Dk Mpango amesema hayo jana Jumatatu jioni wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2018/19.
Kuhusu hoja kuwa Deni la Taifa linakuwa kwa kasi kubwa wakati uchumi unakua kwa kasi ndogo, Dk Mpango alisema deni hilo ni himilivu akisema baadhi ya wabunge wanashindwa kukokotoa hesabu.
Alisema Deni la Taifa liliongezeka kutoka dola 22.3 bilioni za Marekani mwaka 2016 na kufikia dola 26 bilioni ilipofika mwezi Juni 2017 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 17.
“Deni hilo ni sawa na asilimia 31.2 ya GDP (Pato la Taifa) ikilinganishwa na ukomo wa uhimilivu wa asilimia 56. Uhimilivu wa Deni la Taifa hupimwa kwa kuzingatia uwezo wa nchi kulipa deni”
Dk Mpango alitoa takwimu za nchi za Afrika Mashariki za uhimilivu wa deni la taifa kwa nchi hizo akisema Tanzania bado iko vizuri na iko katika nafasi nzuri ya kukopesheka na wataendelea kukopa.
Alizitaja nchi hizo na uhimilivu wa deni lao kuwa ni Uganda ambayo ni asilimia 35.4, Rwanda asilimia 36.6, Burundi asilimia 43.4 na Kenya asilimia 50.4 akisema hali ni nzuri kulinganisha na nchi nyingine.
Alilinganisha nchi hizo na Zambia yenye uhimilivu wa asilimia 57.2, United Republic of Emirates asilimia 60.3, Marekani asilimia 73.8, Morocco asilimia 77 na Uingereza asilimia 92.2.
“Misri ni asilimia 92.6, Msumbiji asilimia100.3, Italia asilimia 132.5 na Ugiriki asilimia 181.6. Kwa takwimu hizi sisi bado tuna nafasi kubwa ya kukopa,”alisema Dk Mpango na kuongeza;
“Tutaendelea kukopa kwa sababu moja tu kubwa. Kwamba ni kwa ajili ya ni kukuza uwezo wetu wa baadaye wa kumudu uendeshaji wa nchi yetu na kulinda uhuru na heshima ya nchi yetu,” alisema.
“Napenda nisisitize hakuna dhambi ya nchi kukopa ilimradi nchi husika itumie fedha hizo za mkopo kukuza uwezo wa kiuchumi na kuzalisha na kurejesha hiyo mikopo,”
“Kama Rais (John Magufuli) alivyosema alivyokuwa ziarani Kagera kwa kweli tutaendelea kukopa mpaka kieleweke ilimradi Deni la Taifa tuhakikishe linaendelea kuwa himilivu.”
Kuhusu benki za biashara nchini kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa mikopo binafsi, mikopo ya biashara na mikopo ya sekta za uzalishaji, alisema hilo limetokea nchi kadhaa.
“Katika miezi 12 iliyoishia Septemba 2017, wastani wa ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi nchini Kenya ilikuwa asilimia 3.8, Tanzania asilimia 5.0, Uganda 5.2 na Rwanda asilimia 10.3.
Dk Mpango alikuwa akijibu hoja za baadhi ya wabunge kuwa amekuwa na kiburi na hana ushirikiano wa wabunge na wakati mwingine hapokei simu za wabunge wanapomtafuta kumshauri.
Kuhusu ushiriki wa sekta binafsi, Dk Mpango alikiri kuwa ndio injini ya uchumi lakini akasema zipo changamoto kiuhalisia na kusema “akili za kuambiwa tuchanganye na za kwetu”
“Akili za kuambiwa mzee Kikwete alituambia lazima tuchanganye na za kwetu kabla ya kuamua kufikia hatua ya kuwa na sekta binafsi yenye nguvu,”
“Kweli natamani sana wawekezaji wa ndani na nje watatupunguzia huu mzigo. Sekta binafsi tuliyonayo bado inahitaji kulelewa ili iweze kubeba jukumu hili.”
No comments:
Post a Comment