Friday, November 24

TPA yawashikilia wezi wa kamba za kutia nanga



Dar es Salaam. Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na Polisi wamewakamata watu saba ambao wamekuwa wakiiba kamba ambazo hutumiwa na meli wakati kutia nanga.
Watuhumiwa hao wamefanya  uhalifu huo kati ya Juni na Septemba mwaka huu kwa kuiba kwenye meli za Mv Northern Decision na Mv MSC Kerry.
Akizungumza  leo Alhamis Novemba 23 Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema wizi huo ulitokea Juni na Septemba.
Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na sehemu ya kamba zilizoibwa ambayo ni mita 150.“Tumewakamata watuhumiwa wakiwa na kamba yenye urefu wa mita 100 kwa kuwa mita 50 walikuwa wameshaiba,” amesema
Amesema wizi huo ulifanyika wakati meli hizo zikiwa zimeegesha nje ya bandari ya Dar es Salaam zikisubiri kuruhusiwa kutia nanga.
Amesema kamba hizo zimekuwa zikitumika kutengenezea nyavu za kuvulia na kuezekea makuti kwa kuwa huwa haziozi.
Amesema watuhumia hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kigamboni na Zanzibar wakiwa katika harakati za kuziuza.
Amesema mbali na kamba, pia wamekamata gari dogo ambalo lilikuwa limebeba kamba hizo.Amesema watuhumiwa hao watafikishwa hivi karibuni mahakamani.
Amesema mamlaka hiyo imeongeza ulinzi bandarini ili kuhakikisha kwamba vitendo vya uhalifu vinakomeshwa.
“Tunachukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa hawa ili kuwaonyesha wenye meli na mawakala kuwa tunadhibiti matukio ya aina hii,” amesema.
Hivi karibuni, uongozi wa bandari ulisema ili kuimarisha usalama, umefunga camera maalum zaidi ya 400 ambazo zinaonyesha kila shughuli inayoendelea katika bandari.

No comments:

Post a Comment