo alirudia kumwambia askofu kwamba serikali imepandikiza wafichua siri ndani ya mfumo wa kanisa, ambao walimpelekea habari rais kuhusu mpango huo.
Dk Lwanga alisema habari nyingi potofu zinapelekwa kwa rais na wanasiasa, watumishi wa serikali, wafanyabiashara, maofisa wa polisi na mashirika ya upelelezi kama Shirika la Usalama wa Ndani (ISO), Shirika la Ujasusi wa Nje (ESO) na Shirika la Upelelezi Jeshini (CMI).
Alikuwa akizungumza katika mkusanyiko wa waumini kwenye viwanja vya Old Kampala ambako maelfu ya watu walihudhuria Ibada Takatifu ya Ijumaa Kuu baada ya kushiriki kumbukizi ya njia ya msalaba, tukio la kila mwaka la kuigiza safari ya Yesu Kristo hadi anafika eneo aliposulubishwa.
Dk Lwanga alisema mpiga simu asiyejulikana alimtaka awe mwangalifu akisema yanaweza kumkuta ya Janan Luwum, askofu mkuu wa Kanisa la Uganda, ambaye aliuawa na vyombo vya usalama vya serikali, Februari 16, 1977.
Askofu Lwanga, ambaye alionyesha mshtuko kuhusu madai kwamba anataka kuipindua serikali aliwataka watoa siri waache kumlisha uongo Rais.
Lwanga alisema baadhi ya watoa habari walifukuzwa kanisani na sasa wanaonekana kuwa watakatifu mbele ya rais. Ametoa wito kwa Rais Museveni kukutana nao ili kupata ukweli.
Pia alimtaka Rais Museveni aonyeshe ukarimu kwa kuwaeleza viongozi wa Kanisa kwamba amepandikiza vijana wa ISO, ESO au CMI. Lwanga, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Pamoja la Makanisa Uganda (UJCC), aliwaambia watumishi kwamba hawawezi kutumia kanisani kufanya kazi za usalama.

No comments:

Post a Comment