Wakati wanachama wa umoja wa waendesha bodaboda katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rulenge wakijitolea kuchangia uniti 27 za damu na Sh20,000 kwa ajili ya maji ya kunywa, Serikali wilayani Ngara imetoa Sh1 milioni kugharamia chakula.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba 10,2017 katika viwanja vya Hospitali ya Misheni ya Rulenge walikolazwa majeruhi hao, wanafunzi 42 na mwalimu mmoja, mwenyekiti wa bodaboda, Agustine Kaloli ameomba makundi mengine ya kijamii na watu binafsi kujitokeza kuwasaidia majeruhi hao ili kuokoa maisha yao.
Akizungumzia michango, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama amesema uongozi wa Serikali wilayani humo umetoa Sh1 milioni kugharamia mahitaji ya chakula na huduma zingine za kijamii kwa majeruhi ambao wanatoka maeneo ya mbali kiasi cha ndugu kutoweza kuwapelekea chakula.
Shirika la Caritas Rulenge nalo kimejitokeza kutoa msaada wa chakula kwa familia za watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Akizungumza na majeruhi wa mlipuko wa bomu uliotokea Novemba 8,2017 na kusababisha vifo vya wanafunzi watano, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mntenjele amepiga marufuku biashara ya vyuma chakavu wilayani humo bila mhusika kusajiliwa na kuwa na vibali maalumu.
“Hata watakaosajiliwa na kupewa vibali, hawataruhusiwa si tu kununua vyuma chakavu maeneo ya shuleni, bali pia kuhusisha watoto katika biashara hiyo,” amesema Mntenjele.
Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Revocatus Ndyekobola amesema baadhi ya majeruhi ambao hakutaja idadi yao wanatarajiwa kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kutokana na uchunguzi kubaini wanahitaji matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment