Mataifa mawili jirani Myanmar na Bangladesh, yamekubaliana kusaidia kuwahamisha hadi mahala salama watu wa jamii ndogo ya Waislamu wa Rohingya, ambao wanaishi katika kambi mbovu za wakimbizi nchini Bangladesh.
Hakuna muda uliowekwa kwa shughuli hizo kuanza- au maelezo zaidi haijatolewa kuhusiana na namna shughuli hizo zitatekelezwa.
Katika mkataba huo, watu wa jamii ya Rohingya wataanza kurudi makwao nchini Myanmar katika kipindi cha miezi miwili tu ijayo .
Mkataba huo wa kuwarejesha makwao Warohingya unamsingi wa mkataba wa awali baina ya mataifa hayo mawili wa mwaka wa 1992, japo mabadiliko machache yameafikiwa kutokana na hali halisia ya sasa katika jimbo la Rakhine Myanmar.
Wakimbizi hao watatakiwa kujaza fomu zitakazothibitisha kuwa wanatoka jimbo hilo la Rakhine, mbali na kutoa chapa cha vitambulisho vya Myanmar.
Aidha watatakiwa kueleza nia yao ya kurejea katika jimbo la Rakhine.
Kambi mbili za kuwapokea wakimbizi tayari zimeshaundwa.
Mkataba huo hatahivyo hauelezei ni majukumu yapi yatakayotekelezwa na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia maslahi ya wakimbizi UNHCR.
Vivyo hivyo hakuna hakikisho lolote la usalama wao uliothibitishwa kwa maandishi wala jeshi la taifa hilo ambalo limelaumiwa kwa mauaji utekaji, uporaji na ubakaji, halijatoa hakikisho la usalama wa Warohingya.
Makamanda wa jeshi la Myanmar wamepinga tuhuma zote dhidi yao na wamesisitiza kuwa idadi halisi ya warohingya waliokimbilia usalama wao ni chache mno ikilinganishwa na idadi inayotolewa na asasi za kimataifa.
Wao wanadai kuwa wengi wao ni watu wa jamii ya Wabengali.
Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi ameanzisha tume maalum kuchunguza ugomvi ulioibuka katika jimbo hilo la Rakhine baina ya raia na jeshi.
Tume hiyo inaongozwa na raia japo jeshi la nchi hiyo linadhibiti vitengo vyote vya taifa.
No comments:
Post a Comment