Wednesday, November 15

Maafisa AAKIA wafurahishwa ulinzi JNIA


 Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia), akitoa maelezo kwa Maafisa wa Idara mbalimbali kutoka kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA) waliofanya ziara ya mafunzo. Kushoto ni Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama JNIA, Bw. Hamis Mashaka.
 Maafisa wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), Bw. Shaaban Kombo (kuanzia wa pili kulia), Bi. Zakhia Mohamed, Bw. Salehe Said na Bi. Fatma Yussuf wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Lugano Mwansasu (kulia) akiwaelekeza jambo wakati wa ziara yao ya mafunzo iliyofanyika jana.
  Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Hamis Mashaka (kushoto), akitoa maelezo mbalimbali yanayohusiana na ulinzi na usalama kwa maafisa kutoka idara mbalimbali za Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) cha Zanzibar jana walipofanya ziara ya mafunzo.
 Meneja Uendeshaji  cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Vedastus Fabian (kulia) akiwapa maelezo mbalimbali Maafisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA) walipofanya ziara ya mafunzo jana.
Afisa Habari katika jengo la Watu Mashuhuri la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (VIP-JNIA), Bw. Kenny Kwenga (kushoto) akitoa maelezo ya namna watu mashuhuri wanavyohudumiwa kwa maafisa kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA), walipofanya ziara jana. Kulia ni Msimamizi wa VIP, Bi. Josephine Mwaisukule. 
.
MAAFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.

Maafisa hao kutoka Idara mbalimbali walitoa kauli hiyo jana katika ziara ya siku moja ya mafunzo JNIA, ambapo walitembelea maeneo mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa husika.

Mkuu wa msafara wa maafisa hao, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Bw. Shaaban Kombo alisema JNIA inaulinzi madhubuti kwa abiria na mizigo hukaguliwa kwa kutumia mitambo maalum kabla ya kupanda ndege au kuingia ndani ya jengo kwa kazi mbalimbali, ambapo wameahidi kufuata nyayo hizo ili kuzuia uhalifu unaofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu.

Bw. Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya msingi ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo pia katika upande wa utoaji wa vitambulisho wamejifunza namna utoaji wa vitambulisho unavyofanyika, ukiwa ni tofauti na AAKIA ambao hutoa vitambulisho vya kudumu mara baada ya taratibu kukakamilika, wakati JNIA hutoa vitambulisho vya muda kwa muombaji ili aweze kuendelea na kazi, wakati akisubiri cha kudumu kikamilike kutengenezwa.

“Tumefaidika na mambo mengi ukiangalia sisi kwetu hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila kwetu kwa kipindi chote mteja anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea na kazi zake eneo la kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa na cha muda kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa katika matengenezo,” alisema Bw. Kombo.

Naye Mkuu wa kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha JNIA, Bw. Lugano Mwansasu alisema ziara ya maafisa wa AAKIA imewafariji na kuanza ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano, ambapo nao wamejifunza kulingana na maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.

Bw. Lugano alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuiga mfano huu wa kupeleka maafisa wake kwenye viwanja mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza utendaji kwa lengo la kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.

“Kila siku mambo ya uendeshaji yanabadilika, basi tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu tujifunze huko, zipo changamoto labda sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu kutoka kwa wenzetu,” alisema Bw. Lugano.
Katika hatua nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA, Bw. Vedastus Fabian alisema faida ya ziara ya mafunzo ni kujijengea uwezo na mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na kingine.

Bw.Fabian alisema ziara hizo zinasaidia katika kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege, ambapo kwa sasa kumekuwa na masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na nyara za serikali.

No comments:

Post a Comment