Monday, November 13

VIJANA 120 KUTOKA NCHI MBALIMBALI BARANI AFRIKA KUHUDHURIA KONGAMANO LA VIJANA NA UONGOZI JIJINI DAR

JUMLA ya vijana 120 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, wanatarajiwa kuhudhuria kongamano la vijana viongozi, litakalofanyika kuanzia Novemba 15 hadi 17 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo lililoandaliwa na kuratibiwa na Shirika la Open Society Initiative For Eastern Africa(OSIEA) kwa kushirikiana na Shirika la Mulika Tanzania, litawakutanisha vijana hao na kuweza kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana wa bara la Afrika huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Waziri, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Waleavu, Antony Mavunde.
 
Akizungumza na waandiishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Ofisa Program Msaidizi wa OSIEA, Adam Antony, alisema kogamano hilo ni mara ya pili kufanyika baada ya lile la mara ya kwanza kufanyika mwaka jana na kushirikisha nchi za Afrika Mashariki pekee.

Antony alisema katika mkutano huo,vijana hao watakaohudhuria ni pamaoja na wale ambao tayari wameshaanzisha biashara  na miradi mbalimbali huku wengi wakiwa kutoka nchini Tanzania.

“Pia tunategemea kuwa na vijana ambao walishawahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali zao  ambao wataweza kutoa shuhuda  mbalimbali za namna walivyoweza kufanikiwa katika kazi zao kama moja ya kuwapa motisha ya kufanya kazi kwa vijana ambao ni viongozi kwa sasa,”alisema Ofisa huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mulika Tanzania, Hussein Melele, alisema mada zitakazozungumziwa katika kongamano hilo ni pamoja na nafasi ya vijana kufikia Afrika tuitakayo(Agenda 2063), vijana kushirikishwa katika ngazi za maamuzi kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.

Jingine ni kujadili masuala ya rasilimali zinazopatikana Afrika na namna zinavyoweza kuwasaidia vijana katika kujiletea maendeleo kwa mmojammoja na jamii kwa ujumla.

Matarajio baada ya kufanyika kwa kongamano hilo, Melele alisema ni kutokana na kongamano hilo kuwakutanisha vijana viongozi na wadau wa maendeleo , mashirika ya kitaifa, mabalozi na wanataaluma ni wazi kwamba baadaye  wataweza kuwaonesha njia ya namna gani wataweza kufanya nao kazi pamoja.

“Aidha kongamano hili litakuwa ni daraja kwa vijana hawa kuweza kutatua changamoto katika sekta mbalimbali hususani zinazowahusu vijana wenyewe ikiwemo za afya, ajira, uongozi, elimu, biashara na mengineyo,”alibainisha Mkurugenzi huyo.

No comments:

Post a Comment