Sunday, November 12

Jumuiya ya Kimataifa inavyobadili kauli, msimamo wa upinzani na serikali Kenya



Rais Uhuru Kenyatta anakabiliwa na mtihani mzito wa kuthibitisha uhalali wake. Matokeo ya ushindi aliopata Agosti 8 yalifutwa na Mahakama ya Juu kwa madai kuwa ulijaa dosari, na hivi sasa zimefunguliwa kesi tatu katika mahakama ileile kupinga ushindi wa uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.
Mazingira yanayomkuta Kenyatta kwa kiasi fulani yanataka kufanana na yaliyomkuta Daniel arap Moi isipokuwa yeye aliwazidi ujanja wapinzani.
Moi aliposhinda urais mwaka 1992, kwa asilimia 36 ya kura zote zilizopigwa, wapinzani wake walihoji juu ya uhalali wa ushindi huo, kama ilivyo sasa kwa Raila Odinga wa National Super Alliance (Nasa) anavyohoji uhalali wa ushindi wa Kenyatta katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.
Habari ni namna alivyopona wimbi la msukumo dhidi yake kutoka asasi za kiraia na upinzani uliokuja kujifunza kutokana na makosa yao. Moi alichanga vizuri karata zake akashirikisha raia na mbinu za kidiplomasia.
Moi alikuwa mwepesi kung’amua na mjanja; mwanasiasa halisi wa Kiafrika aliyekuwa na uwezo wa kuuchezea upinzani kama vikaragosi.
Endapo wangekuwa kitu kimoja, wapinzani wangeweza kushinda uchaguzi kwa asilimia 64 ya kura, ambazo zilikuwa zaidi ya asilimia 61 alizopata Mwai Kibaki mnamo mwaka 2002.
Lakini upinzani uligawika vibaya kati ya Kenneth Matiba aliyeongoza Ford Asili, Jaramogi Oginga Odinga akikumbatia Ford Kenya na Kibaki aliyekuwa kiongozi wa Democratic Party.
Wamarekani wabadilika
Kitu ambacho upinzani hawakujua ni kwamba mchezo ulikuwa umebadilika na Wamarekani ambao walikuwa wakiwaunga mkono, walibadili gia angani na kuonyesha utiifu wao kwa Moi shukrani kwa baa la njaa lililokuwa linaikabili Somalia.
Rais Moi, wakati huo aliamua kuruhusu Kenya kutumiwa na vikosi maalumu vya Jeshi la Marekani. Walipewa eneo la Mombasa ambako waliweka vifaa vya kufuatilia njia za anga na ardhini nchini Somalia hasa zinazoweza kutumiwa na serikali ya Marekani.
Wakati joto la kampeni za uchaguzi mkuu likizidi kuongezeka, na wakati upinzani ulikuwa unazungumzia suala la kususia, Marekani ilimtuma balozi mdogo wa masuala ya Afrika Herman Cohen kuonana na Moi katika ikulu ya Nairobi. Mkononi alikuwa na hundi ya dola za Marekani 5 milioni sawa na Sh500 milioni leo.
Kulikuwa na sababu ya kufanya hivyo. “Moi amekuwa mmoja wa marafiki zetu wazuri barani Afrika. Hajawahi kutukatalia maombi yetu likiwemo la haki ya kutumia bandari ya Mombasa na uwanja wa kimataifa wa Nairobi kwa ajili ya shughuli za kijeshi za Marekani katika Bahari ya Hindi,” aliandika Cohen katika kitabu chake kiitwacho “The Mind of the African Strongman”.
Mapema, wakati wa kelele za kurejeshwa mfumo wa siasa za vyama vingi, Cohen alimfuata Rais Moi na kumwomba awaachie huru wanasiasa waliokuwa kizuizini Matiba na Charles Rubia na wote waliotiwa hatiani kwa uhalifu wa kisiasa – Koigi wa Wamwere, wanasheria Rumba Kinuthia na Mirugi Kariuki na mwanaharakati wa Mwakenya, Kangethe Mungai.
Moi alimjibu Cohen: “Sawa, nitawaachia wote kwani hawana thamani ya chakula tunachowalisha.”
Kama ilivyoelezwa hapo juu Cohen na Moi wamekuwa marafiki kwa sababu. Wamarekani walipokuwa wanamtafuta mtu anayeweza kumshawishi kiongozi wa waasi wa Msumbiji, Alfonso Dhlakama, mkuu wa kundi la Renamo lililoendesha vita vya msituni kupambana na serikali ya kikomunisti ya Frelimo ili aanze mazungumzo na Rais Joaquim Chissano, ni Moi aliyejitolea kusaidia.
Siyo tu aliwapa viongozi wa waasi hati za kusafiria za Kenya bali pia kwa siri alimtuma katibu mkuu Bethuel Kiplagat kusimamia. Oktoba 1992, miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa Kenya mkataba ulitiwa saini.
Basi, Cohen alipowasili Nairobi kabla ya uchaguzi mkuu wa Desemba 29, 1992 waliotazama kwa makini lugha ya mwili kati ya wawili hao waliweza kung’amua haraka kwamba mchezo ulikuwa umebadilika.
Kwingineko familia ya Kennedy iliyokuwa na ushawishi, ambayo pia ilikuwa inaunga mkono upinzani, ilikuwa inajaribu kuandaa mkutano kati ya Cohen na viongozi wa upinzani jijini Nairobi.
Cohen alikataa kwa kuwa kufanya hivyo kungeharibu uhusiano na Moi ambaye msaada wake ulikuwa unahitajika kudhibiti mgogoro ulioanza kuibuka katika Pembe ya Afrika.
Muda mfupi baada ya kikao na Moi, na siku 20 kabla ya uchaguzi mkuu wa Kenya, Rais George Bush (mzee) aliamuru vikosi vya jeshi la Marekani kwenda Somalia, askari wa kwanza wa maji wa “Operesheni Rejesha Matumaini” wakawasili Desemba 10, 1992.
Kwa hiyo wakati Wakenya wakipiga kura, Moi alikuwa na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa Wamarekani ambao walikuwa wakimhitaji. Pia walibaini kwamba Moi atawashinda kiurahisi wapinzani waliogawanyika.
Baada ya uchaguzi, Kanu ilishutumiwa kwamba ilipika namba dhidi ya Matiba (madai sawa na Nasa kwa Jubilee) hivyo upinzani ukaingia katika kampeni za kuhoji uhalali wa ushindi.
Matiba aliitisha mkutano wa waandishi wa habari wa kimataifa jijini Nairobi kuzindua kampeni ya “Moi Lazima Aondoke” na uitishwe uchaguzi mpya.
Mwandishi mmoja wa kimataifa aliuliza: “Lakini Moi si amechaguliwa?” na kwa uwazi Matiba aliyeonekana kukerwa alijibu: “Ni nani amemchagua. Hata nyumbani kwake hakuchaguliwa …”
Haikuwa kweli japokuwa Matiba alikuwa na watu wachache waliomhurumia ndani ya upinzani waliokivuruga chama cha Ford.
Kama alivyoandika mwanahistoria wa Kenya Charles Hornsby katika kitabu chake, Kenya: A History Since Independence, “Moi alishinda urais kiuhalali kwani alipata kura nyingi za ukweli kuliko mgombea mwingine yeyote … mgawanyiko kati ya DP na Ford, na baadaye ndani ya Ford yenyewe, uliinufaisha Kanu kushinda uchaguzi ule kwa wingi mdogo wa kura.”
Baada ya Moi kufanikiwa kumwangusha Matiba kwa makosa ya kiufundi katika kesi ya kupinga ushindi wake, Moi aliingia katika kampeni ya kudhoofidha upinzani. Matiba alifanya kosa kususia vikao vya bunge akisema “ni upotevu wa muda” kwani mahudhurio yake yalikuwa ya kimkakati kuokoa kiti chake.
Chama chake kilidhoofika na kilidhihakiwa na vyombo vya habari. Septemba 1993, miezi tisa baada ya uchaguzi mkuu Matiba alitikiswa kwani Katibu Mkuu Gitobu Imanyara, Mwenyekiti msaidizi Paul Muite, mwanasheria Kiraitu Murungi, na katibu msaidizi wa masuala ya uchumi Robert Shaw walijiuzulu.
Moi akaanzisha ushirikiano na Ford Kenya, akamwalika Odinga katika ziara ya Turkwel Gorge Dam na akaandaa harambee kadhaa majimbo ya magharibi na Nyanza akitumia msemo wake maarufu “Siasa Mbaya, Maisha Mbaya”.
Katika harambee iliyofanyika Bondo, Waziri wa Elimu wa serikali ya Moi, Profesa Jonathan Ngeno alisema kiongozi huyo wa upinzani atamrithi Moi. Lakini hatua iliyofuata ni Moi kuwinda viongozi waliokuwa wanahama upinzani.
Kufikia mwaka 1997 karibu vyama vyote vilikumbwa na msukosuko wa ndani na kujikuta baadhi ya viongozi wakijiuzulu na kujiunga na Kanu. Raila alihama Ford Kenya akatua National Development Party.
Raila aligombea urais mwaka huo na akashika nafasi ya tatu nyuma ya Moi aliyeshinda kwa asilimia 40 na Kibaki nafasi ya pili. Mara ikawa zamu ya Raila kuangukia kwenye “mtego wa ushirikiano” aliouanzisha Moi mwaka 2001; akajiunga na Kanu, akateuliwa kuwa katibu mkuu akitarajia kukwea ngazi ya urais kwa msaada wa Moi 2002. Haikuwa hivyo, Moi akamteua Uhuru.
Hapo Raila, Kalonzo Musyoka, George Saitoti na Joseph Kamotho wakapinga, wengi wao wakajiunga na Liberal Democratic Party (LDP) ambacho baadaye kiliungana na Kibaki kuunda National Rainbow Coalition (NARC). Kibaki alishinda lakini mwaka 2007 Raila alisimama kidete kukataa matokeo.
Jumuiya ya Kimataifa ilisuluhisha akatengewa nafasi ya waziri mkuu. Hivi sasa yuko kiguu na njia akitaka Jumuiya ya Kimataifa imsaidie kukabiliana na mitume wawili wa Moi: Uhuru Kenyatta na William Ruto anaodai walipata ushindi wa hila Agosti 8 na wa marudio Oktoba 26. Raila amekwenda Uingereza na Marekani, je, amejibiwa nini?
Msimamo wa nchi hizo, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, utategemea masilahi yao kwa serikali ya Kenya.

No comments:

Post a Comment