Wednesday, November 1

Mwalimu Nyerere ni Nyimbo au tunamfuata?


Tumemaliza kumbukizi ya miaka 18 ya kifo cha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Nyerere. Apumzike kwa amani. Kwa asilimia kubwa, Watanzania wengi wanamkumbuka Mwalimu na kumlilia na kuimba sifa zake. “Kama siyo juhudi zako Nyerere…”. Ni watu wachache sana wenye matatizo yao ambao wanampiga madongo Mwalimu. Sifa za Mwalimu ni wimbo wa kila siku. Viongozi wa Serikali wakitafuta kukubalika kwenye jamii, wanalitumia jina la Mwalimu. Vyama vya siasa vyote vikitaka kukubalika katika jamii na kwenye siasa zao vinalitumia jina la Mwalimu.
Wapinzani, wanaipiga vita CCM, lakini huwezi kusikia wakimpiga vita Mwalimu, ambaye ndiye mwanzilishi wa CCM. Hawaipendi CCM, lakini wanampenda Mwalimu na kuimba sifa zake.
Swali ni je, wanampenda Mwalimu na matendo yake au wanampenda tu bila kuzingatia yale aliyoyafanya wakati wa uhai wake? Mfano, CCM ambayo aliianzisha na kuisimika. Kwa nini wampende Mwalimu na kuichukia CCM? Je, wanaichukia CCM tu, au na baadhi ya matendo ya Mwalimu?
Hili ni swali kwa Watanzania wote. Tunampenda na kumkumbuka Mwalimu na mambo yake au tunabaki kuimba tu sifa za Mwalimu. Je, sisi ni wafuasi wa Mwalimu?
Ni wazi kuna mambo ya Mwalimu ambayo tuliyazika Mwalimu akiwa bado hai. Ujamaa na Azimio la Arusha, vilizikwa Zanzibar. Mavazi ya Mwalimu, yalitupiliwa mbali alipoondoka madarakani. Suti za kimagharibi zilitawala na kuwa ushuhuda kwamba wakoloni walitutawala hadi kwenye akili zetu. Daima tufanane nao kwa kila kitu hadi mavazi. Tuongee lugha zao, tusomee kwenye shule na vyuo vyao, tuweke fedha zetu kwenye mabenki yao na tuwaruhusu kuja hapa kwetu kuwekeza na kuchota rasilimali zetu kwa faida kiduchu. Wapo wachache ambao bado hadi leo hii wanavaa suti za Mwalimu, zile cha Kichina au Kaunda suti.
Jina la Mwalimu, linatumika kwa mema na mabaya. Wengine wanalitumia kujinufaisha na wengine wanalitumia kujenga jamii iliyo bora na imara. Kuna wanaolitumia jina la Mwalimu, ili wakubalike kwenye jamii. Vyovyote vile ni kwamba swali ambalo mtu anaweza kujiuliza ni je, sifa hizi za Mwalimu zinabaki kuwa nyimbo za kuburudisha masikio na mambo yanaishia hapo au tunamfuata? Je, sisi ni wafuasi wa Mwalimu? Ni wangapi wanafanya yale aliyoyafanya na kuyaishi Baba wa Taifa letu? Mwalimu, alipigania uhuru na umoja wa Afrika nzima. Leo hii sisi hata Muungano wetu uko mashakani, Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, hadi leo Tanzania, inajikokota na mambo mengi yanakwenda polepole kwa vile sisi hatujawa tayari.
Kwa vile Mwalimu alipigania umoja wa Afrika, dunia nzima ilitegemea Tanzania iwe mstari mbele kusukuma na kuhimiza umuhimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hatimaye umoja wa Afrika. Hatuwezi kuhubiri maji wakati sisi tunakunywa mvinyo. Hatuwezi kuziimba sifa za Mwalimu midomoni wakati maisha yetu na matendo ni kinyume kabisa na maisha yake.
Ni wazi kuna mambo mengi ambayo tunafanya kinyume na Mwalimu. Mfano sisi tunawafukuza wahamiaji haramu, wakati Mwalimu, alikuwa ameifanya Tanzania kimbilio la kila Mwafrika hata na wengine nje ya Afrika.
Leo hii Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuwafukuza wahamiaji, ambao wamebatizwa jina la wahamiaji haramu. Inasikitisha kuona kwamba hata watu ambao Mwalimu aliwapatia uraia kwa sababu ya sura zao kufanana na zile za nchi jirani, basi wanahukumiwa kuwa wahamiaji haramu. Kuna wakati Mwalimu alisema Rwanda na Burundi ni nchi ndogo hivyo ni bora watu wengine wakahamishiwa Tanzania. Leo hii sisi tunaoimba sifa za Mwalimu, tunawafukuza watu kwa kisingizio cha wahamiaji haramu.
Mwalimu, hakufungamana na upande wowote, kwa maana kwamba kama ana urafiki na Wachina, na ikitokea Wachina wakachukizana na Wajerumani, basi na Mwalimu, awachukie Wajerumani.
Alikataa katika maisha siasa za kufungamana. Lakini sisi, ukiwa upinzani ukawa na urafiki na CCM, vyama vya upinzani vinakuona wewe ni msaliti.
Pia, CCM hawataki kusikia mwanachama wao ana urafiki na upinzani hata kama ni mgonjwa, ukitembelea, wewe ni msaliti. Huu haukuwa msimamo wa Mwalimu. Yeye hakutanguliza chama chake cha siasa, dini yake na wala hakutanguliza kabila lake.
Orodha ni ndefu. Kwa leo ningependa kujadili machache juu ya Mwalimu na hasa yale ambayo tunafanya kinyume. Sote ni mashahidi kwamba Mwalimu, hakutumia hata mara moja lugha ya mipasho. Mfano mipasho kama “ Watawezaa”, “CCM ina wenyewe”. “CCM nambari one” na mengine yanayofanana na hayo.
Kwa Mwalimu tulisikia “Tanu yajenga nchi” “Mvua za kwanza ni za kupandia” “Siasa ni kilimo”, “inawezekana, timiza wajibu wako”.
Daima Mwalimu alitumia lugha ya kuwaunganisha watu na si kuwatenganisha. Ni bahati mbaya kwamba siasa zetu leo hii zimetawaliwa na lugha za mipasho ambazo kwa kiasi kikubwa zinawatenganisha watu na kujenga chuki. Ndiyo, maana tunauliza, ni kwa nini tunaendelea kuimba sifa za Mwalimu kama tunafanya kinyume?
Pia, tunakumbuka sote kwamba Mwalimu, hakuvaa sare za CCM. Ina maana hakukipenda chama chake? Au hakuunga mkono sare hizo kwa vile zinachochea ushabiki? Au labda kuna mtu anayefahamu sababu, atueleze? Kwa nini Mwalimu, hakuvaa sare za CCM? Yeye alikuwa ni mwenyekiti wa CCM, lakini hakuvaa sare za CCM. Jambo la kushangaza ni kwamba baada ya Mwalimu, waliomfuata walianza kuvaa sare za chama chao. Na kwa vile hadi sasa Mwenyekiti wa chama kinachotawala ndiye Rais wa nchi, basi tunashuhudia Rais wa nchi akiwa kwenye sare za chama chake.
Mwalimu, hakuwa na ushabiki wa vyama siasa. Hatukusikia hata mara moja akisema “tuwachinje wapinzani” au “tukomboe majimbo”. Mwalimu, alijenga hoja, aliitetea na alifundisha. Mwalimu, alikubali majadiliano na kukubali kushindwa kama mtu mwingine alijenga hoja nzito kuliko yake. CCM, na hasa wale walio kwenye vikao vya juu vya chama chao, na hasa wale waliobahatika kufanya kazi na Mwalimu, wakiwa wa kweli wanaweza kutoa mifano hai ya ninachokijadili hapa.
Leo hii, siasa zetu zimetawaliwa na mipasho, ushabiki na ushindani wa kijinga. Kwa maana kwamba, kama mtu wa CCM amejenga hoja yenye mashiko, hoja ya kizalendo kwa nini isiungwe mkono na wapinzani? Au kama mpinzani amejenga hoja yenye mashiko na yenye uzalendo, kwa nini asiungwe mkono na CCM? Kupinga hoja ya mtu bila kutoa hoja ya msingi kumpinga kwa kisingizio cha kutokuwa kwenye chama kimoja cha siasa, ni ushindani wa kijinga. Pia, ni dhambi kuendelea kuimba sifa za Mwalimu, wakati tunaishi na kufanya kinyume.
Mwalimu, hakujilimbikizia mali na wala hakujenga nyumba za kifahari. Watoto wake walisoma shule za Serikali na ndugu zake hawakupata upendeleo wowote kwenye Serikali. Mwalimu, hakupendelea kabila lake au kuwapendelea watu wa Kanda ya Ziwa. Sifa za mtu, zilitosha kumpatia nafasi yoyote ile kwenye Serikali. Leo hii tunashuhudia rushwa, ufisadi na baadhi ya viongozi wakijilimbikizia mali, wanajenga majumba ya kifahari na kuwasomesha watoto wao nje ya nchi.
Ni bahati mbaya kwamba tumebakia kumsifia Mwalimu kwenye nyimbo na kuweka pembeni matendo yake. Inasikitisha kuona nyuma yetu tunaacha kizazi cha mipasho, ushabiki na ushindani wa kijinga. Vijana wetu kama yuko CCM, hataki kusikia chochote upande mwingine. Au kama kijana yuko upinzani, hayuko tayari kusikia lolote la CCM au la chama kingine.
Ni bahati nzuri kwamba Rais wetu wa sasa John Magufuli anajitahidi kwa nguvu zote kupitia kwenye nyao za Mwalimu na kuhakikisha makao makuu ya nchi yanakuwa Dodoma kama alivyotaka Baba wa taifa. Anapambana na mafisadi, rushwa na kuhakikisha raslimali za taifa zinanufaisha Watanzania wote. Ni bahati mbaya kwamba pamoja na kazi nzuri anazozifanya, bado na yeye amefungwa kwenye mipasho na ushabiki wa vyama vya siasa.
Rais wetu anatwambia kila siku kwamba maendeleo hayana chama. Lakini tunashuhudia wimbi kubwa la watu wakihama vyama vya upinzani na kwenda CCM, na yeye anawapokea kwa kushangilia. Kama maendeleo hayana chama na yeye anasema ni kiongozi wa Watanzania wote, kwa nini anafurahi na kushangilia watu wakitoka vyama vya upinzani na kurudi CCM?
Tukitaka kufanikiwa kama taifa, tuache utamaduni wa kuimba sifa za Mwalimu kwenye midomo yetu. Tuache utamaduni wa kuhubiri maji na huku tunakunywa mvinyo. Tumfuate Mwalimu. Tuache ushabiki wa kisiasa, tuache lugha za mipasho, tuache utamaduni wa kuvaa sare za vyama vya siasa, tuache utamaduni wa kufungamana, tuache ushindani wa kijinga. Tushirikiane kulijenga taifa letu kwa kumfuata baba wa taifa.
Kwa vile tunamsifia na kumkumbuka baba wa Taifa kila mwaka na tunamtaka kwa kila jambo ina maana tunayapenda yale aliyoyaishi na kuyatenda. Ili kuhakikisha yanadumu na yanatoa mchango wa kuliendeleza taifa letu basi ni bora tukayaingiza kwenye katiba yetu. Sote tunafahamu Mwalimu alivyokuwa akisisitiza umuhimu wa katiba. Hivyo tujitahidi kuendeleza mchakato wa Katiba mpya. Inawezekana, timiza wajibu wako. Tusimsifu kwa nyimbo tu bali tumfuate Mwalimu, kwa matendo.
Padre Privatus Karugendo.
+255 754 633122
pkarugendo@yahoo.com

No comments:

Post a Comment