Wiki mbili zilizopita tasnia ya usafiri wa anga nchini Kenya ilipata pigo baada ya mmoja wa marubani bora, Kapteni Apollo Malowa kufariki dunia akiwa kazini. Mauti yalimkuta baada ya helikopta ambayo alikuwa akirusha kupata hitilafu na kuanguka katika Ziwa Nakuru.
Malowa anatajwa kuwa alikuwa mmoja wa marubani wenye uzoefu wa hali ya juu, mbunifu na aliyeaminiwa katika Afrika Mashariki. Amewahi kuwa rubani wa ndege za Jeshi la Anga nchini Kenya na hadi anapata ajali alikuwa rubani warubani bora wa kampuni ya ndege za kukodi ya Flex Air, ambako pia alikuwa mkurugenzi.
Katika kampuni hiyo ya Flex Air, alikuwa chaguo la wanasiasa wengi mashuhuri wakiwemo marais wa sasa, wastaafu na wafanyabiashara wazito.
Picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii mara baada ya taarifa za kifo zinaonyesha kwamba Kateni Malowa alitumika katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Tanzania ambako mwaka 2015 alirusha helikopta iliyotumiwa na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli ambaye alishinda kinyang’anyiro hicho.
Pia alikuwa na mkataba wa aina hiyo na serikali ya Uganda wakati Rais Yoweri Museveni akifukuzia kura za kumwezesha kubaki ikulu mwaka 2016.
Kadhalika Kapteni Malowa ndiye alikodishwa kumrusha angani mgombea urais kwa tiketi ya Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga wakati wa kampeni za mwaka 2007. Vilevile, alikuwa rubani rasmi wa Odinga katika kipindi chote akiwa waziri mkuu katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Rekodi zinaonyesha Kapteni Malowa amewahi pia kuwarusha Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete, mshirika mkuu wa Nasa Musalia Mudavadi, kiongozi mashuhuri wa zamani katika Kanu Nicolas Biwott, na mawaziri kadhaa wa serikali ya Jubilee, mfanyabiashara Jimmy Wanjigi, gavana wa zamani wa Kiambu William Kabogo na wengineo.
Kwa miezi kadhaa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 8 mwaka huu, Kapteni Malowa alikuwa rubani wa mgombea wa kiti cha uwakilishi wa wanawake kaunti ya Kirinyaga, Wangui wa Ngirici.
Baada ya kufutwa na Mahakama ya Juu matokeo yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta Agosti 8, alipewa mkataba na Jubilee kwa ajili ya kampeni za uchaguzi wa marudio.
Picha za matukio
Akaunti zake za Facebook na Instagram zimejaa picha mbalimbali akiwa katika maeneo tofauti aliyowahi kutembelea na helikopta yake aliyoitumia kusafirisha wateja wake.
Picha moja ya Instagram Kapteni Malowa anaonekana akiwa amesimama kando ya helikopta iliyosajiliwa kwa namba 5Y-HKK iliyobandikwa picha za Rais Magufuli. Anaonekana pia katika picha nyingine akiwa ndani ya helikopta amevalia kofia iliyoandikwa “Chagua Yoweri Museveni” na nyingine iliyoandikwa kwa kifupi cha NRM yanayoaminika kuwa ni National Resistance Movement— chama cha Rais Museveni.
Katika picha nyingine ya Facebook, anaonekana kwenye helikopta pamoja na Odinga na pia katika picha nyingine yuko pamoja na mchezaji mashuhuri wa mpira wa raga Collins Injera wa klabu ya Kenya Sevens Rugby na mchekeshaji Jasper Muthomi maarufu kama MC Jesse.
Kapteni Malowa anaonekana na helikopta iliyosajiliwa kwa namba 5Y-JNM, yenye rangi za chama cha Jubilee na imeandikwa Wangui wa Ngirici.
Katika Facebook, anatoa maelezo ya kazi yake kuanzia alipokuwa Jeshi la Anga ka Kenya kabla ya kujiunga na kampuni ya GeoAir Limited Novemba 1, 2014 kama rubani mkuu na mkurugenzi wa safari za anga.
Utata wa tarehe
Taarifa zinaonyesha baadaye alihamia Shirika la Ndege la Northwood kama rubani mkuu Aprili 1, 2015 kabla ya kujiunga na Flex Air Charters Oktoba 1, 2016 kama rubani wa kawaida. Decemba 19, 2016 akawa mkurugenzi wa oparesheni katika kampuni hiyo hiyo.
Pamoja na mafanikio yake utata umekuwa ukimzingira Malowa. Mfano mwishoni mwa mwaka jana, alitawala vichwa vya habari kuhusu tukio la kushtua alipotua katika barabara yenye shughuli nyingi za kibiashara eneo la Bondo Kaunti ya Siaya ili kumsalimia tu mama yake wakati kwenye chopa hiyo alikuwemo Odinga.
No comments:
Post a Comment