Waziri Mkuu wa Zamani wa Italia Silvio Berlusconi amempigia chapuo Rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya Antonio Tajani,ikiwa imesalia siku moja kabla ya uchaguzi mkuu nchini Italia.
Berlusconi, ambaye alizuiwa kuwa mgombea kutokana na kukutwa na hatia za udanganyifu, amejiweka katika nafasi ya kuwa mfanya mipango muhimu kupitia uongozi wake wa kundi lenye kufuata siasa za mrengo wa kulia nchini Italia lijulikanalo kama Forza Italia na akiongoza tena vyama vinne vilivyojiunga pamoja, ambavyo vinatarajiwa kujizolea wingi wa kura katika uchaguzi wa taifa hilo siku ya Jumapili.
Sababu za Tajani kuwa waziri mkuu
Tajiri mkubwa, katika tasnia ya vyombo vya habari mwenye umri wa miaka 81, ambaye anazidhibiti siasa za Italia kwa karibu miongo miwili sasa, anasema Tajani anaonesha ishara ya kuwa tayari kuongoza muungano wao, kama ataibuka na ushindi katika mchakato huo wa upigaji kura. Akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Canale 5, kimoja kati ya mtandao wa vituo vyake amesema "Huyu ni mtu ambaye anaijua vyema Ulaya yote."
Duru zinaeleza kuwa, chaguo hilo linaweza kumwingiza Berlusconi katika mikwaruzano na washirika wake wenye wasiwasi na Umoja wa Ulaya, na hasa kiongozi wao Matteo Salvini, ambaye hata yeye anaonesha hamasa ya kuutaka uwaziri mkuu wa Italia. Lakini awali, waziri mkuu huyo wa zamani alifanya jaribio la kujenga dhana ya uwepo wa mgawanyiko mkubwa kati yake na Salvini, pamoja na Giorgia Meloni wa kundi lenye kujiita "Brothers of Italy" - Ndugu wa Italia (Fdl).
Sauti ya mpiga kura
Kufuatia heka heka za uchaguzi huo dereva wa teksi, Giancarlo Paolini anatoa maoni yake "Nitalipigia kura kundi la "5 Star" kwa sababu katika maisha lazima nikabiliane na changamoto tofauti na nipate mawazo. Nataka kubadili jambo na nataka kuliweka kundi hilo katika majaribio. Nataka kuona kama wanatenda wanachosema, endapo watatatua hizi changamoto mpya na kuleta mafanikio."
Lakini safari hii Berlusconi amejitokeza mbele ya vyombo vya habari mjini Roma akisema hakuna tofauti yoyote kati yao na kama kungekuwa na tofauti miongoni mwao, wasingekuwa na muungano, wasingekuwa na chama kimoja. Na kuongeza kwamba wagombea wa muungano huo wote kwa pamoja wanawasiliana kwa njia ya simu karibu kila siku.
Shirika la habari la Ufaransa AFP limesema Berlusconi aliwafunika washirika wake watatu katika tukio hilo kwa kufika mwishoni na kuibuka msisimko na kuimbwa kwa nyimbo zenye kutaja jina lake " Silvio, Silvio" kulikofanywa na wanaharakati wa vyama walikuwepo mkutanoni. Kwa mujibu wa uchambuzi wa mwisho wa maoni kwa uchaguzi huo wa Jumapili, tawi lenye kufauta siasa za mrengo wa kulia ndio pekee lenye nafasi ya kushinda kwa wingi wa kura katika bunge.
No comments:
Post a Comment