Wednesday, November 15

MAHAKAMA YA KISUTU YAMUHUKUMU BOB CHACHA WANGWE MWAKA MMOJA NA NUSU JELA AMA FAINI YA MILIONI 5


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mtoto wa marehemu Chacha Wangwe, Bob Chacha Wangwe kwenda jela mwaka mmoja na nusu au kulipa faini ya shilingi milioni tano baada ya kupatikana na hatia kuchapisha habari za uongo mtandaoni, katika akaunti yake ya Facebook

hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma shahidi ambaye amesema ameridhika na ushahidi ulioletwa mahakamani na mashahidi sita wa upande wa mashtaka na vielelezo vitano, walioweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo.

Bob ambaye ni mwanafunzi wa sheria chuo kikuu na mtoto wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, mkoani Mara na Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara amepatikana na hatia chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015. 

Akisoma hukumu hiyo, Shaidi amesema, Mei 7, 2016 polisi walipata taarifa ya chapisho la Bob ambapo walianza kumfatilia na kumkamata kisha walichukua simu na kuipeleka maabara ya Polisi ili kuikagua.

"Kimsingi Bob hukupinga kuandika maneno hayo lakini umedai kuwa hukuyachapisha katika jamii bali yalikuwa ni siri kwenye akaunti yako,".amesema Shahidi.

Hakimu Shaidi amesema, wakati wa ushahidi imeelezwa kuwa simu yake ilipokaguliwa ilionekana ilitumika kuchapisha ujumbe huo kwa jamii na watu waliujibu, kuashiria ujumbe uliwafikia.

Hiyo inaonyesha dhahiri alikuwa na nia ya kuchapisha taarifa hiyo, kueleza kile ambacho alikiona sahihi kama ingekuwa ni ujumbe wake binafsi basi polisi wasingeweza kumtafuta, na watu wasingejibu-respond,".

Akijitetea asipewe adhabu kali, Bob aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ni mwanafunzi wa masomo ya sheria, pia ni kijana mdogo na ni mara yake ya kwanza kutenda kosa.Hakimu Shaidi alikubaliana na hoja za Bob, kwa kuwa mahakama inamuona kweli bado ni mdogo na anapaswa kufanya mambo mengi mazuri katika jamii.

Pia amesema kama yeye ni mwanafunzi wa masomo ya sheria anapaswa kufanya mambo mema katika jamii vitu ambavyo wengine watamuiga." Mahakama imezingatia utetezi wako ba ule ushahidi wa upande wa mashtaka na inakuhukumu kulipa faini ya Sh. milioni 5 ama uende jela mwaka mmoja na nusu, dhamana iko wazi," Alisema Shaidi

Bob Wangwe alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 12,2016.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa hiyo anadaiwa kuchapisha taarifa za kupotosha katika ukurasa wake wa Facebook, kosa alilotenda Machi 15,2016 ambapo kupitia ukurasa wake wa Facebook aliandika ujumbe usemao: “Tanzania ni ambayo….inajaza chuki wananchi … matokeo ya kubaka Demokrasia Zanzibar ni hatari zaidi ya muungano wenyewe…. Haiwezekani nchi ya Zanzibar kuwa koloni la Tanzania bara kwa sababu za kijinga.”

No comments:

Post a Comment