Lissu tangu Septemba 7 amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma.
Akizungumza leo Jumatatu Desemba 4,2017 katika ufunguzi wa wiki ya msaada wa sheria, mwakilishi wa TLS, John Seka amesema Lissu anawasalimia wananchi.
“Rais wa TLS, Tundu Lissu anawasalimia sana, anaendelea kupata nafuu ila anawaomba Watanzania waendelee kumwombea ili apone haraka,” amesema Seka.
Amesema Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) ana hamu ya kurudi nyumbani aendelee kutoa mchango wake wa kisheria kwa wananchi.
Kuanzia leo hadi Desemba 8,2017 wananchi wanapata fursa ya kupata msaada wa kisheria katika migogoro inayowakabili.
Seka ametoa wito kwa wananchi kufika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na mikoani kupata huduma ya msaada wa kisheria.
Amesema baada ya wiki hiyo kumalizika, wananchi watatakiwa kufika ofisi za TLS kupata msaada wa kisheria kwa kuwa hilo ni moja ya majukumu ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment