Novemba 9, Kampuni ya Udalali ya Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliendesha mnada wa nyumba mbili za Lugumi zilizopo Mbweni JKT na moja ya Upanga jijini Dar es Salaam ambazo zote Dk Shika alifikia bei ya kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni lakini alishindwa kulipa asilimia 25 ya mwanzo.
Akizungumza na Mwananchi mjini Kahama juzi, Bakungile alisema aliona atumie nafasi hiyo kumwita Dk Shika Kahama na hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kwenda wilayani humo.
Baada ya kuulizwa na Mwananchi kwanini alitumia gharama kubwa kumsafirisha kwa ndege Dk Shika huku akijua wazi kwamba Dar es Salaam alishinda mnada na hakuwa na fedha za kulipa, Bakungile alidai kushindwa kulipa kwa fedha za mnada ndilo jambo lililompa umaarufu.
“Najua wazi Dk Shika alishindwa kulipa Sh900 milioni kwenye mnada wa nyumba za Lugumi hivyo katika chuo changu ameahidi kutoa kila mwaka Dola 1 milioni za Marekani (sawa na Sh2.2 bilioni) ambazo akishindwa kuzilipa ataendelea kutangazwa kwamba ameshindwa kulipa hiyo itakuwa fursa ya chuo changu kuendelea kutangazwa,” alisema Bakungile.
Alhamisi iliyopita Dk Shika aliingia mjini Kahama akiwa mgeni mwalikwa wa chuo hicho na baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza alitoa ahadi hiyo ya fedha akisema ataziwasilisha baada ya miamala ya kuhamisha fedha zake kutoka Urusi itakapokamilika.
Hata hivyo, baadhi ya watu walisema ‘bilionea’ huyo hapaswi kupewa heshima hiyo na badala yake anapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuvuruga mnada.
No comments:
Post a Comment