Akizungumza leo Jumanne Novemba 28,2017 mbele ya wajasiriamali wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake (TWCC), Ofisa wa wakala hiyo, Irene John amesema sheria ya wakala wa vipimo zinakataza kupunguza uzito wa bidhaa wanazouza.
“Baadhi ya wajasiriamali wanazidisha uzito wa bidhaa kwenye vifungashio, wengine wanapunguza uzito,” amesema.
Amesema mjasiriamali akizidisha uzito atapata hasara lakini akipunguza uzito kwenye bidhaa akikamatwa anashtakiwa na ikithibitika anaweza kutozwa faini ya hadi Sh20 milioni.
“Lengo la sheria ya wakala wa vipimo ni kumlinda mfanyabiashara ili apate thamani halisi ya bidhaa anazozalisha na mlaji ili asipunjwe,” amesema.
Akitoa mfano, amesema baadhi ya wajasiriamali wa asali wanaipima kwa kutumia lita wakati inatakiwa kupimwa kwa kutumia uzito.
“Matokeo yake wanajipunja na hivyo kupata hasara kwa sababu asali ina uzito mkubwa na haiwezi kupimwa kama maji,” amesema.
Amesema bila kuzingatia vipimo sahihi wafanyabiashara wanaweza wasipige hatua za kimaendeleo kama malengo yao yanavyoonyesha.
Makamu Mwenyekiti wa TWCC, Fatma Kange amesema elimu ya vipimo ilikuwa changamoto kwa wajasiriamali wengi.
“Tunajipunja kwa sababu hatuna elimu sahihi kuhusu masuala ya vipimo, sasa wajasiriamali wengi watajirekebisha,” amesema.
Amesema changamoto inayokikabili chama hicho ni kwa wanachama kutokuwa na umoja.
Kange amesema chama hicho kina wanachama 5,000 lakini hakina kitegauchumi ili kujiletea maendeleo.
“Ni aibu kwa wafanyabiashara wanawake kutokuwa na kitegauchumi kama ilivyo kwa vyama vingine,” amesema.
Amesema pamoja na kuwepo kwa vyama vidogovidogo kwa wafanyabiashara wanawake lakini TWCC ndicho chama kikuu ambacho wafanyabiashara wanatakiwa kukiendeleza.
No comments:
Post a Comment