Thursday, November 9

Kondoo si wapumbavu sana, utafiti wabaini

KondooHaki miliki ya pichaSPL
Image captionKondoo wana uwezo wa kutofautisha nyuso za watu
Kondoo wamedhihirisha kwamba wana uwezo wa kutambua na kutofautisha nyuso za watu wanaowafahamu, kwa mujibu wa utafiti.
Watafiti katika Chuo Kikuu cha Cambridge waliweza kuwafundisha kondoo kutambua nyuso za watu mashuhuri wakiwemo waigizaji Jake Gyllenhaal na Emma Watson, rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mtangazaji wa BBC Fiona Bruce.
Baada ya mafunzo, kondoo walionekana kuchagua picha za nyuso walizozifahamu awali mara nyingi.
Hii inadhihirisha kwamba kondoo wana uwezo wa kutambua na kutofautisha nyuso za watu sawa na wanyama wa familia ya binadamu, tumbili na sokwe.
Utafiti wa awali ulikuwa umedhihirisha kwamba kondoo huweza kutambua na kutofautisha nyuso za kondoo wengine na pia watu wanaowatunza.
"Tulichofanya ni kuuliza iwapo kondoo wanaweza kumtambua mtu kutoka kwenye picha," mtafiti mkuu Prof Jenny Morton amesema.
"Tuliangazia kuhusu iwapo ni kweli au la wanyama wanaweza kufasiri kitu ambacho kina upana na urefu (2D) pekee kwamba ni mtu huyo."
Sheep
Kondoo jike wanane walifunzwa kutofautisha nyuso za watu wanne mashuhuri kutoka kwa mkusanyiko wenye picha za watu wasiowafahamu kwa kutumia chakula kama zawadi.
Kondoo hao walionyeshwa picha tofauti kwenye vioo vya kompyuta mbili; walifanya uteuzi wao kwa kuzuia miali ya infrared kwa kutumia pua na hapo zawadi yao ya chakula ikatolewa.
Baada ya kubainisha uwezo wa mifugo hao kuwatambua watu hao mashuhuri, watafiti hao waliwawekea mtihani mwingine sasa.
Walitaka kujua iwapo wanyama hao wangewatambua watu hao kutoka kwenye upande tofauti.
Kwa mara nyingine, waliweza.
Mwisho, wakataka kujua iwapo wangewatambua watu wanaowatunza kwa kuangalia kwenye picha.
Picha za watu wanaowatunza zilichanganywa na za wengine bila kufuata utaratibu wowote kwenye skrini za kompyuta.
Tena, walifanikiwa kufanya hivyo.
Matokeo hayo yanaonyesha wanyama hao wana uwezo wa kutambua na kutofautisha nyuso sawa na wa tumbili, sokwe - na binadamu.
Watafiti wamesema siku za usoni inaweza kuvutia kutafiti iwapo kondoo wanaweza kutofautisha hisia kwenye nyuso za binadamu.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la Open Biology.

No comments:

Post a Comment