Tuesday, March 6

Kesi nne kutikisa Mahakama ya Afrika Mashariki


Arusha. Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) imeanza kusikiliza kesi zilizofunguliwa na watu binafsi pamoja na mashirika mbalimbali dhidi ya nchi wanachama wa jumuiya na zinatarajiwa kuuanza kusikilizwa hadi Machi 29 mwaka huu.
Kati ya kesi zinazotarajiwa kuvuta hisia za wengi ni kesi namba 7 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Rashid Salum Adiy na wenzake 39,999 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Muungano itakayosikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Monica Mugenyi.
Majaji wengine ni Fakihi Jundu na Charles Nyawello watatoa uamuzi wa awali wa mpeleka maombi aliyetaka mahakama hiyo ihamishie kwa muda kikao chake Zanzibar ili kuwawezesha wananchi wengi kuhudhuria.
Taarifa iliyotolewa leo kwa waandishi wa habari na Msajili wa Mahakama hiyo, Yufnalis Okubo ilisema  pia kesi namba 2 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) itasikilizwa Machi 13 mwaka huu.
Walalamikaji wengine ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) huku mahakama hiyo ikitarajiwa kusikiliza maelezo ya awali juu ya hoja zitakazobishaniwa .
Kesi hiyo ambayo waleta maombi wanadai sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016 inaminya uhuru wa kupata na kutoa habari hivyo kukiuka Itifaki iliyoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ibara ya 6,7 na 8 kwa pamoja zinazotoa haki hizo.
Katika hatua nyingine Mahakama hiyo pia imesema Machi 14 mwaka huu itasikiliza kesi namba 15 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Baraza la Serikali ya Kijiji cha Ololosokwan wilayani Ngorongoro na watu wengine watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania.
Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa na majaji watano wakiongozwa na Jaji Monica Mugenyi, Dk Faustine Ntezilyalo, Fakihi Jundu, Audace Ngiye na Dk Charles Nyawelo. Walalamika wanadai haki zao kukiukwa kwa kuhamishwa kwa nguvu kwenye kijiji chao chenye hati halali za usajili.
Mawakili wawili, Donald Deya na Nicholaus Opiyo wa taasisi ya Pan African Lawyers Union (Palu) wanawawakilisha walalamikaji ambao ni vijiji vinne  ambavyo ni Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo na Arash.
Pia kesi namba 7 ya mwaka 2016 inayotarajiwa kusikilizwa Machi 22 mwaka huu iliyofunguliwa na Mhariri Mtendaji wa Mseto & Hali Halisi Publishers Limited dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

No comments:

Post a Comment