Monday, November 6

Hongera Samatta, wachezaji wafuate njia


Wiki iliyopita, Shirikisho la Soka Afrika, CAF, lilimtangaza nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta kuwa miongoni mwa wachezaji 30 kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika.
Hii ni mara ya tatu kwa mchezaji huyo ambaye kwa sasa anacheza soka katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Mwaka jana aliteuliwa kuwania tuzo hiyo, lakini hakushinda. Mwaka mmoja nyuma yake, alitwaa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza barani Afrika.
Alishinda tuzo hiyo alipokuwa akiichezea TP Mazembe na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2015 akiwa mfungaji bora kwa kupachika mabao saba.
Kwa mujibu wa utaratibu wa CAF, Samatta na wenzake watachujwa katika mchakato wa tuzo hiyo na nyingine zinazowaniwa kwa mwaka huu wa 2017 kwa kupigiwa kura kabla ya kupatikana washindi ambao watapewa tuzo Januari mwakani.
Kutangazwa kwa Samatta kuwa miongoni mwa wanasoka bora 30 Afrika, pekee ni heshima na ni wazi kuwa Watanzania na hasa mashabiki wa soka watakuwa wamefurahi namna nyota na nahodha huyo wa timu ya Taifa, Taifa Stars, anavyoendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa.
Kimsingi, jina la Samatta linazidi kukua tangu alipouzwa na Simba mwaka 2011 kwenda TP Mazembe na kuichezea kwa misimu mitano mfululizo hadi mwaka jana alipouzwa Genk ya Ubelgiji inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Kama tulivyosema, kila mpenda soka anajivunia mafanikio ya Samatta na wachezaji wanapenda kumtumia nyota huyo kama kioo cha kusaka mafanikio kimataifa.
Hapa kuna mawili, kwanza tunaamini kwamba kuteuliwa kwake kwa mara nyingine katika kuwania tuzo hizo kubwa za soka Afrika ni heshima na kwamba mchango wake katika mchezo huo unaonekana.
Afrika kuna wachezaji wengi wazuri waliotapakaa kila kona za dunia, lakini Samatta amepenya miongoni mwao na hilo ni jambo la kujivunia.
Jingine ni somo kwa wachezahji wa Tanzania. Hili kwa kiwango kikubwa linawahusu wachezaji, nalo ni kuwa na ustahimilivu, kujituma na kuwa nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.
Kama Samatta asingezingatia nidhamu ya soka ndani na nje ya uwanja, leo asingekuwa hapo alipo. Tunawakumbusha wachezaji wa Tanzania kutambua kuwa hakuna kilichomfikisha hapo zaidi ya kujitambua kwake, kujituma na kuwa na kiu ya maendeleo ya soka na kwa hakika anaonyesha mafanikio makubwa katika hilo.
Wachezaji wetu wengine hawana budi kuiga maisha ya Samatta, ndani na nje ya uwanja. Wazielewe vyema changamoto mbalimbali alizopitia na anazoendelea kupitia na muhimu katika hilo, kujua namna ya kukabiliana nazo.
Tunawataka wabadilike, waachea kuishi kwa mazoea. Waondokane na mawazo kwamba watapata mafanikio makubwa kirahisi au bila kujituma.
Samatta anatabiriwa kufika mbali zaidi kwa sababu mbali ya kipaji alichonacho, ni mmoja ya wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu na anayejua kutumia ujuzi alionao kujitengenezea maisha yake katika soka.
Tunaamini kwamba Tanzania kuna kina Samatta wengi tu, jambo muhimu kwao ni kujitambua na kujiwekea malengo na mikakati ya kuyafikia.

No comments:

Post a Comment