Saturday, November 4

WIZARA YA UJENZI YARIDHISHWA NA KASI YA JNIA-TBIII

WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imeridhishwa na ujenzi wa mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII), ambapo unatarajiwa kukamilika Septemba 2018. Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa wakati alipotembea maendeleo ya mradi huo unaojengwa na Mampuni ya ujenzi ya Bam International ya Uholanzi.

Mhe. Kwandikwa alisema mradi huo umefikia asilimia 66, ambapo wizara imekuwa ikihakikisha mkandarasi analipwa kwa wakati ili uweze kukamilika kama ilivyotarajiwa, na kukamilika kwake kutatoa picha ya kuelekea kwenye Tanzania mpya.

“Hivi karibuni nilitembelea kiwanja cha KIA (Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro), nikaridhishwa na maendeleo ya ukarabati unaoendelea pale, na nikaona ni vyema pia kutembelea hili jengo na nimeliona na nimeridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea, ninaamini kama wakandarasi walivyosema basi hadi kufikia Septemba 2018 litakuwa limekamilika kabisa,” alisema Mhe. Kwandikwa.

Hata hivyo, Mhe Kwandikwa alisema serikali inajenga awamu ya pili ya mradi huo kwa kutumia fedha za ndani, lakini pia kwa kushirikiana na wadau wengine, ambapo ni ishara nzuri kuwa siku zijazo kutakuwa na miradi mingi zaidi.

“Tunajenga mradi huu kwa fedha zetu za ndani, lakini pia kwa kushirikiana na wadau wengine, hii ni ishara nzuri kwamba sasa tunakokwenda tunao uwezo wa kuwa na miradi mingi zaidi kama hii tuliojenga kwa kutumia fedha zetu wenyewe,” alisema Mhe. Kwandikwa.

Hata hivyo, msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Barton Komba alisema, mkandarasi wa ujenzi huo ameshalipwa fedha zake zote, hivyo kwa sasa hadai serikali na anafanya kazi yake vizuri, ili kukamilisha na kukabidhi jengo pindi litakapokamilika. “Mpaka mwezi wa tisa mwakani utakuwa umekamilika kabisa, lakini pia jengo hili limejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na litatoa huduma kwa watu wote hata ndugu zetu wenye mahitaji maalumu, ,” alisema Mhandisi Komba.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (wa tatu kushoto) akielekea kwenye ukaguzi wa ujenzi wa jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere. Wa pili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Mtengela Hanga.
Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII), Mhandisi Barton Komba (kulia) akimwonesha kitu Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (wa pili kulia), wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo hilo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (wa pili kulia), akizungumza na Mhandisi Barton Komba (wa tatu kushoto) wakati wakitoka kwenye ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

No comments:

Post a Comment