Caracas, Venezuela. Rais Nicolas Maduro amekiri hadharani kwamba serikali yake haina uwezo wa kulipa madeni yake yote.
Maduro alisema hayo jana katika hotuba yake kupitia televisheni kwamba serikali pamoja na kampuni ya mafuta ya taifa, PDVSA, watapitia upya madeni ya nje.
Kampuni hiyo ya mafuta ililipa madeni yenye thamani ya dola za Marekani 1.1 bilioni kiasi kikubwa hasa ikizingatiwa imesaliwa benki na akiba ya fedha za kigeni inayofikia dola 10 bilioni.
"Lakini kwa malipo haya, kuanzia leo, natoa amri kufanyika malipo kidogo kidogo na kupitia upya deni la nje,” alisema Maduro.
Venezuela inakabiliwa na mgogoro wa kiutu huku watu wakikabiliwa na uhaba wa chakula na dawa. Wengi sasa hawawezi kununua mahitaji ya msingi kwa sababu bei za bidhaa zinapaa kuliko vipato vyao.
Thamani ya sarafu ya Venezuela iitwayo bolivar imeshuka sana. Ikiwa serikali ya Rais Maduro itashindwa kufikia makubaliano mapya na wakopeshaji wake kuhusu kupitiwa upya kwa deni, kwa lengo la kujaribu kulipa kiasi, itaishia kukwama kulipa hali inayoweza kuchochea mambo mengi.
Moja ya hatua zinazoweza kuchukuliwa ni wawekezaji wa Marekani na kwingineko duniani wanaweza kutwaa umiliki wa kampuni ya mafuta kama fidia.
Mafuta ndiyo chanzo pekee kikuu cha mapato ya nje na kwa hiyo ndiyo njia pekee ya kupata fedha za kununulia chakula na dawa kwa raia wake wapatao 30 milioni. Kutokana na usimamizi mbovu wa mashamba, Venezuela inalazimika kununua karibu chakula chote kutoka nje.
No comments:
Post a Comment