Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema hayo bungeni leo Ijumaa Novemba 10,2017 alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Angelina Malembeka.
Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itakamilisha upimaji wa maeneo ya shule, soko na zahanati.
"Je kutokana na ukubwa wa gharama za upimaji ni kwa nini kazi ya upimaji isifanyike bure kwa taasisi za umma kupitia halmashauri?" amehoji.
Naibu Waziri Mabula akitoa majibu amesema Serikali iliagiza maeneo yote ya umma yapimwe na yamilikishwe kwa taasisi husika kupitia barua ya Septemba 7,2017.
“Nitoe rai kwa wakuu wa taasisi za umma kuhakikisha wanakamilisha kazi hii mapema na kwa maeneo ambayo yamevamiwa ni vyema wavamizi wakaondoka kwa hiari, wasisubiri mkono wa sheria uwakumbe," amesema.
Amesema gharama elekezi za huduma za upimaji ambazo kwa mara ya mwisho zilifanyiwa mapitio mwaka 2016 si kubwa kama inavyodhaniwa, kwa kuwa upimaji wa ardhi hufanywa kwa misingi ya kurejesha gharama pekee.
Naibu waziri amesema gharama hizo zinahusisha vifaa vya upimaji, shajara, usafiri, matengenezo ya vifaa na mawasiliano ya kitaalamu.
No comments:
Post a Comment