Friday, November 24

MOI ilivyotumia changamoto kuibua fursa ya matibabu bora


Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) ni moja ya eneo limalotazamwa kwa macho mapana na Watanzania wote.
Kwani hicho ni miongoni mwa vitovu vya afya nchini licha ya kuwa ndani ya miaka miwili iliyopita, imepitia kwenye changamoto lukuki kutokana na kutoa matibabu kwa wagonjwa wa ajali na mifupa kwa kusuasua.
Licha ya kuwa si rahisi kuzimaliza changamoto zote za utoaji huduma ya matibabu kwa wagonjwa, lakini kwa mujibu wa viongozi wa hospitali hiyo, wameyapunguza na sasa wameimarisha huduma kwa kiwango kikubwa.
Mkurugenzi wa Tiba wa taasisi hiyo, Dk Samuel Swai alipozungumza na Mwananchi hivi karibuni, alisema changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo ni pamoja na uhaba wa wodi, ucheleweshaji wa matibabu hasa ya upasuaji.
Anasema wagonjwa wengi walilazimika kusubiri huduma hiyo kwa muda mrefu kutokana na uhaba mkubwa wa vifaatiba uliokuwa ukiwakabili.
Pia, kulikuwa na tatizo la uhaba wa vitanda na matibabu ya kibingwa yaliyosababishwa na uhaba wa madaktari bingwa, tatizo hilo alilolitaja lilikuwa mwiba mchungu kwao na kwa wagonjwa.
Hata hivyo, Dk Swai anasema Novemba 9, 2015 ilikuwa siku nzuri kwao baada ya Rais John Magufuli kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kufanya mabadiliko chanya yaliyoboresha utoaji wa huduma na mazingira bora kwa watoa huduma wa nyanja mbalimbali.
“Kabla ya kutembelewa na Rais, hapa kwetu wodi moja tulikuwa tukiwalaza wagonjwa 90 hadi 100, wachache waliweza kulala vitandani lakini majeruhi na wagonjwa wengi tulikuwa tukiwalaza sakafuni, kwenye korido hadi kwenye ngazi na baadhi walilala nje ya wodi. Rais hakuipenda hali ile, hivyo aliamuru tuhamie kwenye hili jengo jipya,” anasema mkurugenzi huyo na kuongeza:
“Aliamuru pia tuletewe vitanda vingi kwenye taasisi hii na tangu wakati huo, ni miaka miwili sasa imepita suala la wagonjwa kulala sakafuni kwenye wodi za Moi limebaki historia.”
Anasema vitanda vya kulaza wagonjwa vimeongezeka kutoka 159 vya awali na sasa wanavitanda 340.
Dk Swai anasema Serikali pia ilitenga fedha nyingi zilizowezesha kupatikana kwa vifaatiba.
Licha ya faraja hiyo, changamoto ya ongezeko la idadi ya wagonjwa bado ipo.
Anasema idadi hiyo huongezeka mwaka hadi mwaka. “Tunafanya upasuaji wa kawaida kati ya wagonjwa 600 hadi 700 kwa mwezi, ukipiga hesabu hawa ni wa dharura, ukichanganya na wa kawaida tunawafanyia upasuaji wagonjwa 10,000 kwa mwaka.”
Anasema fedha zilizopatikana kutoka Serikalini zilinunua vifaatiba vya kuwatibu wagonjwa wa ajali ambao vifaa vyao vinahitajika kwa wingi hasa madereva wa bodaboda, abiria na waenda kwa miguu ambao idadi yao inaongezeka kila kukicha.
Dk Swai anasema majeruhi wengi ni walioumia vichwa, mifupa mirefu, migongo na miguu.
Anasema wengi wao huhitaji kuwekewa vyuma na baadhi hulazimika kuwakata viungo ili kuokoa maisha yao.
Hali iliyovyo sasa baada ya miaka miwili ya msukosuko
Mkurugenzi huyo anasema mazingira ya kutolea huduma kwa sasa yameimarika na mazingira ya kazi pia kwa watendaji wa Moi ni rafiki tofauti na awali.
Dk Swai anasema mazingira ya awali yalikuwa hatarishi kwa watumishi na wagonjwa.
Hata ri kubwa ilikuwa ni ya kupata maambukizi kutokana na ufinyu wa nafasi na idadi ya wagonjwa iliyokuwa ikikpokelewa hospitalini hapo. “Kwa mfano, wodi yenye vitanda 33 ilikuwa inalaza wagonjwa 90 hadi 100,” anasema.
Matibabu ya kibingwa
Mkurugenzi wa Moi, Dk Respicious Lwezimula anasema idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji imeongezeka hadi kufikia wagonjwa kati ya 600 hadi 700 kwa mwezi ikilinganishwa na awali.
Anasema hilo limewezekana kutokana na Serikali kuongeza upatikanaji wa vifaatiba na nafasi ya kulaza wagonjwa.
Anasema ndani ya miaka miwili, taasisi imefanikiwa kuwafanyia upasuaji mkubwa wagonjwa 221 wa nyonga (total hip replacement), 259 wa mgongo (Specialised spine surgery) na 306 wa ubongo (specialized brain surgery).”
Pia, hospitali hiyo imewafanyia upasuaji wa matundu (athroscopy) wagonjwa 314, watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (hydrocephalus and spina bifida) 852, wagonjwa 120 wa magoti, 144 wa mfupa wa kiuno na upasuaji mwingine wa mifupa, wagonjwa 8,615.
Hata hivyo, Dk Lwezimula anasema kwa sasa wamemudu kutengeneza viungo bandia 1,362 baada ya Serikali kurahisisha upatikanaji wa malighafi za kutengenezea viungo hivyo na kuokoa fedha ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kupata tiba hiyo kwa gharama kubwa.
Ujenzi wa jengo awamu ya tatu
Anasema mradi wa ujenzi wa jengo la Moi kwa awamu ya tatu, Serikali imetoa Sh16.5 bilioni kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
“Fedha hizo zimeelekezwa zitumike kununulia vifaa. Pamoja na mambo mengine, Taasisi itanunua vifaa vya uchunguzi vya kisasa vya radiolojia vya CT Scan, MRI na X-Ray 2, ‘C-arm’ na Ultra Sound ya kisasa,” anasema.
Dk Lwezimula anabainisha kuwa mara baada ya MOI kukamilika kutakuwa na uanzishwaji wa maabara ya kisasa ambayo itafanya vipimo vyote vya damu.
Vitanda katika vyumba vya uangalizi maalum ICU vitaongezwa kutoka vinane mpaka 32 na kitengo kipya cha kisasa cha wagonjwa wa dharura.
Pia taasisi itaongeza vyumba viwili vya upasuaji na kufanya taasisi kuwa na vitanda 8 vinavyotoa huduma hiyo.
Aidha anasema kumekuwa na mafunzo mbalimbali ambayo Serikali imekuwa ikiwajengea uwezo wataalamu ndani ya nchi kwa kuleta wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kwa mfano Chuo Kikuu cha Weil Cornel na Taasisi ya Sign ya Marekani ambao walifika kutoa mafunzo.
“Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye upatikanaji wa vifaa tiba na miundombinu MOI imechaguliwa kuwa kituo cha kufundishia cha madaktari bingwa cha COSESCA na CANESCA ambapo wataalamu kutoka mataifa mbalimbali duniani wanakuja kujifunza MOI aidha mafunzo haya yamesaidia kupunguza gharama za kuwapeleka wataalamu wetu nje ya nchi,” anafafanua.
Vyumba vya ICU
Dk Lwezimula anasema nia ya MOI kwa sasa pindi wagonjwa wa ajali wanapofikishwa hawatapelekwa wodini, bali wataingizwa moja kwa moja kufanyiwa upasuaji .
Hii itakuwa tofauti na awali ambapo walifanya hivyo kwa wale wenye vidonda huku waliovunjika mifupa hawana vidonda walipelekwa wodini kwanza ndipo wapangiwe upasuaji.
“Kwa sasa hali itakuwa tofauti tukivifungua vyumba viwili vya upasuaji na kuweka vitanda 16 vya ICU na 16 vya dependence unit. Serikali imetoa Bilioni 16 kumalizia jengo na vifaa tiba na maabara ya damu tunayo tulipata msaada kutoka ubalozi wa Kuwait,” anasema.
Kwa upande wake Dk Swai anafafanua kuwa kupitia maabara hiyo ya damu, lazima huduma za kuvuna mazao aina nane yatokanayo na damu ili waweze kutumia katika upasuaji huo ikiwemo chembechembe nyekundu za damu na mazao mengineyo.
Anasisitiza kuwa MOI imejipanga kuwa na vyumba viwili kwa ajili ya upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na kwamba kwa sasa wamejikita katika kuendelea kutoa ushauri na elimu kwa mama wajawazito.
Dk Swai anasema upasuaji wa kunyoosha migongo uliopinda kwenda pembeni na nyuma pia wamefanikiwa kuanza kuwafanyia watoto.
“Tumewafanyia watoto saba kwa mara ya kwanza nchini na wapo wengine wasiopungua 30 wanasubiri kunyooshwa migongo yao hii imekuja sambamba na ufundishaji wa wataalamu wetu ilianza mwaka juzi Novemba na inaisha Novemba mwaka huu ambapo vijana watatu wa kozi hii wahatimu mwakani,” anasema.
Anasema hata hivyo taasisi hiyo pia inafanya upasuaji wa kuondoa damu kwenye ubongo, “tumenunua mashine kadhaa ikiwemo ya kufungua fuvu kwa haraka na ile itakayosaidia kuona mpaka chini ya fuvu na tutakapopata vifaa vya kuchunguza tunataka hata mishipa inayopasuka kwenye ubongo tuanze kuwafanyia hapa hapa nchini.”
“Hawa wagonjwa wa vivimbe chini ya fuvu lazima waende nje kwa kuwa lazima uwe na vifaa zaidi tuna mpango wa kununua hivi vifaa tutapunguza kwa asilimia kubwa sana gharama za kulepeka wagonjwa nje ya nchi ikiwa tufanya oparesheni zote za kibingwa,” anasema.
Matibabu kwa wakati
Dk Swai anafahamisha kuwa abiria wengi wanaowapokea hugongwa na kurushwa kwenye mitaro, hivyo inakuwa vigumu matibabu yao na wengi wanafikia vichwa hivyo wanaumia kwa kiasi kikubwa maeneo hayo.
Anasema matibabu ya wakati kwa kuzingatia lisaa la dhahabu ‘golden hour’, nchini bado ni tatizo kwani wengi wanafika wakiwa wamechelewa na hata kama kuna mshipa wa damu ulioumia inakuwa vigumu kuunga tena.
“Unakuta mgonjwa anafika ameumia sana nyama zimesagika sana hata ukifanya nini si rahisi kuunga inabidi uondoe hicho kiungo, mapungufu yetu ni vifaa vya kutibia na kugundua mapema maeneo yaliyoathirika na kuungia mishipa ya damu,” alisema.
Akitolea mfano, Dk Swai alisema vifaa bado tatizo kwa mfano mtu ameumia mshipa wa damu kama damu haifiki kwenye viungo inatakiwa haraka sana kuungua huo mshipa hivyo awahishwe hospitalini au kwenye chombo kinachochunguza kubaini iwapo kuna mshipa wowote umejikunja ili aweze kuungwa mapema asipoteze hicho kiungo.
“Pia changaoto nyingine ni kurudishia viungo haraka kwa mfano vyuma vya kumwekea mgonjwa mara moja mapema tu anapoumia, sehemu ya tatu ni upungufu katika kurekebisha nyama ambazo zimeumia sana kama misuli ambayo imekwanguliwa, ngozi na wakati mwingine kurekebisha nyama zisioze hilo bado linatupa changamoto.”
Ukiondoa mapungufu hayo, Dk Swai alisema MOI ina uwezo wa kutibu huku akitolea mfano kwa wanaokatwa viungo kwa sasa wamepungua kutokana na kuongezeka kwa utaalamu na serikali kununua vifaa vya kutosha kwa kipindi cha miaka miwili.
“Kwa sasa wastani wa wagonjwa wanaokatwa viungo ni watano kwa mwezi, hawa unakuta hakuna chochote mabacho unaweza kufanya mishipa ya damu imekatika yote, wameumia sana au mifupa, misuli imesagika kabisa na mfupa wa kukanyagia una vipande zaidi ya ishirini au 30 ambavyo huwezi kuviunga pamoja.”

No comments:

Post a Comment