Zitto katika taarifa aliyoitoa leo Jumatatu Novemba 27,2017 amesema ACT Wazalendo katika uchaguzi wa jana Jumapili Novemba 26,2017 ilisimamisha wagombea katika kata 17.
“Tumepata matokeo ya kata zote na hakuna kata tuliyoshinda. Wapiga kura wameamua na sisi tumekubali. Tunafanya tathmini ya matokeo nchi nzima na tutazungumza na wananchi. Tunawashukuru kwa kura tulizopata. Tutazienzi kwa kuwa ndiyo haki yetu,” amesema Zitto.
Amesema wanajiandaa kwa uchaguzi mdogo ujao ukiwemo wa ubunge kwenye majimbo yaliyo wazi.
Zitto amesema watatumia mafunzo waliyopata kwenye uchaguzi mdogo kujipanga kwa uchaguzi ujao.
“Kwetu sisi chama cha ACT Wazalendo, uchaguzi ulikuwa fursa ya kuzungumza na wananchi na kufikisha ujumbe wetu kwa kuwa kuzuiwa mikutano ya hadhara kunatunyima fursa hiyo. Hatutachoka kuendelea kusambaza sera zetu kwa kuwa tunaamini ni bora zaidi na zinazoweza kuleta unafuu kwa wananchi wetu,” amesema.
No comments:
Post a Comment