Hilo limebainishwa jana na waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage wakati wa ufunguzi wa kongamano la kuzungumzia ushirikiano wa Tanzania na China.
Mwijage alisema kwamba mazungumzo ya ujenzi wake yanaonyesha dalili za kufikia muafaka.
“Katika ujenzi huo, Serikali itashirikiana na Oman na China na tayari wawakilishi kutoka nchi hizo wameshafika kwa ajili ya majadiliano,” alisema Mwijage.
Licha ya upanuzi wa bandari hiyo inayotarajiwa kuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki, alisema kwenye eneo la eka 3,000 kutajengwa viwanda 190 kabla ya mwaka 2020 na kuiwezesha Serikali kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Lengo ni kutaka wananchi washiriki katika uchumi kupitia viwanda hivi vya kuchakata malighafi zinazozalishwa nchini. Kujenga uchumi wa viwanda, lazima nchi iwe na miundombinu wezeshi ikiwamo ya maji, barabara, reli,” alisema Mwijage.
Alisema Serikali itajenga reli ya kisasa itakayokuwa inakusanya bidhaa zilizozalishwa na wakulima na wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wabia kwenye mradi huo utakaokamilika mwaka 2022 na kugharimu Dola 10 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh22.3 trilioni) ni kampuni ya China Merchants Holdings International (CMHI) kutoka nchini China na State General Reserve Fund ya Oman.
Utakapokamilika, mradi huo uliopo kilomita 75 kutoka jijini Dar es Salaam utakuwa na viwanda 700 na kuufanya kuwa eneo la kimkakati kwa uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuchanguia kuinua uchumi wa Taifa.
Katika awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Bandari ya Bagamoyo, taarifa zinaonyesha itaruhusu meli kubwa zinazobeba hadi makontena 8,000 ya futi 20 hivyo kupunguza foleni ya meli za mzigo huku kukiwa na uwezekano wa kuitanua zaidi.
Taarifa ya CMHI inayotarajiwa kutekeleza sehemu kubwa ya ujenzi huo inaonyesha Dola 120 milioni (zaidi ya Sh264 bilioni) zitatumika kujenga eneo la viwanda, Dola 70 milioni (zaidi ya Sh154 bilioni) eneo la utalii wakati Dola 90 milioni (zaidi ya Sh198 bilioni) zikijenga miundombinu ya bandari.
Pia, kutakuwapo na eneo la biashara huria litakalojengwa kwa Dola 70 milioni (zaidi ya Sh154 bilioni) na kiasi kingine kama hicho kwa ajili ya biashara za kimataifa huku Dola 50 milioni (zaidi ya Sh110 bilioni) zikijenga vituo vya sayansi na teknolojia na Dola 20 milioni (zaidi ya Sh44 bilioni).
Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) mpaka Juni 2016, zinaonyesha uwekezaji wa China nchini ulifika Dola 6.62 bilioni (zaidi ya Sh14.7 trilioni) kutokana kampuni takriban 600 zilizowekeza kwenye kilimo, utalii, ujenzi na teknolojia ya habari na mawasiliano.
No comments:
Post a Comment