Hatua hiyo ni utekelezaji wa pendekezo la Rais John Magufuli aliyetaka waziri wa Tamisemi na wa Waziri ya Afya wakae kujadili namna ya kuzifanya hospitali za mikoa kuwa chini ya Wizara ya Afya badala ya kusimamiwa na Tamisemi kama ilivyo sasa.
Jumamosi Novemba 25,2017 alipozindua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), kampasi ya Mloganzila, Rais Magufuli alisema kufanya hivyo kutaondoa mkanganyiko na kupanga watumishi holela kwenye hospitali, jukumu ambalo wamepewa watu wasio na utaalamu wa masuala ya afya.
Rais Magufuli alisema Tamisemi watabaki wanasimamia hospitali za wilaya na nyingine ndogo.
Waziri Jafo amesema leo Jumatatu Novemba 27,2017 kuwa tayari wameshafanya mazungumzo.
"Kuanzia leo hospitali zote za rufaa zitakuwa chini ya Wizara ya Afya na kwetu sisi (Tamisemi) tutabaki na hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati pekee," amesema.
Kuhusu madaraka ya waganga wakuu wa mikoa amesema wataendelea kuwa chini ya Tamisemi lakini waganga wafawidhi wa hospitali watapelekwa Wizara ya Afya.
Amewataka waganga hao kufanya kazi waliyokubaliana na Tamisemi ya kusimamia ujenzi wa vituo vya afya 172 nchi nzima.
Akizungumza mgongano wa madaraka kwa waganga wa mikoa, Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (Afya), Dk Zainabu Chaula amesema hakutakuwa na shida kwa kuwa kila kitu kimewekwa sawa.
Dk Chaula amesema hata kabla ya kupelekwa huko, hospitali za mikoa zilikuwa zikipeleka taarifa moja kwa moja wizarani.
No comments:
Post a Comment