Sunday, November 5

Walivyokuwa awali, si walivyo sasa


Walivyokuwa sivyo walivyo! Ndivyo unavyoweza kuwaelezea baadhi ya wanasiasa katika vipindi viwili tofauti vyenye misimamo miwili tofauti.
Haieleweki kama tofauti hiyo ya misimamo yao ina uhusiano na nafasi walizokuwa nazo na baadaye kutokuwa nazo, lakini kwa kuwaangalia na kuwasikiliza kwa makini wana misimamo tofauti katika vipindi tofauti.
Mitazamo hiyo imekuwa ikitolewa na makada wa CCM kama katibu wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole na wabunge wake akiwemo Nape Nnauye (Mtama).
Wengine ni waliowahi kuwa mawaziri katika utawala uliopita, Khamis Kagasheki na Profesa Mark Mwandosya.
Polepole, aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, amekuwa akizua mijadala kutokana na mitazamo yake ya hivi sasa kuhusu suala la Katiba, tofauti na alivyokuwa wakati Bunge la Katiba likiendelea na vikao vyake.
Akiwa nje ya Bunge la Katiba lililokuwa likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, Polepole alipata umaarufu kutokana na kupingana na jinsi lilivyokuwa likiendeshwa, hasa kutokana na kuachana na Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Kasoro hiyo ilionekana hasa katika suala la muundo wa Muungano na tunu za Taifa. Tume ya Warioba, ambayo Polepole alikuwa mjumbe wake, ilipendekeza Muungano wa serikali tatu, lakini Bunge hilo, likiwa na wajumbe wengi kutoka CCM, lilibadilisha na kurejesha serikali mbili.
Polepole aliitwa na vituo vingi vya televisheni kujadili suala hilo, na akapinga kwa nguvu, akisema Rasimu ya Katiba ilibeba maoni ya wananchi.
Lakini sasa amebadilika. Sasa anazungumzia kitu kinaitwa “ukatiba”.
Mara baada ya kuteuliwa kuwa katibu wa uenezi, amekuwa na mawazo mbadala, akisema kwa sasa Tanzania haihitaji Katiba mpya, bali “ukatiba”.
Hoja hii aliibua Oktoba 19, wakati wa uwasilishaji wa maoni ya wananchi waliohojiwa na taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa Katiba.
Polepole alisema CCM inaamini dhana na uhalisia ambapo kuna ukatiba na katiba na Watanzania kwa mujibu wa Twaweza wana vitu wanapenda kuviona navyo ni ukatiba.
“Ukatiba ni mambo ya jumla, utamaduni, mila, mienendo yetu na mambo fulani fulani tuliyokubaliana. Viongozi wetu wawe wanajua dhamana waliyopewa, wananchi wajue viongozi jukumu lao ni kuwahudumia, kiongozi kuwa na cheo kimoja ili aweze kukimudu,” alisema Polepole.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwapo eneo hilo, alitaka kufahamu kwa nini hakueleza falsafa hiyo wakati akiwa ndani ya Tume ya Warioba, lakini Polepole hakujibu swali hilo.
Nape
Mtangulizi wake, Nape pia amekuwa akiibua mijadala kutokana na kauli zake za hivi karibuni baada ya kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri mapema mwaka huu.
Tangu Machi 23 alipovuliwa uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kutoa mitazamo yake kwa tungo tata na wakati mwingine kuonekana kama anaunanga uongozi wa CCM.
“Wapinzani si maadui, tushindane kwa hoja,” aliwahi kusema Nape. Kauli hiyo ameitoa wakati wanasiasa wa upinzani wakikamatwa kila mara, wengine kufunguliwa kesi na hata kushambuliwa kwa risasi.
Ndani ya Bunge wamejikuta wakiadhibiwa kwa kuzuiwa kuhudhuria vikao na wakati mwingine kulalamikia kiti kutowatendea haki.
Pia amewahi kusema “uonevu husababisha maumivu ya moyo, maumivu ya moyo hutunga mimba ya chuki, chuki huzaa kisasi na matokeo yake ni mauti” bila ya kufafanua. Ni dhahiri kuwa kwa mazingira hayo ya kisiasa, kauli hiyo haiwezi kuchukuliwa kuwa ya kawaida.
Alimpinga Polepole aliyesema kuwa mwaka 2020, wabunge watakaopewa fursa ya kugombea ni wale wanaoishi kwenye eneo wanalotaka kuwakilisha.
Nape pia alisema: “Huhitaji kuwa mkamilifu kuwavutia wengine. Watavutiwa na wewe kwa jinsi unavyoshughulikia mapungufu yako! Mungu kagawanya kazi, wengine kusifu, wengine kukosoa, wengine yote pamoja! kwanini unakerwa na kuhangaika na mgawanyo wa kazi? acha ushamba.”
Hakufafanua alikuwa akimtumia ujumbe nani, lakini Nape alikuwa mtu anayesema wazi anachokiamini bila ya kutumia kauli tata au mafumbo.
Kagasheki
Mwingine anayeonekana kuwa tofauti ni Kagasheki, ambaye amekuwa nje ya siasa tangu mwaka 2015 baada ya kushindwa ubunge wa Bukoba Mjini.
Mitazamo yake imekuwa ikifikirisha, ikiibua gumzo na hasa alipounga mkono kauli ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ya Agosti, 2017 kwamba wapinzani wasichukuliwe kama maadui.
“Nimetafakari kauli ya JK kuhusu vyama Afrika, nakiri kiongozi aliobobea katika uongozi, hukabiliana na muziki hata kama hapendi mdundo wake,” aliandika katika akaunti yake mtandaoni akiweka fumbo pia kuhusu hali ya kisiasa nchini.
Pia, Kagasheki aliweka nukuu ya Ibrahim Bin Adham inayosema: ‘’Kama huwezi kuwasaidia watu katika utatuzi wa matatizo yao basi wafariji kwa maneno mazuri na hata kwa tabasamu.”
Profesa Mkumbo, Anna Mghwira
Wengine katika kundi hili ni katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo na mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambao wote wameteuliwa na Rais Magufuli wakitoka Chama cha ACT- Wazalendo.
Wawili hao walikuwa miongoni mwa wakosoaji, lakini sasa hawataweza na Profesa Kitila ameamua hadi kujivua uanachama wa ACT Wazalendo.
Akizungumzia hali hiyo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Dk Charles Kitima alisema chama na Serikali vinapaswa kuwa tayari kupokea mawazo mbadala na kuyafanyia kazi bila ya kuyabeza.
“Watu wawe huru kutoa mawazo yao na mitazamo wanayoona inafaa, lakini tunaweza kujiuliza hayo mawazo yao ni ujenzi wa taifa au maslahi yao binafasi?” alihoji.
“Na je, chama kiko tayari kuyapokea na kuyafanyia kazi?
“Chama kinapaswa kujinoa na kuona dhana ya upinzani si uadui na demokrasia nzuri ni ile inayoruhusu mawazo mbadala.”

No comments:

Post a Comment